HOJA: KESHO HUANZA LEO

Mwangalizi Mkuu wa WAPO Mission International, Askofu Sylvester Gamanywa.
Kuna kasumba sugu iliyozaa miongoni mwa jamii ya Kikristo inayowafanya wasijishughulishe na kitu kwa juhudu zao wenyewe, badala yake wanajificha kwenye kichaka cha sala na maombezi wakitarajia kupokea miujiza. Kana kwamba hii haitoshi wengi hutoa utetezi kwamba Yesu mwenyewe aliagiza kwamba tusisumbukie ya kesho kwa sababu kesho itajisumbukia yenyewe:

Tafsiri ya 
kutokusumbukia ya kesho

“Msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” (Mt.6:34)

Maandiko niliyonukuu hapa juu yametatanisha wengi hata wakazalisha imani potofu kwa kupata tafsiri potofu. Hata miye nilipata shida kupata maana kamili ya Yesu.  Wengi wetu tunaposoma haya tunadhani Yesu alikuwa akipuuza kutokupanga mipango ya kesho na badala yake kufikiria mambo ya kufanya siku ya leo peke yake. Tena utawasikia wengine wakichombeza kusema “wacha ya kesho bwana kesho itajisumbukia yenyewe. Na hapo ndipo kitendawili kilipo.

Maana ya Yesu katika kusema “msisumbukie ya kesho” ni kutaka kutoa kipaumbele kwa yale yanayotakiwa kufanyika leo kabla ya kurukia ya siku inayofuata. Hapa ni kanuni ya “kupanga vipaumbele” katika “ratiba inayozingatia muda” ili kuweka uzito kwa kukamilisha ya wakati uliopo sasa. Kanuni ya kupanga vipaumbele lazima ianze na mambo yanayotakiwa kufanyika sasa ili hatua kwa hatua hayo yatufikishe kesho ambapo tutaendelea na yaliyoko mbeleni.

Tukumbuke kwamba, kesho ikifika utalazimika kuanzia mahali ulipoishia jana yake. Jana yako ndiyo leo, na leo yako ndiyo kesho. Huwezi kuiruka leo na kudandia kesho. Kwa hiyo kesho huanza leo.

Mambo ya kiroho nayo
 hutumia siku halisi

Tukirejea kwa mambo ya kiroho ambayo ndiyo msingi wa ujumbe ni kwamba, Yesu anatutarajia tufanye maamuzi yote ya kujindaa na kuwa tayari leo na sio kesho. Kuna watu ukiwaambia habari za kutubu dhambi watatoa visingizio vingi kikiwamo cha kufanya uamuzi wa toba kesho badala ya leo.

Wanajisahau kwamba, fursa waliyo nayo ya kufanya uamuzi kama huu ni leo, tena hivi sasa, na sio baadaye; kwa sababu “hiyo baadaye” yenyewe haimo katika uwezo wala udhibiti wao. Yesu alitoa ahadi ya kuja kulichukua kanisa lake ghafla bila taarifa na hivyo akaamuru watu kujitakasa na kuwa tayari leo hivi sasa wasisubiri hiyo kesho.

Je wewe msikilizaji wangu unakabiliana vipi na hizi changamoto za kutokufanya maamuzi leo, na kuyaahirisha mpaka kesho, wakati huna uhakika wa kuifikia hiyo kesho yenyewe? Je umesahau kuna maelfu ya watu wengi ambao hutangulia mbele ya haki, yaani kufariki dunia lakini walikuwa na “ahadi/appointment za kesho ya siku ambayo wamekatishwa ghafla?

Sasa basi ni afadhali wale wanaotanguliwa mbele ya haki lakini walikwisha kufanya uamuzi wa kujenga mahusiano yao na Yesu mapemaaaa. Kuondoka kwa ni faida na sio hasara. Kilio na masikitiko na wale wanaotangulia mbele ya haki kabla hawajafanya uamuzi wa kumpokea Yesu kuwa mwkozi wao binafsi.

Na ndiyo maana Neno la Mungu linasema siku ya wokovu ndio saa na sio kesho. Lakini pia kusudi la kipindi hiki ni kukuombea Baraka za siku ya leo na sio kesho.

Hata utumishi kwa Kristo
 nao hutumia siku halisi

Changamoto nyingine iko kwetu sisi tuliokwisha kufanya uamuzi wa kuwa ndani ya Kristo. Ni kuishi maisha ya kizembe huku tukidhani tutapata thawabu mbinguni wakati ukweli wa maisha yetu hatuna cha maana tunachofanya kinachostahili kulipwa au mtu kutuzwa kwacho.

Hii inatokana na dhana potofu kwamba, utumishi kwa Kristo ni watu maalum “wenye vyeo” kanisani na kwamba “washirika wa kawaida”! kwa dhana hii walio wengine wamewekeza nguvu zao na maisha yao katika mambo ya dunia hii ambayo hana mchango stahiki kwa huduma za Kristo duniani.

Kama kwamba hii haitoshi, hata wengine wakihimizwa kujituma katika huduma za Kristo watasingizia kwamba wao bado hawajasikia wito wa Mungu katika maisha yao kwa hiyo siku watakapoitwa basi wataitika na kuanza kutumika. Sasa basi hebu turejee kwa Paulo aliyekuwa mtume mkuu mwenye hekima jinsi anavyotutahadharisha akisema yafuatayo:

“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele za kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” (2 Kor.5:10)

Unaona jinsi ilivyoandikwa? “….imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo…” Halafu tena “……kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda katika mwili…..” sehemu inayotisha zaidi ni hii “…..kwamba ni mema au mabaya.”!

Wengi tunaweza kujiuliza hii ni hukumu ya namna gani kwa ajili ya nini? Hii inaitwa hukumu ya watakatifu. Mimi na wewe kama kweli una uhusiano halisi na Kristo kiimani. Hukumu hii si ya adhabu bali ni ya kutathminiwa na kupewa tuzo kwa mujibu wa utendaji wa kila mmoja wetu alipokuwa angalipo duniani.

Kwa mantiki hii, ikiwa hukuwa ushiriki wa kiutumishi kwa huduma za Kristo usitarajie kuwa utapata tuzo kwani tuzo hupewa walioshiriki mashindano na kufaulu.

mwisho

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.