SOMO:TANGU TUMBONI MWA MAMA - ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: TANGU TUMBONI MWA MAMA


Kuna mambo mazuri na mabaya ambayo asili yake ni tangu tumboni mwa mama yake.

“Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.” Yeremia 1:4-10

Yeremia anaambiwa na Bwana kwamba ameshafanya maamuzi tayari kabla hajazaliwa ili awe mtu wa kung'oa, kubomoa, kuharibu na kuangamiza ili ajenge na kubomoa. Kuanzia hapo tunaona kwamba kumbe Mungu ameweka kusudi kwenye maisha yetu kamba hatujazaliwa.

“Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu”Zaburi 22:10

Unaweza ukaona umetupwa leo kumbe umetupwa tangu tumboni mwa mama yako,
Zaburi 52:3 wasio haki……

Kuna uharibifu unaoanza tangu tumboni mwa mama yako aliyekuzaa, unaweza kumwona mtu ni mzuri anaheshima anapenda watu lakini anahangaika sana kumbe ameanzia tangu tumboni mwa mamayake. Na huyo anatakiwa afunguliwe leo kutoka kwenye kifungo hicho alichofungwa tumboni mwa mamaye

“Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa.” Matendo ya mitume 14:8

Tunaona watu wengi wanakuwa wameanza kuchukiwa tangu tumboni mwa mama yao, watu wengi wanaishi maisha ambayo walianza kuyaishi tangu tumboni mwa mama yao. Na pia mtu anaweza kuishi maisha ya aina fulani kutokana na jina alilopewa wakati wa kuzaliwa.

Kwenye Biblia tunaona Yusufu akazaa mtoto akamwita jina lake manase maana yake Bwana amemsahaulisha tabu yake, ina maana alikuwa ana shida nyingi kwenye maisha yake na Bwana akaamua kumsahaulisha taabu yake kupitia mtoto huyo, Yusufu akazaa mtoto mwingine Efraimu maana yake 'zaa matunda'.

Hata Tanzania yetu hii matatizo yake yameanzia tangu tumboni mwa mama Tanzania na mpaka atakapoharibiwa ndipo itakapokombolewa na kuwa salama.

Mwanzo 25:23 “Bwana akamwambia,Mataifa mawili yamo tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, na mkubwa atamtumikia mdogo.”

Huyu ni Mama aliyekuwa mjamzito aliitwa Rebeka alikuwa mjamzito wa watoto wawili na tumbo lilikuwa linamuuma sana akaamua kwenda kwa mtumishi wa Mungu na ndipo akamweleza kuwa yapo mataifa mawili ndani ya tumbo lake. Maana yake ni kwamba hata wewe tangu ulipokuwa tumboni Mungu alikutambua kama taifa. Unaweza ukawa una matatizo leo lakini wamekupiga kuelekea kwenye kesho yako, wala usiogope na hao waliokuzuia na kufanya vita na wewe. Mafanikio yako hayajapangwa leo bali yalipangwa tangu tumboni mwa mama yako.

Huyu mama alikuwa ana watoto tumboni mwake ambao walishafarakana tangu tumboni mwa mama yao, unaweza ukawa na kaka yako au dada yako hakupendi na humuelewi usimshangae bali tambua kwamba ameharibika tangu tumboni amelogwa tangu tumboni mwa mama.

Wagalatia 1:15 “Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake”.

Kuna watu wengine ni wavivu hasa wale ambao wamelogwa tangu tumboni mwa mama zao. wokovu wa siku za mwisho ni wokovu wa kujisimamia mwenyewe sio kusubiria mtu akupigie simu akutie moyo; simama ukauone wokovu wa Bwana. Hata kama umeolewa ukaachika simama tena, hata kama umechumbiwa ukaachika simama tena maana ukianguka chini utasimama tena, ukianguka chini simama tena usisubirie kusimamishwa na mtu simama kama askari wa Bwana, Mungu amekupa nguvu ya kuanza tena. Simama kama mhubiri wa injili songa mbele haijalishi maneno wanayoyasema.Yanayokupata yametengenezwa tangu tumboni mwa mama yako.

Kuna watu wamechorewa mchoro wa maisha yao( Kitabu cha michoro ya giza kinazungumzia kiundani michoro ya giza). Unakuta mtu amechorea namna atakavyoishi tangu tumboni mpaka atakaposoma, atakapoolewa na baadae siku ya uovu iliyopangwa imfikie.

“Ukiri”
Kwa jina la Yesu michoro yote ya giza iliyochorwa juu yangu ninaifuta kwa jina la Yesu, Ajali iliyopangwa inipate ninaifuta kwa jina la Yesu. Mchoro niliochorewa na wachawi naamuru upotee kwa jina la Yesu”

Usife na kile ambacho Mungu amekiweka ndani yako vitoe vyote ili utakapokufa uwe umemaliza kazi yako iliyokuleta hapa duniani, Mungu ameweka hazina ndani yako tangu tumboni mwa mama yako. Usione matatizo uliyonayo ni ya kawaida, fahamu wanajua umebarikiwa tangu tumboni mwa mama yako.

Tumeona huyu mama ndani ya tumbo lake kuna mataifa mawili yaliyofarakana na mkubwa atamtumikia mdogo.

Asili ya Mimba.
Mimba ni uhai kati ya mbegu ya mwanaume na yai la mwanamke ambayo zikikutana uhai unaanza kutokea.

Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”

hili ni jambo la ajabu ambalo lilitokea kwa binti mmoja aliyejiliwa juu yake na akawa mjamzito. Roho mtakatifu alimjiia na nguvu za aliye juu zikamfunika na kitakachozaliwa kitaitwa mwana wa Mungu. Hivyo hivyo na mimba ya mtu inaweza ikafunikwa na uvuli wa mauti na nguvu za kutoka chini na kitakachozaliwa kikawa cha shetani.

