SOMO: NITAWEZAJE KUKUA KIROHO ? - MCHUNGAJI MADUMLANa Mchungaji Gasper Madumla

Bwana Yesu asifiwe…

Mpendwa,ifike wakati ujiulize swali hilo maana isiwe unaingia kanisani na kutoka tu,pasipo kuangalia ukuuaji wako wa kiroho. Je ni kweli umeongezeka kiroho? Au umepungua ? Au umebakia vile vile tangu uwe mkristo?

Ni lazima kujikagua afya za roho zetu,kuangalia maendeleo. Nakumbuka nalipokuwa shule tulikuwa tukichora graph zenye kuonesha ukuaji na kushuka kwa takwimu,ndivyo ambavyo nikijiangalia kiroho nikaona kumbe nahitaji pia michoro hii ya graph kuona nipoje kwamba ninashuka kiroho au ninapanda kiroho.

Lakini swali la msingi ni kwamba “nitawezaje kukua kiroho“. Kati ya maswali muhimu kwa mwamini basi ndio hili “nitawezaje kukua kiroho?”. Yeyote mwenye kujiuliza hivi,ni yule asiyelidhika na kiwango chake cha kiroho alichonacho na ni yule mwenye kiu na shauku ya kuhitaji kujua zaidi kwamba afanye nini haswa ili kiwango chake cha kiroho kiwe kikubwa,kikue.

Ikiwa hujiulizi swali hili,basi yawezekana kabisa hujajicheki ulivyo,na kwa sababu ujitizami tena ujitambui ~Lakini ikiwa utajitizama kiroho ni lazima utahitaji ukue zaidi maana hukuaji wetu wa kiroho ni tendo endelevu,hakuna yeyote aliyekuwa akatosheka.

Kama vile mtoto mchanga apitiavyo hatua kadha za ukuaji wake,nasi pia watoto wa kiroho tumepewa hatua za ukuaji. Ni vigumu mtoto mchanga azaliwe kisha kabla ya hatua ya kutambaa, akatembea papo hapo,bali mtoto anahitaji apitie hatua moja hadi nyingine ndipo akue.

Zipo hatua tofauti tofauti za ukuaji wa kiroho,lakini hizi ninazokuandikia leo ni miongoni mwa hatua kadha wa kadha.

01.KUZALIWA KWA MARA YA PILI.

~Ukweli ni kwamba, kuzaliwa kwa mara ya pili(kuokoka)ni hatua ya kwanza na ya awali kabisa isiyopingika. Sababu Tazama kwa mfano ule ule wa mtoto,ili mtoto akue,afanikiwe N.K hana budi kwanza azaliwe. Maana hatua ya kwanza kabisa ya ukuaji wa mtoto hutegemea uwepo wake.

Laiti kama mtoto hajazaliwa basi hatuwezi kufikiria ukuaji ( sizungumzii ukuaji wa mtoto akiwa tumboni,bali ukuaji baada ya kuzaliwa)Kumbuka hili,yeyote aliyezaliwa hutegemewa kukua.

Mpendwa,kuzaliwa mara ya pili ni kumpokea Bwana Yesu awe BWANA na mwokozi wa maisha yako,(Warumi 10:10), ( Yoh.3:3 ).Tendo hili ni hai,na halisi ndani ya mwamini. Ikiwa unahitaji kukua kiroho basi huna budi kuzaliwa mara ya pili kama hatua ya msingi na ya awali,maana ukiokoka umekuwa sasa kiumbe kipya yakale yamepita ( 2 Korintho 5:17 ).

Kumbuka tena,ikiwa utakuwa kiumbe kipya,maana yake wewe si tena mali ya shetani,na kwa hapo sasa BWANA anakuhesabia haki kwa imani,na ndipo roho yako inaanza kuvikwa nguvu ya ukuaji.

(A) Hakikisha unadumu katika fundisho.

“ Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. ” Matendo 2:42

~Mara tu baada ya kuamini,wapaswa kudumu katika fundisho. Kudumu katika fundisho maana yake,ni kukuulia wokovu wako kwa neno na maombi sawa sawa na maelekezo ya baba au mama wa kiroho.

Tunaona waamini wa kwanza kabisa,walipoamini tu,wakabatizwa kisha wakadumu katika fundisho la mitume ambapo ndipo sasa wakakua na BWANA akalizidisha kanisa.

Kupitia mafundisho sahihi ya Bwana Yesu kuhusu wokovu wako ulioupokea yatakufanya ukue kiroho,maana kwa hayo yatakupa nuru, na kuanza kutambua upendo wa MUNGU ndani ya maisha yako.

