SOMO: KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU (5) - MCHUNGAJI MADUMLA

Mchungaji Gasper Madumla
Kusoma sehemu iliyopita Bonyeza Hapa.

Endelea.....

Karama hii imepangwa kwenye kundi la karama za uwezo,kwa sababu inahusisha nguvu katika utendaji wake wa kazi. Hivyo inajulikana pia ni “ Karama ya nguvu” au “ karama maalum” majina haya tofauti tofauti juu ya karama hii hutambulisha uwezo wa kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo tena ni bayana ya mambo yanayoonekana ( katika matendo).

Karama ya imani ni tofauti kabisa na imani ya kumuamini Mungu. Kwa sababu kila mtu anapookoka anapaswa amuamini Mungu yaani awe na imani kwa Mungu wake.

Hivyo basi kitendo cha kuamini uwepo wa Mungu na nguvu zake katika Kristo Yesu ni kitendo ambacho kila mwamini anapaswa awe nacho,na imani hiyo ni imani ya kawaida kabisa wala sio karama. Lakini papo hapo kuna kiwango cha juu cha imani ambacho Roho mtakatifu anakiachilia kwa baadhi ya wapendwa kama apendavyo yeye,kiwango hiki ndicho karama ya imani.

Hivyo basi kumuamini Mungu ni pale tunapohubiriwa neno la Mungu,kisha tunalipokea neno hilo na kuanza kuliishi. Imani hii chanzo chake ni kusikia neno la Kristo,Warumi 10:17. Soma pia Waefeso 2:8,Waebrania 10:38. Bali karama ya imani ni pale baada ya kuamini kisha kutumia uweza wa Roho mtakatifu kutika matendo.

Mfano wa karama hii;

~ Haikuwa imani ya kawaida kwa Nuhu kutengeneza safina kwa miaka 100,Nuhu alihitaji apate uwezo au nguvu ya kuhamisha kile alichokiamini na kukitenda.Katika eneo hili ilihitajika karama ya imani kuwezesha kutengeneza safina kama alivyoambiwa na Mungu. Hatumuoni Nuhu akihoji hoji namna itakavyokuwa bali alifanya kama vile BWANA alivyomuamuru ( Mwanzo 7:5).

Hivyo,karama ya imani haina maswali maswali kwa kile unachokiamini,bali ni kutenda katika uweza wa Roho mtakatifu maana atendaye si wewe bali ni Roho mwenyewe.

~ Petro pia,alikuwa ni mmoja wa mitume mwenye karama ya imani. Jambo hili tunaliona pale alipoamua kumfuata Yesu juu ya maji (Mathayo 14;25-29). Hapo,sio suala la kuamini tu,!! Bali kutenda kwa uweza wa Roho mtakatifu.

Tazama suala la Petro,si rahisi kuamini kwamba ukitembea kwenye maji hautazama hali ukijua kabisa endapo utakanyaka maji basi ni dhahili utazama,uwezo huu ndio karama ya imani~ yaani unaamini zaidi ya mipaka ya kawaida kisha unatenda.

Kanisa la leo limepungukiwa kwa wingi karama hii ya imani maana wengi leo wanaamini kawaida tu,mtu mwenye karama hii ni mtendaji,mahali pale kanisa limeshindwa yeye anaweza kwa msaada wa Roho mtakatifu. Kuamini pekee hakutoshi,bali kile kinachotosha ni kuleta imani ile ya kawaida katika utendaji kazi kwa uweza wa Roho mtakatifu.

Utendaji kazi wa karama hii;

Hutenda katika nguvu,(na uweza wa Roho mtakatifu).

~ Nguvu hii inahusisha pia na nguvu ya mwilini kwamba lazima uchukue hatua ya kutenda maana kuamini pekee haitoshi. Matendo 3:4-7, Ukisoma hapo; utaona Petro akijawa na karama ya imani juu ya uponyaji kwa jina la Yesu Kristo,lakini kule kujawa na imani.

hakukujitosheleza kumponya yule kiwete,bali alihitaji amshike mkono na kumuinua kwa jina la Yesu. Kumbuka,Petro alimuinua yule kiwete akiwa katika hali yake ile ile ya ukiwete akiamini kwamba anakwenda kutembea sasa,hilo sio jambo dogo!

