SOMO: KWANINI NI LAZIMA KUSAMEHE


Utangulizi

Hivi karibuni nimeshuhudia ongezeko la kushuka kwa viwango vya kiroho na imani kati ya jamii ya wacha Mungu na nikashawishika kutafuta shina la tatizo hili ni nini. Niligundua baadhi ya vyanzo vyake mojawapo ikiwa ni pamoja na ongezeko la wahubiri na manabii wa uongo ambao wanatabiri mambo yasiyotimia kwa wafuasi wao.

Lakini nilipotazama hata kwa jamii ya wakristo waaminifu katika imani nilishuhudia tatizo hili la “kupoa kiroho” limeathiri wengi. Na si hivyo tu baadhi yao wanashambuliwa na maradhi ya kitabia yakiwemo saratani, kisukari, shinikizo la damu na maradhi ya moyo, vidonda vya tumbo. Hali hii ndiyo ndiyo ilinifanya nianze kuchunguza kwa kina ili kutafuta shina la tatizo ni nini. Mpaka sasa bado naendelea na uchungi wangu sijamaliza. Lakini kile ambacho nimekibaini katika utafiti wangu ni tatizo la KUTOKUSAMEHE.

Pengine unaweza kuona kwamba KUTOKUSAMEHE haiwezi kuwa chimbuko la matatizo ya kiafya. Msomaji mpendwa, wahenga wa Kiswahili wanasema “kama hujafanya utafiti bora usiseme”! Ninayokwenda kukushirikisha katika mada hii ni matokeo ya utafiti wa kibiblia ambao pia unathibitishwa na taaluma ya tiba na afya. Kupitia mada hii nitakushirikisha sababu 6 ni KWANINI NI LAZIMA KUSAMEHE. Kwa lugha nyingine sababu hizo zinatahadhirsha kuhusu MADHARA YA KUTOKUSAMEHE pia. Sababu hizo 6 ni hizi zifuatazo: 1. Kusamehe ni tabia ya Mungu, 2. Binadamu wote ni wakosaji 3. Kusamehe ni sharti la kusamehewa, 4. Kusamehe kunaimarisha mahusiano, 5. Kusamehe kunaimarisha afya, na 6. Kusamehe ni ufunguo wa kujibiwa maombi.

Askofu Sylvester Gamanywa
Kusamehe ni Tabia ya Mungu

Mahali sahihi pa kuanzia kujifunza habari za kusamehe ni Mungu mwenyewe. Naweza kusema kwa ujasiri na kw aushahidi wa kimaandiko kwamba, Mungu sio tu ni chanzo bali kwake ni tabia. Ni tabia yake Mungu kusamehe, na hufanya hivyo bila masharti. Tunaweza kupata aushahidi huu kutokana na Neno la Mungu mwenyewe aliposema:

“Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” (Isa.43:25)

Maandiko haya yanatudhihirishia kwamba, Mungu husamehe sio kwa sababu tumestahili kusamehewa, au sio kwamba sisi tumemwomba sasa msamaha mpaka akashawishika, badala yake Mungu huamua kusamehe kwa sababu ndiyo tabia yake. Anaposema “niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe” maana ni kwa rehema zake, huruma zake, upendo wake, na ndiyo asili yake.

Ukifuatulia tangu binadamu wa kwanza alipokosa, waliamua kujificha ili kwamba Mungu asiwaone. Mungu akawa anawatafuta japo sio kuwa alikuwa hawaoni, ila wao walifikiri Mungu hawaoni. Adamu Uko wapi?  Adamu anajibu akisema: “Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” (Mw.3:8)

Unaona? Badala ya Adamu kumtafuta Mungu baada ya kukosa ili aombe msamaha kwake, akaamua kujificha. Ndivyo binadamu tulivyo hata sasa. Hatujitumi kumtafuta Mungu ili kutubu na kutengeneza njia zetu. Lakini amemtuma Roho Mtakatifu ambaye ndiye anayetufuatilia huku akituhukumu kupitia dhamiri zetu tugeuke na kutubu ili tupate kudumisha uhusiano wetu na Mungu.

Haya tunapokuja kwa habari ya historia ya dhabihu ya dhambi, ni Mungu mwenyewe aliyeweka taratibu na kanuni  kwa wana wa Israeli za kuomba msamaha. Dhabihu ni kielelezo cha kuomba msamaha toka kwa Mungu. Hii pia ni ishara nyingine kwamba “kusamehe” ni tabia ya Mungu.


Hata suala la ujio wa Yesu duniani, bado ni Mungu mwenyewe katika kutimiza ahadi yake ya ukombozi wa binadamu. Tunaona Mungu ndiye aliyeupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. (YH.3:16)

Suala zima la wokovu wa Yesu Kristo ni jitihadamu zake Mungu za kusamehe. Na ni jitihada anazifanya wakati binadamu wenyewe ndio kwanza tumezama katika uasi na dhambi. Hatun habari na hata tukipata habara hatujali.

Sasa tukirejea kwenye mada ya msingi ya KWANINI LAZIMA TUSAMEHE. Ni kwa sababu wote tuliokubali kupokea msamaha wake, tukafanyika watoto wake, tunawiwa kuwa na TABIA YA BABA YETU ambayo ni KUSAMEHE bila masharti.

“lakini  mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (MT.5:45)

Kwa agizo hili ni dhahiri kwamba, haiwezekani kuwapenda adui zetu; na hata kuwaombea wanaotuudhi, kama hatujajenga au kuwa na tabia ya KUSAMEHE bila masharti kama Mungu Baba yetu. Mpendwa msikilizaji wangu, kwa leo tunajifunza kwamba, kusamehe ni tabia ya Mungu. Na kwamba sisi kama kweli ni watoto wake lazima tuwe na tabia ya Baba yetu ya KUSAMEHE bila masharti.

