SOMO: NAMNA YA KUISIKIA SAUTI YA MUNGU KWA URAHISI ZAIDI


Mwl Furaha Amon
Utangulizi:
Kwa mtu mbaye haelewi mambo ya kiroho unaposema kwamba Mungu ameniambia jambo fulani huwa ni kama kituko kwake, hawezi kuamini na anaweza kukuona kama unafanya mzaha vile au unajifanya unajua sana. Lakini ukweli ni kwamba sauti ya Mungu iko kila sekunde unayoishi na ipo tayari kwa ajili ya kukuongoza, kukushauri na kukuelekeza kitu ambacho Mungu anataka ukifanye kwa wakati huo.

Kwa nini tunajifunza somo:
Tunajifunza somo hili kwa sababu nyakati tulizonazo tunao walimu wengi na watumishi wengi wa ukweli na wa uongo na kufanya kuwe na sauti nyingi katika mafundisho ambapo kama watu hawajafundishwa sawasawa kuisikia sauti ya Mungu ni rahisi kuchukuliwa na upepo wa kila elimu. Lakini watakapojifunza Sauti ya Mungu itawasaidia sana kuwa na msingi imara kiasi kwamba watajua kutofautisha sauti ya Mungu, shetani na yao wenyewe katika kuamua mambo yanayohusu maisha yao ya kimwili na kiroho.

Niliwauliza wanafunzi wangu wa kanisa la vijana ni kwa nini wanapofanya makosa ya kiroho (dhambi) haraka sana wanaamini kwamba Mungu ameshaona na kusikia, na kwa nini wanapofanya maombi hawaamini kuwa Mungu amesikia. Sasa hili ni somo jingine lakini katika somo hili nataka kukupa njia nyepesi kabisa za kusikia sauti ya Mungu kwa mifano.

Kwa mfano:

Mimi niko kurasini hapo Dar na ninataka kumtembelea rafiki yangu Elie Chansa ambaye anaishi Mbagala na labda sina mawasiliano naye ya simu. Wakati nasubiri usafiri wa kwenda Mbagala linakuja wazo ndani yangu kwamba nenda kwanza kariakoo ambako hukupanga kwenda na mimi naamua kutii lile wazo na kupanda gari la kariakoo ambako labda sikuwa na umuhimu sana wa kwenda huko. Lakini ninaposhuka kwenye gari Kariakoo namuona Elie yuko pale kituoni anasubiri usafiri.

Hapo inakuwa lile wazo la kwenda kariakoo halikuwa wazo la kawaida bali ilikuwa ni sauti ya Mungu halisi na kwa sababu nilitii ndio maana sikulazimika kupoteza muda na nauli kwenda Mbagala.

Mtu ni nini?

Ili tuanze vizuri kujenga msingi wa somo hili ni muhimu kwanza kujua mtu ni nini. Kwa mujibu wa Biblia tunajifunza kwamba Mungu alisema na tumfanye Mtu kwa mfano wetu na sura yetu, (Mwanzo 1: 26a) kwa hiyo Mungu aliumba roho kwanza. Ni katika roho tu ndiko ambako wanadamu wote tunafanana na Mungu, kwa maana nyingine hatufanani na Mungu katika mwili ndio maana kuna sisi weusi kama mimi, kuna Wahindi, Wekundu, Wajapani na Wakorea wanjano kuna Wazungu weupe.

Biblia inaeleza kuwa baadae Mungu akachukua mavumbi akaufanya mwili na kisha akapuliza pumzi yake na mwanadamu akawa nafsi hai. Kwa kifupi tunajifunza kwamba mtu ni roho, anayo nafsi na anaishi katika mwili.

Kwa hiyo nafsi na roho zimeunganishwa pamoja ambayo ndio wewe Tunajifunza kwamba baada ya mtu kufa mwili hurudia hali yake ya kuwa udongo, Nafsi na roho ndio mwanadamu mwenyewe atakayeishi milele, aidha mbinguni ama jehanamu kutegemeana na mwenyewe alivyoishi hapa duniani.

Kwa sababu hiyo ni muhimu kuifahamu milango ya fahamu ambayo iko kwenye mwili, nafsi na kwenye roho, hiyo itatusaidia sana kuelewa sauti ya Mungu na umuhimu wake.


Milango ya fahamu ya mwili
Mwili unao milango mitano ya fahamu, ambayo ni;
1.    Kuona,
2.    Kugusa,
3.    Kuonja,
4.    Kusikia na
5.    Kunusa.

Milango ya fahamu ya roho
Roho nayo inayo milango mitatu ya fahamu ambayo ni
1.    Mawasiliano na Mungu,
2.    Uwezo wa kujulishwa (intuition)
3.    na Dhamiri (Conscious).

Milango ya fahamu ya nafsi
Nafsi nayo inayo milango mitatu ya fahamu ambayo ni
1.    KUAMUA (willing).
2.    KUJISIKIA au hisia (emotion) na
3.    MAWAZO.

Mapambano yasiyo na mwisho
Ili tuweze kuijua sauti ya Mungu ni lazima tufahamu kwanza kwamba yapo mpambano yasiyoisha tangu mwanadamu anapotungwa mimba mpaka siku anapolala mauti, ni muhimu kukumbuka kwamba uumbaji wa Mungu bado unaendelea hadi sasa kwa maana ya kwamba mbegu ya baba inapokutana na yai la mama Mungu hutia pumzi yake na hapo ndio mwanzo wa binadamu kuja duniani ambako anakuta tayari kuna mitego ambayo imetokana na maagano ya kimila na laana za kifamilia kutoka kwenye koo na mababu, lakini pia anakuwa anawindwa na roho ya kukataliwa kutokana na jinsi wazazi wake walivyokuwa wamejiandaa kumpokea pamoja na madhira mengine mbalimbali. Kwa sababu hiyo ni lazima tuangalie mbinu ambazo shetani anatumia katika kumshambulia binadamu tukianzia na jinsi anavyoitumia milango ya fahamu ya kwenye mwili nafsi na roho.

