HOJA: KAULI TATA MAARUFU ZENYE KUKINZANA NA NENO LA MUNGUAskofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi MKuu, WAPO Mission International.

Hoja ya leo nimeona niwasilishe baadhi ya “kauli tata” ambazo ni maarufu sana kwa waumini wa madhehebu ya dini kwa kudhaniwa kwamba ni “maneno ya Mungu.”! Sababu ya kuamua kuzichambua ni kwa sababu, zimekubalika kama ni “Neno la Mungu wakati zinakinzana na Neno la Mungu”! Nia ni kuweka waziwazi uongo wa Ibilisi uliojificha kwenye kauli hizo tata ili aliyekuwa amedanganyika afunguliwe fahamu na kuwekwa huru kwa kuijua kweli.

Kauli tata ya 
“Sisi sote ni watoto wa Mungu”

Ni kweli kwamba kwa asili binadamu wote tunatokana na watu wawili ambao ni binadamu wa kwanza walioumbwa na Mungu. Na binadamu hawa waliishi miaka mingi isiyojulikana mpaka wakati walipoasi amri ya Mungu wakaanguka katika dhambi. Kuanzia wakati huo mpaka hivi leo, vizazi vilivyofuata viliathiriwa na dhambi na kujulikana kama watumwa wa Ibilisi kwa sababu hiyo.

Kwa sababu ya upendo wa Mungu, almtuma Mwana wake pekee Yesu Kristo ilia je kutukomboa katika utumwa wa Ibilisi. Tangu ujio wa Kristo duniani, ndipo ukaanzishwa uzao mpya wa kiroho ambayo unatoa fursa kwa kila binadamu mwenyedhambi kuimpokea Yesu na kisha kupata uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu. Kwa hiyo, tangu Yesu alipokufa na kufufuka katika wafu, tuna makundi ya aina mbili ya binadamu hapa duniani. Kundi la “watoto wa Mungu”, na kundi la “watoto wa Ibilisi”.

“Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” (1 YOH. 3:10)

Kwa hiyo si kweli kwamba, kila binadamu aliye hai hapa duniani ni “mtoto wa Mungu.”! Haijalishi aina ya tofauti za madhehebu ya dini na wasio na dini kabisa. Wote ni “watu wa Mungu” kwa maana tu viumbe wake Mungu kwa asili. Lakini sio wote ni watoto wa Mungu ati kwa sababu ni binadamu. Kuwa mtoto wa Mungu ni uchaguzi binafsi ambao unafanywa na mtu mwenyewe.

“Wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika “watoto wa Mungu”, ndio waliaminio jina lake.” (YH.1:12)

Jambo jema na kutia hamasa ni kwamba walio “watoto wa Mungu” sio kwamba tunajiaminisha tu kwa akili zetu wenyewe. Yesu mwenyewe ametusaidia kwa kumtuma Roho Mtakatifu ambaye amekuja kufanya makao ndani yetu. Na tunapompokea Roho Mtakatifu akiisha kujaa kwa wingi ndani yetu, yeye ndiye hufanya kazi ya kututhibitishia na kutushuhudia kwamba sisi ni watoto wa Mungu:

“Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.  Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;” (RUM. 8:15-16)

Je wewe mwenzagu una hakika kwamba ni “mtoto wa Mungu”? Unaamini hivyo kwa sababu ya kauli ya mazoea kwamba “binadamu wote ni watoto wa Mungu”; au ni uchaguzi wako binafsi ulioufanya wa kumpokea Yesu Kristo ili akupe uwezo wake wa kufanyika mtoto wa Mungu?


Kauli tata ya 
“Sisi sote tunamwabudu Mungu mmoja”

Kauli tata nyingine inayokizana na Neno la Mungu lakini imeshika akili za watu wengine ni dhana ya kudai kwamba “Sisi sote tunamwabudu Mungu mmoja”! Ati pamoja na tofauti zetu za kimadhehebu na mitindo mbalimbali ya kuabudu; bado tunamwamubu Mungu mmoja tu iwe kwa kujua au kutokujua!

Tatizo kubwa linaanzia hapo hapo kwenye tofuati ya itikadi na mitindo ya kuabudu. Angelikuwa ni Mungu mmoja yule yule kwanini aabudiwe kwa njia na mitindo tofauti?  Wachiliana mbali tofauti za kiitikadi na kimitindo ya kuwabudu, mbona tunashawishiana na kuvutiana kila upande unafanya juhudi za kupata wafuasi wa itikadi nyingine wajiunge na itikadi yao? Majibu ya maswali yataonesha dhahiri kwamba hata kama yupo Mungu mmoja anayestahili kuabudiwa na sisi sote; lakini sio itikadi zinamwabudu Mungu mmoja.

