SOMO: KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU (1 & 2) - MCHUNGAJI MADUMLA


Bwana Yesu asifiwe…

Si watu wengi wenye kujua maana halisi ya Karama maana wapo watu wenye kulichanganya neno hili na neno kipaji. Kipaji na karama ni maneno mawili tofauti kabisa kwa sababu kipaji ni uwezo wa asili wa kimwili ndani ya mtu wa kutenda jambo fulani ,bali karama ni uwezo wa kiroho wa kutenda sawa sawa na muongozo wa Roho mtakatifu.

Hivyo basi,

Karama ni utendaji kazi wa Roho mtakatifu ndani ya mwamini aliyeokoka.

Kila aliyeokoka amepewa karama fulani kwa kufaidiana katika kuujenga mwili wa Kristo.

Katika fundisho hili zuri,tutajifunza katika vipengele vifuatavyo;

01. Tofauti kati ya ujuzi,kipaji na karama.

02. Tofauti kati ya wito na karama.

03.Aina za karama za Roho mtakatifu.

04. Sifa kuu za karama za Roho mtakatifu.

05. Faida za karama za Roho mtakatifu.

06. Utawezaje kuitambua karama yako?

07. Ni namna gani utachochea karama yako?

08. Ni kwa namna gani karama yangu itampendeza Mungu?

09.Changamoto za utendaji kazi katika kila karama.

01.TOFAUTI KATI YA UJUZI,KIPAJI NA KARAMA.

A)Ujuzi.(Skill)

Ni uwezo upatikanao kwa njia ya elimu fulani. Uwezo huu umuwezesha mtu kutenda au kufanya jambo fulani kwa sababu ya elimu aliyoipata.

Hivyo,UJUZI ni uwezo wa kufanya jambo fulani katika ubora,au katika ufundi fulani kwa sababu ujuzi huo umepatikana kwa kusomea au kujifunza ( Capacity to do something well; technique, ability. Skills are usually acquired or learned, as opposed to abilities, which are often thought of as innate.)

Mfano 01; Mtu anaweza akaenda kusomea ufundi magari,kisha baadaye akawa ni fundi mzuri sana wa kutengeneza magari na hata kuyarekebisha. Ufundi huu uliopatikana kwa kisomo au mafunzo fulani ni ujuzi.

~Ujuzi hauji automatically yaani haumjii mtu moja kwa moja bali ni lazima akajifunze kwanza ndiposa awe mjuzi wa jambo fulani.

Mfano 02. Katika biblia tunaona wapo watu wengi tu waliokuwa na ujuzi wa kufanya mambo tofauti tofauti,mfano tunasoma; “ Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.“Mwanzo 4:20-21

Yabali baba yao,bila shaka alipitisha elimu juu ya ufugaji wanyama. Elimu hii juu ya ufugaji ilikuwa ni ujuzi wa namna ya kufuga wanyama. Katika jamii ya kiyahudi kulikuwepo namna ya kurithisha elimu ya ufugaji kutoka jamii moja hadi jamii nyingine. Mtazame pia Yubali baba yao wapigao kinubi na filimbi. Bila shaka elimu ya namna ya kupiga kinubi na filimbi ilifundishwa na kurithishwa. Na jambo hili tunaliona hadi katika kizazi cha Daudi,Daudi alikuwa ni mpigaji mzuri wa kinubi. Imeandikwa;

“Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.” 1 Samweli 18:10

Ukijaribu kuyatizama maisha ya baadhi ya wanafunzi wa Yesu,wengi wao walikuwa na ujuzi fulani katika maisha yao kabla ya kuitwa kuwa mitume. Mfano Petro alikuwa ni mvuvi,uvuvi huu wa Petro ulitokana na elimu ya awali kutoka kwa baba yake na jamii yake iliyokuwa wavuvi tangu awali. Alikadhalika ukimtazama mwinjilisti LUKA alikuwa na ujuzi mzuri tu wa utabibu kabla ya kuokoka katika misafara ya mtume Paulo. Tazama Wakolosai 4:14

▪Je ujuzi unahitajika katika kanisa la leo?

