SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO (6)

Kelvin Kitaso,
GK Contributor.

Mara ya mwisho kwenye sehemu hii ya malezi tulitazama namna ambavyo Mtoto Yesu alienenda. Unaweza (kubofya hapa) ili kusoma.

©Thy Black Man
Wazazi wana kazi ya kufanya mambo ya msingi ili kuhakikisha kazi ya ulezi kwao haiwi ngumu, na si hili tu bali kuhakikisha watoto wao hukua katika maadili mema wakimpendeza Mungu, wanadamu huku wakikua katika hekima na kimo. Mambo hayo yaliyo yamsingi kufanyika katika familia ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika kimo, hekima, huku wakimpendeza Mungu na wanadamu; katika lugha ya kiingereza mambo hayo uitwa 4p’s, ambazo usimama kwa pray together (ombeni pamoja), play together (chezeni pamoja), plan together (pangeni pamoja) na perform together (fanyeni pamoja):

1. Ombeni pamoja (ibada za pamoja)


Familia nyingi zimekosa uimara na malezi bora kwa watoto kwa sababu ya kukosa ibada za pamoja nyumbani. Ukiachilia mbali zile zinazofanyika kanisani, au za mgawanyiko wa kanisa kwa mitaa na kata (ibada za ushemasi na kanda), familia nyingi huridhika na mikusanyiko hiyo na kusahau kuwa inapaswa kufanya ibada za nyumbani kama familia.

Mungu anasema,.“Wakusanyikapo wawili au watatu mimi nipo katikati yao” neno hli linaonyesha kuwa Mungu anatambua kuwa familia uanzia wawili, kisha watatu (kujumuisha na mtoto) na kuendelea, hivyo anatarajia mke na mume wakikutana pamoja ibada izaliwe katikati yao na waanze kumuabudu yeye na yeye atakuwa pamoja nao/katikati yao, na watakapoongezeka pia waendelee kuwa katika ibada kwa kuwa yeye yupo katikati yao. Anaposema wawili au watatu maana yake anaanzia kwenye familia ya watu wawili mpaka watatu, na pia maandiko katika Waebrania 10:25 usema “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”. Maandiko haya uonyesha umuhimu wa kukusanyika pamoja kwa kila iitwapo leo na katika kukusanyika huko ni lazima mafundisho yawepo na kuonyana ili kuimarishana kwa kuwa siku ile ya ujio wake Yesu imekaribia.

Katika eneo hili ni vyema kwa wazazi kufahamu kuwa familia imewekwa ili kutimiza makusudi ya Mungu na kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu katika ulimwengu huu, na Mungu anatarajia wanafamilia kufanya juhudi sana ili kuhakikisha kila mmoja anaurithi uzima wa milele kwa kuwa ndivyo Mungu akusudiavyo.

Familia ambazo zimefaulu kuwa na ibada za pamoja mara zote huwa ni za tofauti sana, na huzifanya kujengeka katika msingi wa Kimungu. Upo umuhimu mkubwa sana wa kuwa na ibada za pamoja kwa kuwa zinawasaidia watoto kuelewa neno la Mungu kutokana na mafundisho mbalimbali wanayofundishwa katika ibada hizo, na pia kila wapatapo nafasi ya kuhudumu huwajengea ujasiri mkubwa hata nje ya familia hata wapewapo nafasi kuhudumu nje ya familia kwao inakuwa si kazi ngumu; ila ugumu huja kwa mtoto ambaye kwao hakuna ibada za nyumbani huwa ni wa kawaida sana na hata akipewa nafasi kuhudumia wengine anaweza kushindwa kufanya hivyo.

Ibada hizi hutoa nafasi kwa watoto kukuza huduma na vipawa ambavyo Mungu ameweka ndani yao, na uwafanya kumjua sana Mungu na kuna mafundisho ambayo hujifunza nyumbani ambayo kwao ni kama muongozo katika kuishi kwao hata wakutanapo na hali ngumu kwao huwa ni rahisi sana kulishinda hilo gumu na hatimaye kupata kusonga mbele.

Kwenye ibada ya nyumbani wazazi katika nafasi ya ukuhani uwaombea watoto wao na kuwauliza maswali mengi na hata kufanya midahalo mbalimbali ya mada mbali mbali, kwa kufanya hivyo itawasaidia watoto kuwa ni wenye akili njema na ufahamu wao katika Mungu utakuwa mkubwa sana.
Kielelezo no.9 Mfano wa familia iliyo pamoja kwa umoja katika kujifunza neno la Mungu ©Christ Savior SA
Nunua vitabu mbalimbali uwafundishe watoto ukiwa nyumbani na usisubiri waalimu wa Sunday school ndo wawe wakikufundishia kila kitu, waelekeze ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwao, hakika hata wao watakuja kuyafanya hayo katika familia zao na yale uwafundishayo yatakuwa ni mambo ya kukumbukwa katika siku zote.
Familia ni kanisa la nyumbani ambalo lipo chini ya mchungaji baba, akisaidiwa na mchungaji mama.
Kwa kuwa familia ni kanisa kamili ni lazima liwe lina ibada kamili liwapo nyumbani, kama kusifu na kuabudu, kuomba, kusoma neno, na mengineyo mengi yahusuyo ibada isipokuwa matoleo ambayo hufanyika katika kanisa la nje ya familia, katika hili ni vyema kwa wazazi kuchukulia maanani kila kilicho cha muhimu kwa watoto wao ila kuwakuza katika namna ya ibada, washirikishe katika kufunga na kuomba, wafanye kujua kuwa Mungu ni kila kitu kwao ili wajue kufanya jambo lolote kwa kutanguliza maombi kwanza, kama ni ratiba za usiku au alfajiri amka nao uombe nao hata kwa muda mfupi. Kumbuka mambo hayo uwafanyiayo hawatakuja kuyaacha hata watakapo kuwa watu wazima na wewe utaitwa heri kwa kuwafundisha hayo.

Kumbuka kuwa samaki mkunje angali mbichi, akikuwa hakunjiki tena, weka msingi wa mambo haya mapema na ukayatende katika uzuri, usichelewe kwa kuwa msingi huwekwa chini na si katika jengo lililokamilika.

Itaendelea wiki ijayo...
___
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com 

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.