HOJA: TOFAUTI KATI YA AJIRA NA KAZI

Na Askofu Sylvester Gamanywa,
WAPO Mission International.
Toleo la wiki hii nimekusudia kufafanua misamiati ya maneno kati ya “ajira’ na “kazi” ili kuweza kuweka bayana njia bora ya kuinua uchumi binafsi na taifa kwa jumla. Nina hakika ukisoma ukiwa na mtazamo chanya utapata picha nzima ya ni wapi uelekeze dua na nguzu zako kwa habari ya kupanua uchumi wako:

Tafsiri ya maneno
 ya ajira na kazi

Tafsiri ya neno ajira maana yake ni: “Kazi zitolewazo au zifanywazo kwa malipo katika serikali, kampuni au kwa mtu binafsi.” Ajiri “kumpa mtu kazi kwa ujira au mshahara” Tafsiri ya neno kazi maana yake ni: “shughuli anayofanya mtu km kulima, kuandika au kufundisha.”

Kwa tafsiri fupi tumepata picha kwamba “Ajira” na “kazi” ni vitu viwili tofauti. “Ajira” ni “kufanya kazi ya mwingine kwa malipo”! Ni kufanya kazi ya mwingine kwa mkataba unaoweka bayana majukumu ya kufanya na malipo stahiki kwa majukumu hayo.  Lakini “kazi” ni “kufanya shughuli yako binafsi inayotegemea kipaji au ujuzi wako kwa kuzalisha au kutoa huduma kwa wateja ili kupata faida kama mapato yako.”

Tofauti kubwa kati ya ajira na kazi

AJIRA
KAZI
Kazi ya mwajiri
Shughuli ya mtu binafsi
Mkataba unaoanisha majukumu na viashiria vya ufanisi wa kazi kulingana na muda wa kazi
Mipango kazi kwa ajili ya uzalishaji au utoaji huduma ili kutosheleza mahitaji ya wateja
Kulipwa mshahara/mafao ya uzeeni
Kupata faida/ akiba


Malalamiko kuhusu
 ukosefu wa ajira

Sababu kubwa iliyonisukuma kuandika habari ya tofauti ya ajira na kazi ni mkazo mkubwa unaowekwa katika kutafuta ajira kana kwamba hii ndiyo njia pekee ya kuinuka kiuchumi. Na changamoto kubwa iko kwa jamii ya wahitimu wa vyuo vikuu ambapo Ongezeko lao la kila mwaka haliendi sambamba na ongezeko la uzalishaji unaotoa fursa za ajira.

Katika kuweka mkazo kwenye ajira nimegundua kwamba, ufumbuzi wa changamoto ya ukosefu wa ajira ina mbadala ulio bora zaidi isipokuwa wahusika hawana uelewa na kupitia makala hii napenda kuwafunbua macho. Kabla ya kwenda mbali zaidi napenda ziweka bayana sababu tatu ajira si njia pekee ya kuinuka kiuchumi:

Kwanza; katika Kama nilivyotangulia kusema kwamba kutokana na ongozeko kubwa la wahitimu wa vyuo wanaotafuta ajira ni kubwa kuliko fursa zilizopo kwenye soko la ajira. Kwa hiyo sio kila mtu atajaliwa kupata fursa au nafasi ya ajira. Aidha tujikumbushe kwamba “ajira” ni kazi ya mtu mwingine ambaye ndiye anayewajibika kukulipa mshahara kwa kazi utakayomfanyia. Kila mwajiri anayetoa nafasi za ajira ni kulingana na ukubwa wa mradi, biashara au huduma anazozitoa kwa wateja wake.

Hakuna mwajiri anayeanzisha mradi, biashara au huduma kwa msukumo wa kuajiri watu ili wapate kujiendeleza kimaisha. Kipaumbele cha mwajiri ni kuzalisha/kutoa huduma ili apate faida kama sehemu ya mapato ya kazi yake.
Mwajiriwa yupo kama sehemu ya gharama za uzalishaji ili ajipatie faida na sio amnufaishe sana mwajiriwa wake. Ndiyo maana malipo ya mwajiriwa ni kidogo kuliko faida inayokwenda kwa mwajiri.


Pili, pamoja na kwamba watu wengi wanatamani kupata ajira. Lakini sio lazima kwamba kila mtu lazima aajiriwe. Kwanini? Kuna baadhi ya watu wenye uwezo  mkubwa wa ubunifu na uzalishaji kiasi kwamba wao ndio walistahili kutengeneza ajira kwa ajili ya wengine.

Ni ajabu sana ambapo kumkuta mtu ana elimu, ujuzi na uwezo wa kuanzisha kampuni na kupata vibali vya kuendesha miradi au biashara au huduma na kupata faida kubwa; lakini mtu huyo anang’ang’ana na ajira na kutumia vipaji na uwezo wake mkubwa kumpatia faida mwajiri wake! Kumbuka kwamba mtu kama huyu akiondoa woga na kuamua kuanzisha kazi anayoisimamia mwenyewe atasaidia wengi ambao watanufaika na vipaji vyake badala yay eye kumnufaisha mwajiri mmoja.

Tatu, pamoja na kwamba ni watu wengi ambao wanatamani ajira lakini sio wote wenye sifa za kuajiriwa na kuajirika. Ajira ina sifa zake na vigezo vinavyotumika kumthibitisha mtu kuwa ana sifa za kuajiriwa. Ingawa kila mtu “ana haki ya kuajiriwa” lakini sio kila mtu ana sifa za kuajiriwa mahali popote anapotaka yeye.


Hata kama ajira ni chache bado
kila mtu anatakiwa kufanya kazi

Kama wewe sio mlemavu wa viungo, sio mtoto wa umri mdogo, si mzee uliyepita umri wa kufanya kazi; basi ni bora ujue kwamba ni wajibu wako binafsi kujitegemea katika kupata mahitaji yako ya lazima km chakula, mavazi na malazi.

Kuanzia binadamu wa kwanza, tunasoma kwamba mara tu baada ya kuumbwa alikabidhiwa bustani ya Edeni ili ailime na kuitunza. Ile haikuwa ajira bali ilikuwa ni kazi. Wala si Adamu aliyeitafuta bustani ya Edeni bali alikabidhiwa na Muumbaji wake. Huu ni ushahidi kwamba kwa asili binadamu aliumbiwa uwezo, ubunifu, na nguvu za kufanya kazi. Uwezo wa kufanya kazi ni wa kimaumbile na hautegemei elimu, ujuzi wa kitaaluma unaopatikana kwenye taasisi za elimu.

Japokuwa watu wengine wanatafuta ajira na kuzikosa, lakini kila mtu anayo fursa ya kufanya kazi. Maana yake kukosa ajira sio kukosa kazi ya kufanya. Mpaka sasa kuna mamilioni ya watu hawana ajira kabisaaa lakini wanaishi kwa jasho lao bila kuiba au kuwa tegemezi kwa wengine. Maana yake wanazo kazi wanafanya na kumudu maisha yao kwa jasho lao wenyewe.


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.