HOJA: BARAKA ZA KIUCHUMI ZIMEJENGWA JUU YA ARDHI

Askofu Sylvester Gamanywa,
WAPO Mission International.


Tumekuwa na utamaduni wa kuomba na kuamini kupokea Baraka za kiuchumi kutoka kwa Mungu kwa njia ya imani. Lakini tumejijenga upande mmoja na kusahau au kuacha upande wa pili ambao majibu ya maombi yetu hayawezi kuwa halisi kama tusipofanya maandalizi yake. Uchumi katika maana yake halisi hata kama unaanza kwa imani lakini lazima kilele chake ni kuonekana kwa macho. Na kuonekana kwa macho lazima kunahusisha ardhi:

Ardhi ndio msingi wa
Baraka za kiuchumi duniani

Maisha ya kila siku yanafanyikia duniani. Duniani maana yake kwenye ardhi. Kila kitu ulichonacho au shughuli unayofanya inategemea ardhi. Tumeamka pamoja alfajiri tukuwa wapi? Kwenye ardhi. Nyumba na chumba ulimolala leo kipo juu ya ardhi. Unapokwenda leo iwe shuleni, kazini, kwenye ujasiriamali popote ulipo unafanyikia kwenye ardhi.

Kama wewe huna ardhi unayomiliki inayohusiana na shughuli zako, unajua kabisa kwamba sehemu ya mapato yako itakuwa ni kulipia pango za nyumba kuanzia kuishi na sehemu ya biashara. Lakini kama unamiliki ardhi yako ambayo ina nyumba yako ya kuishi au shughulii yoyote ya uzalishaji au unapangisha utaiona ardhi ilikuwa ni sehemu ya mapato yako badala ya kuwa matumizi ya mapato yako.

Kana kwamba hii haitoshi, Yesu Kristo mwenyewe ameitaja ardhi na kuitumia katika mafundisho yake. Lakini zaidi pamoja na mafundisho yake pia aliagiza kufanyika kwa mabadiliko ya kimfumo kuhusu suala zima la uchumi na imani. Yesu aliweka vigezo vya kustahili kuwa wanafunzi wake akiwaamuru wampe yeye Nafasi ya kwanza mioyoni mwao kabla ya jamaa na vitu wanavyovithamini.

Katika Luka 14:26-27; Yesu Aliamuru yeye kuwa kwanza kabla ya wazazi, ndugu na jamaa katika familia.  Katika Luka 14:33; Yesu aliweka msimamo kwamba asiyeweza kumtaguliza Kristo kuliko jamaa na mali hafai kuwa mwanafunzi wake:

Lakini upande wa pili wa sarafu kuhusu mabadiliko ya kimfumo, Yesu alitoa ahadi kwa wale watakaokidhi vigezo vya kuwa wanafunzi wake kwamba kumpa Nafasi ya kwanza, hawatakuwa wakiwa au mafukara. Katika Mathayo 19:29 na Marko 10:29 Yesu anataja walioacha nyumba na mashamba watapata mali hizo mara mia katika ulimwengu huu wa sasa!

Ukitafakari Baraka za kiuchumii alizoamuru Yesu kwa wanafunzi wake zote zinahusiana na ardhi! Mashamba hulimwa kwenye ardhi na nyumba hujengwa kwenye ardhi. Ujumbe wa leo ni kwamba maandalizi ya Baraka zako za kiuchumi lazima yaanze na kumiliki kipannde cha ardhi. Hii ni wajibu wako na haihitaji muujiza.

Kuna mambo Yesu alisema tuombe lakini kuna vingine alisema tutafute. Kimojawapo cha kutafuta ni Ardhi. Kama unacho kipande tayari, basi ongeza kingine. Kama hauna anza sasa kutafuta mpaka upate. Ni muhimu kwa Baraka zako za kiuchumi.

Jinsi mitume walivyotekeleza
mchakato wa uchumi na imani

Maagizo mengi yaliyotolewa na Yesu, Mitume wake walianza kuyatekeleza tangu siku ya Pentekoste pale aliposhuka Roho Mtakatifu. Moja wapo ya utaratibu wa utekelezaji wa maagizo ya Yesu ni kujenga mifumo maalum. Mojawapo ya mifumo hiyo ni “MFUMO WA VIKUNDI VYA NYUMBA KWA NYUMBA.”

“Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,…” (Mdo.2:46)

Huu ulikuwa ni mfumo ambao uliwafanya maelfu ya  waamini kujenga uhusiano wa karibu na Mungu lakini pia uhusiano wa karibu miongoni mwao.

