EE MUNGU BABA YETU, MAPENZI YAKO YATIMIZWE - ASKOFU SYLVESTER GAMANYWA

Askofu Sylvester Gamanywa
Leo nimeona niwasilishe ujumbe maalum unaoendana na siku ya leo. Natambua kwamba baada ya uchaguzi wa leo Tanzania haitakuwa kama ilivyokuwa kabla. Mimi kama mmoja wa wadau wa kuitakia amani nchi yetu, nimetafakari sana kuhusu changamoto zinanzotukabili kitaifa kuanzia leo mpaka matokeo yatakapotoka. Wakati tumekuwa tukiombea uchaguzi napenda nikushirikishe msimamo wangu ambao nimekuwa nao na kigezo cha msimamo huo:

Kigezo cha msimamo wangu kuhusu
 uchaguzi mkuu na matokeo yake.

Mimi kama kiongozi wa kiroho ambaye natambua kuna kundi la wafuasi wanaofuata nyayo zangu, hata kama sijawatuma wanifuate, ninajitahidi kwa kadiri niwezavyo kutokufanya maamuzi ambayo hata kama ni mapenzi yangu binafsi lakini yanaweza kutafsiriwa kinyume kuwa ni maagizo kwa wafuasi wangu, nao wakaamua kuniiga wakisema wanafuata nyayo za kiongozi wao.

Mojawapo ya maeneo yenye utata wa kutenganishwa ni hii la uchaguzi mkuu uliofanyika hivi leo. Nasema hili ni eneo tata kwa sababu kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu; viongozi wa kidini, hususan viongozi wa kikanisa tumegawanyika vibaya sana kinadharia na kimtazamo kuhusu “nafasi na wajibu wa kiongozi wa kikanisa” katika mambo ya kijamii hususani haya ya kisiasa.

Katika mazingira kama haya, mimi ninazo kanuni zangu zinazonisaidia kupambanua nitumie vigezo gani katika kufanya maamuzi makini. Mojawapo ya vigezo vyangu vya kuniokoa kila nifikapo “njia panda” huwa najiuliza swali hili la msingi kama ifuatavyo:

“Hiviiii….Kama Yesu angelikuwepo Tanzania katika mwili hivi leo angelifanya nini wakati na baada ya uchaguzi kumalizika?

Baada ya kujihoji kwa swali hili, hulazimika kuingia katika sala ya kuwasiliana na Bwana Yesu mwenyewe, huku nikiyatafakari maisha yake yote jinsi alivyohusika katika mambo ya kijamii enzi zake katika mwili hapa duniani. Katika kumtafakari Yesu mara hujikuta nikipokea majibu kama haya yafuatayo:

1.     Yesu angalikuwepo katika mwili hapa Tanzania, katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi “Ageliwaombea wagombea wote waliojitokeza kwenye nafasi za udiwani, ubunge na Urasi kwamba wote wafanye kampeni zao kwa kuzingatia sheria na maadili ya uchaguzi na watoe ahadi za kweli kwa wapiga kura watakaowachagua”

2.     Yesu angalikuwepo katika mwili hapa Tanzania “Angeliwaombea washabiki wa makundi ya itikadi za vyama vilivyomo kwenye ushindani wasiendeshe kampeni kwa misingi ya sharia na haki na kuheshimu haki za wengne kama ambavyo kila upande unadai haki zake kuheshimiwa”

3.     Yesu angalikuwepo katika mwili hapa Tanzania “Angelimwombea Rais na serikali yake inayoondoka madarakani amalize muda wake kwa amani na utulivu na kukabidhi madaraka kwa Rais atakayekuwa ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi”

Haya basi, kwa kuwa hivi ndivyo nilivyomtafsiri Yesu kuwa ndivyo angelifanya, basi mimi nami kwa kufuata dhamiri yangu mwenywe nimejitahidi kufanya kama hayo hayo ambayo naamini Yesu mwenyewe angelifanya kama angelikuwapo katika mwili katika mazingira yetu.

Kwa kufuata dhamiri yangu, sio kwamba natafuta kumfurahisha mtu au upande Fulani wa itikadi ya kisiasa au kidini, bali najiandaa kwa ajili ya siku ya kiyama, siku ile ambayo nitasimama mbele za Yesu Kristo uso kwa uso ili kutoa hesabu ya maneno na matendo yangu niliyofanya nikiwa hai duniani.

Huu ni msimamo wangu ambao hapenda kuusimamia kwa mambo ya kijamii ambayo, hayana miongozo ya waziwazi ya kimaandiko, na kwamba tumeachiwa sisi wenyewe kutafuta uongozi wa Roho Mtakatifu katika maamuzi.