JIBU;Ujuzi unahitajika sana katika kanisa la leo. Maana si wote watakaokuwa ni wachungaji au si wote watakao kuwa ni waalimu kanisani bali wapo wengine watakaokuwa ni waamini wenye ujuzi wa mambo fulani yenye kulifaa kanisa liweze kusonga mbele kwa kujitosheleza. Mfano; Kanisa linahitaji wataalamu waliosomea namna ya kuendesha kitengo cha utawala ( Management) yaani jinsi ya kukontroo/ku-control matumizi ya pesa,jinsi ya kuwa na miladi endelevu ya kanisa,jinsi ya kuandaa mikutano,seminas,makongamano ( Maana huduma hizo zote zinahitaji pesa)

Tuangalie kanisa la kwanza lilivyoweza kushughulikia suala hili la utawala, ;

“Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani

Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.” Matendo 6:1-4

Hapo,tunaona kabisa mitume walibidi waweke mambo ya kiutawala(management) ili kukidhi mahitaji ya kila siku ya watu wote. Kipindi mitume wanahudumu mezani pa Bwana,hapo ndipo pakatokea hali ya kutokutenda sawa kwa baadhi ya wajane wa kiebrania kusahauliwa katika huduma ya kila siku. Kumbe basi kanisa likikosa utawala(management team) halitaweza kutenda haki. Lakini pia kanisa la namna hii linaweza likakumbwa na manung’uniko mengi ya kihuduma za kila siku,maana wapo watu ambao watasahaulika katika baadhi ya mambo mbali mbali.

Kumbuka,Kazi ya utawala sio kazi ya mchungaji hapo kanisani kwa sababu kazi ya mchungaji ni kulihudumia lile neno na kuomba (Matendo 6:3-4).

Hivyo basi ,ujuzi unahitajika sana katika kanisa la leo,kumbuka tena watu wa utawala ni lazima wawe na ujuzi wa kuendesha mambo kanisani pasipo upendeleo wowote ule.

Lakini pia watu hawa wenye ujuzi wanatakiwa wawe ni watu safi rohoni,wasiwe na mawaa maana ikiwa watakuwa ni watu ovyo,yaani hawajaokoka wakamaanisha~basi waweza wakapendelea baadhi ya waamini hata kama wamejawa na ujuzi wa kutenda mambo. Tazama mfano wa wale saba waliochaguliwa katika kuongoza mambo ya utawala katika kanisa la kwanza (Matendo 6:3),Watu hawa walikuwa ni watu wema waliojawa na Roho mtakatifu…

(B) Kipaji (Talent)

~Ni uwezo wa kiasili (wa kuzaliwa nao) wa kimwili wa kutenda jambo au kitu fulani pasipo kujifunza. (Natural ability or skill)

Mungu ametoa vipaji mbali mbali kwa watu wake. Mfano,wengine wamepewa wawe waimbaji,wengine mafundi,wengine wachoraji,wengine wacheza sarakasi N.K Mara nyingi vipaji hivi hutumika kama sehemu ya kujiingizia kipato kwa mwenye nacho.

Maana wapo watu ambao ni mafundi wazuri wa mambo mbali mbali mfano fundi radio,ambaye kwa kweli hajasomea ufundi radio bali amezaliwa na uwezo wa kukorokochoa radio yoyote na kisha kugundua tatizo pamoja na kupata uvumbuzi wake,kisha na kujipatia kipato chake kwa ufundi huo. Wengine utakuta ni wachoraji wazuri sana,uwezo wa kuchora pasipo kujifunza mahali popote pale ni kipaji,ambapo kipaji hiki kinatoa kipato.

Ujuzi unatofautiana na kipaji,kwa maana ujuzi unaupata kwa sababu ya elimu fulani uliyoipata darasani wakati kipaji ni uwezo wa kuzaliwa nao wa kutenda jambo pasipo kujifunza darasani. ( Ingawa mtu anaweza akawa ni fundi radio kwa kusomea,ufundi huu ni ujuzi.)

Lakini kumbuka hili; Mwenye kipaji anaweza akaenda shule kwa madhumuni ya kukikuza kipaji chake. Na hapo,ndiposa kipaji kinakuwa kina mapana makubwa ya utendaji kazi.

Je kipaji kinahitajika katika kanisa la leo?