Kila kikundi kilikuwa na nyumba ambayo ilitumika kwa ajili ya mikutano yote kuanzia ibada, maombi, mpaka masuala ya kijamii na kiuchumi. HAWAKUTENGANISHA IMANI NA UCHUMI. Ndiyo maana utakuta imeandikwa waziwazi kwamba, mali zao za viwanja, nyumba na mashamba vilitumika katika kuwezeshana kiuchumi, na hivi ndivyo walivyotekeleza maagizo waliyokabidhia na Yesu:

“Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadri alivyohitaji.” (Mdo.4:34)

“Na Yusufu aliyeitwa na mitume Barnaba (maana yake, Mwana wa faraja) Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.” (Mdo.4:36-37)

Mpendwa msomaji, hapa tunasoma habari za kanisa la kwanza la mitume ambalo Yesu alitabiri kwamba atalijenga na milango ya kuzima haitalishinda. Mitume walijenga msingi wa uchumi endelevu ambao ulitegemea mtandao wa vikundi vya nyumba kwa nyumba na huduma za kiroho na kiuchumi vyote vilienda sambamba.

Changamoto za kanisa
la leo na ufumbuzi wake

Tumeshajionea kwamba Yesu Kristo aliwaachia wanafunzi wake mabadiliko ya kimfumo kwa habari za uchumi na imani akitaka kipaumbele kiwe ni Yeye kwanza na familia na mali vishike nafasi ya pili. Pili, alitoa ahadi ya Baraka za kiuchumi ambazo alitamka waziwazi kuwa watafanikiwa kiuchimi mara mia

Piatumejifunza jinsi ambavyo mitume wa Kristo walivyoyatekeleza mabadiliko ya kimfumo kuhusu uchumi na imani kwa kujenga mfumo wa mtandao wa vikundi vya nyumba kwa nyumba ambamo masuala ya uchumi na imani vilisimamiwa kikamilifu na matokeo yake kanisa la kwanza lilikuwa na kuongozeka kiimani, kiroho na kiuchumi hata likawa tishio kwa madhehebu ya dini ya kiyahudi yaliyokuwepo kabla yake.

“Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadri alivyohitaji.” (Mdo.4:34)

“Na kwa mikono ya mitume zikafanyika isharaa na maajabu mengi katika watu; ….na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; waliaomini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaue na wanawake…” (Mdo.5:12-14)
Tatizo kubwa la kanisa la leo ni dhana potofu ya kutenganisha Uchumi na Imani. Tafsiri ya jumla ni kutafsiri kwamba mambo ya uchumi ni ya kidunia na kimwili na Imani ni mambo ya kiroho ambayo yanajitegemea na hayatakiwi kuchanganywa na mambo ya uchumi. Ikiwa Yesu na Mitume wake hawakutenganisha uchumi na imani, sisi tumeipata wapi hii dhana ya kutenganisha uchumi na imani?

Athari za “kutenganisha uchumi na imani” ni pamoja na kuwafanya waamini wakiuke kanuni za unafunzi kwa Kristo ambaye aliagiza kushika nafasi ya kwanza kuliko vyote: Waamini wakitenganisha uchumi na imani, wanageuka kuwa ndio wamiliki wa uchumi na waamuzi wa mwisho badala ya Kristo. Tayari kwa mujibu wa Yesu wanapoteza sifa ya kwa wanafunzi wake

Athari ya pili ya “kutenganisha uchumi na imani” waamini hawawezi kukua kiimani kwa sababu muda mwingi wanautumia kwenye uchumi tangu asubuhi hadi jioni, jumatatu mpaka Jumamosi. Na shughuli wanazozifanya hazijajengwa kwenye maadili ya kiimani kwa hiyo wanaishi maisha ya mchanganyo.

Athari ya tatu inaliathiri kanisa kihuduma kwa kushindwa kuhubiri injili kwa upana kwa sababu halina nguvu za kiuchumi. Linaendesha huduma zake kutegemea matoleo ya waamini ambao naoo hawatoi kwa viwango kwa sababu wametenganisha uchumi na imani. Mpaka mara nyingine uongozi unalazimika ama kutumia vitisho vya matoleo au kutumia ulaghai kwa kuwaahidi watu kubarikiwa kwa kutoa lakini Baraka zenye hazionekani kama zinavyoahidiwa. Matokeo yake waamini wanapoteza imani na kurudi nyuma.

Ufumbuzi ulioko sasa, ni kurejea kwenye misingi ya iliyojengwa na mitume wa kanisa la kwanza. Kanisa lazima libebe jukumu la kuelimisha na kuhamasisha na hata kuwezesha waamini wake kumililiki ardhi na kuitumia kwa njia za uzalishaji wa mitandao ya vikundi kama ilivyokuwa katika kanisa la kwanza.

Vikundi vya kiuchumi vikianzishwa wajibu wa kanisa ni kufundisha maadili ya kiimani na kuhakikisha sehemu ya mapato inakuja kwenye huduma za kiinjili kama kanisa la kwanza. Hapo ndipo Injili itahubiriwa kwa kishindo, na waamini watainuka kiuchumi, na jamii itajua kuwa hili ndilo kanisa la Kristo Mfalme wa wafalme mbinguni na duniani.  

(mwisho)


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.