SOMO: TARAJIO LISIPOFIKIWA MOYO HUUGUA

Faraja Mndeme,
GK Contributor.


Tarajio ni tumaini alilo nalo mtu kuelekea jambo fulani kutokea, kulingana na aina ya mipango aliyo nayo. Tarajio lolote ambalo halina mipango mara nyingi ni ngumu kutokea maana huwezi kuvuna pasipo kupanda. Tarajio ni mwanzo tu wa jambo, lakini hatua na mipango mbali mbali ya kulifanya tarajio husika litimie ni jambo lingine. Kila mwanadamu anayeishi katika hii sayari ana aina fulani ya tarajio ambalo hutegemea kwamba kuna wakati litatokea na litatimilika.

Mambo Machache ya kuzingatia unapokuwa na tarajio aina yoyote ile.

(I) MIPANGO.

Tarajio lolote lisilokuwa na mipango huyeyuka mithili ya upepo wa kusulisuli. Mipango ni ramani ya tarajio ulilonalo kwa wakati husika. Ili kufikia kiwango cha juu cha tarajio ulilo nalo ni muhimu kuwa na mipango madhubuti juu ya kile unachokiamini kwamba kitatokea. Huwezi kutegemea kuvuna tani nyingi za mazao shambani bila ya kujua aina ya mbegu, ukubwa wa shamba, na zana utakazotumia. Ni muhimu kuwa na mipango madhubuti sana kuhakikisha unafikia tarajio lako. Mipango ya kufikia tarajio lako iwe ya kweli na halisi isiwe mipango ambayo ni ya kufikirika tu ambayo kwa namna moja ama nyingine ukianza kutaka kuitekeleza inakuwa ngumu maana haikuwa kwenye uhalisi wake.

(II) MUDA.

Tarajio lolote ambalo halina muda wa ukomo wake ni tarajio la kufikirika tu. Unapofikiria kitu fulani kutokea kwenye maisha yako halafu hauna muda maalumu uliojiwekea unaweza kujikuta kila siku hakuna jambo ambalo linatekelezeka kwenye maisha yako. Ni muhimu kuwa na muda wa ukomo ili maisha yaendelee. Fikiria Unakuwa na tarajio ambalo halina mwisho kitu ambacho ni hatari hata kwa afya yako maana utaanza kuzalisha misongo ya mawazo na magonjwa mengine ambayo hayana ulazima wa kuyapata. Ni muhimu kuwa na ukomo wa tarajio lako. Unapoona halikuwezekana au limewezekana ni muda wa kuondoka hatua moja na kwenda nyingine ili kujipa nafasi ya kufanya mambo kadha wa kadha kwenye maisha yetu. Muda wa kuishi tulio nao ni mchache na unahitajika kutumika kwenye mambo mengine ambayo yanatuzunguka. Ni muhimu kujiwekea ukomo wa kila unachokitarajia.

(III) IMANI.

Tarajio lako kwenye jambo lolote haliwezi kuzidi kiwango cha imani ulicho nacho moyoni mwako. Kiwango cha kufanikiwa tarajio lako kinategemea kiwango cha imani na juhudi ulizoziweka ili kuweza kufikia kiwango cha tarajio ulilo nalo. Imani bila juhudi ya kukifanya kile unachokiamini kitatokea ni bure. Ni muhimu kuweka imani katika kile unachokifanya lakini pia juhudi za ziada lazima ziwepo kuhakikisha kile unachokitarajia kinatokea. Imani inakuwa ni chachu ya kukufanya utende kwa bidii zaidi huku ukifuata kanuni nyingine muhimu za kulifikia tarajio lako ambalo uko nalo moyoni mwako. Kiwango cha Imani ulicho nacho kinaamua mambo mengi sana kwenye tarajio ulilo nalo. Usiwe na tarajio ambalo hauamini kwamba linaweza kutokea maana itakuwa ni kazi bure. Jenga imani kwenye kile unachotarajia huku ukiongeza juhudi za makusudi kufikia lengo.

(IV) KIWANGO CHA UFAHAMU.

Hauweizi kufanikiwa kufikia kiwango cha juu cha tarajio lako zaidi ya kiwango cha ufahamu ulicho nacho. Ufahamu ulio nao hujenga imani ambayo hupelekea wewe kuwa na mipango sahihi na husaidia kutumia muda wako vyema. Ufahamu sahihi huwa ni injini ya kile unachokitarajia. Siwezi kutarajia kuwa rubani wa ndege bila kuwa na ufahamu sahihi wa namna ya kufikia hatua za kuwa rubani mahiri wa ndege. Ufahamu sahihi ni jambo muhimu sana. Hakikisha unaongeza ufahmu kwenye jambo husika ili kile unachokitarajia kiwe dhahiri kwenye maisha yako ya kila siku. Hauwezi kutarajia kuwa tajiri huku haufahamu kununi muhimu na hatua za kufikia huk. Jenga ufahamu usio na kikomo na usio na mipaka hadi utakapofikia kuona kile ulichokitarajia kinatokea.


Mwisho, tukiwa tumebakiza miezi michache kuweza kufikia mwisho wa mwaka je ni matarjio gani ulikuwa nayo tangu tulipouanza mwaka huu yametimilika? Iwapo hayajatimilika kwanini hayajatimilika? Wapi Umekosea? Hakikisha unajipa muda wa kijitathmini kwa haraka sana kwa kipindi cha muda uliobaki ili kuepuka kuwa msindikizaji na kuwangalia wengine wanapofikia matarajio yao. Ni muhimu kujiuliza na kujihoji kwa kina na undani n a utulivu kujua wapi ulikosea na kipi kifanyike ili tutakapofikia mwisho wa mwaka huu tufurahi na kushangilia pamoja.Tarajio lisipofikiwa moyo huugua na kusononeka. Kwanini moyo uugue na kusononeka wakati bado tumaini lipo? Fanya hima, hakuna jambo gumu lisilowezekana hapa ulimwenguni.


Email : naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless You All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.