2016 NI MWAKA WENYE TIJA

Na Askofu Sylvester Gamanywa
WAPO Mission International.



Leo natabiri kwamba mwaka 2016 ni mwaka wenye tija! Utaniuliza nimejuaje? Kama wewe huamini subiri uone kwa macho ila tu kwako binafsi, kwa kutokuamini kwako, hautakuwa na tija kwa sababu utakuwa umepoteza muda wako ukisibiri kuona ni jinsi gani huu ni mwaka wenye tija. Tafsiri ya Kiswahili sanifu kuhunu neno “tija” maana yake ni “matokeo mazuri yenye faida.”! Unajua kwamba kuna mambo mengi yanayofanyika, tena yanatumia gharama kubwa, lakini hayaleti “matokeo mazuri yenye faida.”

Muda ni kwa ajili ya binadamu na
sio binadamu kwa ajili ya muda

Kumbuka tunaposema habari za mwaka tuna maana ya “kipindi cha miezi kumi na mbili, kuanzia Januari mpaka Desemba.” Hiki ni kipindi cha matumizi ya muda. Kwa asili muda ni “amana” yaani kitu cha thamani kubwa. Muda ukipangwa na kutumiwa vizuri, kuanzia Januari mpaka kuja kufika Desemba lazima utaleta “matokeo mazuri yenye faida.”

Kwa mantiki hii, muda umetolewa kwa ajili ya kumwezesha binadamu kutimiza kusudi la Mungu la kumleta duniani. Binadamu hakuumbwa kwa ajili ya kutumikia muda. Muda umewekwa kwa ajili ya binadamu kulitumikia kusudi la Mungu.

Sasa hebu nikushirikishe ni kwa jinsi gani mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wenye tija. Naomba turejee kwenye kitabu cha kwanza katika Biblia, sura ya kwanza ili tuone chimbuko la kile kinachoitwa “Baraza za Mwenyezi Mungu” kwa binadamu wa kwanza kama ilivyoandikwa:

Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi….” (MW.1:28)

Katika maandiko haya naomba tuchukue haya maneno 3 ambayo ni 1. Zaeni, 2. Mkaongezeke, 3. Mkaijaze nchi na kuitiisha. Kila neno hapa liana uzito wake maalum na ni muhimu tuuzingatie ili kuweza kujua kuna ujumbe gani.

1.    Zaeni- kanuni ya ubunifu na uzalishaji

Wengi wana tafsiri ya binadamu kuzaana wenyewe kwa wenyewe. Hii ni tafsiri finyu sana. Kimsingi neno zaeni linawakilisha kanuni ya “ubunifu na uzalishaji”! Mungu alipowatamkia mbaraka binadamu wa kwanza, aliwatabiria kuhakikisha kazi ya uumbaji wa viumbe na uzalishaji wa mimea na mifugo vinaendelea kufanyika pasipo kuhusisha mkono wa Mungu moja kwa moja.

2.    Mkaongezeke – kanuni ya kuongezeka

Haya kanuni ya ubinufu na uzalishaji unahusika kwenye kupata wazo jipya la kufanya kitu kipya na kulifanyia kazi ili kuleta hicho kitu kipya kwenye ulimwmengu wa asili. Lakini kanuni ya kuongezeka inahusika zaidi na kile kinachotumika katika kuzalisha kisizalishe vichache bali kitumie kanuni ya kuzidisha kwenye uzalishaji. Maana yake ukipanda mbegu moja ardhini, itakapoota na kuzaa zipatikane mbegu kama ile iliyopandwa zikiwa nyingi hata mara mia moja. Kama ulifunga mbuzi au ng’ombe au kuku wakati wanapozaa, wazae zaidi ya mmoja na katika muda mfupi, idadi yao iongozeke kwa kanuni ya kuzidisha na sio kujumlisha.