Baada ya kusema yaliyotangulia, nije kwenye maandiko yasemavyo kwa habari ya Mungu anayestahili kuabudiwa na wote na jinsi ya kumwabudu. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatupa ukweli kama ifuatavyo:

“….jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.  Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.  Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” (MDO 4:10-12)

Unaona? Kisa cha Mungu kumtuma Mwanawe licha ya kutukomboa toka utumwa wa Ibilisi, lakini pia kutuwezesha kumwabudu Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo ambaye ni mlango wa kuingilia patakatifu pa patakatifu pa Mbinguni.

Kwa mantiki hii, hakuna mtu mwingine awaye yote chini ya mbingu ambaye inatupasa kuokolewa isipokuwa Yesu Kristo mwenyewe. Msingi wa maandiko haya ni kukanusha uvumi na itikadi za dini nyingine zote zisizomtambua Yesu Kristo kuwa ndiye peke ambaye anatupeleka kwa Mungu wa kweli kwa sababu Mungu huyo ni Baba yake halisi. Kwa hiyo, dhana kwamba sisi sote tunamwabudu Mungu mmoja si kweli. Kila dini ina Mungu wake ambaye wafuasi wake wanamwabudu. Hata kama majina yanaweza kufanana lakini, kigezo cha kumwabudu Mungu wa kweli ni kupitia Yesu Kristo peke yake.

 Kauli tata kwamba 
“sisi sote twaenda sehemu moja baada ya kufa”

Kauli tata ambayo imeshika hisia na akili za wengi kwamba ni Neno la Mungu, ni dhana hii inayodai kwamba, “sisi sote tukifa tunaenda kumoja, yaani kukaa na Mungu milele.” Ati “SISI SOTE KAMA BINADAMU TUNAELEKEA SEHEMU MOJA BAADA YA KUFA.” Dhana hii inadai kwamba bila kujali maisha ya mtu anayoishi hapa duniani, yawe machafu au masafi kulingana na dhamiri yake kwa itikadi ya dini yake akifa lazima anaenda sehemu moja ile ile ambayo binadamu wanapokufa wanakwenda kuishi na Mungu milele.

Tena wengine wanachanganya zege zaidi, kwamba tofauti za madhehebu ya dini ni sawa na njia nyingi tofauti lakini zinaishia na kuunganika kwa Mungu mmoja baada ya kufa. Ni kweli kwamba, kila anayekufanya atakutana na Mungu siku ya kiyama. Lakini inategemea unakutana na Mungu kwa kupitia NJIA ipi. ZIko njia mbili kuu hapa duniani. Kuna njia iendayo upotevuni, na kuna njia iendayo uzimani aliko Mungu baba.

Kana kwamba hii haitoshi, siku hizi kuna kauli tata za nyongeza zinazotoa faraja kwa wafiwa zinazosema; “Mungu amempenda zaidi.”! Ninatambua sana umuhimu, ya kwamba, wakati wa msiba wafiwa wanahitaji faraja za karibu ili kutuliza huzuni na maumivu yatokanayo na kuondokewa na mpendwa wao. Pamoja na juhudi na huruma za kuwafariji wafiwa, haifai kabisa kutoa kauli ambazo sio Neno la Mungu kwa sababu kwanza zinazidi kushindilia uongo wa kiimani na wengi wanazidi kupotea kwa uongo huo.


Jamani kama ingelikuwa ni rahisi kwamba kila mtu anayekufa anakwenda kukaa kwa Mungu na kupumzika moja kwa moja, pasingelikuwepo haja ya kuwahubiriwa watu Injili ya wokovu wa Yesu Kristo ili watubu na kuzaliwa upya kiroho! (MK.16:16)

Yesu alisema kwamba, “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendnayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.” (MT.7:13-14)

Mfani mwingine unaoshuhudia kwamba sio kweli kwamba watu wote wanapokufa wanaenda sehemu moja, ni mfano vifo vya “Tajiri Lazaro na maskini” kama ilivyosimuliwa katika Injili ya Luka. (Lk.16:19-26) Humo tunasoma Tajiri alipokufa alikwenda mahali pa mateso na maskini alipokuwa alikwenda kifuani pa Ibrahimu mahali pa mapumziko. Hizi ni sehemu mbili tofauti na kila anayekufa huenda upande wake kulingana na aina ya njia aliyoichagua tangu alipokuwa angali hai.

MWISHO

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.