SOMO: KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU (6 & 7) - MCHUNGAJI MADUMLA

Mchungaji Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kusoma sehemu iliyopita Bonyeza hapa

Karibu tuendelee kujifunza;

04.SIFA KUU ZA KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU.

Kila karama ya Roho mtakatifu ina sifa yake ya kipekee kabisa.Upekee huu unaitambulisha karama husika. Mfano sifa za karama za kusema,ni tofauti na sifa za karama za ufunuo,tena sifa hizo zinatofautiana na karama za uwezo(nguvu). Lakini katika hayo yote,zipo sifa zinazofanana ambapo kila karama ni lazima iwe na sifa hizo. Sifa hizo ni kama ifuatavyo;

Karama zote hutolewa na kusimamiwa na Roho mtakatifu.~Yeye Roho ndio atoaye karama na kuzisimamia kama apendavyo Yeye“ lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” 1 Wakorintho 12:11

Karama zote zimejawa na ishara,ajabu na miujiza. ~Mbali na karama ya matendo ya miujiza,bali ukweli ni kwamba;kila karama imebeba miujiza kwa sababu anayepafomu ni Roho mwenyewe. Mfano ukiziangalia karama zote za Roho mtakatifu utagundua kwamba,kuna nguvu isiyo ya kawaida ya wanadamu,nguvu hii ni ishara,ajabu na miujiza kutendeka kwa nguvu hii.

Karama zote hutumia watu,na kutumika kwa watu.~ ili karama ifanye kazi yake,basi ni lazima iwe ndani ya mtu aliyepewa na Roho mtakatifu lakini pia mtu huyo mwenye karama huitaji watu ili karama yake ifanye kazi. Hakuna karama inayotenda kazi pasipo watu.

Zinafungua wale waliofungwa~Kila karama ni lazima iwaweke huru watu hata kama ni karama za lugha,karama za kufasiri lugha au karama za unabii~zote hizi na nyinginezo zinatufanya kufunguliwa. Mfano,karama za lugha,zinaweza kutufungua kiufahamu kile Mungu asemacho kwetu alikadhalika karama ya unabii. Karama za uponyaji,zinatuponya roho,nafsi na miili na yetu.

Karama zote humuinua Mungu.~Karama za Roho mtakatifu ni zile zenye kumuinua BWANA MUNGU. Sifa zote na utukufu wote huishia kwa Mungu. Ukiona mtu anajipa sifa na utukufu katika karama aliyonayo,basi ujue mtu huyo atakuwa amepungukiwa na kitu fulani kwenye karama yake. Mfano;mwenye karama ya uponyaji,aponyaye ni Mungu ndani yake,wala si yeye,hivyo haipaswi kujiinua na kujisifu. Leo shida hii imelikumba kanisa,maana wapo watu wenye kujisifu kana kwamba wanaponya wao,utakuta mtumishi amejiita majina mengi ya sifa,na hata kudiriki kusema yeye ndio Mungu aponyaye,haya ni machukizo mbele za BWANA.

Zinatenda kazi kwa wanyenyekevu na wapole wa moyo. ~Waweza kujifunza maisha ya Bwana Yesu jinsi yalivyo. Yeye ni mnyenyekevu na mpole wa moyo (Mathayo 11:29). Unyenyekevu na upole wa moyo ndio sura yenyewe ya mkristo. Mtu mwenye karama ya aina yoyote ile anapaswa kuwa mnyenyekevu yaani awe ni mtu wa kujishusha wakati wote na kukubali aibu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu. Lakini tazama hali ilivyo leo,utakuta mtumishi hawezi kutembea na miguu ( yaani hata kwa dala dala )aendapo katika huduma,ni lazima akodiwe gari tena gari ya thamani,la kama hakuna gari basi haendi!!!

Mfano ulio hai ni huu hapa; “…mwaka fulani,nilikuwa nimeenda katika huduma huko Tukuyu (Mbeya),nilikuwa nimeambatana na baadhi ya wachungaji na waimbaji niliotoka nao huku Dar,tulipofika Tukuyu majira ya usiku kama saa mbili hivi,kisha tukapelekwa hotelini kwa mapumziko ili kesho yake tuanze huduma ya mkutano wa nje. Tukiwa hotelini,muimbaji mmoja tuliyetoka naye Dar,alikataa kulala katika hoteli ile akisema eti ile ni hoteli ya kiwango cha chini hali yeye ni muimbaji supa staa(muimbaji wa viwango vya juu). Basi,akatuacha, akaenda kulala anakukojua yeye. Akawa analalamika hata allowance ( posho ) aliyolipwa kwamba hamstahili ni ndogo mno.Hivyo akahudumu ili mradi tu,waswahili wanasema bora liende. Mtu huyu alitaraji kulipwa vizuri,ale vizuri na kulala katika hoteli za kisasa ndipo atoe huduma ya uimbaji,~Aah Anyway! Haya yote huonesha hakuna unyenyekevu kabisa yake...”

