HOJA: TUSIDANGANYIKE, MUNGU HADHIHAKIWI

Askofu Sylvester Gamanywa
“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa apandacho mtu, ndicho atakachovuna…” (Wagalatia 6:7)

Ni rahisi sana kudanganyana sisi kwa sisi katika kutumia jina la Mungu kuhalalisha au kuharamisha mambo yetu. Aidha ni rahisi sisi kama binadamu kudanganyika kutokana na wajanja wenye kujipenyeza katika mambo ya Mungu wakidai wametumwa na Mungu kufanya yale wanayofanya. Na sisi kwa sababu ya uchanga, ujinga au udhaifu wetu tunawaamini na kuwakubalia ya kwamba hayo wasemayo au kutenda kwa jina la Mungu ni kweli yanatokana na Mungu. Lakini pamoja na hayo yote, wenye kudanganyika ni sisi, na wala si Mungu hata kidogo. Ndiyo maana maandiko yanatutahadharisha kwamba, tujilinde, tujihadhari tusije tukadanganyika, kwa sababu sisi ni rahisi sana kudanganyika. Na kama ujuavyo sisi sio wa kwanza kudanganyika, historia ya binadamu inatufundisha binadamu wa kwanza kabisa hambao hawakuwa na dhambi kama sisi, nao pia walidanganyika.

Sasa kitendawili kikubwa kiko kwenye kujilinda ili tusidanganyike. Tutapataje kujilinda tusidanganyike? Ni vigezo gani vya kutulinda tusidanganyike? Au ni viashiria gani vya kututahadhalisha kwamba tunaelekea katika udanganyifu? Kwa sababu mjadala hapa si kwamba hakunna udanganyifu. Mjadala ni jinsi ya kuutambua udanganyifu wenyewe.

Uchunguzi wa awali nilioufanya kuhusiana na suala la kutokudanganyika umenionyesha kwamba si kazi nyepesi kujilinda na udanganyifu. Hii ni baada ya kugundua kwamba, jamii ya waaminio wote, wawe wazee wa zamani wa imani au kizazi kinachoinukia, SISI SOTE NI WAATHIRIKA WA KUDANGANYIKA! Kila mmoja wetu kwa njia moja au nyingine amedanganyika katika jambo Fulani aliloaminishwa kuwa ni kweli wakati si kweli.

Na hapa naomba nikumbushie aina ya udanganyifu ninaoulenga hapa ni katika mambo yetu ya imani kwa Mungu. Kila mmoja wetu ni mwathirika wa kudanganyika. Na hata mpaka sasa wengi wetu bado tunatembea katika udanganyifu bila kujua kwamba tumedanganyika! Hii ndiyo maana kitabu cha Mhubiri kinatumia misamiati ya maneno kama haya ya kuwa hii ndio baa na ubatili mkubwa! Kutembea katika udanganyifu huku tukidhani tuko kwenye kweli.

Vyanzo vya tatizo la
kutembea katika udanganyifu

1.    Kuzaliwa na kukulia katika mazingira ya udanganyifu wa kidini

Na hapa wengi wetu tumeathirika pasipo sisi kuhusika wenyewe. Tumezaliwa ama katika madhehebu ya dini zetu tukafundishwa mapokeo ya dini zetu kama miongozo ya kiimani. Huko nyuma niliwahi kudokeza kwenye makala na mafundisho kuhusu “kila dini kuaminisha wafuasi wake kwamba Mungu wanayemtaja ndiye MUngu wa kweli; na njia za kumwabudu ndizo sahihi kuliko nyinginezo”!

Napenda kurejea kutahadharisha kuhusu udanganyifu mwingine ndani ya udanganyifu huu. Iko dhana kwamba madhehebu ya dini ambayo yamekuwepo kwa miaka mingi duniani ndiyo yaliyo sahihi zaidi, kwa sababu yanao wafuasi wa kudumu toka vizazi hadi vizazi. Na kwamba madhehebu yanayoazishwa miaka ya karibuni ndiyo yenye udanganyifu wa kiimani.

Kwa ikumbukwe kwamba kigezo cha usahihi wa imani sio kuwepo duniani kwa muda mrefu. Shetani amekuwepo muda mrefu zaidi kuliko dini zote zilizopo na hatuaminishwi kwamba ameacha kuwa mdanganyifu. Pili, dhana hii ni propaganda za kidini za kulinda waumini wasiondoke kwenye madhehebu hayo. Tatu, udanganyifu ndani madhehebu ya dini mara nyingi ndio msingi wa kuanzishwa kwa dini hizo tangu mwanzo.

