SOMO: NAMNA YA KUFIKISHA HABARI NJEMA ZA YESU KWA WATU WENGI MAHALI ULIPO

Mfano katika picha watoto wakifundishwa neno la Mungu ©imgarcade
UKITAKA KUFIKISHA HABARI NJEMA ZA YESU KWA WATU WENGI MAHALI ULIPO,TUMIA WATOTO

Na Mchungaji Gasper Madumla

Bwana Yesu asifiwe…

Leo ninakupa siri ya ajabu ambayo itakusaidia hakika kama utaitumia katika huduma yako mahali ulipo. Watu wengi tunapenda kufikisha habari njema za ufalme wa Mungu kwa watu wote,lakini wengi wetu tunafeli kuwafikia watu wengi kwa haraka,kwa sababu tumekosa maharifa ya kugundua siri hii ambayo ninakuambia leo.

Watoto ni kundi la watu wenye kusikia haraka na kushika kile walichofundishwa na kuwa tayari kukisema huko nje sawa sawa na walivyofundishwa pasipo kumuogopa mtu.

Yamkini wewe waweza kuogopa kumkabili mtu usiyemjua,au hata yule unayemjua lakini ukashindwa kumuendea na kumuhubiria injili,lakini watoto wamepewa ujasiri huo wa kusema na watu wote pasipo kuangalia imani zao,kwamba ni wakristo au watu wa imani nyingine sawa sawa na vile ulivyowafundisha.

Mfano; chukulia majirani zako wanaokuzunguka nyumbani kwako hawajaokoka na wala hawana mpango wa kuokoka maana wamefungwa na nguvu za giza lakini sasa wamebarikiwa kuwa na watoto wao.

Kwamba majirani zako,ukiwaambia waje kwako waombewe au wafundishwe kweli ya neno la Mungu ili waokoke,wanakataa~hivyo itakuwa ni vigumu kwako kuwafikia watu hawa maana wamekataa kuja. Lakini ikiwa utawakusanya watoto wako na watoto wao kisha ukawaambia habari za Yesu,na miujiza yake jinsi anavyoponya,anavyookoa na wakashuhudia ukiombe familia yako;basi uwe na uhakika ujumbe huo utawafikikia wazazi wao na watakuja kupitia watoto wao.

Maana watoto wao watasema “baba,baba jana tulifundishwa jinsi ya kumpenda MUNGU,… alafu mwalimu akatuombea,alafu,alafu nini vile… ehee! nimekumbuka mwalimu akamuombea John akapona,kichwa kikampona….”

Kwa maneno kama hayo,yanamfanya mzazi kufikiri mara mbili mbili,na ujue ikitokea shida kwake basi ni lazima atakutafuta tu sababu amehubiriwa na mtoto wake kwa kile ulichomfundisha. Umeona! Yaani badala ya wewe kuenda kwa kila mtu,watoto wanaenda wao na kuisema kweli.

Ikumbukwe kwamba;chochote utakachomfundisha mtoto ndicho atakacho kisema nje hasa kwa wazazi wao.

Kwa siri hii,hauitaji kujitangaza kwa kupaza sauti na kusema mimi ni mchungaji jamaniii,bali unachohitaji anza na kundi la watoto mahali ulipo kwa kuwafundisha neno la MUNGU na maombezi kisha utashangaa wazazi wao watapata habari ya kwamba wewe ni mchungaji na yupo Yesu Kristo nyumbani mwako.

Kumbuka ya kwamba sisemi tusiwafuate watu majumbani kwa kuwahubiria injili,lah!au sisemi tusisimame mitaani kwa kuhubiri injili lah hasha! Injili ni lazima tukaihubiri kwa njia zote iwe ni mtaa kwa mtaa,masokoni,barabarani,vituoni barabarani,majukwaani N.K Ila kile nikisemacho hapa,ni kuipeleka injili na kumtangaza Yesu kwa watu wengi hapo mtaani kwako haswa kwa wale wabishi wasiotaka kuokoka,ukitumia lasilimali watoto.

Hii ni njia iliyopimwa ikapimika,walioitumia wamefaidika kumtangaza BWANA Yesu kwa kasi sana.