Karama hazina gharama za kulipia pesa.~ umepewa bure,toa bure.( Mathayo 10:8)

“Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.” Matendo 8:18-22

Simoni alidhania kwamba karama inaweza kununuliwa kama bidhaa,kumbe karama ya Mungu haipatikaniki kwa mali. Hali ya namna hii hata leo ipo,tunaona baadhi ya watu wakiomba kupewa karama kwa pesa au mali zao. Utakuta mtu kanisani unapewa wadhifa fulani wa kiroho kwa sababu anapesa na mali nyingi,wengine huitwa wazee wa kanisa,wengine hata huitwa manabii,lakini ukichunguza watu hao utagundua utumishi wao ni kwa sababu ya pesa wanazotoaga. Lakini utambue kwamba sifa ya karama haipatikani kwa pesa. Wengine,watumishi wa Mungu hawafanyi maombi mpaka ulete pesa kwanza tena sio kajipesa,bali pesa ya kueleweka. Hii ni hatari sana,mtu wa namna hii kwa kweli hakutumwa na MUNGU bali amejituma yeye mwenyewe na hukumu ipo juu yake.

Karama hutegemeana~Sifa hii ni ya muhimu sana,maana haiwezekani mtu mmoja akapewa karama zote tisa. Bali kila mmoja hupewa kwa sehemu ili kufaidiana sote. “ Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.” 1 Wakorintho 12:7. Ni ajabu kumkuta mtu mmoja yeye hunena,hutafsiri lugha,hutoa unabii,kisha akawa na neno la hekima,kisha neno la maarifa,kisha akapambanua roho,tena mtu huyo huyo akawa na karama ya imani,akawa na uponyaji kisha akawa na karama za miujiza. Ukimuona mtu wa namna hiyo lazima ujiulize je inawezekana?!! Bali tumepewa karama kwa sehemu tu ili tufaidiane.

Karama yoyote ile haipatikani kwa kusomea shule~ Huwezi kusomea karama,bali karama zinatolewa na Mungu. Mfano mtu hawezi kwenda kusomea karama ya kunena kwa lugha. Au mtu hawezi kusomea karama za miujiza. Shida hii imeikumba kanisa la leo,maana wapo watu wameenda kusomea karama alafu baadae wakajiita majina mbali mbali ya karama hizo. Mfano naliona mahali fulani wanafundisha kozi ya kuwa nabii. Huwezi kusomea karama ya unabii,kisha ukawa nabii wala karama ya aina yoyote ile haisomewi. Bali mtu anaweza kuwa na karama fulani kisha akaenda shule kupanua mipaka zaidi ya karama yake katika utendaji kazi kimaarifa. Shule ni muhimu sana kwa kutoa maarifa katika ufanisi wa utendaji kazi…

06. UTAWEZAJE KUITAMBUA KARAMA YAKO?

~Ukweli ni kwamba watu wengi leo hawazitambui karama zao hali wao ni wakristo. Hali hii inawapelekea kushindwa kulijua kusudi la Mungu ndani ya maisha yao. Ikumbukwe ya kwamba,kila mmoja anakusudi maalum;hakuna aliyezaliwa bahati mbaya!Awali ya yote tujikumbushe tena; kila mkristo ana karama yake kwa kumfaidia mwingine maana sote tu viungo vya Kristo ~1 Wakorintho 12:12. Mkristo mwenye karama ni yule aliyeokoka yaani ni yule aliyempa maisha yake BWANA YESU,naye huongozwa na MUNGU.

Ikumbukwe tena; Siku ile ya wito wako pale unaokoka,Roho mtakatifu anaweka kipawa chake ndani yako,kipawa(karama) cha kutumika katika ufalme wa Mungu. Kutoka siku hiyo karama imezaliwa ndani yako,tayari kwa ajili ya kutumika. Hivyo Karama inaachiliwa na Roho mtakatifu ndani ya mtu,mara nyingine Roho anamtumia mtumishi wake. Tunaona hili kwa Paulo huko Rumi;“ Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara.” Warumi 1:11

“ Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.” 1 Wakorintho 7:7 Kile asemacho Paulo hapa,ni kwamba anatamani kila mtu akautumie uweza wa ki-Mungu uliopo ndani yake yeye mwenyewe. Huwezo huu ni kipawa cha Mungu mwenyewe kilichopo ndani yako wewe. Njia zifuatazo zinaweza kukufanya utambue karama yako;

(i) Kudumu katika mfumo wa maisha ya mafundisho na maombi~njia hii ni ya kwanza kabisa yenye kumtengeneza mtu aliyeokoka kukuulia wokovu wake. Kipindi hiki,cha mafundisho ya neno la MUNGU na maombi kinakufanya ukue kiroho maana karama inategemea ukuaji wako wa kiroho. Kukosa mafundisho ya neno la Mungu ya kina pamoja na maombi endelevu kumewafanya wengi wasiweze kutambua karama zao. Waweza kujipima wewe mwenyewe kiwango chako cha kula neno la Mungu kwa siku pamoja na maombi kikoje?,kisha jiangalie kwa mwezi,sasa;tathimini maisha yako ya wokovu kwa ujumla,kwamba yakoje? Je ni kweli umedumu katika fundisho na maombi? Utagundua kwamba si kweli,hujakaa sawa sawa kimafundisho wala maombi,na hali ikiwa ndio hivyo, basi je utatambuaje karama yako?

