SOMO: UFUNGUO WA KUITEKA TANZANIA - ASKOFU GWAJIMAASKOFU MKUU Dr. JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: Ufunguo Wa Kuiteka Tanzania.

Biblia sio kitabu cha dini ni kitabu kinachohusu Sheria za Ufalme wa mbinguni, ni kitabu kinachohusu katiba ya Ufalme wa mbinguni, ni kitabu kinachohusu mila ya Ufalme wa mbinguni , ni kitabu kinachohusu ushawishi wa ufalme wa mbinguni, ni kitabu kinachohusu nguvu ya Ufalme mbinguni hapa duniani.

“Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.” Danieli 11:32

Watu kuokolewa ni mpango wa Mungu?, je kwanini watu wote hawajaokoka?, mambo yanayoendelea mabaya na maovu Mungu anapenda yawepo?, kwani Mungu hana nguvu za kuyaondoa mambo mabaya yanayoendelea duniani?

Watu wengi tangu mababu zetu hawamjui Mungu ndiomaana wanaabudu miungu ya sanamu na mambo mengine. Mambo ya Mungu hayakai katika maneno bali ni katika nguvu, kitu kinacho fanya utofauti hapa duniani ni katika nguvu.

“Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mathayo 16:13 -19

“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote” wakolosai 2:13

Unapo okolewa unahama kutoka kwenye ufalmewa giza(shetani) na kuingizwa kwenye ufalme wa (Nuru)Mungu kwahiyo sisi tupo kwenye Ufalme wa Mbinguni na Yesu ndiye mlango wa huo Ufalme. Kwa kumwamini Yesu na kumkubali Yesu tunaingia sebuleni ndani Ufalme na kuna watu wengine wanakaa hapo sebuleni mpaka wanakufa bila kuingia kwenye vyumba na kumiliki, kwenye sebule hii unapewa ufunguo za utajiri, funguo za biashara, funguo ya ndoa, unatakiwa ufungue na uingie na kumiliki kwa jina la Yesu. Watu wengine wanaingia kwenye sebule hii wakiwa na funguo nyingi wanashindwa jinsi ya kufungua ili wamiliki unakuta wanabakia na funguo zao huku wakisema wana amani na furaha.

Zamani wanafunzi wa Yesu walipokuwa wakiingia kwenye miji walikuwa wakibadilisha miji hiyo na kuirithisha mila ya mbinguni na kubadilisha tamaduni zao na ndiomaana serikali za warumi ziliwakama na kuwauwa kikatili kwa jinsi walivyokuwa wakibadilisha miji kwa hofu ya kuwahofia kama wanasiasa wanataka kupindua nchi zao.

Mfano wakina Paulo walipokuwa wakipita watu walikuwa wakifurika na kupoywa kupitia wao, viziwi walisikia, vipofu waliona na wakati huo wafalme wa kirumi walipokuwa wakipita wao walikuwa hawapokelewi kama vile Paulo na Petro walivyokuwa wakipokelewa kwasababu walikuwa ni wanasiasa.

Ndivyo ilivyo kwenye serikali za nyakati hizi zinahofia watu wa Mungu kwa jinsi wanavyokusanya watu kwenye njia kama wakina Petro kwa hofu ya siasa na kuwaona kama watu wa mapinduzi, lakini huo sio ukweli bali ni nguvu za Mungu zimachiliwa tena duniani zaidi ya karne ya kwanza ili Ufalme wa Mungu na mila zake zijengwe na kutawala juu ya nchi.

NGUVU ZA MUNGU

Kwenye Biblia neno nguvu limeandikwa mara 91. Kwenye kitabu cha Danieli anasema siku za mwisho watu wanaomjua Mungu wao watakuwa hodari na kutenda mambo makuu na ya ajabu, wakati huo ni leo hii na ulimwengu huu sio ulimwengu wa kisiasa bali ni ulimwengu wa nguvu za Mungu kudhihirika kwenye tawala za wanadamu kwa namna isiyo ya kawaida. Nguvu hiyo ni ile inayoweza kuwabeba na kuwageuza wachawi na waganga wa nchi wakawa makuhani wa Mungu na nguvu hii haiwezi kuzuiwa sababu atakaye shindana nayo atapondwa kabisa.

