SOMO: UPONYAJI UPO TAYARI KWA KILA AAMINIE - MCHUNGAJI MADUMLABwana Yesu asifiwe…

Uponyaji ni nini?

Ni tendo la kiimani la kupokea uzima katika roho au mwili kwa njia ya kuombewa,kuwekewa mikono au kulisikia neno sahihi la Kristo Yesu. Tendo hili la kiimani humletea mwamini uzima wa kiroho na afya ya kimwili pale ilipopunguka,kumbuka~wengi walipoponywa udhaifu wa miili yao,waliponywa pia na roho zao.

Kumbuka tena ya kwamba package ya uponyaji ilikwisha achiliwa pale msalabani maana Yeye mwenyewe Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu katika mwili wake ili tulipokuwa wafu kwa dhambi zetu,tuwe hai kwa mambo ya haki na kwa kupigwa kwake sisi tumeponywa ( 1 Petro 2:24 )

Hivyo basi,uponyaji haufanywi na mtu awaye yoyote yule isipokuwa Mungu. Hata madaktari bingwa wao hawaponyi bali hutoa tiba tu,mwenye kuponya ni Mungu.Watumishi wa Mungu pekee ndio hufanyika kama daraja au chombo cha kuleta uponyaji ulioachiliwa na Bwana kwa muhusika mwenye kuhitaji.

Kumbe basi wapakwa mafuta wa BWANA ni watu wa muhimu sana sababu wao hufanyika kama chombo cha kuleta uponyaji,bali Mungu ni wa kuogopwa mno Yeye ndie mponyaji mwenyewe.

Yeyote atakaye liamini jina la Yesu Kristo,uponyaji ni mali yake. Hata kama mtu akiwa wa dini nyingine,lakini akija sasa kuliamini jina la Bwana,uponyaji ni sehemu yake,na kupitia huo uponyaji ataokoka. Uponyaji umekwisha achiliwa kwa watu wote wenye kuliamini jina la Yesu Kristo sababu Roho wa Bwana naye ameachiliwa tayari kwa watu wote kushughulika na maisha yetu,thus why ~ ninasema uponyaji upo tayari hata kwako,amini tu na itakuwa hivyo katika jina la Yesu Kristo aliye hai.

~ Uponyaji wa kiroho na wa kimwili waweza kufanyika kwa njia zifuatazo;

▪ Kuwekewa mikono.

▪ Kuombewa.

▪ Kulisikia neno sahihi la Kristo Yesu.

▪Uponyaji kwa njia ya kuwekewa mikono.

~ Mtu aliyekuwa dhaifu aweza kupokea nguvu ya Mungu kwa kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu. Hata kama mtumishi hakuukemea udhaifu huo,lakini kitendo cha kuweka mikono yake juu ya kichwa cha mgonjwa ni dawa tosha ya kuleta uponyaji. Maana imeandikwa;

“ watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Marko 16:18

Pia waweza angalia jinsi Bwana Yesu naye alivyoitumia njia hii pale alipomponya mamaye mkewe Petro,imeandikwa;

“ Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia.” Mathayo 8:14-15

Biblia haituambii kwamba Bwana Yesu alimwombea huyu mama,bali tunachoweza kuona ni kwamba Bwana Yesu alimgusa mkono,homa ikamwacha. Mguso tu wa mtu wa Mungu ni dawa tosha,hata kama hakuomba sababu upako ungalimo ndani yake. Maana hata wakina Petro waliweza kuponya wagonjwa kwa kivuli chake tu,sababu ya upako. (Matendo 5:15)

▪ Uponyaji kwa kuombewa.

~ Mtu dhaifu wa mwili anahitaji kuombewa ili apokee uponyaji wake. Kwa kuombewa~mgonjwa anaweza akawa Marekani katika bara jingine na mtumishi wa Mungu akawa Tanzania Afrika bara jingine lakini uponyaji ukafanyika saa ile ile ya maombezi maana maombi hayana umbali.