Karama nyingi zinavikwa kwenye maombi katika Roho. Kwa njia ya maombi,wengine uanza kunena,kupata maono,kujawa na ujasiri wa kuhubiri,kupokea nguvu ya imani (Matendo 13:2) N.K ~Maombi yanasababisha karama nyingi kujitokeza taratibu. Mfano ni huu; unaweza ukawa una imani fulani hivi,ile imani ya kawaida kabisa. Lakini kupitia maombi endelevu,gafla unajikuta ukivikwa imani isiyo kawaida,kiasi kwamba unaona mambo yatarajiwayo na hakika. Hii,sasa inavumbua karama ya imani. Wakati mwingine Roho mtakatifu anaweza akakuonesha orodha ya watu wa kuwaombea,na ukaanza kuwaombea kwa muda mrefu hivi,na kumbe Roho anamakusudi ya kukuonesha karama yako ya uponyaji iliyojificha.

Neno la MUNGU lina nafasi kubwa sana katika kuitambua karama yako. Maana vile unavyozidi kukaa ndani ya neno ndivyo ukaavyo ndani ya Yesu,naye Yesu hukaa ndani yako,hapo waweza kuomba lolote ikiwa pamoja na kuomba kufunuliwa karama yako na utatendewa~Yoh.15:7

(ii) Hakikisha unajitenga mbali na maisha ya dhambi~ Mimi ninakuambia hivi kwamba; inawezekana kukaa mbali na anasa za dunia ya leo,tena inawezekana kuishi maisha matakatifu.

Dhambi inaficha karama yako,tunaweza kuona mifano ya watu ambao walitakiwa watumike katika kuinjilisha lakini dhambi ilificha uinjilisti wao,tazama yule mwanamke msamalia aliyekutana na Yesu kisimani. Mwanamke huyu alikuwa ni mwinjilisti,lakini dhambi ikaficha karama yake. Baada ya kuonana na Yesu,tunaona akaenda kuinjilisha;

“Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?Basi wakatoka mjini, wakamwendea.” Yoh.4:28-30.Kitendo cha kuzitangaza habari za Yesu,ni kitendo cha kuinjilisha~Ona sasa,biblia inaeleza kwamba watu wa mjini baada ya kuelezwa habari za BWANA Yesu walitoka mjini na kumuendea.

Mfano mwingine waweza kuona kwa yule mtu aliyekuwa na jeshi la mapepo. Baada ya kutokwa na nguvu hizo za mapepo,alioshwa kwa neno la Bwana Yesu,kisha tunaona akienda kuhubiri habari za Bwana Yesu ndani ya miji kumi~Dekapoli ( Marko 5:1-20)

Leo hii;Wapo watu waliookoka nusu nusu kwamba Mungu kidogo dhambi kidogo tena papo hapo ukiwakuta wanaomba,maombi yao ni ya kulia kwa habari ya kutaka kuzijua karama zao. Watu hawa wamesahau kuwa,maovu yao yanawafarikisha wao na Mungu ( Isaya 59:2 ). Walokole wengi leo wameshindwa kujua karama zao sababu ya kushindwa kuishi maisha matakatifu,hii ni shida kubwa sana. Jitahidi kuepukana na maisha ya kidunia,wewe ni mwana wa Mungu.

(iii) Angalia unapenda kutumika eneo gani,yaani unapenda kufanya nini haswa katika ufalme wa Mungu. ~ Ni lazima ujihoji mwenyewe kile ambacho unapendelea kufanya katika kazi ya BWANA. Je unapenda kuimba,na ukiimba unapata bubujiko la rohoni? Au,Je unapenda kuinjilisha,unajisikia furaha ya moyoni ukilinena neno la Bwana,Au Je unapata ndoto mara kwa mara,kisha ndoto hizo zinajidhihilisha? Au Je unaona mambo ya siri ambayo wenzako hawaoni?.N.K

Vyote hivyo vinaweza vikawa vyanzo ya karama yako. Ukiona unapitia katika hali hiyo,basi ujitahidi kuomba kwanza umwambie Mungu azidi kujidhihilisha na akueleze ni nini haswa cha kufanya. Tena,ni lazima ukimbie kwa mchungaji wako na umueleze unaona nini,unaota nini,unajisikiaje ndani yako,ili mchungaji naye akusaidie katika ushauri na maombi.

(iv) Toa nafasi ya kipekee kuombewa na mtumishi wa Mungu kwa kuwekewa mikono,na umuelezee unajisikia unapenda nini katika kazi ya Bwana.~ Mtumishi wa Mungu anayo nafasi kubwa ya kuifichua karama iliyofichwa katika maombi maalum. Akiomba,Roho hushuka na kugusa moyo wako. Je umeshawahi kumueleza mtumishi wa MUNGU vile ujisikiavyo? Fanya hivyo leo,maana inawezekana wewe mwenyewe huelewi cha kufanya,basi nenda kwa mtu wa Mungu akusaidie…

ITAENDELEA…

~ Kwa huduma ya maombezi,usisite kunipigia kwa simu yangu hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.