DAR ES SALAAM WALIHITAJI TAMASHA LA PASAKA

 Na Mwandishi wetu.

Wadau wa muziki wa injili wa jijini Dar es Salaam wameingiwa na hofu juu ya Tamasha la Pasaka kama mwaka huu litafanyika ama litaishia mikoani kwa mara ya kwanza katika historia yake tangu lianzishwe mwaka 2000.

Hofu ya wadau hao kwa tamasha hilo inatokana na hatua ya waratibu wake Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam kuitaja mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga pekee, hivyo wapenzi na mashabiki wa jijini Dar es Salaam kuhoji kulikoni.

Akizungumzia hilo, Anastazia Ferdinand Malinza wa Machimbo, Temeke jijini Dar es Salaam, alisema ameshtushwa kuona waratibu wanataja tamasha hilo mikoani tu na kujiuliza kuna kitu gani kimetokea.

“Kwa miaka mingi tumezoea liwe Tamasha la Pasaka au Krismasi, limekuwa likianzia jijini Dar es Salaam ndipo liende kwingineko mikoani kulingana na uwezo wa waratibu, lakini safari hii tunasikia tu Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,” alisema Annastazia.

Alisema akiwa mpenzi na shabiki wa tamasha hilo ambalo limekuwa likifanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa miaka mingi na baadaye kuhamia uwanja wa Taifa kwa miaka ya hivi karibuni, kama litafanyika mikoani tu, wao wa Dar es Salaam watakuwa hawajatendewa haki.

“Kama Msama na Kamati yake wataamua tamasha hilo lifanyike mikoani tu, jamani watakuwa hawajatutendea haki kabisa kwa sababu ni tukio ambalo tumelizoea kila mwaka tumekuwa tukienda kupata baraka na watoto wetu,” alisema.

Ameongeza kuwa kama ni kweli Tamasha hilo halitafanyika jijini Dar es Salaam, litakuwa ni pigo kwa wapendwa ambao mara zote wamekuwa wakiliunga mkono tukio hilo ambalo mbali ya kubeba ujumbe wa neno la Mungu, pia huyafariji makundi maalum.

Akizungumza kwa njia ya simu jana kuhusu maoni hayo, Msama alisema ni kweli Tamasha hilo limekuwa likianzia jiji Dar es Salaam kila mwaka kabla ya kwenda mikoani, lakini mwaka huu wamepanga lifanyike mikoani tu kutokana na sababu maalumu.

Alisema, sababu ya kuifanya hivyo ni kutokana na matamasha mengi kufanyika jijini Dar es Salaam, hivyo mpango uliopo ni kuhamia mikoani kwa miaka mitatu mfululizo na kuwataka wadau wa mikoani kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.