SOMO: JAMBO LA KUFANYA MAMBO YAKO YANAPOHARIBIKA

Utangulizi  
Katika maisha ya kawaida kama wanadamu tumekuwa tukishuhudia mambo yetu au ya watu wa karibu yetu yakiharibika na kwenda sivyo. Wakati mambo yanaharibika watu wengi hutafuta kujua sababu ya mambo hayo kuharibika, japo pia wapo watu ambao hawachukui hatua yoyote bali wao hutulia na kukubaliana na hali halisi.

Waswahili hupenda kutumia msemo wa "kutafuta mchawi", wengi hutafuta mchawi wa matatizo yao na hatimaye hujikuta kuangukia kwa mtu au kitu na kuanza kukilaumu kuwa ni kisababishi cha kushindwa kwake.

Watu wote ni wahanga wa tukio la kulaumu mtu, Mungu, shetani, wewe binafsi, hata mazingira, swali linabaki kuhoji kuwa nani alaumiwe katika jambo lako ambalo limeharibika? 
Katika somo hili mwandishi anakushirikisha mambo makuu matano kibiblia ambayo yatakusababisha kuwa vyema wakati mambo yanapoharibika.

Karibu upate kujifunza mambo haya ambayo yatabadilisha maisha yako na kukufanya kuwa mtu usiye wa kawaida hata kama umeshawahi kushindwa sana.

Mwalimu Kelvin Kitaso
VIFAHAMU VITU MUHIMU VITAKAVYOKUSAIDIA KUTATUA TATIZO LAKO NA KUKUTOA MAHALI ULIPO


Sehemu ya Kwanza
Shituka, Zingatia ya Moyoni Mwako

Luka 15:17, “Alipozingatia moyoni mwake, alisema Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa”

2 Wafalme 6:5 “Lakini mmoja wapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimwa kile.”
Nyakati hizi za mwisho kupoteza viwango vya ubora kwa wakristo wengi imekuwa ni kawaida sana na kimekuwa ni kilio cha wakristo wengi. Na imekuwa ni rahisi sana kumkuta mkristo akawa anakuelezea jinsi alivyotembea na Mungu wakati wa zamani, jinsi Mungu alivyojifunua kwake katika nyakati za zamani. Pamoja na masikitiko ya jamii kubwa ya waamini katika kupoteza viwango wengi bado hawajashituka na wanadhani ni majira na nyakati za wao kuwa hivyo au Mungu ameruhusu wao kuwa katika viwango hivyo.

Usidharau na kuona ni kawaida, toka katika uonaji wa kawaida na ushituke. Hauwezi kupata majibu ya tatizo lako kama hujashituka na kuona hilo ni tatizo. Kama unaona ni kawaida na kama umelitafutia lugha nzuri ya kulitetea hili tu lisionekane ni tatizo kamwe haliwezi kuisha. 

Kanuni za ugonjwa hauwezi ukatibika kama haujajulikana ni aina gani ya ugonjwa, kuna hatua za matibabu lakini iliyokuu ni ya mgonjwa mwenyewe kushituka na kukubali kuwa alilonalo ni tatizo na hakuna budi ni lazima lianze kutafutiwa tatizo.

Nina ujasiri mwingi wa kukueleza kuwa huwezi ukatibu tatizo kama hujashituka kuwa unaishi na tatizo.

Tazama mfano wa watawala wa serikali za dunia hii mara nyingi hawawezi kutatua matatizo yanayowakabiri kwa kuwa ni watu wanaopenda kuyafukia matatizo kwa kuyatafutia majina mazuri ili waendelee kuonekana wema machoni pa watu wanao watumikia. 

Tazama hali unayopitia sasa pengine uliwahi kuwa mtu wa aina Fulani au mwenye wadhifa Fulani katika ulimwengu war oho na mapepo kila waliposikia habari zako walitetemeka na kujisalimisha kwa Mungu unayemuabudu, lakini hali ipo tofauti sana kwa leo kwa kuwa hata pepo mmoja ndani ya mtu ukimkemea hatoki, wengi wetu katika hali ya ubinadamu tunapenda kujitetea kuwa nyakati zinabadilika, au majukumu yamekuwa mengi, na sababu nyingine nyingi zifananazo na hizi, ila kwa mtu mwenye kuzingatia moyoni kama mwanampotevu ni lazima ashituke kwanza na kuanza kujifanyia tathimini itakayomsaidia kujua ni wapi ameanguka.

Ukiitazama historia ya yule mwana wa nabii, shoka ilipoingia ndani ya maji hakuridhika kuwa kwa kimo cha maji yale hatoweza kuifuata ile shoka na haitoweza, hakuridhika kupoteza kitu kilichokuwa mikononi mwake. Alishituka sana na akaona bora nipaze sauti yangu kuomba msaada kwa mtu wa Mungu maana kuna kitu kisicho cha kawaida kimetokea katika maisha yake. Sisi pia hadithi zetu hazitofautiani kabisa na hadithi ile ya mwana wa nabii kwa kuwa talanta tulizo nazo si zetu ila tumepewa ili zizalishe na kujenga katika ufalme wa Mungu, na pia karama na huduma tulizopewa ni kama ile shoka ya mwana wa nabii zinatumika kutafutia miti ya kujengea ufalme wa Mungu, au mahali ambapo Mungu atajiwekea maskani. Ukiona shoka/huduma/karama yako imeangukia kwenye maji usitazame hiyo hali kama ni kitu cha kawaida, ni lazima ushituke kwa kuwa hilo jambi si jambo la kawaida, shituka piga kelele hata watu wa Mungu wakusikie maana wanaweza kukusaidia ukairejesha tena shoka yako ili upate kuendelea kuitumia tena.

Zingatia kuwa, Ukishituka shoka lako waweza kulipata tena na waweza rudi kwa baba yako na ukapokelewa tena.


Wiki ijayo tutatazamia namna ya kutibu tatizo lako kwa kuanza kulitafuta chanzo.


Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.