SOMO: KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU (3 & 4) - MCHUNGAJI MADUMLAKama hukusoma sehemu ya kwanza na ya pili bonyeza hapa

Kama tayari unaweza kuendelea na sehemu ya tatu na ya nne chini. Barikiwa

Karibu tuendelee;

Bwana Yesu asifiwe…

03.AINA ZA KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU.

Karama hizi ni miongoni mwa karama ambazo biblia imeziorodhesha katika 1 Wakorintho 12:8-10. Ili kuelewa vizuri na kupata mpangilio mzuri,basi nimekupangia karama hizi katika makundi makuu manne;

A.Karama za kusema.

(i) Lugha.

(ii) Kutafsiri lugha.

(iii)Unabii.

B.Karama za Ufunuo.

(i) Neno la hekima.

(ii)Neno la maarifa.

(iii)Kupambanua Roho

C.Karama za uwezo.

(i) Karama ya imani.

(ii)Karama za uponyaji.

(iii)Matendo ya miujiza.

Roho mtakatifu ametoa ufunuo mbali mbali kwa kufaidiana kama apendavyo Yeye 1 Wakorintho 12:8.

A.KARAMA ZA KUSEMA.

(i)Karama za lugha

~Karama za lugha nazo zimegawanywa katika sehemu kuu mbili;

Lugha katika kulijenga kanisa, kuhutubu.

Udhihirisho wa Roho wa namna hii ujulikana pia “lugha ya ibada” Hiki ni kipindi cha kuwajenga waamini,kuwatia moyo,kuwatia nguvu kwa maneno yenye kueleweka vizuri (1 Wakorintho 14:3). Sifa mojawapo ya karama hii ni kwamba,ili ifanye kazi inategemea hadhara ya watu walioandaliwa kupokea ujumbe. Kuhutubu,kunamfanya yeye aliye mjinga kupata nafasi ya kuelimika kwa neno la Mungu.

Lugha katika kunena(kunena kwa lugha mpya)

Uhidhihirisho huu ni wa aina ya pili,ni udhihirisho wa Roho mtakatifu katika kunena kwa lugha.Kunena kwa lugha ni kutamka maneno katika Roho yasiyopangwa kutamkika,na yasiyoeleweka maskioni mwa watu hata shetani haelewi kabisaa!isipokuwa roho ya mtu hunena mambo ya siri na Roho wa Mungu~ Matendo 2:4.

Kumbuka;kupo kunena kwa lugha mpya baada ya Roho mtakatifu kushuka (Matendo 19:6,Matendo 2:4) Lakini pia kupo kunena kwa lugha kwa namna ya karama rasmi. Kile ninachozungumzia hapa ni unenaji wa lugha katika karama.

Mtu mwenye karama hii,muda wote aweza kunena kama apendavyo Roho mtakatifu. Haitaji kuanza kutafuta uwepo kwamba aabudu kwa kipindi kirefu ndipo anene,bali anaweza akaabudu kidogo tu kisha akanena,au akawa akinena katika maombi.

(ii) Kutafsiri lugha.

Karama hii inategemea malighafi ya udhihirisho wa Roho mtakatifu wa kunena kwa lugha. Maana ili utafsiri,unahitaji lugha iliyonenwa lakini haikueleweka,au haieleweki katika hadhara husika,ndiposa hitaji la kufasiri hujitokeza. Karama hii inawezeshwa na Roho mwenyewe,kwa sababu hakuna awezaye kufasiri lugha kwa kutumia akili zake mwenyewe pasipo kuongozwa na Roho mtakatifu. Wala hakuna ujanja ujanja unaohitajika katika kufasiri lugha pale lugha mpya itolewayo,ni kwa msaada wa Roho mtakatifu tu.

~Je karama hizi mbili yaani,karama ya kunena katika roho,na kufasiri zinatumikaje?

JIBU;Yapo mazingira mawili ambapo yakupasa kuyajua kwamba ni kipindi gani haswa cha kufasiri lugha na kipindi gani haswa si cha kufasiri lugha pindi mmoja anenapo(na huu ni ufunuo)

Hivyo basi ili tuweze kuyajua haya yote hatuna budi kujua aina za unenaji wa lugha,zipo mbili nazo ni;

(a)Mtu akizungumza na MUNGU wake kwa njia ya lugha.

(b)MUNGU akizungumza na watu wake kwa njia ya lugha.

Tazama,Mtu akizungumza na MUNGU wake kwa njia ya lugha,haitaji mtafsiri maana mtu huyu hunena mambo ya siri katika roho yake,wala hasemi na watu~ 1 Wakorintho 14:2. Lakini,Mungu anaweza kuzungumza na watu wake kwa njia ya lugha akimtumia mtumishi wake,hapa ndipo pana hitaji mwenye karama ya kutafsiri lugha aingie kazini kwa msaada wa Roho mtakatifu ili kuwezesha ujumbe wa Mungu ueleweke kwa watu wote ~ 1 Wakorintho 14:13

(iii)Unabii.