“Kanisa kama halina nguvu za Mungu hilo sio kanisa la Yesu.”
“Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]” Mathayo 6:13

Ufalme wa Yesu ndani yake kuna nguvu ambayo ni uweza wa kulifanya jambo lolote linalotakiwa liwe kwaajili ya makusudi ya Ufalme baada ya kuwa nguvu imetumika na lile jambo lililokusudiwa linaonekana. Jambo hilo lililotokea linaitwa Utukufu, mfano mtu amekufa na akaamshwa kwa jina na Yesu, akiamka lile tendo linaitwa utukufu, Sisi ni wana wa Ufalme wa Mungu, ni wana wa Utukufu wa Mungu, sisi tumezaliwa msalabani kwenye nguvu za Yesu kristo na mambo ya nguvu yanatufuata na sisi na imani yetu imejengwa kwenye nguvu za Bwana.

“Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.” Mathayo 9:34

Yesu alikuwa na nguvu za Mungu mpaka mafarisayo(watu waliosoma Sheria) wakachanganyikiwa, mafarisayo hao walikuwa wakiamini nguvu zipo lakini hawakuamini kama ni ngvu za Yehova bali ni za shetani pekee ndizo zinaweza kufanya kazi.

Nguvu za Ufufuo na Uzima hazijaenda likizo bado zipo zinatenda kazi duniani.

“Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.” Mathayo 14:2

“ Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,” Matendo 1:1

Dunia yote watu wanajua kulogwa kupo, wanajua nguvu za shetani zipo maraisi na mawaziri wanajua nguvu za shetani zipo japo hawawezi kukiri hadharani lakini ukiwauliza nguvu za Mungu kama wanazijua unaweza kushangaa hawazijui. Mashetani ni malaka waliohasi na wanaweza kujibadilisha kuwa umbo lolote.

“Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.” Luka 11:21

Kumbe shetani ana nguvu zake na analinda ikulu ya Tanzania, analinda bunge la Tanzania, analinda mahakama ya Tanzania, analinda madini na gesi ya Tanzania na amepatikana mtu mwenye nguvu kuliko yeye wa kumwendea na kumshinda na kumnyanganya silaha zake zote alizokuwa anazitegemea ambaye ni kanisa na vitu vyote alivyovishika na kumtupa mbali kwa jina la Yesu.

“Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.” 1Wakorintho 1:18

Mungu anawachagua wanyonge wa dunia anawapa nguvu ili awaaibishe wakuu wa dunia, anawachagua wale watu ambao hawafananii ili awaaibishe wenye hekima wa dunia kama akina Petro na Yohana ambao hawakuwa na elimu yeyote lakini waliwaaibisha wenye hekima wa dunia wa kipindi kile kwa nguvu za Mungu.

Ule ujasiri wa kwenda kumfuata maiti na kumfufua ni ushindi tosha kabisa haijalishi amefufuka au hajafufuka nenda kawafuate utashangaa maajabu ya nguvu za Mungu aliye ndani yako.

“Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.”1wakorintho2:4

“Lakini nitakuja kwenu upesi, nikijaliwa, nami nitafahamu, si neno lao tu waliojivuna, bali nguvu zao. Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.” 1 Wakorintho 4: 19 – 20

“Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.” 1 wakorintho 15:24

“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu” Waefeso 3:20

Yohana mbatizaji hakuwa anavaa vizuri au kula vizuri au kulala mahali pazuri bali alikuwa anavaa mavazi ya ngamia, anakula asali na nzige na alikuwa analala porini na wanyama lakini watu walikuwa wakitoka Yerusalemu kwenda porini kumfuata kwasaabu alikuwa ana nguvu za Mungu zisizo za kawaida na leo hii nguvu zile zipo ndani yetu hivyo tunatakiwa tutoke kwenda kila sehemu kuzidhihirisha juu ya nchi ili nchi ibadilike na kuwa ufalme wa Mungu na mila ya Ufalme ienee.

“Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.” Wakolosai 2:12

Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasiondoke Yerusalemu mpaka watakapopokea uweza utokao juu, na maana yake alifahamu kuwa kwenye dunia hii kuna uweza utokao chini kuzimu. Kwenye dunia watu wanatoa elimu za kubadilisha fikra ili wabadilishe nafsi za watu na kuwaaminisha kuwa unaweza kuijaza nafsi yako kwa elimu zao na hiyop ndiyo itakayokuwa hatima yako bila ya kumtegemea Mungu kitu ambacho sio kweli.

