SOMO: YAKUPASA KUJIFUNZA TOBA HALISI ILETAYO MAJIBU - MCHUNGAJI MADUMLABwana Yesu asifiwe…

Sasa ni wakati wa kutubu mbele za Mungu. Lakini utawezaje kutubu kwa kina ikiwa huzijui hatua za muhimu za toba ya kweli? Ni vigumu kuzama kilindini katika toba pasipo kujua hatua za muhimu za toba ya kweli. Zipo hatua kadhaa za kuifikia toba halisi yenye majibu iletayo masamaha ya dhambi,hapa leo ninakupa hatua chache tu,zile za muhimu.

Toba ni neno lenye asili ya lugha ya kiebrania lenye maana ya “geuka”. Neno hili linapotumika katika biblia lina maana ya kugeuza mawazo mabaya ya dhambi, maneno mabaya na matendo machafu kwa kumaanisha kuyaacha hayo yote kisha kumlingana Mungu katika maungamo kwa msaada wa Roho mtakatifu.

Tazama mfano wa Paulo,asemavyo;

“ bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.“Matendo 26:20

Alipowahubiri kwamba watubu yaani wageuke na kumwelekea Mungu,hii ikiwa na maana watu wale waliohubiriwa walipaswa kugeuka toka katika uovu na kumuelekea Mungu.

Hivyo basi toba ni tendo la imani la kurejesha roho ya mwamini iliyokuwa dhambini imuelekee MUNGU kwa njia ya maungamo kwa msaada wa Roho mtakatifu.

HATUA ZA MUHIMU KATIKA TOBA YA KWELI.

01.KUJUTIA DHAMBI NA KILA UOVU ULIOUFANYA.

~Toba ya kweli na yenye majibu ni ile toba yenye majuto ndani ya moyo wako.

~Kujutia dhambi ni ile hali ya kuumia moyo kwa sababu ya dhambi ulizozitenda. Ni pale ambapo unahukumiwa moyoni ya kwamba umefanya dhambi.

Daudi anasema;

“ Ee Mungu, unirehemu,Sawasawa na fadhili zako.Kiasi cha wingi wa rehema zako,Uyafute makosa yangu.Unioshe kabisa na uovu wangu,Unitakase dhambi zangu.Maana nimejua mimi makosa yanguNa dhambi yangu i mbele yangu daima.Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,Na kufanya maovu mbele za macho yako.Weweujulikane kuwa una haki unenapo,Na kuwa safi utoapo hukumu.” Zaburi 51:1-4

Hayo maneno yalikuwa ni majuto ya moyo,akiomba rehema kwa sababu ya dhambi iliyoumiza moyo wake.

Pia,twaweza kujifunza kwa habari ya Petro pale alipomkana Yesu,aliweza kutoka,kisha akajutia ile dhambi kwa machozi,imeandikwa;“Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.” Mathayo 26:75

Pia imeandikwa;

“Kwa maana nitaungama uovu wangu,Na kusikitika kwa dhambi zangu“Zab.38:18

02. KUZICHUKIA DHAMBI ZAKO ZOTE.

Ikumbukwe kwamba dhambi zote ziko sawa,hakuna dhambi ndogo wala dhambi kubwa. Yule aliyedanganya na yule aliyeua wote katika ziwa la moto. Hivyo basi huwezi kuchagua dhambi za kuchukia kisha nyingine ukazipenda na kuziona ndogo. Bali yakupasa kuzichukia dhambi zote,tunasoma;

“ Umependa haki, umechukia maasi;Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta,Mafuta ya shangwe kupita wenzio.” Waebrania 1: 9

Kumbuka dhambi ni uasi.

1 Yoh.3:4“Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” Hivyo katika Waebrania 1:9 ilipoandikwa “ umependa haki,umechukia maasi” neno “maasi ” linasimama kuwakilisha dhambi. Hivyo ni sawa na kusema“…,umechukia dhambi…”

Kumbe yakupasa kuzichukia dhambi zote ulizozifanya katika toba yako hapo ndiposa Mungu akupake mafuta ya shangwe kuliko wengine.