Mathayo 17:18~ Yesu amkemea pepo,naye pepo atoka kisha kijana akapokea uzima.

~ Mara nyingi njia ya kuombewa huambatana na kuwekewa mikono ~ Matendo 28:8

▪ Uponyaji kwa kulisikia neno la Kristo Yesu.

~Kuna wakati ambapo mtu aliyekuwa dhaifu huponywa kwa neno la Mungu tu,sababu neno la Mungu ni silaha tosha. Mtu mwenye imani ya uponywaji,akifungua moyo wake na kuliluhusu neno la Bwana lipite basi ujue neno halitapita bure ni lazima liponye,ligange,lihuishe kila kitu ndani ya mwili na roho pia. Isaya 55:10-11

Tuangalie mfano mmoja,kamailivyoandikwa;

“ Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. “Matendo 14:9-10.

Mtu huyu hakuombewa,wala hakuwekewa mikono bali alilisikia neno la Mungu lenye uweza lililokuwa likihubiriwa na Paulo,kisha alipoonekana ana imani ya kuponywa~aliambiwa asimame na aende zake,maana uponyaji ulikuwa ni mali yake,sababu aliamini. Ndio maana leo ninakuambia kwamba uponyaji ni mali yako wewe unayeliamini jina la Bwana Yesu Kristo.

Wakati napata wazo hili la kuandika ujumbe huu mzuri,nikagundua kwamba kila mtu anahitaji uponyaji maana kila mtu ana shida yake ambayo kwa hiyo haiwezekani kuponywa na mwingine awaye yoyote yule isipokuwa Mungu tu. Hata wewe pia una shida ambayo kwako ni msimba usioweza kushughulikiwa kibinadamu isipokuwa kwa Mungu tu.

Ndiposa nikawaangalia matajiri,nikaona na wao pia wana shida nzito zinazomuhitaji Mungu aingilie kati au kama la! Watakufa na pesa zao pamoja na shida zao za magonjwa na roho zao zitaenda motoni kuteseka milele ikiwa watakataa wokovu mkuu namna hii maana pesa,mali au farasi haziwezi kumpa mtu wokovu,yaani haziwezi kuiokoa roho,imeandikwa;

“ Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. ” Zab.33:16-20

Hapo ndipo nilipoanza kumuangalia Naamani jemedari wa jeshi la mfalme wa Shamu. Mtu huyu alikuwa ni mtu mwenye cheo,mkubwa serikalini lakini alikuwa na ukoma. ( 2 Wafalme 5:1,&2-14 ).

Pesa zake hazikuweza kumsaidia Naamani kuondokana na ukoma,bali Naamani alimuhitaji Mungu amponye. Laiti kama Naamani asingelikubali kuamini na kutii sauti ya Mungu kupitia nabii Elisha,basi ni dhahili angelikufa na ukoma wake ingawa alikuwa na pesa.

Watu wengi wanafanana na Naamani,kwamba kweli wanaumwa lakini hawataki kuliamini jina la Bwana Yesu. Au hawataki mambo ya wokovu kisha wanajikuta wanakufa na ukoma wao. Naamani naye alianza kukataa neno la Mungu kwa sababu ya mitazamo yake ( 2 Wafalme 5:11 ).

Naamani alilitaka Mungu afanye vile alivyotaka yeye,na si atakavyo Mungu kupitia nabii Elisha. Haya ni makosa sana,kumpangia Mungu kwa kukataa kile anachokuambia mtumishi wa Bwana.

Sijui unapitia katika jaribu gani ndugu mpendwa,lakini hata kwa hilo bado waweza kupona. Maana hakuna jambo gumu linalomshinda Bwana, yote yapo katika uweza wake. Waweza pia kunipigia kwa simu yangu ili tuombe pamoja,

piga kwa namba hii kwa maombezi; 0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.