(ii) Karama ya uponyaji.( 1 Wakorintho 12:9)

Ikumbukwe kwamba Yeye aponyaye ni Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu. Hivyo,hii ni karama yenye uweza wa Roho mtakatifu katika uponyaji. Ikumbukwe pia uponyaji ni mali yetu sote tuliookoka,kila aliyeokoka anapaswa awe na nguvu ya kutamka neno la uponyaji kwa wengine kisha kupokea uponyaji huo.

Uwezo huu ni ule uwezo wa kawaida kwa kila aaminie “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Marko 16:17-18

Huo ni uwezo wa kawaida ambao sio karama ya uponyaji. Karama yenyewe ni pale Roho mtakatifu anaweka uweza wake wa uponyaji kwa watu aliopenda kuwapa,sio watu wote. Watu wa namna hii ni zaidi ya madaktari wa kawaida,maana maneno yao yanaganga mioyo,nasfi na miili yetu pia sababu si wao waponyao bali ni Roho mwenyewe akiwa kazini.

(a) Kusudi la karama ya uponyaji.

Kulithibitisha neno la Mungu katika uweza wake.

~ Neno la Mungu limejawa na uponyaji tosha,karama hii ulithibitisha neno la Mungu kwamba linaponya kwa sababu karama hii hutenda kazi chini ya msingi wa neno la Mungu. Kwa lugha nyepesi ni hivi;kama hakuna neno la Mungu,basi hakuna karama ya upinyaji. Tukimwangalia Yesu, Yeye Neno alijawa na uponyaji “ Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.” Mathayo 8:8

Kuwavuta watu kwa Yesu,

~ roho za watu wengi leo zimeokoka kwa sababu waliponywa magonjwa yao. Hata wale wasioamini,waliamini baada ya uponyaji kufanyika katika maisha yao. Karama hii imevuna roho za watu wengi sana,na bado itaendelea kuvuna na kuvuna pasipo idadi kabisa. “ Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani” Mathayo 4:24-25

Kuwafungua waliofungwa kwa magonjwa na mateso mengi.

~ Kusudi hili ni la muhimu sana katika maisha yetu. Sababu ibilisi amejaribu kupanda pando la magonjwa kwenye miili ya watu wengi hivi leo,lakini kwa sababu ya karama hii~ watu hao wanafunguliwa mbali na magonjwa na huru na afya zao Matendo 10:38.

Kumtwalia BWANA Mungu utukufu.

~ Mungu wetu ni Mungu aponyaye ~ Kutoka 15:26. Karama hii ya uponyaji inamtambulisha Mungu tuliyenaye kwamba yupo tofauti kabisa na miungu,kwa sababu miungu haina uweza wa kuponya bali mwenye uweza wa kuponya ni mmoja tu,naye ndiye BWANA MUNGU wetu,JEHOVA. Karama hii inampa MUNGU utukufu mno.

(b) Utendaji kazi wa karama ya uponyaji;

Uponyaji ufanyika katika jina la Yesu Kristo pekee.

~ Karama hii hutenda kazi ndani ya jina la Yesu pekee. Hakuna jina jingine litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina la Yesu tu~Matendo 4:12.,Yoh. 14:14 Ukiona uponyaji unaofanywa nje ya jina hili,basi ujue uponyaji huo sio wa Mungu bali ni mazingaombwe ya shetani tu~na ukimbie,utoke eneo hilo.

Kuponya roho,nafsi na mwili.

Roho mtakatifu huponya roho zetu,tazama pale tulipokuwa nje ya Kristo tulikuwa wafu. Roho mtakatifu akatuhuisha roho zetu. Pia,nafsi zetu hazikuwa hai,lakini ziligangwa pamoja na miili yetu ilikuwa ikiugua ugua,ikaponywa nayo. Karama ya uponyaji ushughulikia vyote hivyo na kuponya.

