HOJA: UTATA WA KIIMANI BAADA YA MATOKEO YA UCHAGUZI

Askofu Sylvester Gamanywa.

Kanisa linahitaji kujifunza upya jinsi ya
kupokea majibu ya maombi toka kwa Mungu

Baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kuanza kutangazwa, na baada ya mgombea wa chama tawala kutangazwa mshindi, nimehojiana na baadhi ya jamii ya waombaji ambao walikuwa mstari wa mbele kuombea uchaguzi nikitaka kujua wanasema nini kuhusu matokeo ya uchaguzi. Majibu ambayo nimekuwa nikiyapata kutoka kwa baadhi ya waombaji ndiyo yamenifanya niandike makala hii - si kwa nia ya kubeza au kulaumu bali kuingilia kati hali ya hatari inayolikabili kanisa kiimani kutokana na hali ya kuchanganyikiwa iliyomo ndani ya waumini.


Utata uliojitokeza kiimani kwa waombaji
kulingana na matokeo ya uchaguzi

Hivi sasa kuna utata wa kiimani ambao unaendelea ndani ya kanisa ambao unahitaji kushughulikiwa haraka iwezekanavyo vinginevyo athari zake ni mbaya kwa kanisa kuliko vile inavyoachwa hivi hivi kiholela. Mcango wangu katika makala haya unaanza nan uchambuzi wa mgawanyiko wa makundi ya waombaji walikuwa wakiombea uchaguzi. Naweza kuwagawa wanamaombi katika makundi manne yafuatayo:

1.   Kundi la waombaji ambao walikuwa wakimwombea mgombea wa chama chao ndiye ashinde uchaguzi

Hili ni kundi la waombaji ambalo kwa mtazamo wao waliamini kuwa wanayo haki ya kumwendea Mungu na kumwomba lo lote kama ahadi za Mungu zilivyo katika neno lake kwa tukiomba lolote kwa jina la Yesu tutapata sawasawa na haja ya mioyo yetu.

Kwa hiyo, kila mtu kwenye maombi yake alikuwa akimwombea mgombea wake wa urais, bunge na udiwani ndiye ashinde na kushika madaraka baada ya uchaguzi mkuu. Utata wa kiimani katika kundi hili ni kukosa maarifa ya Neno la Mungu linasemaje kuhusu kupata viongozi wa kiserikali.

Sasa utata uliojioteza ni kuvunjika moyo kwa waombaji ambao mgombea wao hakushinda kwenye uchaguzi huu. Wamekasirika na kuona maombi yao hayajajibiwa kama walivyoomba na hivyo kila mtu anasema la kwake mtaani tena katika hali ya kuchanganyikiwa.

Na niseme kwamba utata huu unanchangiwa zaidi na viongozi wa kikanisa kutokuwa na ufahamu wa aina moja kibibilia kuhusu eneo hili la jinsi ya kupata viongozi au watawala wa kiserikali kutoka kwa Mungu.


2.   Kundi la waombaji ambalo lilikuwa liombea mfumo wa uchaguzi ufanyike kwa uhuru na haki

Kundi hili ni la waombaji wale ambao ufahamu wao kiimani uko kwenye mtazamo wa kuwapata viongozi wa kiserikali kwa kupitia mifumo ya uchaguzi iliyowekwa kwa mujibu wa sharia za uchaguzi. Kindi hili linaamini kwamba, Mungu hateuwi viongozi moja kwa moja kama wafalme wa Israeli, bali anatumia mifumo ya kisiasa iliyo hivi sasa katika chaguzi za kiraia.

Kwa hiyo, wanaamini ili Mungu aweze kuwadhihirisha viongozi anaowataka lazima taratibu na sharia za mifumo ya uchaguzi zifuatwe kwa haki na kwa njia ya haki wale watakaoshinda kwa haki basi ndio hao Mungu aliowaridhia washike madaraka ya utawala.

Kutokana na mtazamo huu, waombaji walikuwa wakiombea Mungu azuie kabisa njia zote za wizi wa kura, na adhibiti kila njama za kuhujumu matokeo ya wapiga kura.

Kwa bahati mbaya, kundi hili limechanganyikiwa sana na dosari za utata wa takwimu zenye kuashiria uchakachuaji wa matokeo ya kura. Kundi hili linaona uchaguzi umehujumiwa na hivyo wagombea walioshinda hawakupita kwa haki, na hivyo matokeo si halali hata kama yametangazwa na mamlaka kamili inayotambulika kisheria. Hawa nao wanaosha shetani ameingilia kati na kufanya hujuma zake kwa hiyo maombi yao yamezuiliwa na mkuu wa anga anayesimamia hujuma dhidi ya uchaguzi.