JIBU;

Kipaji kinahitajika sana katika kanisa la leo sababu watu hawa wenye vipaji wanaweza kutumika kama chachu ya kuwakusanya watu wengi sehemu moja,kisha baada ya hapo wakahubiriwa na muhubiri na hatimaye kuvuna roho za watu hao.

Mfano;Wenye vipaji vya uchezaji,wanaweza wakacheza mahali pa mkutano wa injili kabla ya muhubiri kupanda,gafla waweza kuona kundi kubwa la watu wakitekewa na machezo ya nyimbo za sifa kwa Bwana kupitia wale wenye vipaji vya kucheza,kisha katika hali hiyo hiyo ndiposa muhubiri aja kuzikomboa roho za watu wale waliokusanyika. Mfano huu mimi ninaufananisha na mvuvi aliyezitega nyavu zake baharini kisha samaki kunaswa na zile nyavu zake.

Kumbuka;kipaji ni zawadi ya bure itolewayo na Bwana Mungu kwa watu bila kuzingatia itikadi za imani zao. Maana mtu anaweza akawa hata aamini kabisa!yaani mpagani lakini akawa bado ana kipaji kizuri tu cha kufanya jambo fulani,Tofauti na karama,maana karama inamtaka mtu aokoke kwanza.

C)Karama(Spiritual gift)

Ni utendaji kazi wa Roho mtakatifu ndani ya mwamini aliyeokoka.

Zifuatazo ni baadhi ya tofauti chache kati ya ujuzi,kipaji na karama;

(i)Ujuzi ni uwezo upatikanao darasani,kipaji ni uwezo wa kuzaliwa,karama ni uwezo wa Roho mtakatifu wa utendaji kazi baada ya kuokoka.

(ii)Ujuzi ni kwa kila atakayesomea,kipaji ni kwa kila mtu sawa sawa na alichopewa,karama ni watu wachache waliokoka kwanza na kudumu katika wokovu.

(iii) Ujuzi una gharama ya pesa katika upatikanaji wake,kipaji hakina gharama ya pesa maana mtu hawezi kununua kipaji kwa pesa,karama ina gharama ya kuyauza maisha yako kwa Bwana Yesu ili Yeye Bwana awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.

(iv)Ujuzi ni jitiada za mtu mwenyewe,kipaji hutoka kwa Mungu,Karama utolewa na Roho mtakatifu kama apendavyo Yeye.

Kila aliyeokoka ana karama yake,kwa sababu sote tu viungo vya Kristo “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.” 1 Wakorintho 12:7. Hivyo basi karama ;hutolewa na Roho mtakatifu kama apendavyo Yeye kwa wale watu wake wanaomcha.

Kumbuka;mtu wa mataifa asiyeamini hana karama,mpaka anapokuja kwa Bwana,akiokoka ndipo upewa karama moja wapo kwa kadri ya Roho mtakatifu apendavyo. Hata wewe mpendwa ipo karama yako ikiwa utakuwa ndani ya Yesu na Yesu awe ndani yako.

~Je mtu anaweza kuipata karama yake kwa kusomea darasani?

JIBU;

Karama haipatikani kwa kusomea darasani,kwa maana Yeye atoaye kila karama ni Roho mtakatifu.( 1 Wakorintho 12:8). Bali mwenye karama anaweza kwenda darasani kwa lengo la kuikuza karama yake kimaarifa ili atakapokua akiitumia aweze kuwa na wigo mkubwa wa matumizi ya karama hiyo.

Jambo hili leo limekuwa ni shida kubwa inayoisumbua kanisa la leo,maana wapo watu wanaohudumu kiroho huko makanisani kwa sababu walienda kusomea karama zao kisha baada ya mafunzo wengine wakajiita au kuitwa ni wachungaji,mashemasi,mitume,manabii N.K

pasipo Roho mtakatifu kuhusika kuwapa nyadhifa hizo. Mfano; Uchungaji hausomewi bali utolewa na Roho mtakatifu,kisha baada ya kupewa huduma hiyo mtu aweza kwenda shule kupata mwanga zaidi juu ya uchungaji alikadhalika na karama nyingine zozote zile.

