SOMO: SIKUJA KULETA AMANI DUNIANI BALI UPANGA - MCHUNGAJI MADUMLABwana Yesu asifiwe…

Imeandikwa; ” Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. “

Hayo ni maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo,Bwana wa utukufu akiwaambia wanafunzi wake. Kupitia maneno hayo ndiposa mtu mmoja akauliza inakuwaje basi Yesu mnaemfuata amekuja kuleta upanga duniani na sio amani?

Nami nikagundua kwamba ipo haja ya kueleza watu ile kweli iliyopo ndani yetu sisi tunaomfuata Yesu Kristo,mwana wa Mungu aliye hai. Maana si wote wenye kujua kile kilichomaanishwa katika andiko hilo.Nianze kwa andiko hilo hilo hapo juu;

Kwanza kabisa yatupasa kufahamu nini kazi ya upanga. Upanga unakazi kubwa ya kukata na kugawanya kile kilichokuwa kimoja viwe viwili yaani viachanishwe kila kimoja. Upanga ugawanya na ndio maana hata neno la Mungu likaelezwa kwamba ni zaidi ya upanga ukatao kuwili. (Waebrania 4:12)

Sasa ifahamike ya kwamba kabla ya ujio wa Yesu ambaye mwenye kuachamanisha kwa kukivunja kiambaza cha kati sisi sote tulikuwa watu wa mungu wa dunia hii,yaani hatukuwa watu wa Mungu aliye hai. Tulikuwa wafu tulioungana na miungu yetu ya dunia hii ( Waefeso 2:1) maana ujue yupo mungu wa dunia hii kama ilivyoandikwa:

” Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” 2 Wakorintho 4:3-4 ( & 1 Yohana 4:4,1 Yoh. 5:19)

mungu huyu wa dunia hii,ana falme yake aliyoihimarisha na ana watu wake wenye kuutumikia ufalme wake ndio hao wachawi,waganga,washirikina,walozi,waabuduo sanamu N.K na wale wote ambao wenye kufanya matakwa yake ya kidunia. Katika ujio wa Yesu duniani,amekuja na nuru kutenganisha kati ya falme ya nuru na giza,amekuja kuugawanya/kuukata ufalme wa mungu wa dunuia hii kama vile upanga ukatao kuwili.

Katika hali hiyo ujue hakuna amani maana dunia ilisimama kinyume naye Yesu Bwana wa mabwana . Amani haiwezekani kupatikana pindi ufalme mmoja wa giza unaboharibiwa maana hapo ndipo wana wa ufalme wa huo husimama kinyume na wana wa Mungu.

Hapo ndipo mtu atamfitini babaye, na binti na mamaye,mkwe na mkwe mtu kwa ajili ya Kristo Yesu (Mathayo 10:35). Kwa lugha hiyo sasa,wale waliokuwa wamoja wakimtumikia mungu shetani wamepangalanyika wengine wamefishwa na kugeuza nia zao kwa kuokoka,na wengine wamebakia pale pale. Sasa watu hawa hawawezi tena kuketi pamoja katika madili yao ya kidunia maana nuru na giza haviendi pamoja.

~ Lakini pia tunapozungumzia habari ya upanga ambao Yesu Kristo anasema kauleta ina maana kubwa nyingine nayo ni hii.

Kufanyika mkristo halisi mwenye kuyafanya mapenzi ya Baba MUNGU ni kutangaza vita dhidi ya dunia~vita vya upanga wa kumwaga damu.

Ikumbukwe kwamba sehemu kubwa ya wanafunzi wa Yesu wa awali waliuwawa kwa upanga kwa ajili ya kumpata Kristo. Ilibidi kuishindania imani hata kumwaga damu kwa upanga

”Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa.

Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. “Matendo 12:1-2 soma pia;( Mathayo 5:12,& Matendo 14:22,Matendo 21:13 ). Hii inatuonesha kwamba kuwa mkristo ni kuwa kinyume cha dunia hii,pale ambapo dunia inapofuata tamaa za anasa za kila namna wewe wa rohoni umekataa kuzifuata na kuwafuata wa dunia. Hapo ni lazima dunia itakuinukia.

Upanga huu wa aina ya pili ni mateso,chuki,adha na udhia kwa wale wote wenye kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wako kisha wakadumu katika kufanya mapenzi yake Mungu katika maisha yao kama tulivyosoma hapo juu.

Wapo wakristo wa leo wenye kujidanganya kwamba ukiokoka basi hakuna mateso yajayo yoyote yale. Watu wa namna hii siku zote wamekuwa ni chakula cha wachawi,wakipigwa na mapepo ya kila aina maana hawafahamu thamani ya kufanyika mkristo duniani,maisha ya wakristo wa namna hii yamejawa na zinaa,anasa za dunia hii hali wao ni wakristo.Mkristo yeyote aliyeokoka katika imani sahihi ni lazima atainukiwa na dunia,mateso ni sehemu yake naye mkristo huyo huleta upanga mahali alipo chini ya jua.

Ni lazima ifahamike kwamba Yesu Yeye ndiye mfalme wa amani. Luka 19:38,hivyo hana haja ya kuleta amani,bali Yeye mwenyewe ni amani tosha maana kila ampokeaye Yesu amepokea amani ipitayo amani zote. Ujio wa Yesu ni amani tosha kwa kila mtu amwaminie. Mfano mdogo tu ni huu,ikiwa Tanzania tunaomba amani basi hatuna budi kumpokea Yeye ambaye ni amani yetu,ambaye ndiye Yesu Kristo.

Kwa huduma ya maombi nipigie 0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya Bible fellowship church. (Kimara,Dar~Tz)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.