3.   Kuna kundi ambalo lilikuwa linaombea kuon’goka kwa chama tawala madarakani

Kundi hila la tatu la woambaji, ni kundi ambalo mtazamo wake lilikwisha kuwa kinyume na mwenendo wa chama tawala na wanataka utawala mpya usiotokana na chama tawala. Kwa hiyo, mzigo wa maombi yao wakati wa uchaguzi, walikuwa wakiomba muujiza wa kung’oka kwa chama tawala madarakani.

Kwa kundi hili, hata kama mgombea wa chama tawala ana sifa za kutawala, lakini linamini hataweza kutawala vema akiwa chini ya chama tawala ambacho wao wamekichoka na hawakitaki.

Niliwahi kusikia kauli za baadhi ya wenye mtazamo huu wakisema; “hataka akiwekwa shetani na chama tawala wao watampigia kura shetani kuliko chama tawala.”! Mtazamo huu ulikuwa mkali kiasi cha sio kutisha tu, lakini mtazamo uliopitiliza mipaka ya kiimani.

Kutokana na matokeo ya uchaguzi, wapinzani wa chama tawala wamekwazika kwa sabbau maombi yao ya kung’oka kwa chama tawala hayajajibiwa. Bado chama tawala kimebaki madarakani tena kwa njia za ubabe na wizi! Mtazamo wao hawa ni kwamba ushindi wa mgombea wa chama tawala si halali na haki.

Sasa basi, utata wa kiimani wa kundi hili uko wapi? Utata uko kwenye kutokujua kwamba Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa kubaki au kung’oka kwa chama tawala. Hata kama waombaji hawa walikuwa na sababu zote za haki na kweli za kutaka chama tawal king’oke, uhuru wao katika kuomba Mungu ni kuwasilisha hoja zao kwa Mungu, na suala la Mungu kutenda kama vile walivyoomba hilo liko katika mamlaka yake Mungu mwenyewe. Wanafunzi walimuuliza Yesu dakika za mwisho za kuagana naye wakisema; “Je wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?.....”; Yesu akawajibu akisema, “….si kazi yenu kujua nyakati wala majira Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe…” (Mdo.1:6-7

4.   Kundi ambalo lilikuwa linaomba kwa yule ambaye ni chaguo la Mungu ndiye ashinde

Kundi hili la nne ni dogo naa lenye watu wachache kuliko makundi mengine yaliyotangulia. Kundi hili lenyewe mtazamo wake ni kwamba Mungu mwenye kujua yote na muweza wa yote, ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa nani anafaa kushika madara ya kuongoza nchi.

Kimsingi hili ni kundi la akina “mapenzi yako yatimizwe”. Sana sana lenyewe lilijikita katika kuombea suala zima la amani na utulivu ili matokeo ya uchaguzi yatangazwe kwenye mazingira ya amani na utulivu.

Kwa mtazamo wangu, naweza kusema kundi hili ndilo limebaki salama kiimani baada ya kutangazwa matokeo ya mshindi wa nafasi ya urais, pamoja na washindi wengine wa ngazi za ubunge na udiwani. Nasema ndilo limebaki salama kiimani kwa kuwa katika maombi yao hawakuwa wanatafuta matakwa yao wenyewe, bali walikuwa tayari kupokea mapenzi yake Mungu kwa namna yoyote ambayo Mungu atairidhia. Pili, kwa habari ya amani na utulivu maombi haya yamejibiwa waziwazi hata kama kuna mitafaruku iliyojitokeza hapa na pale, lakini hakuna anayebisha kwamba uchaguzi haukufanyika katika mazingira ya amani na utulivu.

Ushauri wangu kwa uongozi wa kikanisa

Mgawanyiko wa makundi ya waombaji ambaoyo nimeyaanisha katika makala haya, ni ushahidi kamili kwamba, kanisa limegawanyika kiimani kuhusu “theolojia ya utawala” katika awamu ya agano jipya. Ndiyo maana nasema ni wakati wa kurejea katika msingi wa neno la Mungu linasemaje kuhusu habari za ushiriki wa kanisa katika mambo ya utawala wa kisiasa. Inahitaji mijadala ya kina ili kuganga mioyo ya waamini iliyojeruhika kwa sababu ya kukosa uongozi makini katika eneo hili.

Vinginevyo natumia fursa hii kutangaza rasmi kwamba, tuyakubali matokeo kama yalivyotangazwa, tuache upinzani na kurejea katika magoti ili kutubu pale ambavyo tulipotoka na pia kuliombea taifa letu Mungu alirehemu kwa upya. Hakuna kiongozi yeyote anayeingia kaenye madaraka ya nchi basipo ridhaa ya Mungu. Mungu ibariki Tanzania.Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.