SOMO:UVUMILIVU NI NGAZI YAKO YA MAFANIKIO - MCHUNGAJI MADUMLA

Mchungaji Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kila mtu chini ya jua anapenda kufanikiwa kiroho na kiuchumi pia katika nyanja mbali mbali za maisha. Mimi sijawahi kuona mtu anayechukia mafanikio yake yeye binafsi tuseme labda kwamba anaupenda umaskini au anapenda siku akifa aende motoni.

Uvumilivu ni siri kubwa ya mafanikio. Maana wale wote waliofanikiwa sana,walivumilia sana maishani mwao,na hii ni kanuni ya kawaida kabisa. Kwa lugha nyepesi nikuambie mafanikio yako yamefichwa katika uvumilivu.

Neno uvumilivu linaweza kutafsiriwa kuwa hali ya utulivu na utayari wa kukubali maumivu kwa jambo au tabia isiyokubalika.

Uvumilivu ni tabia ya Mungu wetu.

“ rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. ” Yoeli 2:13 soma pia 2 Petro 3:9

Tazama hata Yesu Kristo Yeye mwenye kuanzisha na mwenye kuitimiza imani yetu jinsi alivyojaa uvumilivu. Pale alipoteswa na kusubishwa Yeye akasema “ Baba,uwasamehe,kwa kuwa hawajui walitendalo” Neno “ uwasamehe” linawakilisha kuwachukulia,kuwahurumia,pia kuwavumilia kwa yale yote waliyokuwa wakimtendea kwa maana hawajui walitendalo.

Ikumbukwe kwamba kila mmoja wetu amepewa mafanikio fulani hivi hata kama yamejificha,tena ingawa tunatofautiana katika mafanikio. Na ikumbukwe kwamba yapo mafanikio ambayo hayapatikani mpaka uwe na moyo wa uvumilivu. Na hapa yupo baba yetu wa imani,Ibrahimu anayetupa mfano mzuri jinsi alivyoweza kuvumilia hata Isaaka akazaliwa.

Watu wengi hawajui kwamba Ibrahimu mbali na kuwa na imani na Mungu lakini pia alikuwa na moyo wa uvumilivu. Sababu katika biblia hatuoni mahali popote pale ambapo Ibrahimu alimuacha BWANA Mungu akaambatana na miungu mingine katika mapito yake tazama katika hali hiyo hiyo,Ibrahimu anatazamia kupata mtoto kwa Sara ambaye amekoma kuzaa kwa desturi ya mwanamke,naye Ibrahimu ni mzee;Lakini Ibrahimu akatulia na Bwana hatimaye akafanikiwa kupata mtoto Isaaka katika umri wa uzee wa miaka mia ( Mwanzo 21:1-7 )

Ikiwa Ibrahimu aliweza kusubiri katika miaka yote hiyo,wewe je?. Vipi mbona wakata tamaa mapema ~ mbona huwezi kusubili? Au je unafikiri ulivyovumilia kwa muda huo ndio watosha? Jifunze kwa Ibrahimu na Sara.

Wapo watu ambao ndani yao hakuna neno “ uvumilivu”. Wao muda wote hukata tamaa na kupoteza muujiza wao pindi wanapopitia mazingira magumu. Mfano waweza kumkuta mtu mwenye kapawa cha uimbaji kanisani,lakini ikaja gafula majaribu kutoka kwa waamini wenzake au hata mchungaji wake,kisha ukamkuta akiiacha imani na kukimbia kanisa!!! (Mathayo 13:20-21). Mtu wa namna hii,amekosa moyo wa kuvumilia,na kwa sababu amekosa moyo huu,amekosa pia mafanikio yake yaliyokuwa tayari katika uimabaji wake.

Katika jambo unalolipitia,uvumilivu unahitajika sana huku ukiwa magotini pa Mungu maana upo wakati wa Bwana wa kuvuka hapo ulipo. Haijalishi ni jambo gani,lakini Bwana atakuvusha wewe uliyekuwa mvumilivu.

Ukihitaji mafanikio ya kiroho huna budi kuvumilia. Tena ukihitaji mafanikio ya kiuchumi huna budi kuvumilia. Jifunze kwa mfano wa Hana (1 Samweli 1:1-20) jinsi alivyokaa kwenye line ya Bwana Mungu akiomba mtoto. Jifunze pia kwa Ayubu jinsi alipovumilia yote ambayo Bwana aliruhusu yampate,na hatimaye akapata mafanikio ya kupata mara mbili ya yote aliyopoteza ( Ayubu 42:10 ).

Angalia mfano wa uvumilivu wa mkulima jinsi unavyokuwa ngazi ya kufanikiwa kwake. Mkulima hupanda,kisha uvumilia hata mvua ya kwanza na ya mwisho hata kuvuna gunia na gunia. “ Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. “ Yakobo 5:7.

Mpendwa unahitaji kuvikwa moyo wa uvumilivu katika yale yote uyapitiayo maana kwa uvumilivu ndipo kuna ushindi mkubwa. Yawezekana ipo shida,au mitihani fulani ya kimaisha unayapitia,na umeomba lakini bado unaona hakuna majibu,basi nakusihi usiwache kuomba wala usiwache kukaa katika line hiyo ya MUNGU.

Nami nakuomba tuombe pamoja leo katika hayo unayoyapitia kwa kunipigia simu yangu,

Kwa huduma ya maombi nipigie;+255 655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.