TAFAKURI: HAKIKA WEMA NA FADHILI ZITANIFUATA SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU

Na Pastor Mdaki,
GK Guest Contributor.


ZAB. 23:6

Nimekuwa natafakari huu wimbo wa Daudi. Wimbo wa 23, na jinsi alivyoumalizia kwa kuapa! Anaimba HAKIKA wema na fadhili zitamfuata! Siyo yeye atazifuata, bali wema na fadhili zitamfuata. Tena huu wema na fadhili haumfuati siku moja tu, bali siku zote za maisha yake. Hadi kifo wema na fadhili kamwe hakuzitafuta, bali zilimfuata.

Huu wimbo ulinifanya nianze kutafakari maisha ya Mfalme Daudi.

Maisha yake hayaanzii jinsi alivyozaliwa! Maisha yake yanaanzia na kutengwa na babaye! Kutotambuliwa na nduguze, jamaa yake!

Samweli alipokuwa anaenda nyumbani kwa Yese kufanya ibada ya kumtia mafuta mtoto mmojawapo awe mfalme, Mzee Yese hakuona kama Daudi anafaa kuwa mfalme. Aliona Daudi ni mtu anaefaa kuwa na mikia ya ndama, mikia ya mbuzi, mikia ya kondoo. Ile ibada ilikuwa haimhusu Daudi hata kidogo. Aliona watoto wengine ndio wanaofaa lakini si Daudi.

Yawezekana hata wewe haushirikishwi kwenye mambo ya familia kama Daudi. Haushirikishwi kwenye mambo ya ofisini kama Daudi. Haushirikishwi kwenye mipango, umetengwa, wamekuona huwezi. Wanakupangia kwenye mikia kama Daudi. Wanakupangia vitu vya hovyo ovyo. Wamekuona hufai. Ndugu mpendwa usihofu, usiwe na shaka, wewe fanya! Nenda huko walikokutupa! Nakuhakikishia wema na fadhili zitakufuata huko huko. Zitakufuata huko huko kwenye mikia.

Kwani wale watoto ambao mzee Yese aliowaona wanafaa, mbele za Mungu hakuna hata mmoja aliyekuwa ana uwezo wa kubeba kusudi la Mungu. Hadi Samweli aliuliza wameisha watoto wako wote?

Ndipo yule mzee alipomwambia yupo mmoja huko porini anachunga mifugo yangu.

Samweli aliwaambia wazi, ibada haiendelei hadi huyo wa kwenye mifugo, huyo wa porini aletwe hapa.

Wao si wamesema hufai? Si wanasema hapo hutakiwi? Usihofu ndugu, nenda huko porini. Nenda huko kwenye mikia. Lakini nakwambia, kuna vitu haviwezi kuendelea hadi uwepo pale. Ibada zao zitasimama hadi uitwe. Shughuli zitakuwa si chochote hadi uwepo wako!

Ndugu, si wamekutenga kwenye mipango yao ya familia, si wamekutenga kwenye biashara, si wamekutenga ofisini kwako, si wamekuona hufai! Si wamekuona si chochote! Usiwe na haja ya kusema chochote na mtu, huko walikokuweka, we sema na Mungu wako tu!

Hao walikukataa, leo ndo nafasi yako. Hao waliokutenga, hakifanyiki kitu hadi uwepo. Hao wasiokushirikisha, leo wataona aibu wao!

Usihofu, hakuna atakaeweza kuchukua nafasi yako. Kazi yako ipo tu. Subiri wema na fadhili za Mungu, zinakufuata huko uliko

Samweli alipomuona Daudi anakaribia kwenye ibada, akatambua huyu ndiye! Samweli akamtia mafuta Daudi awe mfalme wa Israeli, yule waliemtenga kwenye ibada!

Cha ajabu Daudi alipotiwa mafuta awe mfalme, hakukimbilia ikulu; bali alirudi porini tena akiendelea kutunga nyimbo na ndama wake!

Daudi hakuwa na watu wa kupiga nae stori. Yeye na ndama, mbuzi, kondoo ndo walikuwa marafiki zake! Hakuwa na rafiki wa kufarijiana naye kule porini zaidi ya wanyama. Kumbe ndo maana alijifunza kusifu Mungu kule porini. Alijifunza kunyenyekea kama kondoo! Ndo maana aliwatetea sana wanyama kwa sababu ndo walikuwa marafiki zake! Alipambana na Simba, hata Dubu ili mnyama asife! Pamoja na kupakwa mafuta, Daudi haendi ikulu anarudi kwa marafiki zake, wanyama.

Tukio la pili ni la vita! Vita kati ya Wafilisti na Waisraeli. Yese tena haoni kama Daudi anafaa kuwepo vitani! Yese anapeleka watoto wengine, anamuacha Daudi. Maana Daudi hafai.

Siku kaka zake wakaishiwa mkate. Daudi anatumwa kupeleka mkate kwa ndugu zake walioko vitani! Anapofika kule anakutana na ndugu zake. Daudi anaulizia habari za vita! Jibu la ndugu zake lilikuwa la kumuondoa kule vitani. Kaka yake anamuuliza Daudi, ,"wale ndama umewaacha na nani?"

