SOMO: AMRI YA KWANZA YENYE AHADI - MCHUNGAJI MADUMLA

Binti akiwa katika hali ya heshima kwa mkubwa wake ©africancelebs

Na Mchungaji Gasper Madumla

Bwana Yesu asifiwe…

Amri za Bwana ziko nyingi lakini ipo amri moja iliyokuwa ya kwanza iliyobeba ahadi ya BWANA juu yetu ikiwa tutaishika. Amri hii sio amri kuu,wala sio mojawapo ya mri kuu alizozisema BWANA (Marko 12:28-31).Bali amri hii ni;

“Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia. ” Waefeso 6:2-3

Biblia imeweza kuweka amri hii wazi kabisa kwa kila mtu,kwamba ni amri pekee ya kwanza yenye ahadi kwa maana yeyote atakaye waheshimu wazazi wake mtu huyo amebarikiwa,na si hivyo tu bali amepewa maisha marefu katika dunia hii.

Kumbuka ya kwamba mbaraka una kanuni yake,katika eneo hili~mbaraka umeachiliwa kwa kila atakaye muheshimu baba na mama yake. Na aliyebarikiwa amebarikiwa. Ndio maana wapo watu wengine wamebarikiwa kwa kupewa maisha marefu hata kama bado hawajaokoka kwa sababu ya kuwaheshimu wazazi wao tu.

Kumbe basi tumepewa majibu ya kubarikiwa kwa kupokea maisha ya siku nyingi katika dunia ni kumuheshimu baba na mama zetu waliotuzaa.

Ukweli ni kwamba,baba na mama yako waliteseka na waliangaika sana kwa ajili yako katika malezi yako. Hawakukutupa bali walikutunza na kukupa malezi yote ya ukuaji tazama pale ulipoumwa usiku,wao walikubeba na kukupeleka hospitali ili wewe upone. Walipoona shida fulani walikusaidia kwa hali na mali,wakakukinga na uadui wote,N.K

Ingawa wazazi wako hawajaokoka,lakini usiache kuwaheshimu na kuwapenda kwa jinsi ile ile walivyo.

Kumbuka hata kama wazazi wako wakoje. Yamkini baba na mama yako wanaweza kuwa ni watu waliofarakana na MUNGU,yaani ni watu wasiotaka kumpokea BWANA YESU. Au ya kwamba yawezekana wakawa ni watu duni machoni pa watu,kwamba ni maskini wa kutupa!hawajasoma kama wewe ulivyosoma lakini nakuambia wazazi hawa watabaki kuwa ni wazazi wako tu. Maana pasipo wao wewe husingelikuwepo.


Wapo watu ambao hawawaheshimu wazazi wao,kisha wakajikuta wakilaaniwa. Labda anza kujiangalia wewe mwenyewe,waweza kujua kuwa mikosi mingine imetokana na kushindwa kuwaheshimu wazazi wako. Hata mateso mengine uyapatayo hivi leo yametokana na kushindwa kuwaheshimu wazazi wako. Yawezekana wala hujalogwa,bali umejiloga mwenyewe kwa kuwadharau wazazi wako.

Kumbuka hili,mzazi ni mzazi tu hata kama yukoje. Shida kubwa iliyopo leo kwa baadhi ya wana wa MUNGU ni kushindwa kuwaheshimu wazazi wao kwa kigezo kwamba hawajaokoka. Mimi nalimkuta binti mmoja wa kilokole anasema hawezi kushauriwa na mtu yoyote wa mataifa hata kama ni mama yake au baba yake mzazi.

Tena basi ilikuwa wazazi wake hawaokoka kipindi hicho. Mimi nikamshangaa binti huyo,asiyetaka ushauri kwa mama yake eti kwa sababu mama yake hajaokoka!!! Nikajiuliza mbona hapo zamani alishauriwa sana na kuongozwa na wazazi hao hao,iweje leo? Kulikoni?

Leo utakuta mtu anajitoa kwa mali nyingi kwa wachungaji, na kushindwa kutoa hata tshs 3,000.00 kwa baba yake au mama yake mzazi. Mtu anapeleka mchele kilo 5,unga kilo kadhaa,nguo nzuri,pamoja na pesa ya vocha na pesa za mafuta ya gari hapo hapo baba na mama yake hawajapelekewa chochote kile. Yaani wazazi wake wamepauka,nguo zao zimechakaa utafikiri hawakuzaa mtoto,kumbe mtoto yupo lakini akili zake ni kupeleka kila kitu kwa wachungaji na watumishi kanisani tu.

Kumbuka,sio vibaya kupeleka mapochopocho kwa watumishi wa MUNGU maana ipo mbaraka mkubwa sana kwa kila ampokeaye mtumishi wa MUNGU,maana hata ukiniletea mimi,mimi nitakuombea na kufurahi;Lakini je umefanya hivyo hivyo kwa wazazi wako? Ubaya unakuja pale unapopeleka mafedha yoote kisha ukawasahau wazazi wako waliokuzaa kwa damu na nyama.

Kuwaheshimu wazazi (baba na mama yako) ni pamoja na kuwapa mahitaji ya fedha na mahitaji mengine kama vile chakula,mafazi N.K

Ile namna ya kumwambia baba shikamoo peke yake haitoshi!!! Shikamoo pasipo pesa ya chakula haina maana kabisa!!!

Wapo watoto wenye shikamoo nyingi za kavu kavu kwa wazazi wao pasipo kuwapa chakula chochote, namna hii sio heshima.

Siri iliyopo ya kuongezewa siku za kuishi duniani ni kuwaheshimu wazazi wetu.

Tukihitaji kuwa na maisha marefu basi tuwadhamini wazazi wetu. Ni jambo la ki-MUNGU kuwaheshimu wazazi wetu waliotuzaa. Inawezekana ikawa wazazi wako walifaliki miaka mingi iliyopita kipindi ulipokuwa mdogo,lakini hata hapo bado una nafasi ya kuwaheshimu wazazi wengine. Na kwako wewe ikiwa umebahatika kuwa na wazazi walio hai hata sasa,basi waheshimu sasa maana wapo wengine wenye kutamani kuwa nao lakini hawakuweza.

~Kwa huduma ya maombi na maombezi nipigie,+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.