Ukiri:
“Ndani yangu kuna nguvu za Mungu”

Mungu alipomuumba mwanadamu na kumpulizia Pumzi ya uhai ambayo ni Roho, baada ya Pumzi hi na mwili vilipoungana vikatengeneza nafsi hai.

Ukiri:
“Mimi ni roho na sio mwili”

Mungu ni Roho na wote waliozaliwa kwake ni roho
“Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.” Yohana 3:6

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”Yohana 1:12

“Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.” Zaburi 82:6

Kilichozaliwa na mbwa ni Mbwa, kilicho zaliwa na nyoka ni nyoka, kilichozaliwa nap aka ni paka na kilicho zaliwa na Roho ni Roho. Roho ya mwanadamu ndiyo mwanadamu mwenyewe. Jina lako sio jina la mwili wako bali ni jina utakaloenda nalo mpaka mbinguni, roho yako ndiyo wewe na ndiyo inayobeba jina lako na roho ya kila mtu inatoka mbinguni ndiomaana kila mtu anajua mema na mabaya.

Katikati ya Roho ya mwanadamu kuna nafsi ya mwanadamu ambayo ni daraja la kuingia mwilini kutokea rohoni. Mungu anapomimina uweza anaujaza rohoni na Mungu anapotaka atoke aje mpaka kwenye mwili ili uweke mikono yako juu ya wagonjwa wapone, mikono yako inakuwa mikono ya Mungu, mwili wako unakuwa mwili wa Mungu na akili yako inakuwa makili ya Mungu, kila utakachokisema kitakuwa kinatokana na Mungu, Unapokuwa unanena kwa lugha ni roho yako inazungumza na Mungu.
Kwanini uwezo wa Mungu haudhihiriki na unazo nguvu zisizo za kawaida? Unaweza ukawa unanena kwa lugha kwenye ibada na ukitoka kwenye Ibada unajisikia unazo nguvu za ajabu lakini ukimwombea mtu haponi, kwenye roho yako kuna Ufalme wa Mungu ambao unatakiwa utoke ndani yako uingie katika nchi lakini umenasa kwenye nafsi hautoki nje ya mwili. Kuna wahubiri wengi wana maelezo ya elimu nzuri lakini hawana nguvu za Mungu, na kuna watu wana nguvu za Mungu lakini wanaugua kwasababu zimebakia ndani yao.

SIRI YA UDHIHIRISHO WA NGUVU ZA MUNGU DUNIANI.

“Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.” Zaburi 103:1

Kuna wakati Mungu anatoka rohoni na kushika midomo ya watu na kuanza kuongea kupitia wao Zaburi 89.]

Mtu ana sehemu kuu tatu ambazo ni Roho, Nafsi na mwili. Ndani ya nafsi kuna vipengele vine ambavyo ni

1. UTASHI. Utashi ni idara iliyo ndani ya nafsi ambayo inamwongoza mtu kuwa na hali ya kutaka, shetani alimwingilia Adamu na Eva akawapa tunda lakini Mungu hakuingilia kati ili awakataze kwasababu amempa mtu utashi wa kuamua atakalo kulifanya lakini Mungu hawezi kukuzuia kwasababu ya nguvu ya Utashi. Ndani ya mtu kuna nguvu ya utashi ambayo mtu mwenyewe ndiye atayeweza kudhibiti.

2. HISIA. Ndani ya nafsi kuna kitengo cha hisia ambacho husababisha Kujisikia kumchukia mtu, kujisikia kumpenda mtu, kujisikia kukata tama, kujisikia hali ya huzuni, kujisikia hali ya kutokuacha, kujisikia kupuuzwa.

3.MAWAZO. Idara ya mawazo inajumuisha, elimu, utaratibu, fikra. Ndani ya nia ndipo mtu anaweza kuweka elimu ambayo inambadilisha jinsi ya kuongea na kutembea, mtu anabadilika kutokana na mazingira aliyoishi, elimu aliyoipata ambayo inakaa kwenye nia ya mtu, tofauti ya mtu na mtu ni nia zao na Biblia inasema tuwe na nia kama aliyokuwa nayo Yesu kristo.

