HOJA: TUACHE HOFU BALI TUWE TAYARI HATA KUFA

Askofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission International 
©ebibleteacher
Wiki hii nzima kwenye vipindi vya TUAMKE PAMOJA kupitia WAPO Radio nimewasilisha jumbe mbali mbali zenye kuwaandaa washiriki wangu kujengeka kiimani ili waweze kukabiliana na changamoto za kiimani zinazotukabili kila siku. Sehemu ya jumbe hizo ni pamoja na kujitahidi kupambana na hofu pale tunapokabiliana na vitisho na badala yake tuwe tayari hata kufa kuliko kiikana imani kwa kuogopa kufa:

Kupiga yowe kwa hofu

“Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, jipeni moyo ni mimi; msiogope.”(MT.14:26-27)

Yowe maana yake ni “kilio cha hali ya juu sana, hasa kwa kuomba msaada.”! Hofu inapomwingia mtu haina jambo la matumaini, ila ni vitisho vya maumivu makali na mauti. Na nafsi ya binadamu inatishwa sana na kila tisho la mauti.

Hawa ni wanafunzi wa Yesu waliomwona akija huku anatembea juu ya maji, wakamdhana kuwa ni mzuka/mzimu/ na mara wakaogopa kwamba, unakuja kuwazamisha majini.

Hali hii inaendelea kuwatokea wacha Mungu katika maisha ya kila siku. Mara tunapojikuta ghafla tunakabiliana na hali ya hatari inayotishia maisha, tunaingiwa na hofu na kuanza kupiga mayowe= kuna maombi ya mayowe.

Kuna vilio vya hali ya juu sana vinavyofanyika kwenye nyumba za ibada na huduma za maombezi ili kuomba msaada kwa Mungu lakini si kwa njia sahihi. Huwezi kuomba na kujibiwa huku umejaa hofu. Ndiyo maana kitu cha kwanza kuwatuliza wanafunzi wake ni kuwaambia

“Jipeni moyo” Maana yake “dhibiti wenyewe kwanza hali ya kuogopo” kulikopitiliza.
Ukitafakari msamiati wa “kujipa moyo” utagundua hapo si suala la kupata msaada kutoka mahali! Kumbuka Yesu hakusema “nawapeni moyo ili msiogope” bali alisema “jipeni moyo msiogope”

Ni suala la “kujitawala kibinafsi” yaani “kujizuia kibinafsi usitawaliwe na hofu”! Unajua hofu haimwingii mtu pasipo kuiruhusu. Kila mtu ana uwezo kamili wa kuzuia hofu isimwingie, tatizo hatuna elimu ya kuutumia.

Natambua kwamba si jambo jepesi “kudhibiti hali ya kuingiwa na hofu” kwa sababu vitisho vyake pia si mzaha wala nadharia tu na mazingira halisi na hali halisi. Lakini pamoja na hali halisi, bado kila mmoja wetu ameumbiwa uwezo wa “kudhibiti hali ya kuingiwa na hofu”! Ni wakati wa kuanza mazoezi ya kiroho ya kudhibiti hofu.

Na njia pekee ya kudhibiti hofu ni IMANI kwa Yesu Kristo. Ukifanya zoezi la kuchochea imani ikajaa moyoni, kamwe HOFU haiwezi kupenya na kuingia moyoni mwako hata kama uko kwenye mazingira hatarishi kupindukia. Utashangaa katika mazingira ambayo watu wengine wanaogopa mpaka wanazirai, wewe ndio unafanya kazi ya kuwafariji na kuwahimiza “wajipe moyo wasiogope.”

Unajua wacha Mungu wengi wanaogopa wakidhani hii ni sifa ya kuwasaidia kupata msaada kutoka kwa Mungu. Mungu anavutiwa na IMANI tuliyo nayo kwake na si HOFU tuliyo nayo kwa Shetani. UNAPOJAA HOFU MAANA UNAMFANYA SHETANI KUWA NA NGUVU KULIKO MUNGU na hali hii inamuudhi Mungu. LKINI UKIJAA IMANI kwa Mungu unadhihirisha kwamba MUNGU ni Mkuu kuliko Shteni na vitisho vyake, na MUNGU ni MWAMINIFU kwa ahadi zake, hata kama zinaonekana kuchelewa bado zitatimia.

Yesu anatarajia wanafunzi wake
kuwa waaminifu hata kifo

 “Usiogope mambo yatakayokupata, tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, name nitakupa taji ya uzima.” (Ufu. 2:10)

Usiogope yatakayokupata: Unajua maana yake? Maana yake kuna mambo yatakayokupata; mambo hayo hayatoki kwa Mungu bali yanatoka kwa Ibilisi; na mambo hayo si mazuri bali ni mateso na kashfa na vitisho vya mauti.

Yesu hakusema “Usiogope hayatakupata”; alisema usiogope “mambo yatakayokupata”! Mara nyingi sisi tunaomba sana Yesu atuepushe “mambo magumu na mabaya yasitupate. Lakini tunasahau kwamba yeye mwenye alikwisha kututahadharisha kwamba ulimwenguni tutachukiwa na kuudhiwa kama yeye mwenyewe alivyochukiwa na kuudhiwa. Ndio maana hapa hasemi hayatawapa bali vumilia yatakapowapata.

Natambua sana sisi tungependa kuendelea kuishi maisha yasiyo na misukosuko ya kiimani. Na ni maombi yangu kwa ajili yako kwamba uweze kuishi katika utulivu usiona na maudhi na majaribu. Lakini changamoto haziko kwa Mungu bali zinatoka kwa adui Ibilisi. Na ameruhusiwa kwa muda mfupi atumie fursa ya kutujaribu ili tuthibitike kiimani kwamba tunampenda Mungu kwa utashi wetu au tumeshinikizwa.

Lakini wakati wote ambapo tunapitia katika mitihani ya imani Mungu yuko pamoja nasi kuhakikisha kwamba hatujaribiwi kupita uwezo wa imani yetu kwake. Vigezo vya kujaribiwa kwetu vimezingatiwa kikamilifu.

Hata hivyo sehemu ya ujumbe huu iko kwenye tamko la Yesu kuhusiana na ukomo wa kuvumilia. Yesu anasema hivi “…..uwe mwaminifu hata kufa…….”! Sisi huwa tunajiwekea muda wa kuvumilia mambo magumu tunayopitia kwa kufikiri kwamba ukomo huo ndio kigezo cha Mungu kutuondoa katika mapito magumu. La hasha. Kigezo cha Mungu kwetu ni tunapovumilia mpaka mwisho wa uhai wetu.

Tunamwamini Mungu na kumtumia yeye bila kulegeza msimamo wa imani yetu MPAKA KUFA. Tunavumilia katika mateso dhidi ya IMANI mpaka KUFA. Hata tukifanyiwa maovu kwa makusudi ili kutushawishi tubadili msimamo kwa ajili ya kupunguza ukali wa mateso bado tunasimama imara kuvumilia MPAKA KUFA.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.