Mawazo ni nini?
Kwa sababu nia ya somo hili ni kutaka ufahamu kusikia sauti ya Mungu kwa urahisi zaidi, nimeshawishika kuanza na mojawapo wa milango ya fahamu uliopo kwenye nafsi ambao unaitwa mawazo.

Mawazo ni njia mojawapo ya mawasiliano kati ya mtu na ulimwengu wa roho, na viumbe ambavyo viko katika ulimwengu war roho. Mawazo ndio chombo kikuu cha mawasiliano kati ya ulimwengu wa Roho na Mtu. Mungu na shetani wanaishi katika ulimwengu wa roho, njia ambayo huwasilian na watu ni kupitia katika mawazo.

Mungu anapokuja kwa mtu hukaa kwenye roho, lakini anapoongea na mtu, huongea kupitia mawazo. Shetani anapokuja ndani ya mtu hupitia kwenye mwili na kufika kwenye nafsi na anapoongea na mtu huongea kupitia mawazo. Mtu mwenyewe pia huwa na matakwa yake, hivyo naye anayo mawazo yake. Matakwa ya mtu huitwa nia.

Baada ya wazo kumfikia mtu hilo wazo likipata kibali kwake linahamia kwenye mlango fahamu wa maamuzi ili likaamriwe kufanyika au hapana. Wazo likifika kwenye mlango fahamu wa maamuzi hapo huamriwa litendeke au lisitendeke. Iwapo wazo likikubalika kutendeka linapelekwa kwenye mlango fahamu wa hisia.

Mlango wa hisia ndio mlango wa utekelezaji wa jambo. Hapo mwili huwa unaamriwa kutenda wazo ambalo limeruhusiwa kutendeka. Kama ni zinaa hapo mwili wote unawakaka tamaa ya kuitenda dhambi hiyo. Iwapo ni jambo la ki Mungu, basi mwili wote utakuwa na shauku au hamu ya kulitenda hilo jambo. Daudi mfalme anasema mwili wangu wakuonea shauku (Zaburi 63:1).Eee Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu wakuonea shauku, katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.

Jambo likifika hatua hii ni vigumu kulizuwia kutendeka. Huwa vigumu sana kwa mtu aliyeokoka afike hatua ya kutenda dhambi, kwa sababu kuna hatua ndefu sana tangu ulipoingiwa na wazo chafu hadi ufikie hatua ya kutenda dhambi. Hivyo unayo nafasi kupingana na hilo wazo chafu kabla halijaingia katika mlango fahamu wa mawazo, ikishindikana hapo bado kuna mlango wa fahamu wa maamuzi, pigana naye hapo hasa wakati unaposikia sauti mbili zinabishana kuwa fanya nyingine inasema usifanye, usingoje hadi jambo lifike kwenye hisia, hapo itakuwa kazi kubwa sana kuchomoa.

Biblia inasema ; maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili, maana silaha zetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii kristo. (2Korintho 10: 3,5).

Iwapo mtu hajaokoka nafsi yake inatawaliwa na roho waovu hivyo wazo la kutoka kwa Mungu haliwezi kupita na kupata kibali. Mambo ambayo yatapata kibali ni yale ya shetani. Hivyo hivyo hata kwa mtu aliyeokoka, nafsi yake inatawaliwa na Mungu, hivyo wazo kutoka kwa shetani halitapata kibali.

Kwa kifupi kitu ambacho nilitaka ufahamu hapa ni kwamba mawazo ndiyo masikio ya rohoni. Mungu au Shetani akiongea na wewe utasikia wazo. Wazo la Mungu au la shetani husikika kama mtu mwingine ambaye si wewe akikuongelesha, hili ndio ujue ni wazo kutoka kwa Mungu au kwa shetani. Wazo la shetani liko kinyume na Mungu, wazo kutoka kwa Mungu linakubaliana na neno la Mungu.

Iwapo wazo ni lako mwenyewe hutalisikia kama mtu wa pili akikuongelesha, bali nafsi yako itakuwa inajiongelesha yenyewe (nia). Hivyo, iwapo ni sauti ya shetani utaisikia kama mtu wa pili akikuongelesha katika mawazo yako. Pia iwapo ni sauti ya Mungu utasikia kama mtu wa pili akikuongelesha katika mawazo yako.

Mfano
1.    Unaweza kusikia sauti ikikushauri unaonaje kama ukiiba. (hii ni sauti ya shetani).
2.    Unaweza kusikia sauti ikikushauri usiibe (sauti ya Mungu)
3.    Ninatamani kuiba (Nia) 

Hizi sauti ya kwanza na ya pili zote unazisikia kama mtu wa pili akikuongelesha. Lakini sauti ya tatu wewe mwenyewe ukijiongelesha, yaani unasikia unajiongelesha wewe mwenyewe.

Sauti ya Mungu au yako mwenyewe inasikika kwenye mawazo. Pepo anakuja kwa njia yeyote ile lakini kituo cha kwanza kabisa ni kwenye mawazo, baada ya hapo ni kwenye maamuzi na baadae hisia, tayari kwa utekelezaji.

Kwa utangulizi huu tuishie hapa kwa leo, awamu ijayo tutazama utendaji kazi wa milango ya fahamu ya roho. Tukutane Ijumaa.

Mwalimu Furaha Amon ni Mchungaji wa Kanisa la Vijana (KLPT) Tanga anapatikana kupitia namba 0713461593 na barua pepe mwakasege.furaha@yahoo.com


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.