SOMO: ROHO MTAKATIFU NA KARAMA ZAKE (3)

Askofu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu WAPO MIssion International.
Wiki iliyopita tulifanya  uchambuzi wa fungu la karama za NGUVU ambazo ni karama ya Imani, Matendo ya miujiza na karama za kuponya magonjwa. Leo tunahitimisha kipengele hiki kwa kuchambua fungu la mwisho la karama za MAWASILIANO ambazo ni karama ya unabii, aina za lugha na tafsiri za lugha:
Tafsiri ya Karama ya unabii

Fungu la karama za mawasiliano ambazo ni “karama ya unabii”; “karama ya aina za lugha” na “karama ya tafsiri za lugha” Nitaanza na “karama ya unabii.” Kwanza kabla ya kutafsi karama tuanze na msamiati wa neno “unabii” kwa mujibu wa Biblia.  “unabii” ni ujumbe maalum kutoka kwa Mungu, ukiletwa na Roho Mtakatifu na kufunuliwa kwa mpokeaji/nabii/mtu aliyeteuliwa kwa wakati huo kuuwasilisha ujumbe huo kwa walengwa.

Ujumbe huu wa kinabii unapotangazwa na msemaji aliyeupokea, lazima uwasilishwe kwa lugha inayojulikana na wasikilizaji. Lazima ujumbe huo uwe umebeba taarifa ambazo mlengwa akiusikia atajitambua kuwa ujumbe huo ni wa kwakwe. Kwa maelezo mengine, unabii ni ujumbe wa Mungu kupitia kwa mpokeaji ili auwasilishe kwa walengwa pasipo yeye kuingiza mawazo yake ya kibinandamu.

Sasa tuje kwenye tafsiri ya “karama ya unabii”. Tafsiri nyepesi kueleweka kwa wazi zaidi ni “mpokeaji kupokea “zawadi ya kutumika kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo walengwa wa unabii huo; “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, kuwafariji, na kuwatia moyo.” (1 Kor.14:3)

Watu wengi wana tafsiri ya unabii kama ujumbe unaotabiri kuhusu mambo yajayo au kutabiri mambo yatakayompata mtu binafsi. Hii ni tafsiri ya unabii katika Agano la Kale japokuwa hata kwenye agano jipya ziko aina za unabii wa jinsi hii, hasa kwenye maneno ya Yesu kuhusu mambo yatakayotokea siku za mwisho.

Lakini ukichunguza aina za unabii wa Agano jipya kwa kanisa, utakuta ni ujumbe uliolenga kuwafariji waamini waliokuwa wakipitia mateso kwa ajili ya Kristo, kuwatia moyo waliokuwa wanapambana na changamoto za kiimani ili wajipe moyo wasikate tama, na ujumbe mwingine ulikuwa ni Mungu akiwajenga kiroho waweze kuendelea kuwa mawakala wa siri zake kupitia Injili kwa watu wote.

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba “karama ya unabii” ni ujumbe ambao ukitangazwa na mpokeaji, wale wanaosikiliza wanatambua moja kwa moha kuwa hiyo ni sauti ya Mungu akiongea na watoto wake kama Baba na ni ujumbe unaojitofautisha na binadamu anaposema maneno ambayo ni mawazo yake mwenyewe ya kuwafariji wafuasi wake.

Jumbe ambazo si karama ya unabii ni pamoja na:

1.     “kuwatabiria watu mambo binafsi ya kimwili km maelekezo ya kuoa au kutokuolewa na mtu Fulani,
2.     nabii za kutoza watu fedha ili wapate kuombewa uponyaji wa magonjwa au kutendewa miujiza;

Karama ya unabii huwasilisha ujumbe kwa kanisa au kundi la waamini waliokusanyika pamoja kwa madhumuni ya ibada na ndipo Roho Mtakatifu hutumia fursa hiyo kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Mungu waliyekuwa wakimwabudu kwa wakati huo.