Ndugu, wewe si wa kwanza kufukuzwa kwenye nafasi yako. Pia kutokusikilizwa wewe, si mtu wa kwanza. Yawezekana ndugu wamekataa kukusikiliza, achana nao! Songa mbele. Wazazi hawataki kukusikiliza, usikae nao vikao, we songa mbele! Yawezekana hata wakwe hawataki kukusikiliza, usiwe na haja na vikao na hao watu! Watakupotezea muda, songa mbele. yawezekana ofisini kwako wamekuona hufai wewe songa mbele ng'anga'nia msalaba. Biashara, familia, ndoa yako; hivi vyote visikupotezee muda. Usipoteze muda kwa ajili ya maridhiano! Achana nao, songa mbele! Wema na fadhili za Mungu zitakufuata!

Daudi alipoona ndugu wamekataa kumsikiliza, aliuliza watu wengine! Alienda kupata habari kwa watu wangine! Aliweka vikao na watu wengine! Wale watu wengine wakampasha habari Daudi juu ya ugumu wa ile vita. Namna Mfilisti Goliati alivyowatukana Waisraeli na Mungu wao. Na alikuwa anafanya hivyo asubuhi na jiioni. Goliath alikuwa anataka mtu wa kupambana naye.

Alipotaka kujua juu ya upande wao! Walimwambia wazi wanaogopa. Wakamsimulia wasifu wa Goliati jinsi ulivyo! Kisha wakampa "live" hakuna wa kupambana naye.

Daudi akakumbuka vita yake na simba. Akakumbuka vita yake na Dubu kule porini. Hakuangalia tena yale mazingira aliyokuwa nayo bali alimwangalia Mungu aliyemuokoa na simba. Daudi hakuangalia watu wa kumsaidia, bali alimtazama Mungu aliyemshindia kwa Dubu kule porini. Daudi alikuwa peke yake kule porini wakati simba wanavamia wanyama. Alikuwa peke yake kule porini wakati dubu wanavamia wanyama.

Baada ya tafakari ile, Daudi akasema nitakwenda. Tatizo sisi huwa tunatafakari uwezo tulio nao badala ya kutafakari uwezo wa Mungu. Tunaangalia mazingira, na watu wanautuzunguka na sheria za duniani badala ya kumwangalia Mungu. Leo badili mtatazamo wako. Mwangalie Mungu, usiangalie wanadamu. Tazama msalaba wa Kalvari, usitazame uwezo wako. Msalabani ndiko kwenye ushindi.

Daudi akawaambia wale watu juu ya dhamira yake ya kupambana na Goliati. Kisha wale watu wakamwambia zawadi ya mfalme aliyotangaza. Daudi hakuangalia ile zawadi bali alitafakari wema na fadhili za Mungu zinazo mfuata. Wale watu wakampeleka Daudi kwa mfalme Sauli. Basi wakampasha Goliati yakuwa yupo mtu wa kukabiliana naye. Wakati Goliati kule anajiandaa na pambano, huku upande wa Daudi anamsifu Mungu, Bwana wa majeshi kwa chorus hii; "jeshi lijapojipanga kupigana nami, moyo wangu hautaogopa."

Acha wakae vikao vya kukuharibia, we mtukuze Mungu tu. Wakati wao wa kutambua wewe umeuwa makumi elfu umefika sasa! Wakati wa wao kukushangilia, umefika sasa. Acha wajipange, wao watafadhaika kwa aibu.

Baada ya Daudi kuwa tayari, mfalme alivua mavazi yake ya kijeshi na kumvika Daudi. Daudi alipoyajaribu yale mavazi, alisema haya mavazi siyawezi na sikuzoea. Siko tayari kutumia. Acha kutumia staili ya wenzako. Acha kuiga wanavyofanya walimwengu. Nenda na mbinu ambazo Bwana huwa anakushindia

Wakati ukafika wa kwenda kupambana na Goliati. Yule anaewatukana majeshi ya Bwana. Yule aliyezuia sanduku la agano. Wakati ni sasa wa kupambana naye.

Goliati anakuja na mavazi ya chuma, mkuki, tena na mtu wa kumshikia ngao. Lakini Daudi anaenda na jina la Bwana! Hana silaha nyingine zaidi ya jina la Bwana. Mungu ndiye ngao yake. Hana msaidizi wa kumshikia ngao. Tangazo la Daudi liko hivi; "wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi unaemtukana.

Anza kukiri sasa jina la Bwana juu ya vita yako! Nenda kwa jina la Bwana juu ya tatizo lako. Wakati wa ushindi ndio huu, nenda kwa jina la YESU.

Baada ya Goliati kupigwa na kuanguka, yawezekana ndugu zake hawakuamini! Hawakusadiki kilichotokea, lakini ukweli Goliati yuko chini. Daudi akamkimbilia Goliati, akasimama juu yake. Daudi hana upanga! Upanga ule uliokuwa autumie Goliati kwa kumuulia Daudi; Daudi aliutumia kumuulia Goliati.

Usihofu adui zako! Zile silaha walizopanga kukumaliza, zitawamaliza wao! Lile shimo walilokuchimbia, watatumbukia wao! Ule mti ulio tayari kwa ajili ya kukutundikia, watatundikiwa wao! Ule moto walioundaa kwa ajili ya kukuteketeza, watateketezwa wao! Panga la kumuulia Daudi, Daudi alilitumia kumuulia Goliati.

"Hakika wema na fadhili zitanifuata, siku zote za Maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele".

NAKUTAKIA TAFAKARI YA USHINDI.
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.