SOMO: ROHO MTAKATIFU NA KARAMA ZAKE (2)

Askofu Sylvester Gamanywa, mwangalizi mkuu, WAPO MIssion International
(1 KOR. 12:4-11)

Jumatatu iliyopita tulifanya  uchambuzi wa fungu la karama za mafunuo ambazo ni neno la hekima, neno la maarifa, na kupambanua roho. Leo tunaanza fungu jipya la karama za NGUVU ambazo ni Imani, karama za kuponya magonjwa, na karama ya matendo ya miujiza.

Karama ya Imani

Awali ya yote, kabla sijaichambua karama ya imani, hebu nitoe tafsiri fupi ya msamiati wa neno imani kibiblia ina maana gani. Imani ni "hisia ya rohoni ya kuwa na hakika na mambo ya ki-Mungu zikiwemo ahadi zake pamoja na kutambua uwepo wake kama Mungu Muumbaji na mwenye uwezo wote, asiyeshindwa lo lote na yuko mahali pote na anajua mambo yote.

Kitabu cha Waebrania kimeandika kwamba: "Basi, imani ni KUWA na hakika ya mambo yatarajiwayo, na bayana ya mambo yasiyoonekana bado." (EBR 11:1)

Imani hii chanzo chake ni Injili ya wokovu inapohubiriwa kwa mwenye dhambi, akaisikia ndipo hushawishika na kuanza KUWA na hakika ya ukombozi wa Yesu Kristo. Kitabu cha Warumi kimeandika chimbuko la Imani kuwa: "chanzo cha imani ni kusikia, na kusikia kunatokana na Neno la Kristo." (Rum.10:17)

Kila mwamini aliyeokoka anayo imani ya Kristo. Kwa imani hiyo, amepokea wokovu na kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Haya sasa tuje kwenye tafsiri ya karama ya Imani kama ifuatavyo:

Karama ya Imani ni uwezo maalum wa Roho Mtakatifu unaoshukia au kujazwa ndani ya mtu ambaye amejaliwa/kutumiwa na Roho kwa ajili ya kufanya jambo/tendo kubwa ambalo liko nje ya uwezo wa kawaida wa kibinadamu. Karama ya Imani ni uwezo maalum wa KUWA na hakika/ujasiri wa kuchukua hatua kufanya jambo ambalo linahitaji uwezo kutoka kwa Mungu peke yake ndipo lifanikiwe

Karama ya imani humwezesha mhusika kukabiliana na changamoto au upinzani mkali na akamudu kushinda wakati waamini wengine wamekata tamaa kabisa. Karama ya imani ni moja ya karama za nguvu ambayo pia huzichochea zile karama za kuponya magonjwa na matendo ya miujiza kutenda kazi zake. 

Na pia ili karama nyingine ziweze kufanya kazi lazima karama ya Imani imwingie muhusika na kumpa uwezo wa kutumiwa kwenye maeneo mengine. Kwa mfano kitendo cha Yesu kutembea juu ya maji kilihusisha karama mbili mojawapo ikiwa ni karama ya imani. 

Kitendo cha kufufua wafu kilihusisha karama mbili ikiwemo karama ya Imani. Kitendo cha Yesu kubariki mikate michache wakala watu zaidi ya elfu tano kilihusisha karama mbili mojawapo ikiwa ni karama ya Imani. Kwa hiyo karama ya Imani ni kama ufunguo wa utendaji wa  fungu la karama za NGUVU.

Hapo awali nilisema kila mwamini Aliyezaliwa mara ya pili anayo imani ambayo ndiyo ilimwezesha kupokea wokovu na baraka za kiroho. Kwa imani hiyo mwamini anahesabiwa haki mbele za Mungu. Lakini si kila mwamini ambaye anaweza kutumiwa na Karama ya Imani.

Karama za kuponya magonjwa

Jana tulianza kulichambua fungu la karama za nguvu ambazo nj Imani, karama za kuponya magonjwa na karama ya matendo ya miujiza: na tukapata kuichambua karama ya imani Leo nataka tuchambue karama ya pili, ambayo ni karama za kuponya magonjwa.  Kabla ya yote nitoe maelezo ya msingi kuhusu suala zima la uponyaji wa magonjwa. 