Kumbuka tena, ikiwa umeokoka pasipo kudumu katika fundisho unakuwa kama mtoto aliyezaliwa kisha hakui. Picha ya kawaida ya mtoto aliyedumaa katika utoto wake ni uvaaji wa nepi kwa muda mlefu. Alikadhalika ikiwa kama hujakua kiroho ni sawa kabisa na umevaa nepi za kiroho pasipo kujijua. Shida kubwa iliyopo hivi sasa makanisani mwetu ni waamini wameshindwa kudumu katika fundisho.


Hali hii inapelekea mwamini kupenda sana miujiza isiyotokana na neno la Mungu,na miujiza ya namna hii,haimfanyi mtu kukua kiroho bali inamfanya mtu kuyumba yumba kiimani sababu ikiwa kama atasikia kule kuna nabii afanya miujiza basi huenda,kesho tena akisikia huku kwengine kuna miujiza huenda mwisho wa siku~roho ya mtu huyu hukaa katika hali ile ile ya kudumaa.

Miujiza sio mibaya,maana tunahiitaji sana ili ikadhihilishe kazi ya MUNGU ndani yetu. Lakini sio kitu cha kuchukuliana sana kiasi kwamba ukashindwa kudumu katika neno la Bwana.

(B) Hakikisha unakuwa mwombaji.

Fundisho lolote ulipokealo halikai sawa kama litakosa maombi sababu fundisho ni kama mbegu,maombi ni kama maji. Kama vile mbegu isivyoweza kukua pasipo maji alikadhalika neno/fundisho haliwezi kuwa na matunda kama litakosa maombi ya kutosha.

Maombi huatamia fundisho ulilolipokea ili fundisho au neno hilo likapate kuzaa matunda ndani yako. Maombi haya,yatakupa nguvu ya kuliendea fundisho kimatendo. Kwa kuwa imani pasipo matendo imekufa ( Yakobo 2:17 )

Ikumbukwe kuwa maombi ni silaha tosha dhidi ya kila nguvu ya giza maishani mwako. Ukiokoka tu,ni sawa na kutangaza vita dhidi ya falme ya giza. Sasa falme ya giza haiwezi kukubali kirahisi rahisi tu kwamba upokee fundisho la BWANA bali ni lazima watapambana na wewe ili usielewe tena ukate tamaa na hatimaye ushindwe kupokea neno sahihi. Katika hali hiyo,yakupasa uombe ili kumpinga kabisa yeye azuiaye.

Kuwa muombaji si jambo zito,bali ni jepesi tu. Ni hivi; ukiweza kuchukua muda wako na kujichanganya na wale waombaji,basi hapo taratibu na wewe unaanza kufanyika mwombaji. Ukweli ni kwamba,maombi yanaambukiza upako wa kuomba. Inawezekana hujui hata uombaje,lakini ukijitengea muda wako kisha ukaingia kwa waombaji basi tegemea kupokea upako wa maombi.

Mimi huwa ninafananisha kuwa,maombi ni kama kaa la moto.Sikia; Ili mkaa mmoja wenye moto uzidi kuwa na moto zaidi,ni lazima uambatane na mkaa mwingine wenye moto kwa maana chuma hunoa chuma ( Mithali 27:17 ). Vivyo hivyo ukiwa muombaji au ukiwa unatamani kuomba na ukijiambatanisha na mwombaji basi na wewe ni lazima utakuwa mwombaji mzuri.

02. KUVIKWA TUNDA LA ROHO.

“ Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Wagaratia 5:22-23

~Ni lazima ufahamu kwamba wokovu pasipo tunda la roho,haujakamilika. Kwa sababu tunda la Roho ni sehemu ya wokovu.Mtu wa imani katika Kristo Yesu ni yule mwenye kujawa na upendo,furaha,amani,uvumilivu,utu wema,fadhili,uaminifu,upole, na kiasi. Ukiona kama hujajawa na tunda hili,basi ujue unahitaji kukuwa zaidi kiroho.

Jambo moja linalofanyika wakati mtu anapompokea BWANA YESU ni kupewa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu ndio wale waliaminio jina lake ( Yoh.1:12 ). “Kufanyika watoto wa Mungu” ni kupewa kipawa cha tunda la Roho,kwa maana watoto wa MUNGU ni wale wote wenye kuongozwa na Roho wa Mungu (Warumi 8:14).

Swali,Je nitawezaje kuvikwa tunda hili la Roho?( yaani upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole,na kiasi; )…

ITAENDELEA….

Inawezekana kabisa umeguswa na mafundisho haya mazuri,na inawezekana unahitaji maombi katika imani yako,basi sasa waweza piga simu kwa namba yangu hii +255 655 11 11 49.

Mch. Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.