4. MOYO. Kipengele kingine ni Moyo wa mtu ambao ni kitengo ndani ya nafsi (subconscious) hizi hisia zako, utashi wako, nia yako inapokaa sana inahamia kwenye moyo na kuwa sehemu ya maisha yako. Maana yake vile vitu unavyovifanya mara nyingi tena na tena vinakuja kukaa kwenye moyo na kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku, unavyo zini mara kwa mara, unaposema uongo mara kwa mara, unapo iba mara kwa mara, inafika sehemu inakuwa sehemu ya maisha yako na kuacha inakuwa ni kazi, mtu anapofanya ukahaba mwisho unakuwa sehemu ya maisha ya mtu sababu ya kuutenda mara kwa mara.

Aishivyo mtu leo ndivyo atakavyokuwa maisha yake ya baadaye, Biblia inasema alivyo mtu moyoni mwake ndivyo alivyo nafsini mwake.Mambo haya unaweza ukakuta mtu ameyafanya tena na tena mpaka yamekuwa sehemu ya maisha yake.

Mungu yupo rohoni na unapokuwa unaomba unanena kwa lugha na Mungu anaanza kupita kwenye nafsi ili aiguse dunia kupitia mwili wako lakini akifika kwenye nafsi yako anakuta nafsi imejaa“mazagazaga” na daraja la kuunganisha roho na mwili limevunjika hakuna mawasiliano. unawaza kukuta mtu anamtoa pepo aliye ndani ya mtu lakini pepo huyo hatoki kwasababu Mungu ameshindwa kupita kwenye daraja la nafsi kufika mwilini amtoe pepo huyo. Japo mtu huyo anampenda Yesu na anaomba kwa bidii na kumtafuta Bwana lakini nafsi yake imetekwa na mambo ambayo yanamzuia Mungu asidhihirike duniani.

Nafsi ikisafishwana kuwa safi hapo ndipo unapoweza kuiambia serikali ifanye jambo fulani na ikafanya sababu Mungu ndiye amesema, hapo ndipo vivuli na leso vinapoanza kuponya watu na udhihirisho wa Nguvu za Mungu unadhihirika kwenye dunia kwa namna ya ajabu.

Vitu hivi vinaingia kwenye nafsi za watu kwa njia ya kuona, vitu watu wanaviona kwenye movies, kwenye televisheni, kwenye picha kupitia macho na watu wanahamishia kwenye familia zao na maisha yao ya kila siku. Unaweza kumwona mtu anampenda Mungu na amevalia kiajabu na hajui sababu nafsi yake imejaa vitu hivyo na kwenye hali hiyo Mungu aliye rohoni anapotaka kutoka anakutana na nafsi imejaa mambo ya ajabu ya kwenye movies, na mambo mengine anaamua kurudi rohoni japo mtu huyu ameokoka na anampenda Bwana lakini nguvu za Mungu hazidhihiriki kwake. Unaweza kumkuta mtu anaishi maisha ya kwenye Movie ambayo hata watu wanayoigiza hawaishi maisha yale lakini yeye anayaishi maisha yale na kushawishi mke/mume wake ayaishi sababu yamesajiliwa kwenye nafsi yake NAFSI IMEIBIWA. Nafsi inaweza kuibiwa pia kupitia milango kama ya kile unachoona, unacho kisikia, unacho kigusa, unacho kishika humo ndipo mnapoingiza mazagazaga hayo kwenye nafsi yako.
Mungu yuko ndani ya Roho yako anataka kuibeba dunia na falme za dunia ziwe za mwanakondoo. Mungu amehama rohoni anaingia mwilini. Uwezo wako wa kuondoa uchafu kwenye nafsi ndiyo uwezekano wako wa kutumiwa na Mungu na kutenda mambo ya ajabu.

1Wafalme 8:48
“Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote; yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu)” 2Nyakati 6:28

“Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wafilipi 4:7

“Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo” Waebrania 10:16

“Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika ndipo anenapo,” Waebrania 9:22

“Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama.” Zaburi 104:3

Takasa nafsi yako kwa damu ya Yesu ili Mungu aitumie kupita kuiteka dunia kwa nguvu zake

“Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake. 4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa. 18 Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote;” 1 wakorintho 14: 2,

Ukitaka kupenya kwenye maisha zingatia usafi wa nafsi yako mbele za Mungu. Nena kwa Lugha siku zote na usizoee kuseme unaingia kwenye maombi sababu unakuwa unamaanisha unatoka kwenye maombi na sio lazima mdomo wako utoe sauti. Unaponena unaharibu mambo mengi ya ufalme wa giza, ukinena kwa lugha dakika mbili unakuwa na nguvu ya dakika mbili, ukinena muda wote unakuwa na nguvu muda wote.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.