SOMO: USIMNENEE MABAYA MKUU WA WATU WAKO -MCHUNGAJI MADUMLABwana Yesu asifiwe…

” Mkuu wa watu wako” ni kiongozi wa mamlaka fulani haswa mamlaka ya kiserikali mwenye kutawala kwa mujibu wa sheria za nchi husika. Mtu wa namna hii hujulikana kuwa ni mkuu wa watu,au kwa lugha ya kiofisini anaweza kuitwa mkubwa wa kazi-Yeye husimamia shughuli zote za eneo lake na huongoza kundi la watu.

Kiongozi wa namna hii,anaweza akawa ameokoka au la! hajaokoka.Kazi yake kubwa ni kuongoza watu sawa sawa na mamlaka aliyopewa. Kila mmoja anapaswa kufuata sheria za nchi zinazoongozwa na mkuu huyo akiwa ameokoka au hata kama hajaokoka,kwa sababu mamlaka yoyote imewekwa na Mungu;

” Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. “Warumi 13:1

Haupaswi kumnenea mabaya kiongozi wako eti kwa sababu amekuudhi au amekwenda kinyume nawe katika yale unayoyataka yafanyike,au kwa sababu hajaokoka kama wewe ulivyookoka. Ninaposema ” Kumnenea mabaya ” nina maana ya kumtukana,kumkashifu kwa lugha mbaya za matusi n.k

Wapo watu wenye kunena mabaya kwa wakuu wao,kana kwamba wao wanaweza kuongoza. Leo neno la Mungu linatuonya,kuzuia vinywa vyetu visinena mabaya kwa viongozi wetu,bali vinywa vyetu vinene yaliyomema yenye kujenga nchi au mahali husika,hata kama mkuu amekosea katika utendaji wake wa kazi bali tumia muda huo kumlekebisha kwa maombi,na kinywa kinene juu ya matengenezo.

Tumuangalie Paulo mtume alipokamatwa na kuonewa na mkuu wa watu wake,jinsi ilivyokuwa. Tunasoma;

” Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.” Matendo23:3-5

Paulo alijaribu kumnenea vibaya kuhuni mkuu kwa maana hakujua kwamba mtu huyo ni kuhani yaani ni mkuu wa watu,mwenye mamlaka. Ndio maana aliweza kujirudi haraka na kusema ” sikujua ndugu zangu ya kuwa yeye ni kuhani mkuu…” kwa lugha nyepesi ni kwamba Paulo hakupaswa kutamka mabaya juu ya mkuu wa watu.

Ikiwa Paulo mtumishi wa Bwana hakupaswa kutamka neno baya kwa kuhani mkuu,basi hata sisi hatupaswi kutamka mabaya kwa wakuu wetu,na makuhani wetu mahali tunapoabudu. Kumbuka ya kwamba mkuu wa watu,huwekwa na Mungu hata kama baadaye atageuka na kuwa dikteta,mkuu wa namna hii ( dikteta ),BWANA atashughulika naye.

Mtu yeyote asiyetii mamlaka za serikali mtu huyo hufanya dhambi. Tena hajakamilika katika imani yake hata kama ameokoka kama tulivyo leo.

Jiulize ni mara ngapi umemnenea mabaya mkuu wa watu wako mahali ulipo na ukadhani ya kwamba upo sahihi? Au ni mara ngapi ulinena mabaya kwa kuhani wako mahali unapoabudu kisha ukaona ni sawa ? Tena ukadhani kuwa si dhambi,au ukaona ni dhambi ndogo ndogo tu?

Bali mimi ninakuambia leo,kwamba ikiwa ulifanya hivyo basi ujue ulifanya dhambi na ukumbuke kwamba hakuna dhambi ndogo wala dhambi kubwa,dhambi zote ziko sawa-lakini dawa ya dhambi ni kuitubia kwa kumaanisha kuiacha,tubia uovu huo wa kuwanenea vibaya watu waliowekwa na Mungu katika nafasi mbali mbali.

Leo,watu wanajikwaa sana katika vinywa vyao kwa kuwasema vibaya watumishi wa Mungu ( makuhani ) wakidhani wapo sawa. Utakuta waamini tena watenda kazi kutwa ni kumsema vibaya kuhani wao. Ni dhambi ukifanya hivyo.

Ikumbukwe kwamba;hutakiwi kunyanyua kinywa chako na kumnenea mabaya mtu aweye yote. Zipo njia nyingi za kuwalekebisha wakuu wenye makosa wawapo madarakani lakini sio kwa kuwanenea mabaya.

Sasa ikiwa unahukumiwa ndani yako katika dhambi ya namna hii pale ulipochukua muda wako na kumnenea vibaya mkuu wa watu,iwe ni kuhani wako mahali pale unapoabudu,au iwe ni kiongozi wowote wa serikali. Basi muda huu ni muda mzuri wa kukisogelea kiti cha rehema ili utubie dhambi hiyo. Ninaomba tusaidiane wote mimi na wewe katika maombi hayo kwa kunipigia sasa kwa namba yangu ya simu hii 0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

S.L.P 55051 Dar,Tanzania.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar-TZ )

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.