HOJA : TUSIDANGANYIKE, MUNGU HADHIHAKIWI - (mwisho) - ASKOFU GAMANYWA

Askofu Sylvester Gamanywa, Rais wa WAPO Mission International
Tusidanganyike, Mungu hadhihakiwi

“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa apandacho mtu, ndicho atakachovuna…” (Wagalatia 6:7)

Jumapili iliyopita tulianza mada ngumu kidogo ya kutokuendelea kudanganyika kiimani kwa sababu Mungu tunayemwabudu yeye hadanganyiki. Humo tulibaini kwamba udanganyifu wa kidini ni mgumu kuupambanua kwa sababu ummejengwa katika misingi ya utetezi wa mambo ambayo yako nje ya uwezo wetu. Aidha nilianza kudokeza baadhi ya vigezo vinavyoweza kutusaidia kutambua tatizo la kutembea katika udanganyifu ambavyo baadhi yake ni 1. Kuzaliwa na kukulia katika mazingira ya udanganyifu wa kidini tangu utoto; 2. Mwiko wa kutokuhoji usahihi wa mapokeo ya itikadi za imani zetu. Leo tunaendelea na uchambuzi wa mada hii tata lakini inayolenga kutufungua kutoka kwenye udanganyifu wa kiimani kwa sababu hakuna lisilowezekana kwa Mungu:

Tamaa ya kutajirika
 kwa njia za mkato

Kigezo cha tatu kinachotumika kupelekea watu wengi kudanganyika upesi kupitia mambo ya imani katika dini, ni tama ya kutafuta mafanikio kwa njia za mkato. Karne za zamani dini nyingi zilijenga imani za wafuasi kuishi maisha ya umaskini kama njia ya kutafuta utakatifu na kigezo cha tabia ya unyenyekevu. Waasisi wa dini enzo hizo walitumia mbinu hii ya kuchukua mali za wafuasi kwa kisingizio cha ushashiwi wa kutoa mali zao na kumtolea Mungu.

Basi watu walitoa mali zao kwa viongozi hao makuhani wa kidini na kuhakikisha wafuasi wanazidi kuishi maisha ya umaskini lakini wao wakineemeka kupitia udanganifu huo. Mpaka hivi leo bado yako madhehebu ya dini yenye kuamini katika udanganyifu huu na huwezi kubadilisha misimamo na mitazamo yao.

Kwa kadiri miaka ilivyozidi kusogea, mbinu mpya ya udanganyifu za kiimani zikazidi kubuniwa. Safari hii, zikaja mbinu za kuwahamasisha wafuasi wa dini kutoa mali zao kwa imani za dini husika ili wapate utajiri wa miujiza. Bila shaka wajanja hawa wa kidini walipoona maendeleo ya viwanda yameleta mageuzi ya kiuchumi ulimwenguni na jamii ya watu wamegundua umaskini unaweza kuepukwa kwa kufanya kazi na kujiwekea akiba ya mapato.

Wakati huo jamii ya watu wengi wakawa wanahama kutoka vijijini na kuelekea mijini ambapo kuliwa na fursa za kufanya kazi viwandani. Lakini pia si wote waliokimbilia mijini walipata fursa za ajira, na hivyo wakalazimika kuishi maisha ya kubangaiza huko na huko wakitafuta maisha kwa njia kijasiriamali.

Kupitia mazingira haya, wajanja wa kidini wakapata “mafunuo hewa” ya kuendesha kampeni za kuhubiri dini huku nia ikiwa sio kuwarejesha watu katika kumwamini Mungu watubu na kuishi maisha ya uadilifu; bali kuitumia njia ya kuhubiri dini kama njia ya kujipatia utajiri kwa wao kuhubiri kitu ambacho siku hizi ni maarufu kama “injili ya utajirisho”

Kampeni za Injili ya utajirisho hutumia maandiko ya misahafu ya dini kuwaaminisha wafuasi kutoa mali zao kwa Mungu ili wafunguliwe milango ya kupata utajiri kwa njia za utoaji fedha na mali na kuwapa wahubiri hao kama “makuhani walioteuliwa kuwa “”mawalii” wa kutoa Baraka za utajiri.