3.    Kujaza nchi na kuitawala – Kanuni ya kumiliki

Kujaza nchi na kuitiisha na kutawala yote yanawakilisha mamlaka ya kumiliki ardhi na mali. Kumiliki ndiko kunakotimiza kusudi la Mungu kumuumba binadamu la “kutawala”! Kumbuka kwamba kanuni ya kutawala inalenga kutawala viumbe hai, ardhi na mazingira yake, lakini sio “kumtawala binadamu”! Pili, kila binadamu alikuwa na fursa hii ya kuzalisha na kuzidisha na “kumiliki uchumi” kama sehemu ya Mbaraka wa Mungu kwa binadamu. Suala la binadamu kumtawala binadamu mwenzake ni matokeo ya anguko la bunadamu katika dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.

Kupitia uchambuzi uliotangulia hapa juu, tunapata picha kwamba, Baraka za Mungu kwa binadamu hazikutarajiwa kumfikia akiwa amelala bustanini bali alitakiwa kufanya kazi maalum. Ubunifu wa kupata wazo jipya na kulitendea kazi liwe kitu halisi hii ni kazi. Kusimamia mchakato wa uzalishaji unaoongezeka nayo ni kazi. Hata kukusanya na kusimamia milki nayo pia ni kazi. Hakuna mahali mtu atakaa abweteke halafu mambo yanajiendesha yenyewe pasipo ushiriki wake.

Imani na uchumi
havitenganishwi

Lakini jambo jingine la kujikumbusha hapa ni kwamba, Kusudi la Mungu kumwumba binadamu ni kutawala nchi kwa kwa niaba ya Mungu. Na utawala uliotajwa ni wa viumbe, ardhi na mazingira yake. Maana yake “kutawala matunda ya uchumi” unaotokana na rasrimali asilia za Mungu mwenyewe. Na hii ndiyo inatuleka kwenye kipengele kingine muhimu kinachogusa “Imani na uchumi havitenganishwi”!

Sijui ni nani mwasisi wa kitheolojia aliyeanzisha nadharia ya kutenganisha “imani na uchumi” katika dini ya Kikristo. Utafiti wangu katika Biblia kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka ufunuo, sina kifungu wala andiko linalotenganisha “imani na uchumi”! Labda nifafanue ni nini ninacho maanisha kuhusu “imani na uchumi”.

Imani ni uhusiano binafsi kati ya binadamu na Mungu. Ni mfumo wa maisha yanayotegemea uongozi na Baraka za zitokazo kwa Mungu. Pamoja na dhana ya “kuishi duniani kwa kujilinda na vishawishi hatarishi vya kidunia” ikilenga kwamba Ibilisi hutumia fedha na mali za duniani kumtenganisha binadamu na Mungu kimahusiano; hiyo haina maana kwamba, binadamu anayemtegemea na kumwamini Mungu aache/ajitenge/asijihusishe na utafutaji na umilikaji wa mali pindi angalipo hapa duniani.

Hii ni kutokana na jinsi binadamu mwenyewe alivyoumbwa na Mungu. Suala la kumiliki mali ni la kimaumbile. Ni kama suala la ndoa. Ni la kimaumbile. Mungu amepiga marufuku matumizi ya tendo la ndoa kabla nan je ya ndoa lakini Mungu anatarajia binadamu kuoana kwa halali kwa sababu ni jambo la kimaumbile. Hali kadhalika na kumili uchumi. Mungu anamtarajia binadamu amtegemee, yaani atumie “imani yake kwa Mungu” kuanzia kubuni, kuzalisha, kuzidisha mali na kumiliki mali, na kuhakikisha anazitumia kwa ajili ya ufalme wa Mungu hapa duniani!

Kwa hiyo, mwaka huu 2016 ni fursa nyingine kwa kila binadamu anayemcha Mungu kutumia imani yake kwa Mungu kupokea na kutunza Baraka za kiuchumi kwa ajili ya ufalme wa Mungu hapa duniani. Mbaraka wa Mungu alioutamka kwa binadamu wa kwanza ulikuja kurejewa na Yesu Kristo pale aliposema “Tafute kwanza ufalme na hayo yote mtazidishiwa….” (MT.6:33) pamoja na “atapata mara mia katika ulimwengu huu wa sasa…” (MK.10:30)

Heri na Baraka za mwaka mpya kwa wote
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.