Hatuwezi kuwa wachungaji,mitume,walimu kwa vyeti tu kwa sababu kinachohudumu kanisani sio cheti bali kile kinachohudumu ni roho ikiongozwa na Roho mtakatifu. Kama ndio hivyo,basi ni dhahili kabisa Roho mtakatifu ndie agawaye karama tofauti tofauti kama apendavyo Yeye.

~ Je mtu mmoja anaweza akawa na karama zote?

JIBU;

Mtu mmoja hawezi kuwa na karama zote,bali hupewa karama fulani kwa kufaidiana na mwingine ( 1 Wakorintho 12:14-20).

~Je mtu mmoja aweza kuwa na ujuzi wa jambo fulani,kisha akawa na kipaji na papo hapo akawa na karama?

JIBU; Ndio,mtu aweza akawa na ujuzi wa jambo fulani,akawa na kipaji kisha akawa na karama. Mfano mtu kabla ya kuokoka alikuwa na kipaji cha uimbaji wa nyimbo za kidunia,

then alipookoka ule uimbaji wake wa awali ukabadilishwa kwa Roho mtakatifu~ kile kipaji cha uimbaji kikavuviwa na Roho mtakatifu akawa na karama ya uimbaji,kisha mtu huyo akaonelea si vyema kubakia na karama hiyo pasipo kuijua kiundani hapo akaenda chuo cha mziki kwa ajili aikuze zaidi karama yake kwa ujuzi huku Roho mtakatifu naye akahusika kuikuza karama hiyo. Kwa hiyo umeona,mtu huyo amekuwa na ujuzi,kipaji pia karama.

~Je karama inahitajika kwa kiwango gani katika kanisa la leo?

JIBU;Karama inahitajika sana kwa kiwango cha juu katika kanisa la leo. Maana karama ndio utendaji kazi wa Roho mtakatifu,hivyo inahitajika. Kumbuka;mambo ya kanisa ni mambo ya kiroho na mambo ya rohoni huongozwa na Roho.

Hivyo basi ujuzi,kipaji na karama kila kimoja kinatofautiana na mwenzake haswa katika utendaji wa kazi. Tofauti hizi ndizo haswa zinazohitajika katika kanisa la leo ili makusudi mwili wa Kristo ujengwe.

02.TOFAUTI KATI YA WITO NA KARAMA.

Ipo tofauti iliyopo kati ya wito na karama,ingawa mara nyingine wito wa mtu inawezekana ndio ikawa ni karama yake.

A) Wito.(calling)

(i)Wito ni sauti kamili ya Roho mtakatifu juu ya kazi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya yule aitwae. Mfano tunaona akina Barnaba na Sauli; “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.”Matendo 13:2

(ii) Wito ni kazi maalumu ya kiroho,au ofisi maalumu ya kiroho itolewayo na Roho mtakatifu kwa Yeye apendaye kumpa. Mfano katika zile huduma tano (Waefeso 4:11) ni wito uliotolewa na Roho mtakatifu,biblia inasema “Naye alitoa…” maana yake “ aliwafanya kuwa~ kwa wito.”

Tofauti iliyopo ni hii; mtu anaweza akaitwa awe mchungaji lakini katika uchungaji akapewa karama ya miujiza. Ndio maana waweza kuona wapo watu walioitwa kuwa wachungaji lakini wamejawa na matendo ya miujiza.

Kumbuk;wito huu ni uchungaji,bali karama katika uchungaji wake ni matendo ya miujiza. Mfano mwingine;mtu aweza kuitwa katika ofisi ya ualimu,lakini akapewa karama ya matendo ya huruma.

Ndio maana unaona walimu wengine makanisani wamejawa na matendo ya huruma sana. Mfano tena,mtu anaweza akitwa katika ofisi ya unabii lakini katika unabii wake akapewa karama ya kunena kwa lugha mbali na wito wa unabii.

Na mtu mwingine akawa na wito wa uinjilisti lakini akapewa ziada ya karama ya neno la maharifa,hivyo katika wito wake wa uinjilisti akawa amejawa na neno la maharifa. N.K


ITAENDELEA…

Kwa huduma ya maombezi tafadhali usisite kunipigia simu yangu hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.