Maadili ya karama ya unabii ni pamoja na pale msemaji anapotoa unabii lazima wawepo wengine wenye karama za kupambanua roho wahakiki kama kweli huo ni ujumbe kutoka kwa Mungu, au ni roho/pepo ya utambuzi au mawazo ya msisimko wa binadamu.

Jambo la kuzingatia ni kwamba karama ya unabii ni mojawapo ya njia ya mawasiliano kati ya Mungu na watoto wake katika kanisa ambao wanahitaji kusikia sauti na kujua anawataka wafanye nini, ili kuchukuliana na mazingira waliyomo.


Tafsiri ya Karama ya aina za lugha

Hii ni karama maarufu sana kwa sababu ndiyo karama ya kwanza inayoanza kutenda kazi kwa kila mtu anayempokea na kujazwa Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza. Aidha hii ndiyo karama ambayo hufanya kazi kwa mwamini kwa muda mrefu kuliko nyingine zote na ndiyo inayofanya kazi ya kuzichochea utendaji wa karama nyingine ili zipate kutenda kazi.

Karama ya aina za lugha ina maana ya uwezo wa mtu kujaliwa kusema lugha mpya amabyo hajawahi kujifunza na maneno yake hayatoki kwenye kumbukumbu ya akili zake kama ilivyo kwa lugha nyingine za kibinadamu. Ni uwezo wa kiungu wa kuzumgumuza lugha mpya, lugha isiyofundishwa na binadamu na isiyotokana na kumbukumbu ya akili za kibinadamu.

Inaitwa aina za lugha kwa sababu ziko aina mbali mbali tofauti za lugha za mawasiliano. Hapa naweza kusema mafungu makuu 3 ya aina za lugha. Fungu la kwanza ni lugha za binadamu ambazo ziko lukuki duniani. Lugha nyingine zilikwisha kufanya na ni nyingine zinazaliwa. Lakini zote ni lugha za binadamu kwa sababu huzungumuzwa na binadamu katika mawasiliano.

Fungu la pili la lugha ni “lugha za viumbe waitwao malaika”. Kumbuka Paulo aliwahi kudokeza kwenye nyaraka zake akisema: “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.” (1 Kor.13:1) Unaona? Hapa tunaambiwa habari za uwepo wa “lugha za wanadamu” na pia kuwa “lugha za malaika”. 

Malaika ni viumbe wa Mungu wanaofanya utumishi katika ufalme na mamlaka zake Mungu. Na kwa sababu nao ni nafsi hai wana akili, hisia na utashi, wanazo lugha zao za mawasiliano. Kusema “lugha za malaika” maana yake ziko aina mbali mbali za lugha za malaika.

Fungu la tatu la lugha ni “lugha ya Mungu” mwenye katika mawasiliano kati ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii ni lugha maalum ambayo ilikuwepo kabla ya lugha nyingine za viumbe hazijakuwepo. Kwa hiyo unaporejea kwenye hii “karama ya aina za lugha” maana yake Roho Mtakatifu ambaye anazijua lugha zote hizi, anao uwezo wa kumwezesha mwamini kunena lugha mojawapo au aina zote za lugha kama atakavyopenda yeye mwenyewe.

Pamoja na hayo yote, lugha muhimu ambayo Roho humjalia kila mtu kuinena kwa mara ya kwanza na kuwezeshwa kuendelea kuongea ni hii “lugha ya Mungu mwenyewe” kwa sababu ndiyo lugha pekee ambayo binadamu akiwasiliana na Mungu, hakuna kiumbe yeyote awe binadamu au malaika anayeweza kugundua maombi au dua zinazowasilishwa kwa Mungu zinahusu nini. Ndiyo maana Paulo akawakumbusha wakorinto wasijisahau kwamba wanaponena kwa lugha hiyo, wasijisumbue kutaka kujua ni nini kinachoongelewa kwa sababu ni siri kati ya mnena na Mungu:

“”Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.” ( 1 Kor.14:2) Unaona hii karama ya kunena lugha ya siri kwa ajili ya mawasiliano ya faragha ambayo hapaswi mtu kuyaingilia kwa kuyajua kwa kuwa hayamhusu.