Luka 1:15 “Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.”

kumbe upo uwezekano wa roho ya kuzimu ikakuingia tangu tumboni mwa mama yako na ukawa mtu wa aina fulani. Kumbe kuna roho inayowekwa ndani ya mtu tangu tmboni na makao yake yakawa ya tofauti sababu ya roho aliyowekewa tangu tumboni.

Yohana alipozaliwa alikuwa wa tofauti sababu ya roho iliyomwingia tangu tumboni ndio iliyompelekea kuwa vile alivyo. Kuna roho inaweza kumwingia mtu akawa anastaili ya maisha ya tofauti kwenye kula na kuvaa.

Mtu ana roho iliyomwingia tangu tumboni ikambadlisha hatima yake na kupindisha maisha yake asiwe mahali anapotakiwa kuwa kwasababu walichungulia wakaona asili yako tangu ukiwa tumboni mwa mama yako ni kustawi, utajiri, mafanikio, utawala hivyo wakaamua kupindisha maisha yake ili asije akatimiza lile kusudi lake.

“Ukiri”
“kwa jina la Yesu roho iliyotumwa inifanye kama nilivyo leo ninarudi mpaka kwenye tumbo la mama kwa jina la Yesu”

Mungu ana macho ya kumwona mtu hata kama akiwa mbali, akakuita. Alikuwepo mtu mmoja aliyeitwa Samsoni ambaye alizaliwa na wembe haukupita kichwani mwake sababu alichaguliwa na Bwana tangu tumboni. Hapa katikati wakajaribu kuingilia kusudi lake la kuzaliwa na kumtoboa macho huku wakianza kufurahia wasijue kusudi la Mungu huwa halizuiliki na aliyopangiwa mtu hayawezi kuzuilika.

Na makosa yako yasikutenge na Bwana wala shida yako isikutenge na Bwana wewe simama ukatimize kusudi ulilopangiwa na Bwana. Haijalishi vifungo ulivofungwa kusudi la Mungu kwenye maisha yako lazima litimie kwa jina la Yesu.

Haijalishi wamekutoboa macho yako, waliokuzomea, waliokufunga minyororo lazima iwe mwisho wao kwa jina la Yesu. Wakati samsoni anazomewa na wafilisti mkuu wa wafilisti alikuwepo, na majeshi ya wafisti yalikuwepo, na mungu wao wafilisti alikuwepo na wote wakateketezwa na Samsoni siku ile.

Penina alikuwa anazaa wakati hana alikuwa hajazaa na akawa anamzomea sana hana. Na Hana alipoona madharau yale akaamua kwenda kwa Bwana akaanza kuomba na mtumishi wa Mungu akamwona na kumwuuliza anataka nini ndipo akamjibu na yeye akamwambia nenda imeshakuwa kwako. Leo Bwana anasikia maombi yako na tayari ameshakujibu kama ulivyoomba.

“Maombi ya mwongozo”

“Katika jina la Yesu ninakomboa tumbo lililonizaa kwa jina la Yesu, magonjwa niliyopandiwa tangu tumboni ninayateketeza kwa jina la Yesu, naharibu balaa na mikosi yote iliyopandwa tangu nilipokuwa tumboni mwa mama yangu kwa jina la Yesu…. Endelea kukomboa tumbo la mama yako ili kuharibu vizuizi vyote ulivyofungwa tangu ulipokuwa tumboni, haribu kwa jina la Yesu, komboa hata matumbo ya bibi wa bibi waliopita kwa jina la Yesu na utakuwa huru. Mashetani na majini mliotumwa kwangu kuanzia sasa vunjika, anayeharibu bahati zangu vunjika kwa jina la Yesu, namharibu aliyeharibu sura yangu kwa jina la Yesu, mtu yeyote aliyeharibu maisha yangu tangu tumboni namharibu yeye kwa jina la Yesu, namharibu aliyeharibu moyo wangu kwa jina la Yesu, navaa umbo la moto ulao natekeza kila aliyeharibu ndoa yangu kwa jina la Yesu, ninasafiri kwenye ulimwengu wa rohoni namfuata aliyeharibu biashara yangu, watoto wangu namharibu kwa jina la Yesu, kila aliyenichorea michoro ya giza namharibu yeye kwa jina la Yesu, aliyeniibia nyota yangu namharibu yeye kwa jina la Yesu, namharibu aliyeharibu ukoo wangu na familia yangu kwa jina la Yesu, katika jina la Yesu kila aliyeharibu njia zangu nambomoa kwa damu ya Yesu, kila aliyeharibu elimu yangu namharibu yeye kwa jina la Yesu namteketeza kila aliyeharibu maisha yangu tangu tumboni kwa jina la Yesu, narudi kwenye kusudi nililopangiwa na Mungu kwa jina la Yesu, naamka tena kwa jina la Yesu, nasimama tena kwa jina la Yesu”.

Luka19:42 - 44 “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”

Bwana Yesu alikuwa akionyeshwa mji wa Yerusalemu jinsi ulivyokuwa mzuri lakini yeye aliuona kama mji ulioharibika na kuangamia, kwasababu aliingia kwenye mji huo lakini wao hawakumpokea na wala hawakufahamu kama amefika kuwakomboa.

Unatakiwa utambue kwamba Mungu ametembelea maisha yako na umekombolewa kutoka kwenye tumbo la mama na yale mabaya uliyopandiwa kwenye maisha yako yameondolewa na umerudi kwenye asili yako uliyotoka nayo mbinguni kwa jina la Yesu kristo Amen.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.