SOMO: UMUHIMU WA NENO LA MUNGU - MCHUNGAJI MADUMLANa mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Zipo faida nyingi sana za neno la Mungu maishani mwetu,faida hizi ni nyingi mno kiasi cha kushindwa kuzieleza zote hapa. Lakini tuangalie faida kumi na tano (15) tu ambazo nazo ni chache kati ya nyingi zilizopo.

~Awali ya yote ikumbukwe kwamba neno la Mungu katika biblia ni sauti ya BWANA MUNGU iliyohifadhiwa kwenye maandishi. Ni MUNGU mwenyewe akizungumza na wote wenye mwili.

Sauti hii ya Mungu imekusudiwa kwetu katika Kutufundisha,kutuonya makosa yetu,kutuongoza katika njia sahihi na kutuadabisha katika haki~ 2 Timotheo 3:16

Tunapaswa kujifunza na kulitii neno la Mungu kila siku iitwapo leo kwa maana katika neno la MUNGU ndipo tunazungumza na MUNGU na ndipo mahali ambapo tunakamilishwa ukristo wetu. Tuangalie umuhimu wa neno la MUNGU kama ifuatavyo;

01. NENO LA MUNGU LINA UZIMA.

~Neno la MUNGU ni la uzima,lenyewe ni roho kamili iletayo uzima wa kiroho ~Yoh.6:63.

Pia kumbuka ya kwamba Yesu ni neno,anasema Yeye ndio njia kweli na uzima.(Yoh.14:6). Kwa lugha nyepesi ni kwamba mtu akiwa ameketi katika neno la Mungu la usahihi,mtu huyo amepewa uzima maana atakuwa ameketi ndani ya Yesu yaani ndani ya neno.

02. LINATOA NAFASI YA UTENDAJI KAZI WA ROHO MTAKATIFU.

~Hii ni siri kubwa ya utendaji kazi wa Roho mtakatifu. Roho mtakatifu hutenda kazi katika neno lake. Ukisoma hapo katika kitabu cha Mwanzo 1:1-3,utagundua kwamba neno lilipotamkwa ndipo Roho mtakatifu naye akaingia kazini kulitimiliza. Hata leo ni vivyo hivyo.

03.LINAUMBA.

~Tunajua ya kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu.(Waebrania 11:3). Hapo utagundua pia neno la Mungu litokalo kinywani mwako linafanya kazi ile ile ya kuumba ndio maana tukitamka neno la uponyaji,uponyaji ufanyika,tena tukitamka neno la kuvuka,tunavuka kwa jina la Yesu Kristo.Soma pia ~( Zab.33:6,9 )

04.LINAPONYA.

Bwana Yesu alitamka neno kwa wadhaifu,nao wakapona. Sisi nasi leo,twataamka neno la Mungu kwa wadhaifu,wagonjwa nao hupona. Ukisoma katika Mathayo 8:7-8,13. Pia Matendo 14:8-10. Maandiko hayo yote mawili yanaonesha kwamba neno la Mungu linaponya,ona~Yesu alitamka kisha mgojwa akaponywa pia Paulo naye alitamka neno kwa yule kiwete naye akaenda saa ile ile.

05.LIMEBEBA MIUJIZA YA KWELI.

~Suala la miujiza lipo hata kwa shetani lakini ukweli ni kwamba miujiza ya Mungu ndio miujiza ya pekee yenye ukweli kwa sababu imejengwa katika misingi ya neno la Mungu,(tazama hili katika miujiza ya Musa na ya wale waganga, maana Musa alifanya nyoka,nao wakafanya nyoka lakini nyoka wa Musa akawala nyoka wao.shetani anaweza akafanya ajabu fulani,lakini muujiza wa Mungu ni mkuu kuliko hiyo ya shetani.)Tazama neno la Mungu lilivyobeba miujiza na ishara~Marko 16:20

06.LINATAKASA ROHO ZETU.

Imeandikwa“Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.”Yoh.15:3. Andiko hilo linatuonesha ya kwamba usafi uliofanyika hapo umetokana na neno la Mungu.