Lakini pia, hii “karama ya aina za lugha” haiishii kumwezesha mtu kunena lugha isiyojulikana kwa watu wala malaika; pia “karama ya kunena aina za lugha” humwezesha binadamu kusema hata “lugha za malaka”. Na hasa wakati wa maombi, kuna wakati Roho Mtakatifu anaweza kumwezesha mwombaji kuanza kuongea lugha ya malaika wakiwa wanaagizwa kuchukaa hatua au kufanya mambo Fulani ambayo yanahusiana na mwombaji au wale anaowaombea katika roho. Kwa hiyo katika maombi mtu anaweza kuneneshwa lugha ya Mungu, kisha akaneneshwa lugha ya malaika na pia anaweza kuneneshwa lugha za binadamu ikiwa wako watu wasio wasiojua lugha nyingine za kigeni na Mungu akaamua kuwasiliana kwa lugha yaao wenyewe.

Katika huduma hizi za ujazo wa Roho Mtakatifu pamoja na utendaji wa karama zake  kuna mambo mengi yaliyoko nje ya uwezo wa binadamu kufikiri na kutenda isipokuwa kwa kuwezeshwa na Roho mwenyewe.
 
Tafsiri ya karama
ya Tafsiri za Lugha

Karama ya tafsiri za lugha hufanya kazi sambamba na “karama ya aina za lugha.” Kabla ya yote nifafanue kwa ufupi kwamba “karama ya aina za lugha” nayo iko katika wingi badala ya umoja. Maana yake ni uwezo wa kiungu wa kutafsiri lugha zote zisizoeleweka kwa walengwa. Na hasa wenye kuhitaji tafsiri za lugha ni binadamu na malaika.

Tafsiri ya aina ya kwanza ya lugha ni: Ujumbe kutoka kwa Mungu unaokuja kwa lugha isiyojulikana au lugha ya Mungu mwenyewe. Pale ndipo inalazimika Roho huyo huyo aliyeshusha ujumbe huo kwenye kundi la wasiojua lugha hiyo, huteua baadhi ya washiriki kuoa tafsiri ya ujumbe uliosemwa kwa lugha isiyojulikana upate kujulikana kwa lugha inayoeleweka kwa walengwa.  Hii ndiyo Mtume Paulo alikuwa akiitolea mwongozo kwa wakorintho akisema:

“Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja afasiri.” (1 Kor.14:27)

Kuna watu wanaoyatafsiri visivyo maandiko haya wakidai Paulo alikuwa akikataza watu wasinene kwa lugha kanisani. Lakini ukweli halisi alikuwa akizuia watu kusema ujumbe kanisa ambao ni lugha isiyojulikana kwa walengwa.

Na aina ya lugha inayotajwa hapa ni lugha ile ambayo Roho Mtakatifu anashusha ujumbe kutokaa kwa Mungu kuja kwa watoto wake katika kusanyiko. Ili ujumbe huu uwafikie walengwa lazima mwenye kuusema ahakikishe anakuwepo mwenye karama ya kutafsiri lugha aweke sawa jambo hilo. Lakini Paulo hakupiga marufuku kunenaa kwa lugha wakati waombaji wanapowasiliana na MUngu kwa mambo yao ya siri katika roho.

Aina ya pili tafsiri ya lugha ni waombaji wanapojaliwa kuongea lugha za malaika katika ulimwengu wa  roho.  Kama nilivyotangulia kusema huko awali kwamba, Roho Mtakatifu anaweza kuwajalia waomba kutoa tafsiri ya lugha ya Mungu akiwaagiza malaika wafanya mambo kwa ajili ya waombaji au watu wale wanaowaombea. Hii ni tafsiri kwa ajili ya malaika ambao hufanya kazi kwa ajili ya watakaourithi wokovu. Kama ulivyoona karama zote tatu unabii, aina za lugha na tafsiri za lugha zote zinahusiana na mawasiliano tu. 


Itaendelea toleo lijalo...
Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.