Kuponya ardhi,mazao,mifugo (kufanya ukombozi)N.K

~ Rafiki yangu mmoja alikuwa akifuga paka nyumbani kwake. Siku moja paka wake alikunywa sumu huko nje katika mizunguko yake,kisha gafla sumu ikamlevya na kale kapaka kakazidiwa kalikuwa hakapumui kabisaa! Basi wakachimba shimo wakafukie. Sasa huyu rafiki yangu alipoingia nyumbani mwake akaona ndio wanamfukia paka wake,akasikia sauti;

“ muombee” kisha akawakataza wasimfukie. Akaanza kumuombea paka,gafla kakaanza kupumua kwa mbaliii,baadae akapata nguvu,kakatembea~ kaleee,mara kakachangamka! Umeona!!! Karama ikafanya kazi hata kwa mifugo.

~Ardhi pia inaweza ikawa imekufa, kisha ikakombolewa. Hata mazao pia yanaweza yakawa ni dhaifu,karama ya uponyaji ikayainua tena na kuwa hai.

Hutegemea watu ili ifanye kazi.

~ Ikiwa hakuna watu,uponyaji hautaonekana kabisaa. Bali tunauona uponyaji kwa sababu wahusika wenye kuhitajika kuponywa wapo. Karama hii inafanya kazi ndani ya watu.

(iii) Karama ya miujiza. 1 Wakorintho 12:10

~ Karama zote zimejawa na miujiza,mfano karama ya uponyaji,karama ya imani N.K Lakini karama hii,ni zaidi ya muujiza ya kawaida bali ni matendo makuu ya MUNGU mwenyewe. Matendo haya ni karama apewayo mtu kama Roho apendavyo Yeye. Karama hii inathibitisha uhai wa BWANA YESU yakwamba yupo hai hata sasa…

“Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” Matendo 4:13

(a) Utendaji kazi wa karama hii;

Kutumia jina la BWANA Yesu.

Karama zote ni lazima zitumie jina la Yesu Bwana wetu. Miujiza pia,ni lazima ifungamanishwe na Yesu mwenyewe maana Yeye ndie aifanyae yote hayo,U hai. Tazama miujiza fake,haitumii jina la Bwana Yesu,au hata kama wakidanya hadhara kwa kulitaja jina la Bwana basi ni dhahili kabisa watakuwa wakilitaja tu,na wala si kulitumia. Kutaja jina ni tofauti na kulitumia. Hivyo karama hii inahusisha sana matumizi ya jina la Yesu.

Kumfunua Mungu kwa watu wote.

Mungu hutambulikana pia katika miujiza. Wapo watu waliokuwa hawafahamu uwepo wa Mungu chini ya jua,lakini kwa njia ya karama hii wamemtambua Mungu. Tazama mfano,wako ambao hawakuamini kabisa uwepo wa MUNGU na wengine wamediriki kusema “hakuna Mungu” lakini walipoziona ishara na miujiza wakaamini.

Hutegemea imani.

Inafahamika wazi kwamba imani ni daraja lako la kupokea muujiza. Kumbe kama imani itakosekana hapa,basi inawezekana usipokee muujiza wako. Karama hii ya miujiza hutegemea kiwango chako cha imani,pia yule mwenye karama hii ni lazima ajawe na imani katika jina la Yesu Kristo.

(b) Matokeo ya karama ya miujiza.

~ Yapo matokeo mengi kuhusu utendaji kazi wa karama hii ya miujiza. Matokeo haya yote ni mazuri,ila ubaya ni pale namna watu wanavyoyapokea wao wenyewe.

Karama hii,imesababisha kuenea kwa injili kote ulimwenguni.

~ Tunaweza tukaanza kuangali hata katika kipindi cha Yesu. Kabla Yesu hajaanza kutenda miujiza hakuna mtu aliyemfuata popote. Bila shaka alikuwa amehubiri mara nyingi katika masinagogi,kwani LUKA 4:16,Anasema kwamba ilikuwa ni desturi yake.

Lakini miujiza katika Luka 4:33-35, ilipotendeka tu,tunaona sasa Habari za Yesu zikienea katika nchi ile. Imeandikwa; “ Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.” Luka 4:37

Hivyo basi,matendo haya makuu ni ya Bwana mwenyewe akiyaweka ndani ya wale aliowapenda Yeye,ili kusudi wakayadhihilishe nje. Na pindi yanapodhihilishwa nje huwa ni karama ya miujiza sasa…

ITAENDELEA…

~ Kwa huduma ya maombezi,usisite kunipigia kwa simu yangu hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.