ZAWADI YA GARI LA KIFAHARI KWA MCHUNGAJI WAKE LAMTIA MATATANI MWIMBAJI NYOTA AFRIKA YA KUSINI

Gari la kifahari jipya kabisa lililonunuliwa na mwimbaji huyo kama zawadi kwa mchungaji wake
Mwimbaji nyota Afrika ya kusini aitwaye Sifso Ncwane aliyetamba na wimbo wa 'Kulungile Baba' alijikuta katika wakati mgumu wiki iliyoisha baada ya watu kumshambulia kwa maneno kutokana na kuweka picha ya gari la kifahari alilolitoa kama zawadi kwa mchungaji wake ikiwa shukrani yake ya pekee kwa matendo makuu ambayo Mungu amemtendea yeye na familia yake.

Mwimbaji huyo ambaye alitoa album mpya mapema mwaka huu ikifahamika kwa jina la 'Bayede Baba' amenunua gari la kifahari aina ya Mercedes Benz GL 63 AMG V8 2015 ambalo ni toleo jipya kwa mwaka huu lenye thamani ya Randi milioni 1.9 za Afrika ya kusini na kulitoa zawadi kwa mchungaji wake aitwaye Fransis Anosike anayehudumia huduma ya 'Rock of Victory Ministries'. Kitendo cha kutoa zawadi hiyo kisha kuweka picha za kile alichokifanya kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kulifanya wengi waanze kumponda wakisema Biblia inakataza kutoa ili watu wajue kuwa umetoa bali alitakiwa atoe pasipo kutangaza ili thawabu yake iwe kuu mbinguni.

Sifso akizungumza jambo huku mkewe akiwa ameshika ufunguo wa gari juu, mezani tuzo mbalimbali za mwimbaji huyo


Aidha kwa upande wa mashabiki wengine na wafuatiliaji wake waliandika mwimbaji huyo alitakiwa kufanyia jambo lengine la maana pesa yake kuliko alichokifanya, kwakuwa aliyemtendea ni Mungu na sio huyo mchungaji wake, kitendo chake ni kujionyesha, kwakuwa anasema alikuwa maskini kwanini basi hakutumia pesa zake kuwakumbuka maskini, kwakuwa mchungaji ni mtumishi wa Mungu haitaji kuzawadiwa bali Mungu mwenyewe atamzawadia na kumalizia kwa kumtusi mwimbaji huyo ambaye alionyesha unyenyekevu wakutolumbana na watu hao.

Kwa mujibu wa Ncwane ambaye aliambatana na mkewe aitwaye Ayanda pamoja na watoto wao
katika kukabidhi zawadi hiyo, amesema, Mungu amemtendea makuu likiwepo suala la kuponywa ugonjwa wa moyo uliotaka kumuangamiza, lakini pia kwakumbariki kwa mvua ya tuzo mbalimbali kupitia huduma yake pamoja na Mungu kuilinda familia yake dhidi ya maadui kimwili na kiroho na zaidi kumwamini na kumpa kipawa cha kuhubiri neno kupitia huduma yake.

Kitendo cha kushambuliwa mwimbaji huyo kilifanya waimbaji wengine akiwemo mwanadada Tebello Sukwene mwimbaji wa zamani wa Joyous kuandika suala hilo kwenye ukurasa wake wa Facebook kutaka kusikia kwa mashabiki kwanini watu wanapata shida na tukio alilolifanya mwimbaji mwenzao kwa mchungaji wake.

Mchungaji Anosike akimuombea Sifso na familia yake baada ya kupewa gari hilo©RVM

     Tazama 'Kulungile Baba' live kutoka kwa Sifso Ncwane wimbo uliompa umaarufu

 
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.