Pia soma Matendo 2:37-38.,hapa tunaona watu waliposikia lile neno wakachomwa mioyo yao,Petro akawaambia tubuni… kuchomwa moyo ni hali ya kuhuzunika,kukereketwa,kuchukia uovu~Walipomuuliza Petro na mitume wengine wafanyeje,wakaambiwa tubuni mkabatizwe.. Je wewe unapolisikia neno kama hili la toba,unachomwa moyo? Yakupasa uugue moyo,kisha uchukie dhambi na kutubu.

03.TUBIA DHAMBI ZAKO KWA KINA.

~Hatua hii ndio hatua ya kueleza dhambi zako kwa Mungu ili urehemewe. Ili toba yako iwe ni toba nzuri yenye majibu basi huna budi kupitia vipengele vifuatavyo;

(A) KUMSHUKURU MUNGU KWA FURSA YA TOBA.

Ukweli ni kwamba kutubu ni fursa ya kipekee maana wapo waliotamani waipate fursa hii ya toba lakini hawakuipata,wengine wameshakufa~ jiulize,Je wewe ni nani hata uipate? Je haikupasi kuanza toba kwa shukrani kwa nafasi hiyo uliyoipata ya kutengeneza na Mungu? Biblia inatuambia“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”1 Wathesalonike 5:18

Toba ni mapenzi ya Mungu kwako katika Kristo Yesukwamba usipotee dhambini maana Mungu hapendi mtu yeyote apotee bali afikirie toba.(2 Petro 3:9). Hivyo hii ni hatua ya kwanza katika toba yako,ni lazima uanze kwa shukrani.

(B) KUOMBA MSAADA WA ROHO MTAKATIFU.

Toba ni maombi,na maombi pasipo Roho mtakatifu sio maombi bali ni makelele. Kila jambo la kiroho ni lazima liongozwe na Roho mtakatifu maana sisi wenyewe hatuwezi kufanya jambo lolote lile pasipo kuongoza na Roho mtakatifu;

“ Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”Warumi 8:26 Hivyo baada ya kushukuru,anza kuomba msaada wa Roho mtakatifu ili akuongoze katika toba yako.

(C) KILI DHAMBI ZAKO ULIZOZIFANYA KATIKA KWELI YOTE.

~Hatua hii pia ni ya muhimu sana,yakupasa uweze kueleza mambo yako yote wazi wazi,wala usiifiche dhambi yako uwapo mbele za BWANA. Maana ujue Yeye Mungu anazijua dhambi zako zote,bali anataka ukili kwa moyo na kinywa ili akusamehe kabisa,Yeye Mungu akujua vyema kuketi kwako hata kuondoka kwako hivyo ziweke wazi dhambi zako zote upate rehema.

Biblia inasema ;“Nalikujulisha dhambi yangu,Wala sikuuficha upotovu wangu.Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.” Zab.32:5.

Shida ipo leo,wapo watu wenye kujihesabia haki hali ni wadhambi wa kutupa!!! Watu wa namna hii huyaficha maovu yao wakidhania ya kwamba wao ni wasafi mno,lakini tazama biblia inatuambia;

“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.” 1 Yoh.1:8-10

Yakupasa ukili kwa kinywa chako ya kwamba umemkosa Mungu kwa dhambi. Eleza dhambi zako zile unazozikumbuka,hata uombe rehema kwa zile ambazo huzikumbuki,eleza pia dhambi zile ulizozitenda kwa makusudi,na zile zote ulizozitenda kwa kutokujua yaani kwa bahati mbaya, eleza wazi wazi dhambi zote zilizotokana na kushindwa kutimiza wajibu wako.

(D) OMBA MSAMAHA WA KWELI.

Hapa ndipo mahali ambapo damu ya Yesu inahusika kusafisha dhambi. Ikumbukwe kwamba damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani ,ilimwagika kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi,imeandikwa“kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” Mathayo 26:28

~Katika toba yako ni lazima uihusishe damu ya Yesu ili ikusafishe. Damu ya Yesu hutakasa dhambi,damu ya Yesu huondoa dhambi,damu ya Yesu inaleta ukombozi na masamaha ya dhambi“ Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Waefeso 1:7

Hivyo kila atakayeiomba damu ya Yesu kwa kumaanisha ataipokea ili imuoshe dhambi zake,maana kila aombaye atapata…Mathayo 7:7

(E) KUKILI KUZIACHA DHAMBI.