Kwa imani yangu kama kuna kundi limeamua kuiga msimamo huu, nina hakika sitahukumiwa na Bwana wangu Yesu Kristo kwamba nilipotosha kondoo wake alionipa kuwachunga. Na kama nitakuwa nimewapotosha basi nitakuwa mimi ndiye niliyetangulia kupotoka kwa vile nilichofanya nilikuwa naamini nafuata nyayo za Yesu Kristo mwenyewe kama naye angelikuwepo hapa Tanzania.

Tukubali kupokea matokeo
yawe mazuri au mabaya

Hapa ninapenda tena kusema na wale ambao bado wanaamini ni wachaji Mungu, na hasa kundi la waombaji waliofunga na kuombea kampeni za uchaguzi.

Nasema na kundi hili kwa sababu tunajua kanuni za kupokea majibu ya maombi yetu kama kweli tulipokuwa tunaomba tulikuwa na tunamaanisha kwamba ni Mungu atakayeongoza na kudhibiti mchakato mzima wa uchaguzi mpaka matokeo yake. Ndiyo maana nasema kwamba, tujiandae kupokea majibu ya maombi yetu hata kama majibu hayo hayatakuja sawasawa na mapenzi yetu.

Napenda kusisitiza haya kwa sababu ninajua kwamba, kuna waombaji wengine wanaweza kukwazika kwa majibu yatakayotokea kinyume cha matarajio yao. Tena wengine wanaweza hata kuchanganyikiwa wakipinga kwamba matokeo hayo si majibu kutoka kwa Mungu. Wanasahau kwamba, kama matokeo yatakayotokea yangekuwa hayana kibali cha Mungu, Mungu anao uwezo wa kuyazuia kabisaaaaaa yasitokeeeee kama yatakavyokuwa yametoka.

Naomba nirejee tena kusema kwamba maneno haya nisemayo si kwa ajili ya jamii ya wasioamini hata kidogo. Walengwa wangu ni jamii ya waaminio, waombaji wa dhati, wachaji Mungu kweli kweli, hao ndio ninaosema nao. Na ninasema kwamba ninasema na kundi hili kama bado watakuwa wamesalia na kusalimika baada ya “kupepepetwa kupitia mchakato wa kampeni za uchaguzi zilizomalizika jana”.

Baada ya kuweka bayana mwongozo huu, sasa naomba turejee maneno ya Bwana Yesu aliyosema kwenye dua ya usiku wa kukamatwa kwake kule Gethsemane.

“…Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” (Luk.22:42)

Haya yalikuwa ni maombi ya Yesu Kristo ambaye kimsingi tunajua kwamba, tangu mwanzo alikuwa anajua amekua duniani kwa ajili ya “kukinywea kikombe cha mateso” kwa ajili yetu. Lakini kwa kuwa alikuwa ameuvaa mwili ambao ni dhaifu ndiyo maana alilazimika kuwasilisha dua kama hii. Lakini akiwa bado yuko kwenye mtazamo wa kibinadamu akiwakilisha ubinadamu wetu alikiri na kukiri kukubali kupokea majibu ya Baba yake ambayo ni “matokeo ya dua zake”.

Mazingira haya ndiyo yanayolikabili kundi la wachaji Mungu ambao kwa vipindi mbali mbali tumeombea uchaguzi tena kwa mitazamo na misimamo tofauti. Hata kwenye kupiga kura kila aliyepiga kura kamchagua yule ambaye anaamini ndiye chaguo la Mungu.

Sasa, kinyanganyiro ni kwenye kupokea matokeo. Kila mwombaji angependa majibu yaje kulingana na jinsi alivyochagua yeye kwenye sanduku la kura. Lakini yakiwa kinyume, asikimbilie kutafsiri kwamba matokeo hayo si mapenzi ya Mungu ati kwa kuwa tu majibu hayakumtoa yule aliyempigia kura. Tusisahau kwamba suala la kupiga kura limegubikwa na ubinadamu mwingi sana, nap engine mpaka ushetani pia.

Lakini Mungu mweyewe yuko juu sana na uwezo wake hauko chini ya udhibiti wa mtu yeyote. TUKUBALI KWAMBA MATOKEO YATAKAYOTANGAZWA NDIYO MAPENZI YA MUNGU KWETU. Asiyeamini haya ni sehemu ya jamii ya wasioamini Mungu wa kweli, na kwake hiyo ndiyo imani yake.

Mungu ibariki Tanzania.


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.