Kwa wale wasomaji wa maandiko ya Biblia katika Agano Jipya, ni mashahidi kwamba, (pamoja na ukweli kwamba Utoaji wa fedha na mali kwa ajili ya Injili ya Kristo husababisha watoaji kubarikiwa na Mungu kiuchumi ili wazidi kuwa wafadhili wa huduma za injili); lakini wako wajanja wengi tangu enzi za mitume waliojikita katika kuhubiri “injili ya utajirisho” kwa nia ya kujipatia faida: “ na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida..” (1 Tim.6:5)

Ninatambua sana ukweli wa Baraka za utoaji kwa mujibu wa maandiko na pia ni mhubiri wa utoaji kwa washirika wengi. Lakini tofauti ya mafundisho sahihi kuhusu utoaji ni nia ya mfundishaji na matumizi ya mapato ya matoleo yanayotolewa kama yanakwenda kwenye injili kweli kweli au yanaishia mikononi mwa watu binafsi kwa visingizio vya “wapakwa mafuta”!

Ni kutokana na udanganyifu huu wa watu kushawishiwa kuwa wakitoa fedha na mali zao wakawapa wenye kutabiri utajiri basi wataupata utajiri wa miujiza. Kwanza huu ni sawa na ushirikina wa watu waendao kwa waganga wa tunguri ili kutafuta bahati za utajiri, vyeo na umaarufu. Na huko huambiwa kutoa sio fedha tu bali hata makafara ya damu za wanyama na siku hizi mpaka “makafara ya viungo vya binadamu.”!

Katika kuhitimisha kipengele hiki nataka kusisitiza kwamba, pamoja na udanganyifu wa kidini unaotumia udhaifu wa binadamu wenye tamaa ya kupata utajiri wa miujiza; bado Mungu hadhihakiwi. Mungu hawezi kuruhusu jina lake litumike kwa njia za udanganyifu, watu waibiwe fedha na mali zao kupitia jina lake. Pamoja na kutumia jina lake kuwaibia watu, bado watu wenyewe hawaupati huo utajiri wa miujiza kwa sababu Mungu anadhibiti udanganyifu huo.

MUngu hazuii watu wanaokubali kudanganyika na kutoa mali zao kwa jina lake; bali anadhibiti wasiupate utajiri huo kwa jina lake kama walivyodanganywa. Kwa hiyo, hutoa sana na bado hubaki masikini hivyo hivyo mpaka hapo watakaposhtuka wenyewe na kuhoji usahihi wa mafundisho hayo potofu na kuutafuta ukweli kamili.

Kanuni ya kibiblia za kupata utajiri
wa kweli wa Baraka za Mungu

Tangu mwanzo wa kuumbwa binadamu wa kwanza, tena kabla ya anguko katika dhambi, Baraka za Mungu zilitokana na “kufanya kazi” katika bustani ya Edeni. Mungu mwenyewe ndiye aliyeiteengeneza bustani hiyo na kumkabidhi Adamu ailime na kuitunza. (Mw.2:15)

Jambo ambalo inatupasa kulivalia njuga ni kuamua kuvunja dhana potofu ya kupata “utajiri wa miujiza” kutoka kwa Mungu; kwa sababu kwa mujibu wa Neno la Mungu; ni “kupokea nguvu za kupata utajiri”:“Bali utamkumbuka BWANA, MUngu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” (Kumb.8:18)

Maandiko yametuonyesha kwamba, hatupokei utajiri moja kwa moja kutoka kwa Mungu hata kama tukitoa sadaka nyingi sana kwa Mungu. Tunapokea “nguvu za kupata utajiri” ili tufanye kazi kwa bidii na kasha Mungu kubariki kazi za mikono yetu.“Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.” (Efe.4:28)

Tunaanza kujenga kwanza mahusiano ya kiroho na Mungu kwa kuzaliwa mara ya pili kiimani kwa njia ya Yesu Kristo. Baada ya kuzaliwa upya kiroho, ndipo tunakuwa wana wa agano jipya ambalo mwanzilishi wake ni Yesu Kristo mwenyewe. Kisha tunabadili mfumo wa maisha ya dhuluma na uvivu na kuanza kufanya kazi zilizo halali na nzuri na ndipo sasa tukimtolea Mungu sadaka tunabarikiwa kwa njia ya kuboreshwa nguvu za afya zetu.


Mwisho

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.