Lakini pia imeandikwa “ Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;” Waefeso 5:25-26

07.LIMEBEBA UWEZA NA NGUVU.

Ipo tofauti kati neno uwezo,na neno uweza. Uwezo ni nguvu fulani ya kawaida ya utendaji kazi,lakini uweza ni nguvu ya ki~ungu,ambayo hakuna mwenye nayo isipokuwa MUNGU tu. Uweza huu upo pia katika neno lake MUNGU. Neno la Mungu linapotamkwa basi ujue ipo nguvu ya utofauti kabisa ifanyayo kazi na lile neno.( Mwanzo~Ufunuo)

08.NENO LA MUNGU NI KWELI YOTE.

Kama vile tulivyoona hapo juu ya kwamba neno la Mungu linatakasa,maana neno lake ndio kweli ~Yoh.17:17. Hakuna mahali pengine ambapo tutapata kweli yote isipokuwa ndani ya neno la Mungu tu.

09.HUTUTUNZA KWA USAFI.

~Wale waliookoka,kisha wakadumu katika neno la Mungu hujikuta wakizichukia dhambi walizokuwa wakizifanya hapo awali. Na kile kinachowafanya kuchukia dhambi ni kiwango cha neno la Mungu ndani yao. Zab.119:11

10. LINAHUSIKA KUTUZAA UPYA KWA MARA YA PILI.

~Mpendwa,nje ya neno la Mungu hakika hakuna awezaye kuokoka. Maana inawezekanaje mwenye dhambi akaokoka pasipo kuvutwa na lile neno la Mungu? Basi sharti alisikie neno ndipo afanye maamuzi. “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.” 1 Petro 1:23

11.NENO LA MUNGU LINAKUZA ROHO ZETU.

~roho zetu hazikui kwa chakula cha kibinadamu bali zinakuwa kwa chakula cha kiroho ambacho ni neno la Mungu. Hivyo kama tujuavyo kazi ya chakula ni kumkuza mtu,kumpa nguvu,kumpa kuishi. 1 Petro 2:2

12.NENO LA MUNGU NI SILAHA DHIDI YA NGUVU ZA GIZA.

~Yesu alimshinda shetani kwa neno tu ( Mathayo 4:1-11) Ikiwa Yeye Bwana alimshinda shetani kwa neno la Mungu basi nasi ni lazima tutumie silaha hii ya neno la Mungu; ili tumshende shetani,Soma tena Waefeso 6:17 N.K

13.NENO LA MUNGU NI MBEGU IPANDWAYO MIOYONI MWETU.

~“Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.”Luka 8:11 Soma habari ya mpanzi yote~Mathayo 13:1-43

Tarajio kubwa kwa mbegu iliyopandwa ni kukua na kuongezeka.

14. LINATUPA NGUVU YA KUOMBA.

~Ikumbukwe kwamba neno ni mbegu,maombi ni kama maji. Mbegu pasipo maji kamwe haikui,bali hufa pia maombi pasipo neno la Mungu hayana muelekeo mzuri. Neno la Mungu litakuongoza katika maombi yako ya kwamba nini cha kuomba na nini si cha kuomba kwa wakati. Tazama maisha ya akina Danieli,Hanania,Mishaeli na Azaria,wakaomba ,maana walikuwa na maarifa ( Danieli 2:17-19)

15. NI CHAKULA CHA ROHO ZETU.

~ Mwili hulishwa kwa chakula cha kibinadamu,roho hulishwa kwa neno. Mtu hataishi kwa mkate tu ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu~ Mathayo 4:4

~Hayo ni machache kati ya mengi,nimeona nikuandikie hayo ili uyapate kuyajua. Lakini wapo watu ambao wana ugumu mkubwa sana wa kusoma neno la Mungu. Wengine wakianza kusoma tu,mara husinzia. Wengine wakisoma hawaelewi hata kidogo,uchovu gafla uwakamata. Naomba ukiwa wewe ni mmoja wapo kati ya watu wa namna hiyo,naomba unipigie simu hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.