SOMO: KWANINI NI LAZIMA KUSAMEHE (2)

Jumatatu iliyopita tulianza mada kuhusu kusamehe. (bofya hapa kusoma) Nilitaja kuwepo kwa sababu sita muhimu zinazoweza kutusaidia kujua kwanini ni lazima kusamehe. Tuliweza kujifunza sababu nne ambazo ni: 1. Kusamehe ni Tabia ya Mungu, 2. Binadamu wote ni wakosaji, 3. Kusamehe ni Sharti la kusamehewa, 4. Kusamehe kunajenga mahusiano. Leo tunaendelea na sababu mbili zilizosalia:
©Life Hacker
Kunaimarisha afya binafsi

Ni ajabu lakini kweli kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya kutokusamehe na baadhi ya matataizo ya kiafya yakiwepo magonjwa ya kitabia (Non communicable diseases)! Amini usiamini kutokusamehe kuaathiri afya ya mwili. Maandiko yamedokeza kwamba:

"mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo." (EBR. 12:15)

Hapa tunasoma kuhusu “shina la uchungu” moyoni kwamba “linatia unajisi”! Biblia inaposema unajisi ni pamoja na maradhi au magonjwa yatokanayo na athari za kuvunjika kwa uhusiano na Mungu. Uchungu moyoni ni “hali ya kutokusamehe” ndani ya moyo wa mtu.

Askofu Sylvester Gamanywa
Na uchungu ni “Hisia hasi” ambayo husababisha madhara ya kiafya katika mwili kuanzia saratani, maradhi ya moyo, vidonda vya tumbo, maumivu makali mwili na kwenye viungo. Baadhi ya tafiti za kisayansi zinaonesha 61% ya wagonjwa wa saratani wana matatizo ya kutokusamehe. Leo tunayagundua haya kwa sababu ya kuongezeka maarifa ya sayansi. Lakini Biblia ilikwisha kututahadharisha mapema yakisema kwamba:

"Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;  tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi." (EFE. 4:31-32)

Unaweza ukajiuliza kwamba utajuaje kwamba una tatizo la kutokusamehe? Mojawapo ya dalili za kutokusemahe ni kuwa na mtazamo hasi  dhidi ya mtu aliyekukosea. Uzito moyoni wa kutomkubali mtu aliye kuudhi. Kutokutaka ukaribu naye. Kujiepusha au kumkwepa. Kila unapomkumbuka presha inapanda au kichwa kuuma, kukosa hamu ya kula kwa sababu ya mawazo mazito kuhusu makosa uliyotendewa! 

Hasira kupanda kila unapokumbuka alivyokuudhi au anavyoendelea kukuudhi. Mara nyingi hisia hasi dhidi ya mkosaji wako huwa mhusika hana taarifa ya kinachoendelea upande wako mpka uwasiliane naye. Lakini kwa sababu ya tafsiri yako kwamba kila mhusika alifanya au anafanya makusudi kukuudhi unaamua kuchukua hatua dhidi yake za kumkomesha au kumkomoa au kutaka na yeye apate maumivu kama yanavyokusumbua wewe.

Faida za kusamehe ni kurejea kwa mtazamo chanya na hisia chanya juu ya mtu uliyemsamehe. Msongo wa mawazo unaondoka na urafiki unajengeka na afya yako inajengeka.

Kusamehe ni ufunguo wa
kupokea majibu ya sala kwa Mungu

tumekwisha kusoma sababu muhimu 5 za ni kwanini ni lazima kusamehe. Hii sababu ya 6 ni ufunguo wa kujibiwa dua, sala, na maombezi yetu mbele za Mungu. Ufunguo huu unarokana na maandiko yafuatayo:“Kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.” (Mk.11:25)

Haya ndiyo maneno ya Yesu kwetu ya kwamba, kila tunapokusanyika pamoja ili kusali, kufanya ibada au kuomba, sharti la kwanza na muhimu ni KUSAMEHE kama tunalo neno juu ya mtu yeyote.

 Unaona? Maana yake kusamehe ni ufunguo wa kusikilizwa kwa sala na maombi yako mbele za Mungu. Tena ni ufunguo wa kupokea Baraka zitokazo kwa Mungu ikiwamoo kipawa cha Roho Mtakatifu, uponyaji, kufunguliwa katika vifungo vya giza, na mahitaji  mengine.

Tukitazama upande wa pili wa sarafu ni kwamba, KUSALI/KUABUDU/KUOMBA kabla ay pasipo KUSAMEHE ni kizuizi cha kusikilizwa na Mungu, na kutokupokelewa kwa sala na maombi yako.

Ndiyo maana watu wengi wanaokusanyika pamoja kwa ajili ya ibada au maombi hawapokeo majibu ya maombi yao kwa sababu mioyo yao ni najisi mbele za Mungu.

Naomba kueleweka kwamba KUTOKUSAMEHE sio kwamba ndiyo sababu pekee ya KUTOKUSIKILIZWA na MUNGU, ila KUTOKUSAMEHE ni dhambi mbele za Mungu na hivyo kuwa mojawapo ya vizuizi vya kusikilizwa na Mungu.

Kusamehe ni sharti la kufunguliwa
kutoka vifungo vya giza

Kwa kuongezea uzito katika ufunguo wa kupokea majibu ya maombi ni suala la kufunguliwa kutoka kwenye nguvu za giza. Hapa napenda kusisitiza kwamba, kupokea uponyaji wa magonjwa au kufunguliwa kutoka vifungo vya shetani, ni aina mojawapo ya kujibiwa sala au maombi yetu kwa Mungu.

Uponyaji ni majibu ya Mungu kwa mgonjwa, na kufunguliwa katika pepo wachafu ni majibu ya Mungu kwa aliyekuwa amefungwa.

Katika mazingira kama haya, sharti la Mungu katika kumponya au kumfungua mtu katika vifungo vya Shetani, ni mhusika kusamehe wale waliomkosea au kumtendea mabaya.

Ndiyo maana sala au maombi ya uponyaji lazima yaanze na toba ya dhati. Toba ya dhati ni uamuzi kutoka moyoni wa kuziacha njia mbaya za kuasi, na kumgeukia Mungu kwa ajili ya maisha ya utakaso. Katika kutubu ili kupokea msahama wa Mungu unaambatana na sharti yaw ewe kuwasamehe wengine waliokukosea. Na ndiyo maana ya Yesu kujumisha suala la kusamehewa kuhusishwa na jinsi sisi tunavyokuwa tayari kusamehe waliotukosea.

Je! Umekuwa ukihudhuria maombezi ya uponyaji au kufunguliwa kutoka vifungo vya Shetani na bado hujapokea uponyaji wako au kufunguliwa kutoka vifungo hivyo. Basi mojawapo ya sababu au vikwazo ni KUTOKUSAMEHE. Kama wewe una kinyongo, au uchungu wa madai dhidi ya mtu au watu unaowahukumu kwa makosa waliyokutendea wewe, basi, ujue kwamba unastahili kusamehe bila masharti ili na wewe upate kufunguliwa. MUNGU AKUBARIKI

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.