“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Mithali 28:13

Kuacha dhambi ni kuzingatia moyoni kugeuka kutoka dhambini kwa kukataa kushiriki matendo yote ya mwilini kisha kumfuata Bwana Yesu. Matendo ya mwilini ndio haya;

“Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.“Wagaratia 5:19-21

hatuna budi kuyakataa matendo haya,ni machukizo mbele za Bwana Mungu. Haiwezekani ukaokoka lakini ukawa umejawa na matendo haya ya mwilini,ikiwa utaona kwamba ipo tabia moja wapo ya tendo la mwilini basi yakupsa uchukue hatua ya kutubia kwa kina tabia hiyo,ili ikuachie kabisa kabisa.

Tazama mfano mzuri wa mwana mpotevu alipokili kuiacha njia mbaya,biblia inasema;

“Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;” Luka 15:17-18

(F) KUSAMEHE WOTE WALIOKUKOSA.

Kanuni moja wapo ya kusamehewa dhambi zako,ni kuwasamehe watu wote makosa yao. Imeandikwa;

“ Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” Mathayo 6:14-15

Kusamehe watu waliokukosa ni kuwaachilia kutoka moyoni kwa msamaha wa dhati.

~Tazama leo hii wapo watu makanisani ambao wenye mizigo ya dhambi ya kutokusamehe,yaani wameshindwa kuwasamehe watu makosa yao,lakini papo hapo wanaomba rehema kwa Mungu. Yakupasa uwasamehe kwanza watu makosa yao.

Zakayo alipoijua siri hii,alimwambia Bwana Yesu;“…Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyanganya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Luka 19:8

(G) KUMSHUKURU MUNGU KWA MSAMAHA ULIOUPATA.

~Tendo la kushukuru,ni tendo la muhimu sana maana shukrani huwakilisha ya kwamba yale yote uliyoyaomba umeyapata na yamekuwa yako. Tazama mfano wa mfungwa anapoachiliwa huru kwa kusamehewa basi ni dhahiri mfungwa huyo atajawa na shukrani kwa Mungu wake na wale wote waliohusika kumuweka huru mbali na kifungo;

Hivyo ndivyo ukiwa ni mdhambi unakuwa kifungoni kuhukumia,lakini inakuwaje basi ikiwa utasamehewa hukumu hiyo? Je hutamshukuru Bwana Mungu wako? Hakika utamshukuru Bwans Mungu,na ndivyo ukimaliza kuomba toba yakupasa kushukuru ukiamini ya kwamba umesamehewa Bwana Yesu anasema ;“Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Mathayo 21:22

FAIDA ZA TOBA YA KWELI.

~Zipo faida nyingi zinazopatikana katika toba halisi. Nalionelea nikupe faida tatu tu kwa ufupi;

01. KUREJESHA SURA NA MFANO WA MUNGU NDANI YETU.

Kumbuka ya kwamba,dhambi inaondoa sura na mfano wa Mungu. Lakini kwa njia hii ya toba,ndio njia ya kipekee yenye kuleta ule mfanano uliokuwa umepotea, biblia inasema;

“ lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”Isaya 59:2

01. KUPOKEA UPONYAJI.

~Magonjwa mengi huletwa kwa sababu ya uwepo wa dhambi ndani ya mtu. Biblia inatuambia ya kwamba mmoja anaposamehewa magonjwa pia huponywa,imeandikwa ;“Akusamehe maovu yako yote,Akuponya magonjwa yako yote,Aukomboa uhai wako na kaburi,Akutia taji ya fadhili na rehema,” Zab. 103;3-4

02. KUPOKEA BARAKA.

Ipo mibaraka ya Mungu kwa yule aliyetubu na kuacha dhambi. Tazama mfano wa mwana mpotevu,biblia inasema akiwa mbali baba yake alimuona kisha baba yake akaenda kumlaki tena akapewa vitu ambavyo wala hakuomba kabisa,hiyo sasa ndio mibaraka yenyewe

Ana heri aziungamaye dhambi zake

“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”Mithali 28:13

Inawezekana fundisho hili limekugusa,na unahitaji maombi;tafadhili usisite kunipigia simu,piga sasa +255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.