Binadamu wote ni wakosaji

Sababu ya pili ya ni kwanini ni lazima kusamehe ni kwa sababu BINADAMU WOTE NI WAKOSAJI. Sasa hapa naomba tuvue vazi la unafiki tuukabili ukweli kwamba binadamu wote ni wakosaji ikiwa ni pamoja na wewe na mimi na binadamu wenzetu.

Kwa hiyo, hakuna mwenye haki ya kumhukumu mwenzake hata kama anayo sababu ya kufanya hivyo, kwa kuwa mwenye kutaka kuhukumu yeye mwenyewe ni mkosaji vile vile.

Naomba nijenge hoja yangu kwa mifano hai ya Biblia. Maandiko yanasema kwamba, “walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kos ala Adamu, aliye mfano wake atakayekuja.” (Rum. 5:14)

Unaona? Kosa la binadamu wa kwanza lilisababisha uzao wa binadamu wote waliofuata kuathiriwa na tabia ya kukosa japokuwa sio kosa lile lile walilokosea binadamu wa kwanza.

Ni kweli unaweza kuwa na madai tofauti au umetendewa isivyo haki wala halali na wengine na ukawa na madai tofauti yanayojitegemea. Lakini hii haifuti kwamba na wewe unao uliowakosea kivingine na kwamba nao wana madai dhidi yako ambayo ni tofauti na madai yako dhidi ya wengine. Kama unavyokosewa na watu ndivyo na wewe kwa kutaka au kutokukusudia unawakosea wengine.

Lakini hii hali ya kukosa haikuasisiwa na sisi wa kizazi hiki bali imetokea mbali kwa binadamu wa kwanza kama iilivyoandikwa kwamba: “Kwa sababu  kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliinngizwa katika hali ya wenye dhambi,……” (Rum.5:19)

Kama tulivyojifunza kipengele cha jana kwamba Mungu ana tabia ya kusameme bila masharti, leo kwenye kipengele hiki cha BINADAMU WOTE NI WAKOSAJI, ni lazima tujenge tabia ya kusamehe wengine kwa sababu kwanza hatuna haki ya kutoa hukumu dhidi wanaotukosea wakati sisi wenyewe tuna watu wanaotuhesabu wakosaji wao.

Hapa sina maana ya kwamba tufumbie macho maovu na kwamba tusiwaguse wakosaji kwa mujibu wa sharia zilizopo. Kusamehe sio kufumbia macho uovu. Kusamehe ni kutokumhesabu mkosaji kama binadamu anayestahili kupewa second chance ya kujirekebisha. Lakini pia kusamehe kunakotajwa hapa ni kutokuwa na kinyongo pamoja na visasi dhidi ya wakosaji wako, badala yake kumbuka na wewe umesimamaje machoni pa wengine ambao wanakuhesabu umewakosea.

Kabla ya kutunga kidole wakosaji wako angalia vidole vinakuelekea wewe mwenyewe na kujihoji kama unatenda haki stahili. Na mwisho vile inavyotaka kuwatendea wakosaji wako ndivyo unavyotaka na wewe utendewe na wenye madai dhidi yako?

Turejee kisa cha Yesu kuletetewa mwananke aliyekamatwa akizini na washtaki wake wakataka sharia ichukue mkondo wake, Yesu naye akawajibu ambaye hana dhambi kama hiyo awe wa kwanza kutoa adhabu, na wote wakatoweka bil akuaga. Yesu akamwambia mwanamke yule enenda zako USITENDE DHAMBI TENA.

Kusamehe ni Sharti la kusamehewa

Kipengele cha tatu ambacho ni KUSAMEHE NI SHARTI LA KUSAMEMEWA. Sababu hii inatokana na kauli ya Yesu Kristo mwenyewe aliposema: “Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.” (Mk.11:26)

Haya ni maneno ya Yesu Kristo mwenyewe. Kuna kisa ambacho Yesu alisimulia kuhusu mtu aliyekuwa anadaiwa na akakamatwa ili aadhibiwe akaomba msamaha apewe nafasi ya kulipa deni lake, na akasamehewa deni hilo. Kumbe mtu yule yule alipokutana na mtu ambaye anamdai tena kiasi kidogo kuliko madeni anayodaiwa yeye, aliamua kumwadhibu mdeni wake bila huruma na akasahau kwamba yeye amesamehewa madai kama yale.

Unyama wake huyu ulimfikia yule aliyekuwa amemsamehe na akamwita na akaamua kumwadhibu vikali kwa sababu yeye alishindwa kuonyesha ubinadamu kwa mwenzake.

Kutokana na kisa hiki Yesu aliweka waziwazi msimamo wa Mungu kuhusu KUSAMEHE. Licha ya kwanza anataka sisi kama watoto wake tuwe na tabia ya KUSAMEHE bila masharti; bado Mungu amekufanya KUSAMEHE kama sharti la KUSAMEHEWA.

Bila shaka Mungu anajua kwamba sisi binadamu tuna ubinafsi na kujipendelea pamoja na kujisahau kwa habari za mahitaji ya wengine. Tunapofikia kiasi ambacho hatuko tayari KUSAMEHE wengine, njia peke ya kuturejesha kwenye mstari ni KUTOKUSAMEHEWA makosa yetu wenyewe kama hatutaku kuwasamehe wengine.

Hii ndiyo maana ya kipengele cha sala ya Bwana kinachosema; “utusamehe makosa yetu kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea.” Unaona. Kiwango kile kile tunachosamehe wengine ndicho kiwango tunachosamehewa na sisi mbele za Mungu.

Itaendelea Jumatatu ijayo...


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.