HOJA: PASIPO YESU HATUWEZI KUFANYA CHOCHOTE

Askofu Sylvester Gamanywa.
WAPO Mission International.
©The Living Truth Fellowship
“Mimi ni mzabibu; ninyi ni matunda, akaaye ndani yangu name ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (YH.15:5)

Kwanini Yesu alisema bila
yeye hatuwezi kufanya lolote?

Kufahamu maana ya kile alichomaanisha Yesu hatuna budi kurejea mwanzo wa kauli zake katika habari hii. Alianza kwa kusema kwamba “Yesu ndiye mzabibu; na wanafunzi wake ni matawi. Na akasema kwamba kazi ya matawi ni kuzaa matunda. Kisha ndipo alipofikia kusema kauli hii kwamba “wanafunzi wake ambao ni matawi, hawawezi kuzaa matunda yanayotarajiwa kama hawatadumu katika uhusiano kati yao na shina la mzabibu.”!

Kwa hiyo, kile alichomaanisha Yesu kwenye kauli yake kwamba “Pasipo yeye haiwezekani kufanya lolote” aliwalenga wanafunzi wake kuwa makini kwamba, katika kutekeleza majukumu aliyowakabidhi watafaulu tu pale wakidumu katika maadili yake ya kimahusiano na si vinginevyo.

Najua kwamba mfano huu ni mgumu kuutafsiri kiroho kwa sababu mfano wa mti na matawi ni vitu vilivyoshikamana tangu mbegu inapochipuka kutoka aridhini. Sisi kama binadamu kila mtu yuko kipekee na hata wanafunzi wenyewe ambayo wanaitwa matawi hawakuwa wameshikamana kimwili na Yesu.

Lakini siri ipo kwenye hili neno “mshikamano”! Mshikamano! Mshikamano! Tafsiri ya neno hili maana yake ni “hali ya watu kuwa na msimamo na ushirikiano wa karibu katika kutimiza azma Fulani.”  Na tafsiri ya neno azma maana yake ni “jambo linalokusudiwa kufanywa; au madhumuni, au makusudio, au lengo.”

Haya kwa ufafanuzi huu hebu sasa turejee kwenye kauli ya Yesu kuhusu mshikamano kati yake na wanafunzi wake. Hapa ndipo kuna siri ya kujifunza kiufunuo. Kumbuka Yesu aliwatuma wanafunza waende wakazae matunda. Lakini aina ya matunda waliyotumwa kuzaa yalihitaji ushirikiano wa karibu kati yao na Yesu, na sio kufanya wao kivyao vyao!

Ni matunda ya namna gani
 tuliyoagizwa kuzaa sana?

Tumeanza na msamiati wa kile Yesu alichomaanisha aliposema pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya lolote. Na tumejifunza kwamba alilenga sisi kama wanafunzi-matawi ili tupate kuzaa kama ilivyo asili ya mtu, lazima tuwe tumeshikamana na shina la mti ambalo ni Yesu mwenyewe. Na tumejifunza mshikamano unaotakiwa ni mtazamo na ushirikiano wa karibu kati yetu na Yesu katika kutekeleza azma yake.

Sasa ni muhimu tujifunze kuhusu msamiati mwingine ambao unatakiwa kujulikana maana yake. Nao ni neno “matunda”! Nii matunda ya namna gani tunatarajiwa kuzaa? Majibu ya swli hili yanaweza kutofautiana kwa sababu ya nadharia mbali mbali za kimapokeo.

Kuna nadharia inayofundisha kwamba matunda “ni idadi ya watu wanaohubiriwa Injili na kuzaliwa katika ufalme wa Mungu kwa kumwamini Yesu Kristo”. 

Nadharia ya pili yenyewe inafundisha kwamba matunda ni “ tabia za uungu (ambazo ni Tunda la Roho) zinazonekana katika maisha ya kiroho ya wale waliomwamini Yesu”.

Nadharia ya tatu inafundisha kwamba, kuzaa matunda ni “kufanya matendo mema kwa wajane yatima na maskini”!

Sasa ukizichunguza nadharia zote utagundua kila moja ina uzito na uhusiano wa kimatunda aliousema Yesu.

Majibu yangu kwa kadiri ya uzito wa kila nadharia, naweza kusema “Matunda” yanayotarajiwa ni jumla ya nadharia zote tatu bila kuteganishwa. Kila mwanafunzi wa Yesu lazima ajulikane kupitia tunda la Roho ambalo linajumuisha mambo yote, yakiwemo matendo mema kwa wahitaji, lakini wakati huo huo na karama za kuwafungua watu kutoka nguvu za giza nazo zinatenda kazi kama alivyoagiza Yesu kwamba “Ishara na miujiza” vitaambatana na hao waaminio.

Kwa majumuisho yangu katika kujibu swali letu la ni matanda ya aina gani tunayotarajiwa kuzaa nahitimisha kwa kusema hivi: “Tabia za uungu ambano ni tunda la Roho zikiambatana na huduma za kijamii na kiuchumi kwa wahitaji na kusababisha watu wengine kuzidi kuzaliwa upya katika ufalme wa Mungu.”!

Je! Tunazaa matunda
kama Yesu alivyoagiza?

Jibu la swali hili linategemea na mtazamo wa kila mtu binafsi, ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa kinadharia. Wako watakaosema wanazaa matunda kwa kulinagana na mtazamo wao kinadharia, na wako wengine watasema hawazai kabisa. Kwa hiyo, majibu yaweza kuwa lukuki yenye kutofautiana. Kutokana na mazingira haya, naomba majibu yangu mimi pia yasitafsiriwe kuwa ndio ukweli wa mwisho. Roho Mtakatifu na amshuhudie kila mtu ndani yake kuhusu ukweli maana yeye ndiye Roho wa kweli aliyetumwa kwetu.

Majibu yangu kwa swali hili ni kwamba nina imani kwamba “tunazaa matunda”. Lakini kwa kiwango cha chini mno. Hatujazaa kama Yesu alivyotuagiza akisema “Akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;…” (Yh.15:5b)  Huu ndio mtazamo wangu na mimi ndivyo ninavyojitathmini mimi mwenyewe. Sioni kama “ninazaa sana matunda” kwa kiwango kile alichoagiza Yesu. Natamani kuzaa sana. Napenda kuzaa sana. Mpaka kulia nalia sana kwa kutaka kuzaa sana. Lakini zisai kama inipasavyo kuzaa.

Na sitaki kutoa visingizio vingi ni kwanini sizai sana, maana bado havitasaidia kama vile malalamiko yasivyosaidia kuondoa tatizo. Lakini naugua sana rohoni mwangu kwamba, Bwana wangu Yesu anisaidie katika udhaifu wangu wa kutofikia viwango vya kuzaa sana kama alivyoagiza. Namlilia anipe fursa nyingine tena ya kuzaa sana. Na fursa ninayoiomba, ni KUDUMU KWA AMANI NA UTULIVU WA TANZANIA WAKATI NA BAADA YA UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU. Kwangu hii itakuwa ni FURSA NYINGINE Mungu kanirehemu ili niweze kuzaa sana. EEH BWANA WANGU NA MUNGU WANGU NIREHEMU KWA MARA NYINGINE TENA!

MWISHO

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.