JE NITAWEZAJE KUKUA KIROHO ?~ Sehemu ya mwisho.Na Mchungaji Gasper Madumla

Endelea kusoma sehemu ya mwisho wa somo hili.

Bwana Yesu asifiwe…

Karibu tuendelee…

06.KUTEMBEA KATIKA IMANI.

Mwaka fulani nilitoka na timu ya wainjilisti tukaenda kuhubiri huko Tanga sehemu moja hivi. Tulipokuwa tumefika na kukaribia kuanza mkutano wa jioni siku ya kwanza,gafla mama mmoja alitujia mwenye kuaminika yakuwa ni mchawi sana katika kile kitongoji akaingia ndani tulipokuwa tumeketi na kudai anahitaji maombi maana anasingiziwa kuwa yeye ni mchawi.

Lengo lake ilikuwa ni kutupima kiwango cha uwezo wetu kiroho ili apate kutuangamiza,lakini ashukuliwe Mungu tukamtambua mapema katika hila zake,hivyo mitego yake iligonga mwamba.

Na tangu siku hiyo,na kuendelea tukawa tukitembea katika imani kimatendo. Si kana kwamba tulikuwa hatuna imani,bali ile imani tuliyoiamini kwa kujifunza darasani tuliileta kimatendo kupambana na mchawi uso kwa uso. Na hapo sasa imani yetu ilikamilishwa na matendo.

Mwamini katika Kristo Yesu mfano ndio wewe anaweza kukua kiroho kwa kuileta imani yako katika matendo.kishasasa ndipo weweza kujipima kuwa imani yako ikoje;La sivyo hutajua kiwango chako cha imani.

Yakupasa kuchukua mazoezi ya hatari ili kukuza roho yako kwa kile unachokiamini. Mfano mwingine ni huu;

Siku moja tulienda kufanya mazoezi ya imani kimatendo kwa nia ya kukuza roho zetu,tulitoka na kuelekea hospitali ya ocen road kwenda kuwasaidia wahitaji kwa maombi na misaada ya kawaida kama vile chakula,nguo N.K.

Huko tulibahatika kuwaombea wagonjwa na baadhi yao walipata uponyaji lakini mpaka tulipofanikiwa kufanya maombi tulikutana na mikiki ya kiimani,maana wengi tuliwakera,wengine hawakutaka kabisa na hata hivyo mwishowe tulifukuzwa tukaambiwa basiii,kisha tukaondoka huku tukiwa tumejifunza kutembea kiimani.

Hivyo inakupasa kujifunza kiundani kuhusu imani yenye matendo,hiyo ndio inakuza roho zetu na wala si imani ya kwenye vitabu tu kwa sababu imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:17).

Twaweza kujifunza kutembea na imani katika matendo kwa kumuangalia Yeye ambaye ni mwanzilishi wetu wa imani Bwana Yesu. Mara nyingi Bwana Yesu alikuwa akitenda kile alichokiamini;tazama muujiza wa kufufuliwa Lazaro;

“Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. ” Yoh.11:11Na baada ya hapo tunaona Yesu akienda kumuamsha Lazaro aliyekufa. Je unafikiri laiti kama Bwana Yesu angeomba tu huko huko aliko,muujiza wa kufufuka kwa Lazaro usingelitokea?

Ukweli ni kwamba,muujiza ungelitokea maana Yeye Bwana ni MUNGU,lakini kwa nini alihitajika kufunga safari kwenda kwa akina Lazaro? Hii yote ni kwa sababu anatufundisha ya kwamba imetupasa kutenda katika yale tuyaaminiyo.


Sijui kwako wewe! Kama kweli unajipa mazoezi ya imani katika matendo kwa kusudi kuimarisha roho yako. Nakuambia pasipo mazoezi ya kiroho,huwezi kukua kiroho. Kama vile mtu anavyokuwa shupavu akiwa na mazoezi ya mwili wake,ndivyo alivyo mtu wa rohoni awavyo shupavu akifanya zaidi mazoezi ya kiroho.

Mfano mdogo;Waweza kujipa mazoezi ya kiroho wewe mwenyewe ili kuifanya roho yako ikue zaidi.~Chukua muda wa kuwafundisha watu neno la Mungu na kuwaombea,tafuta wale watu wako wa karibu na badala ya kupiga nao story za kawaida,basi watake wakusikilize kisha wafundishe neno la Mungu japo kwa ufupi kwa kile kile unachokijua wewe,kisha waombee. Nakuambia waweza kuanza kwa udogo sana,lakini sivyo utakavyokuwa baadaye ikiwa utaendelea kujipa mazoezi haya ya kiimani.

Tena,kama vipi anza na watoto wako au watoto wowote wale,waketishe na uanze kuwafundisha neno la Mungu. Hapo,utaona ukianza kukua kiroho katika kiwango hadi kiwango. Wengi wameanzia hivi hivi,leo ni watumishi wa kubwa kiimani.

Mimi nilianzia kujipa mazoezi ya kutembea kiimani kwa kuhubiri chumbani. Nilikuwa ninahubiria kabati na vyombo,ndoo na muda mwingine majiko ndani kwangu,kisha kumbe kwa mazoezi yale yakanipa ujasiri mkubwa wa kutoka,nikaanza kujifunza zaidi mpaka pale Roho wa Bwana aliponiita katika utumishi wake huu nilionao hivi sasa.

Imani uliyonayo je inakukuza kiroho? Kama la,! Basi jifunze kuifanyia kazi kimatendo ili roho yako izidi kuhitaji kujifunza zaidi kupitia Bwana Yesu.

~ Kwa huduma ya maombi usisite kunipigia kwa namba yangu ya simu ;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.