Kuna tofauti kubwa kati ya uponyaji na tiba. Tiba ni inahusiana na matumizi ya dawa katika kutibu magonjwa. Uponyaji ni uwezo wa kuondoa magonjwa au kurejesha afya njema pasipo matumizi ya dawa au lishe maalum.
Ni kutokana na aina hii ya uwezo wa kuondoa maradhi au magonjwa katika mwili wa binadamu na akarejea kwenye afya njema, akawa mzima inaleta msamiati wa kibiblia wa "Karama za kuponya magonjwa"!

Yesu Kristo ndiye mwanzilishi wa huduma za kuponya magonjwa na akiwa ndiye Mponyaji Mkuu wa magonjwa yote. Aidha, ni Yesu ALIYETOA mamlaka kwa wanafunzi wake wanapotangaza Injili yake wafanye maombezi ya kuponya magonjwa.

Sasa tuje kwenye utendaji wa hii karama za kuponya magonjwa. Hii inaitwa karama za kuponya magonjwa katika wingi badala ya umoja. Maana yake karama za kuponya ziko zaidi ya karama moja. Hizi karama za kuponya magonjwa ziko katika wingi kwa sababu na magonjwa yako ya aina nyingi pia. Kwa mantiki hii kila aina ya ugonjwa ipo karama maalum ya kuushughulikia. 

Lakini pia karama za kuponya ziko katika wingi kwa maana kwamba, Roho Mtakatifu huzigawa karama za kuponya kwa waamini tofauti tofauti badala ya mwamini mmoja kutumiwa katika karama za kuponya magonjwa yote. Wako waamini wanaotumiwa kuponya aina fulani ya magonjwa, au kuponya baadhi ya magonjwa na sio magonjwa yote.

 Huu ni mgawanyo wa Roho Mtakatifu akitaka kuwatumia waamini tofauti ili kudhibiti mtu mmoja kuhodhi kila karama kwa magonjwa yote.


Karama ya matendo ya miujiza

Karama ya matendo ya miujiza maana yake ni uwezo wa kiungu wa kufanya mambo ambayo yako katika uwezo wa asili wa kibinadamu. Kwenye karama ya miujiza kama jina lake lilivyo kazi yake kufanya mambo ya kushangaza na kutisha yaliyoko nje ya uwezo wa kanuni za asili. Maana ndani ya karama ya miujiza ndimo ulimo uwezo wa uumbaji wa kimungu. Mathalan, Yesu kutungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ni karama ya matendo ya miujiza.

Huko nyuma nimeeleza kwamba karama ya kutenda miujiza hufanya kazi bega kwa bega na “karama ya Imani” maana zinategemeana sana, tofauti na karama za kuponya magonjwa. Karama ya matendo ya miujiza inahusisha matendo yote kuanzia kurejesha upya viungo vya mwili vilivyoharibika mpaka uwezeshaji wa vitu chache kutosheleza mahitaji makubwa kuliko uwezo wake wa kawaida.

Kwa kupitia karama ya miujiza, Roho Mtakatifu ndani ya mwamini anaweza kumtumia kufanya jambo ambalo ni la kushangaza na waisoamini wakamtukuza Mungu kwa ajili ya tukio hilo.

Naomba kutoa tahadhari hapa kwamba, kuna vituko vingi siku hizi katika huduma za kimaombezi ambavyo vinaitwa miujiza lakini sio utendaji wa “karama ya miujiza”. Mfano vitendo vya watu kuanguka chini kwa mkupuo vinatafsiriwa kuwa ni “karama ya miujiza” wakati ukweli sio.

Ni kweli kwamba Inashangaza kwa macho! Shetani naye anaweza kuangusha watu saaana tu. Sasa kitu ambacho Ibilisi anaweza kukitumia kwa urahisi kudanganya watu kama kiini macho au mazingaombwe hakiwezi kutafsiri kuwa hiyo ni karama ya miujiza inayotendwa na Roho Mtakatifu.

Karama ya miujiza hutenda jambo ambalo Ibilisi hawezi kuigiza au kulifanya kwenye mazingira ambayo Roho Mtakatifu anatawala.

Kwa mfano watumishi wa Ibilisi nao wanaweza wakacheza na mapepo kwenye mikutano ya hadhara, lakini sio kwamba huwa wanatoa pepo. Wao “wanapunga pepo” badala ya “kutoa pepo”. Lakini matukio yote yanahusisha udhuhuriko wa mapepo. Hapa ndipo inahitaji ile “Karama ya kupambanua roho” ili kutofautisha muujiza wa Roho Mtakatifu na mazingaombwe na viini macho vya Ibilisi.

Itaendelea toleo lijalo
Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.