1 Wakorintho 12:10

Hapo zamani mtu mwenye karama hii alikuwa akijulikana kuwa ni “ mwonaji” Imeandikwa“ (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) “1 samweli 9:

Hivyo basi,karama hii inampa mtu kuona mambo yajayo katika ulimwengu wa roho kwa kadri Roho mtakatifu anavyojifunua kwake. Karama hii ni zawadi nzuri ya kupata taharifa za matukio yajayo,ili uweze kuyashughulikia sasa. Hata kanisa,haliwezi kwenda bila nabii,yeye aonaye mambo ya sirini. Ikumbukwe ya kwamba unabii hautolewi kwa sababu ya mapenzi ya mtu fulani bali kwa sababu ya mapenzi ya Roho mtakatifu;

“ Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” 2 Petro 1:20-21

(B.)KARAMA ZA UFUNUO.

(i) Neno la hekima.(1 Wakorintho 12:8)

Awali ya yote yakupasa kujua nini haswa maana ya hekima.

Hekima;ni moyo wa adili wa kuhukumu katika haki na ni uwezo wa kupambanua mema na mabaya (1 Wafalme 3:9)

( Ni moyo mwelevu unaotambua kila jambo kwa mtazamo wa kiungu na neno lake. Au hekima ni kunena au kusema jambo sahihi,kwa watu sahihi na wakati sahihi.)

Moyo huu wa adili wa kupambanua mema na mabaya katika haki ndio karama yenyewe ya ufunuo. Lakini hatusemi “ karama ya hekima” bali “ karama ya neno la hekima“. Mfano katika biblia; katika Luka 20:19-26,hapo utaona waandishi na wakuu wa makuhani wakijaribu kumkamata Bwana Yesu kwa hila zao,wakimtega kwa kumuuliza kwamba ni halali wao kumpa kodi Kaisari au la?

tunaona hapo Bwana Yesu akitumia karama ya “neno la hekima ” kuwajibu,na hatimae wale wenye hila walistaajabu na kunyamaa.Mifano mingine katika biblia;Soma Yoh. 8:3-11,Matendo 6:1-5,Matendo 15:25-29,Matendo 27:23-24. N.K

Utendaji kazi wa karama hii ya neno la hekima;

~Uwezesha kufanya maamuzi kwa usahihi na kwa haki.

Mtu mwenye karama hii,anaweza akawaamua na kuwaongoza watu wake kihekima. Kanisa linahitaji karama hii,ili pasiwepo na upendeleo wowote ule.

(ii) Neno la maarifa. 1 Wakorintho 12:8

Neno la maarifa ni mojawapo ya karama ya ufunuo wa Roho mtakatifu wa kujua mambo mbali mbali katika uhalisia wake. Pia, ni sehemu ndogo ya maarifa ya Mungu ndani ya mwenye karama hii. Tuangalie mifano michache kuhusu karama hii ndani ya Bwana Yesu.

Yesu alifahamu kweli iliyopo ndani ya Nathanaeli kabla hata hajakutana naye,imeandikwa;“Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.” Yoh.1:47-48.

Kupitia andiko hilo,tunaona ya kwamba Yesu akiwa na neno la maarifa kuhusu Nathanaeli wa kana ya Galilaya. Pia waweza kusoma Yoh.4:18-20,(Yesu akiwa na maarifa kamili juu ya mwanamke msamalia kwa kujua yote aliyokuwa nayo kabla ya kukutana naye.),

Soma pia habari za Anania na Safira mkewe, Matendo 5:3,jinsi karama ya neno la maarifa ilivyofanya kazi ndani ya Petro,kiasi cha kujua siri yote aliyoifanya Anania na Safira mkewe katika mauzo ya kiwanja.N.K

Kumbuka;neno la maarifa ni tofauti kabisa na maarifa ya mwanadamu ya asili. Hii ni karama yaani ni utendaji kazi wa Roho mtakatifu katika maarifa yake. Hivyo maarifa haya ni tofauti na maarifa ya kusomea,tena ni tofauti na maarifa ya asili bali ni Roho mwenyewe.

Utendaji kazi wa karama hii;

(a) Kufichua dhambi. ~Matendo 5:1-3

~Kupitia karama ya neno la maarifa,dhambi hufichuliwa. Maovu pia hufichuliwa kwa sababu mwenye karama hii amepewa kuona kimaarifa.

(b) Kuwa na wigo mpana wa kutatua tatizo.

Karama hii,inampa wigo mkubwa muhusika wa kutatua tatizo kwa maana anakuwa na maarifa ya ki-Mungu juu ya tatizo. Kuna kipindi fulani ambacho unahitaji neno la maarifa ili uweze kushughulikia tatizo la kiroho kiundani haswa.

(c) Karama hii inakuwezesha kushauri,kuomba,au kuombea wengine kimapana.

~Tazama, mtu akijawa na karama ya neno la maarifa huweza kujua jinsi impasavyo ya kutoa ushauri mzuri kwa mtu mwenye kuhitaji kushauriwa,kwa maana wakati mshauriwa anaeleza hapo mwenye karama anaweza kujua jambo sahihi la kumshauri na lipi asimshauri kwa maana atakuwa akiona na kuyapima maneno yote ya mshauriwa hata kama hajamaliza kumsimulia. Karama hii ya neno la maarifa itamuwezesha mtumishi ajue namna gani ya kumuombea pia.