Kwa hiyo, sio kweli kwamba madhehebu ya zamani ndiyo yako sahihi kuliko mapya. Na upande wa madhehebu mapya nako kuna dhana potofu kwamba yameanzishwa kufanya matengenezo na urejesho wa imani sahihi ambazo madhehebu ya zamani yametopeza. Huu nao ni nusu ukweli. Sio kweli kwamba kila madhehebu mapya yana imani sahihi ya kufanya matengezo. Kwa hiyo, kila upande una udhaifu ule ule wa kubeba udanganyifu na hali kadhalika kila upande una usahihi wa imani ambao unaweza kushuhudiwa na wengine katika kila kizazi. Kwa hiyo kigezo cha “uzamani” au “upya” hakina ukweli wa kudhihirisha usahihi au udanganyifu wa imani.

Lakini ni ukweli kwamba kuzaliwa na kukulia katika madhehebu yaliyokengeuka kiimani, kuna athari za kiimani kwa mtu na inamchukua muda mrefu kuja kufikia mahali pa kuanza kupambanua usahihi wa imani nje ya mapokeo ya itikadi aliyoirithi tangu alipozaliwa.

2.    Mwiko wa kutokuhoji usahihi wa mapokeo ya itikadi za imani zetu

Kuna dhana sugu ya karne nyingi ambayo wafuasi wa madhehebu mbali mbali ya dini wameingiziwa katika akili zao, nayo ni kutokuthubutu kuhoji, au kutaka kujua kwa hakika usahihi wa mapokeo na itikadi ya madhehebu ya dini zetu. Kwa sababu mambo ya imani yamepewa nafasi ya pekee ya kutokuhojiwa na mtu na hasa pale ambapo mapokeo yenyewe yamekuwepo toka vizazi vilivyopita.

Eneo jingine linalotisha zaidi kwa wengi kuhofia kuhoji usahihi wa itikadi za madhehebu ya dini zetu ni “dhana ya misahafu ya dini zetu kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja kupitia mitume waasisi wa dini zetu.” Misahafu hii kamwe hakuna wa kuihoji usahihi wake kwa sababu waasisi waliopokea kwanza hapo duniani tuwahoji, lakini pia hakuna mwenye mamlaka ya kusahihisha kilichoandikwa humo.

Kwa hiyo, mwamini akianza kuwa na mashaka-mashaka kuhusu itikadi au mapokeo ya dini yake, anachoweza kufanya ni kuasi au kujitenga nayo kibinafsi na si vinginevyo. Ni kutokana na dhana hii ya kutokuhoji usahihi wa mapokeo na itikadi za dini zetu ndio unaendeleza watu wengi kuendelea katika udanganyifu wa kidini. Hawezi kuhoji kwa sababu hata wakihoji hawatapa majibu sahihi. Na wakihoji wataonekana waasi na hivyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa mapokeo ya itikadi ya dinii husika.

Ukweli wa mambo, binadamu tumeumbiwa hiari ya kuchagua kukubali au kukataa jambo lolote, hata kama ni kumkataa au kumkubali Mungu mwenyewe. Ni Mungu mwenyewe ametuumbia uwezo huu wa kutumia utashi wetu kumtii au kumuasi hata kama ni kwa hasara yetu wenyewe.

Kwa nini Mungu alitupa uhuru na uwezo huu kimaumbile? Moja wapo ya sababu ni “tumkubali kwa moyo wa kumpenda kwa hiari ili ushirika na uhusiano wetu uwe wa maridhiano na ambao sio shinikizo la lazima”! Ikiwa Mungu muumbaji alituumbia uwezo na uhuru huu, tusipoutumia wenye kuathirika ni sisi wenyewe na Mungu hawezi kulaumiwa.

Isitoshe, Mungu mwenye haogopi kuhojiwa usahihi wa jambo lolote linalomhusu kwa sababu utawala wake haukujengwa kwenye misingi ya woga wala kujihami kutokupinduliwa na kiumbe yeyote. Tena mwenyewe ametoa idhini kwa wanaotafuta ukweli au wenye hoja nzito wazipele kwake kupitia sala ili wapate majibu sahihi kutoka kwake. “Haya leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.” (ISA.41:21)

Itaendelea toleo lijalo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.