Tazama mfano mdogo mwingine,mimi ninakijana wangu mdogo ambaye kwa huyo wengi wananifahamu,utakuta ninajipitia zangu tu,alafu mtu anasema “baba Isaac,BWANA YESU asifiwe,” Au “ baba Isaac,za asubuhi…” Sasa najiuliza hivi “mbona huyu mtu mimi simjui? Yeye amenijuaje lakini?” Kumbe amenijua kupitia mwanangu.

Sasa fikiria, ikiwa kama ninatumia muda kumfundisha mwanangu na watoto wenzake habari za Yesu,ujue vile vile nao watapeleka ujumbe walioupata kwa watu wengine ambao hata mimi siwajui.

Yesu Kristo,naye alizungumzia jambo hili la watoto kwamba waende kwake; Imeandikwa; “Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. ” Mathayo 19:14

Leo BWANA anatuambia sisi wazazi tuwapeleke watoto wetu kwa Yesu,lakini cha ajabu wapo wazazi wenye kuwafungia watoto wao ndani wasiende kanisani,au wasiende kujifunza neno la MUNGU. Muachilie mwanao akapate maharifa ya ki-MUNGU kanisani.

Watoto hushika sana kile wanachofundiswa tofauti sana na sisi watu wazima.

~ Na ukitaka kujaribu hili,fanya hivi~ Waulize wazazi mmoja mmoja wanaotoka ibadani kwamba wamefundishwa nini,na ni maandiko yapi walioyasoma hata kama wayataje machache tu? Kisha waulize pia watoto kile walichofundishwa sunday school, alafu ndio ujionee mwenyewe!!! Kwamba ni kundi lipi litakalokujibu vizuri,watoto au watu wazima?

Tena watu wazima hufundishwa sana lakini hawayatendi hata! Bali watoto ukiwafundisha kitu,ujue watakitenda tu. Mfano mtu mzima waweza kumwambia “usitukane,ni dhambi” kisha ukamuacha kwa muda,gafla ukamfuatilia sana,utakuta akitukana kama vile mwanzo tu,maana mtu hujidanganya kwamba si atatubu tu!!!

Lakini mtoto ukimwambia maneno hayo hayo “usitukane,ni dhambi” basi ujue ataogopa kutenda dhambi,na endapo hata akimuona mwenzake ametukana ambaye hakufundishwa basi atamwambia“usitukane,ni dhambi,” kwamba naye anafanyika kama daraja la kupeleka injili ile aliyoisikia kwa mwingine.

Mtu yeyote akifanikiwa kuwafundisha watoto habari za ufalme wa mbinguni,basi ujue mtu huyo amefanikiwa kuzungumza na wengi kwa wakati mdogo. Tena amekuwa akiitanza huduma yake ya Mungu.

Jaribu njia hii,kisha utaniambia ya kwamba vile utakavyofanikiwa katika utumishi wako. Sikia,yawezekana ulipo wewe hata hawakujui kwamba wewe ni mtumishi wa MUNGU,kwa sababu unaaingia nyumbani na unatoka pasipo kufanya chochote kile hapo mtaani kwako.

Sasa jaribu kuwaalika watoto wa majirani zako ,kisha wape ukarimu wote ~tumia muda mfupi wa kuwafundisha,kuimba na kuwaombea uone kama utumishi wako haujajulikana na hapo wengi watakuja kwa Yesu,nawe utakuwa kama chombo cha kuwavuta watu waje kwa BWANA YESU.

Lakini yawezekana ukawa hujafanikiwa bado kuwa na watoto nyumbani kwako,~ hata hapo,tumia kuwaalika watoto kwa kutengeneza ka program hivi,mfano wawekee tv za katuni,kisha mnaanza kuimba nyimbo za BWANA then unawafundisha vizuri tu,na hatimaye utakuwa umeikuza huduma yako mtaani ulipo kwa kumtangaza BWANA YESU kwa watu wote.

Anza sasa,kuitumia siri hii ya kuwahubiria watoto wako na wa majirani zako habari za Yesu. Bado hujachelewa.

Kwa huduma ya maombi na maombezi,piga +255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.