HOJA: YOTE YANAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE


©Purity for Life

Yote yawezekana kwake aaminiye ni kauli ya Yesu kwa mtu aliyekuwa na mashaka kama Yesu yuko tayari kumponya mgonjwa wake au la. Katika kumhakikishia kwamba suala la kuponywa au kutokuponywa liko kwenye uwezo wake kiimani:

Sisi wenyewe tunawajibika
kwa mambo yote kuwezekana

Kutokana na maelezo ya Yesu mwenyewe hapa juu inaashiria kwamba, kuwezekana kwa baadhi ya mambo kunatutegemea sisi wenyewe tumesimama vipi kiimani. Sio suala la rehema na huruma za Mungu kwa kila jambo bali sisi tumekaaje katika kuamini na kutegemea na kutarajia kuuona utendaji wake.

“Lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.” (Mk.9:22-23)
Askofu Sylvester Gamanywa

Najua kwamba tumekuwa na uzoevu wa kujizoesha kukiri kwamba HAKUNA LISILOWEZEKANA KWA MUNGU. Natambua kwamba hili ni neno la Mungu na ndivyo lilivyo. Lakini si mambo yote yanaangukia kwa upande wa Mungu peke yake. Kwanza naweza kusema kwamba ni rahisi kukiri HAKUNA LISILOWEZEKANA KWA MUNGU kwa sababu yanamhusu Mungu mwenyewe; na pia ni rahisi kumtupia lawama Mungu kama mambo hayakufanyika kama tulivyomwamini.

Lakini hii kauli ya Yesu kwa mtu mwenye shida yake akiomba asaidiwe na akaambiwa “YOTE YAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE” hii ni changamoto inayoturudia sisi wenyewe. Kumbe sisi wenyewe tunawajibika na tunahusika katika kusababisha MUNGU KUFANYA MIUJIZA YAKE kwetu.  Na pia tunawajibika pia ikiwa Mungu hatafanya miujiza kwa kuwa hatujamwamini ipasavyo.

Hakuna ubishi kwamba Mungu hafanyi sio kwa sababu hataki kufanya bali kwa sababu sisi wenyewe hatujaamini itupasavyo. Kuamini kwetu ndiyo mikono ya kupokelea majibu ya maombi yetu na kuziona nguvu za Mungu zikijidhihirisha katika maisha yetu.

Najaribu kujiuliza huyu aliyemwuliza Yesu akisema UKIWEZA alikuwa na maana gani hasa. Alikuwa na maana tatizo la mgonjwa wake ni kubwa sana ambalo Yesu atashindwa kulitatua? Au alikuwa na maana kwamba Yesu ana hiari ya kumponya au kutokumponya  mgonjwa? Swali la kwanza sioni kama lina mwelekeo huo. Lakini hili na hairi na utashi wa Yesu wa kuponya au kutokuponya laweza kuwa na mantiki zaidi.

Huu ulikuwa ni mtazamo alio nao kwa Yesu kwamba, suala la kupona au kutokupona linategemea ridhaa yake, utashi wake, na utayari wake wa kuponya. Lakini Yesu akamgeukia kwa mshangao akiuliza UKIWEZAAAAAA!!!!! Yote yawezekana kwake yeye aaminiye. Maana yake si suala la hiari na utashi wa Yesu wa kuponya bali ni suala la mwenye tatizo kuamini kwamba inawezekana!

Yote yawezekana tukiwa
na hakika tunaposali

Baada ya kutambua kwamba, suala la kuwezekana kwa mambo yote kunategemea sana imani yetu, na sio utashi wake Mungu peke yake; napenda kuhitimisha kwa kufafanua mchakato kulingana na mwongozo wa Bwana Yesu mwenyewe pale aliposema:“Yoyote myaombayo mkisali aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu.” (MK.11:24)

Pamoja na uwazi wa maandiko niliyonukuu hapa juu, wakristo wengi bado wanapokuwa katika kuwasilisha mahitaji yao kwa Mungu; huwa hawana hakika kwamba yale wanayoomba wanayapokea kutoka kwa Mungu kama walivyoomba.

Kumbe suala la kupokea majibu ya maombi letu liko kwenye ahadi za Mungu mwenyewe kwamba, tukiomba tunapokea wakati huo huo tunapoomba, na ndipo majibu yanafanyika halisi. Nimeshuhudia maelfu ya watu wanaokuja kwenye huduma za maombezi ya ujazo wa Roho Mtakatifu, uponyaji na kufunguliwa kwenye vifungo vya pepo wachafu.

Naanza kwa kutoa neno kama mwongozo wa kuwaandaa kiimani ili wakati wa maombezi wawe tayari kupokea. Lakini bado wengine huwa hawapokei kitu na kurudi kama walivyokuja. Cha ajabu zaidi, wengine waliokuwepo pamoja kwenye maombezi wanapokea uponyaji na ujazo wa Roho Mtakatifu papo kwa papo na wanashuhudia mbele ya kusanyiko ukumbini.

Suala hili limekuwa ni changamoto kwa wengi wakihoji kwamba labda Mungu ana upendeleo. Anabagua kwa kuwajaza wengine na wengine hataki kuwajaza. Hii ni mitazamo hasi ya wengi hasa pale wasipojibiwa wao wakati wengine wapokea majibu ya maombi yao.

Siko hapa kumtetea Mungu maana yeye anajitegemea wala hatetewi na mtu, na wala hahitaji msaada wa mutu kumsaidia jinsi ya kufanya kazi yake. Changamoto ziko kwetu sisi tunaomtafuta Mungu mara nyingi tunashindwa kuzingatia kanuni alizotuwekea katika kuwasiliana naye.

Kama maandiko tuliyosoma yalivyoelekeza ya kwamba, wakati na muda ule ambapo tunawasiliana naye katika maombi, na hasa wakati wa kuomba kupokea vitu vile ambavyo yeye mwenyewe Mungu ameahidi na amekwisha kuvitolea majibu tayari, Yesu ametoa mwongo ulio wazi; kwamba wakati ule tunapoomba ndio wakati huo huo wa kupokea majibu ya maombi yetu.

Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu. Kama ni suala la ujazo wa Roho Mtakatifu, wakati huo huo unapoomba ujazo amini kwamba ujazo huo unafanyika wakazi huo huo unaposali mahali hapo ulipo na sio baadaye. Kwa wenye kuamini hivyo ndio unakuta wanajazwa pale pale na kuanza kufurahia majibu ya maombi yao.

Inawezekana nawe unalo hitaji pengine umelipombea sana kwa muda mrefu, na pengine umeshaanza kukata tamaa ya kujibiwa. Neno la leo ndio hili “Yoyote myaombayo mkisali aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu.”

Mwisho
Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.