(iii)Kupambanua Roho.

~Hii ni mojawapo ya karama ya ufunuo yenye umuhimu sana katika kanisa la leo. Kupamanua roho ni kipawa cha kuzipima roho (is the power of testing spirit)maana nyakati hizi za mwisho zipo roho zidanganyazo(1 Timotheo 4:1). Pia kupambanua roho,ni kipawa cha kuhakiki roho,kuzinyambua nyambua roho. Uwezo huu ni wa umuhimu sana,maana kwa njia ya karama hii ndiposa mtu aweza kutofautisha roho za mashetani na Roho wa Bwana.

Ufanyaji kazi wa karama hii ni kama ifuatavyo;

(a)Kuzipima roho za watu mbali mbali.

Roho za watu mbali mbali zenye kunena habari za Yesu,lazima zipimwe kwa kupitia karama hii. Maana si wote wananena sahihi,bali wengine wengi wamejawa na tamaa zao na wala si watu wa Mungu kwa kazi wazifanyazo. Mfano tuangalie hapa;

“Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” Matendo 16:16-18

Kijakazi huyu alikuwa na pepo wa uaguzi,ambapo pepo huyu ni roho ya shetani. Ingawa kile alichokisema kilikuwa sawa maana aliwasemea akina Paulo kwamba ni watumishi wa Mungu aliye hai,wenye kuhubiri njia ya wokovu lakini roho hiyo iliyoyasema ilikuwa ni roho ya pepo,ndio maana Paulo aliweza kumkemea na kumtoa. Paulo aliweza kupamanua roho ndani ya yule kijakazi.

Sasa waweza fikiria kwamba kama Paulo asingelikuwa na karama hii,wewe unafikirije? Je ni kweli angeweza kumkemea? Ukweli ni kwamba angemuacha yule kijakazi aendelee kusema maneno yale,tena angekubali kabisa kwamba waandamane wote katika kuhiubiri injili. Na laiti kama angeambatana naye pasipo kuijua roho itendayo kazi ndani ya yule kijakazi,basi ni dhahiri huduma ya Paulo ingemsumbua baadae.

Na hili ndilo linaloendelea hata leo katika makanisa yetu. Maana wapo watu ni wapunga pepo hali wakijifanya ni watumishi wa kweli. Na kwa sababu ya kuikosa karama hii,tumejikuta tukiwakumbatia watu hao na kuwapa nafasi mbali mbali za kiutumishi~ sasa mwishoe hatujui ipi miujiza ya kweli,na ipi ni ya uongo kwa sababu ya kushindwa kupambanua roho.

(b)Kuzipima roho za watumishi wa Mungu.

~Wapo watumishi wa Mungu wa ukweli ambao hufanya kazi ya Mungu kihusahihi kabisa. Lakini baadhi yao wanaweza wakatumiwa na roho za kishetani pasipo wao kujijua ya kwamba wanatumika kipindi hicho,inawezekana katika kipindi hicho cha kutumika na roho mbaya wao wakawa wamejisahau,labda waliruhusu hasira,uchungu,magomvi,hofu.N.K,

hivyo hayo yote yakawa ni mlango wa shetani,kisha roho ya pepo ikaingia ndani yao. Hapo sasa roho itakayotenda kazi kipindi hicho siyo Roho mtakatifu bali ni roho mtakafujo roho ya shetani hali mtumishi huyo ni wa Mungu. Tumeona mara nyingi maneno mabaya yakiwatoka watumishi wa Mungu,mpaka tunashangaa kwamba ni kweli mchungaji huyu huyu tunayemfahamu?!! Au mwingine,?!!

Mfano tuangalie hapa;

“ Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mathayo 16:21-23

Petro alikuwa si shetani,bali ni mtumishi wa Mungu kweli kweli. Lakini katika andiko hili tunaona Yesu akamwambia “Nenda nyuma yangu,shetani;u kikwazo kwangu...” Yesu aliweza kutambua ya kwamba roho iliyokuwa ikitenda kazi saa ile haikuwa roho ya Petro bali ilikuwa ni roho ya shetani.

Si Roho yule wa Bwana kwa kipindi kile bali ni roho ya shetani ndio ilikuwa ikinena ndani ya Petro,Yesu akaipambanua kisha akatambua. Ikumbukwe kwamba Yesu alipoanza kuwaonya juu ya mateso yake,huyu Petro aliingiwa na hofu,kumbuka ;hofu ni mlango wa shetani,hivyo Petro aliweza kufungua mlango na roho mbaya ikamuingia ndiposa akaanza kumkemea Yesu kwa kuyakataa yale ambayo Yesu alikuwa akiwaambia.

Katika eneo hilo,si rahisi kujua roho ya shetani na Roho wa Mungu ikiwa kama huna karama hii ya kupambanua roho. Karama hii ikikosekana,wengi hunaswa katika roho za miujiza ya shetani wakidhani ni ya Mungu….

ITAENDELEA…
~ Kwa huduma ya maombezi,tafadhali usisite kunipigia simu yangu hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.