HOJA: MAOMBI NA CHANGAMOTO ZAKE

Askofu Sylvester Gamanywa,
WAPO Mission International.

©Daily Prayer US
Kama ilivyo kawaida katika mwanzo wa mwaka mpya, suala la maombi lazima lipewe kipaumbele kwa kila mwamini kwa sababu Ukristo umesimama katika maombi na Neno la Kristo. Leo nataka kudokeza vipengele muhimu juu ya dhana nzima kuhusu maombi. Biblia imeandika taarifa kuhusu maombi zaidi ya mara 138. AK mara 78 na AJ mara 53 na Yesu mwenye ametaja neno maombi mara 15 katika AJ. Pamoja na ushahidi wa kimaandiko katika Biblia lakini uzoefu unaonesha Maombi yana changamoto nyingi na baadhi yake nitazijadili  katika hoja hii. Nitawasilisha kwa mtindo wa maswali na majibu:

Kwanini kuomba ni lazima?

Kuna sababu nyingi za kibiblia lakini nizitaje 2 muhimu kwa mujibu wa somo la leo. Sababu ya kwanza ni “Agizo la Mungu la kuwasiliana na yeye” kwa ajili ya kudumisha ushirika na Mungu. Hili ndilo kusudi la msingi la kumuumba binadamu. Kuwa na ushirika naye. Hakuna ushirika pasipo mawasiliano.

Kabla ya anguko la binadamu wa kwanza, Mungu alikuwa na kanuni ya kukutana na alasiri na Adamu na Eva na kuzungumuza nao. Itakumbukwa pia siku binadamu alipoanguka dhambini bado Mungu alimfuata wakafanya mawasiliano. Kitabu cha Mwanzo sura nzima ya tatu inaonesha mawasiliano ya mwisho kati ya Mungu na binadamu kabla ya kufukuzwa kutoka Bustani ya Edeni

Sababu ya pili kwanini kuomba ni lazima ni “Binadamu kumtegemea Mungu 100%”! Kwa asili binadamu aliumbwa kufanya mambo yote kwa uongozi wa Mungu na sio kujifanyia maamuzi yake kivyake vyake. Mungu anataka tumtegemee yeye kwa kila jambo, liwe kubwa au dogo.

Na njia pekee ya kumwonyesha kwamba tunamtegemea ni sala. Kumshirikisha, kutafuta kujua mapenzi yake ni nini, kufanya maamuzi yatokanayo na maagizo yake, yote yanaashiria “kumtegemea Mungu 100%.

Tunajifunza ukweli huu kutoka kwa Yesu mwenyewe ambaye hakufanya jambo lolote ambalo hakuagizwa na Baba yake. Ndiyo maana kila mara alikuwa na vipindi vyake vya kuomba akiwasiliana na Baba yake kwa ajili ya kudumisha USHIRIKA PAMOJA NAYE na pia kwa ajili ya KUTAFUTA UONGOZI WA BABA 100% kwa utumishi wake duniani.

Na ndiyo maana akawaagiza wanafunzi wake kuendelea tabia ya maombi kwa sababu ni kwa njia hiyo hiyo wangedumisha USHIRIKA pamoja naye akiwa mbinguni na pia kupata uongozi wake kwa ajili ya utumishi.

Mwisho kabisa ndiyo maana alimtuma Roho Mtakatifu aje kufanya makazi ndani yao pamoja na wote watakaompokea Yesu kupitia injili yao; ili zoezi la kuwasiliana na Mungu liwe endelevu na lenye tija.

Kwanini kuomba ni kitu
kigumu kwa wengi?

Pamoja na kwamba, maombi ni muhimu sana kwa kila mwamini anayemfuata Yesu Kristo, pamona kwamba kila mtu angependa kuwasiliana na Mungu mara kwa mara ili kujenga uhusiano imara na Kristo; ni jambo la kushangaza sana kuona kwamba “kuomba” kimmekuwa kitu kigumu kutekelezeka kwa walio wengi.

Sala nyingi zinanzofanyika ni zile ambazo hazina tija na za maigizo tu ya kukariri ili kuridhisha nafsi kwamba ni ibada. Lakini hazina matokeo yoyote na wanaosali hata kama naafsi zao kwa ndani zinapenda lakini uhalisia ni kuwa hawajisikii kuwa na uhusiano wowote wa karibu na Mungu.

Haya, hivi ni kwanini kuomba ni kitu kigumu namna hii? Imenichukua muda mrefu kutafakari, nikianza na changamoto ninazopambana nazo mimi mwenyewe katika zoezi hili la kiroho, na kasha kujifunza kwa wakristo wenzangu wengine, hasa wale walionitangulia katika mambo ya imani na utumishi huu. Bado nimegundua kwamba, hakuna bingwa wa kujibu swali hili kwa ujasiri.

Ni kutokana na uzito, au unyeti wa changamoto hii ya “kushindwa kuomba” wakati hii ndiyo njia pekee ya kufanikiwa kiroho na kimaisha. Majibu yangu yaweza yasiwe ndio mwisho wa yote; lakini nina imani yatasaidia kuutafakari ukweli kwa jicho la maandiko matakatifu na bila shaka ufumbuzi ukaanzia hapo.

Kuna vikwazo vikubwa viwili vinavyokwamisha waamini kumwomba Mungu. Cha kwanza ni “Udhaifu wa mwili”! Hii ni kwa mujibu wa Yesu Kristo alipowaambia wanafunzi wake akisema: “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (MT.26:41)

Kumbuka kisa cha wanafunzi kushindwa kuomba pamoja na Yesu, wakazidiwa na usingizi wakalala badala ya kukesha wakiomba. Mara tatu Yesu alikuwa akija kuwaamsha ili waombe na akiondoka wanalala usingizi.

Yesu akasema, “mwili ni dhaifu”! Tendo la kuomba ni la kiroho. Na roho ya binadamu ambaye asili yake ni kutoka kwa MUngu ndiyo ina shauku ya kuomba. Lakini mwili asili yake ni udongo hautaki mambo ya kiroho. Ndiyo maana umekataliwa kwamba “hautaingia mbinguni” Kwa hiyo. Mwili unatumiwa sana na nguvu za Ibilisi kuleta mgomo dhidi ya tendo la kuomba.

Ufumbuzi wa tatizo hili, ni zoezi la kujikana kweli kweli na kuutiisha mwili ukubali kutumika kuomba, Maana kimaumbile roho zetu haziwezi kuomba pasipo mwili kushiriki kwa sababu wenyewe ndio umeshikilia mifumo ya mawasiliano. Kwa hiyo, tujue kwamba, kamwe mwili kwa asili hauwezi kutuhamasisha sisi kuomba, wala haupendi sisi tuombe, kwa sababu wenyewe hauna faida na hayo yajayo katika ulimwengu wa roho.

Kikwazo kingine kinachozuia wengi kutokuomba ni “kutokujua kuomba ipasavyo”! Hii tunafundishwa na Mtume Paulo pale alipowaandikia warumi akisema: “ Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” (Rum.8:26)

Hapa kuna mchanganyiko wa mambo mengi yenye kuhitaji maelezo ya kina. Kwanza tunaona habari ya msamiati wa “udhaifu wetu”….. tunao udhaifu wetu katika suala la kuomba, na udhaifu wenyewe ni kuwa “hatujui kuomba itupasavyo…” Maana yake tunatumia akili na hisia zetu kuomba vitu ambavyo sio kipaumbele kwa Mungu, au tunaomba huku tumeathiriwa na shida na matatizo au masukosuko au msongo wa mawazo na kudhani kwamba hayo ndiyo mahitaji yetu mbele za Mungu.

Yote hayo ni “udhaifu wa kutokujua kuomba itupasavyo” Sasa ufumbuzi wa tatizo hili ndiyo maana Yesu akamruhusu Roho Mtakatifu ashuke na kufanya makazi ndani yetu ili yeye ndiye ashike hatamu za kuomba kwa niaba yetu.

Nafasi ya imani katika maombi

“Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” (MK.11:24)

Haya tayari tumejifunza umuhimu wa maombi na vikwazo vyake na hapa nataka tujifunze kuhusu nafasi ya imani katika maombi. Tukichukulia mfano wa kibinadamu tu ambapo mtu anaondoka kwenda kukopa fedha kwa mtu mwingine. Sasa mpaka hapa baadhi yetu tunanweza kuw hatujui kwamba, mpaka mtu achukue hatua ya kumwendea mtu, “tayari amekwisha kumwamini mtu huyo moyoni kwamba, anazo fedha na kwamba atakubali kumkopesha tu.” 

Na sababu za kumwamini zaweza kuwa ni uwezo wa kifedha aliona nao mhusika, na uhusiano wa karibu walio nao baina yao.

Na hata ikitokea mtu akakosa kupata mkopo kutoka kwa huyo mtazamo wake juu ya mtu huyo haubadiliki. Anajua ameamua kutokumkopesha tu amekataa au amemnyima nk. Lakini haamini kwamba hana uwezo na kwamba hawana mahusiano mabaya kiasi cha kumtokubali kumkopesha.

Mpendwa msikilizaji, kama waamini tungefanikiwa kumwamini Mungu angalau kwa kiwango hiki kila tunapoamua kumpelekea mahitaji yetu, bila shaka tungepata mrejesho wa kushangaza kutoka kwa Mungu!

Hivi unajua kwamba “Imani ni mtazamo na nia juu ya Mungu” Mungu anasema kwamba “kila amwendeaye yeye lazima aamini kwamba yuko, na kwamba huwapa thawabu wamtafuato.” (HBR.11:6)

Wengine wetu tunapomwendea Mungu huwa hatuna uhakika 100% kwamba tutapata yale tunayokwenda kumwomba. Tunahisi kwamba, yeye ni mkali sana mtakatifu sana kiasi kwamba hata kutusikiliza hajali hasa tunapokuwa tumemkosea kwenye mambo Fulani Fulani. Mtazamo wa jinsi hii unatufanya tuwe na picha tofauti na Mungu alivyo kwetu!

Mungu kwetu ni Baba na ni zaidi ya baba wa kidunia. Amekwisha kuweka kila hitaji letu sawa sawa na anachosubiri ni sisi wenyewe kumwendea kwa shauku tukijua kwamba yeye ni mwaminifu kwa ahadi zake na kamwe hawezi kutuangusha. Ni kufuru kumwamini binadamu kuliko Mungu.

Mwisho.
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.