SOMO: NAMNA YA KUISIKIA SAUTI YA MUNGU KWA URAHISI ZAIDI (3)

Mara ya mwisho tumejifunza kuhusiana na utendaji kazi wa milango ya fahamu ya roho, kama hukupata fursa basi bofya hapa kusoma sehemu ya pili ya somo hili. Lakini pia unaweza kusoma sehemu ya kwanza ya somo kwa kubofya hapa, kisha tuendelee na sehemu ya tatu ya somo letu.

Sauti ya Mungu katika Kutenda Miujiza

Hakuna mtu yeyote anayeweza kutenda muujiza kwa maamuzi yake mwenyewe, hata kama ni mtumishi wa Mungu anayetumiwa kwa kiwango cha juu sana. Miujiza yote inayotendwa, Mungu huzungumza na watakaotenda. Huzungumza nao kwa njia ya Rhema.

Mwalimu Furaha Amon
Katika kitabu cha Waebrania sura ya kumi na moja yote inazungumzia watumishi wa Mungu waliotenda miujiza mikubwa enzi za agano la kale. Wakristo wamezowea kuwaita mashujaa wa imani. Mambo hayo hawakuamua yatendeke kwa mawazo yao wenyewe, bali mungu aliwaagiza kuitenda miujiza hiyo. Tofautisha mawazo yako na imani; mawazo yako hayawezi kutenda miujiza hata siku moja. Bali kama Mungu akikuagiza kutenda kwa kusikia sauti yake, ukitenda ndipo muujiza hutendeka. Wakristo wengi hawalijui jambo hili, hivyo wanapokuwa wanataka jambo fulani litendeke hufikiri imani itakuja kutokana na kutamani kwao. Baada ya hapo wanayangoja yatokee  wakisema wanayangoja kwa imani kwa imani huku wakisema kuwa “maana imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo.”

Hivyo hata na wao wako katika kutarajia. Pia wanaendelea kusema kuwa, imani ni bayana na mambo yasiyoonekana, hivyo wanayoyatamani yatokee hayaonekani, lakini wanayangoja yaonekane. Ndugu  yangu tofautisha mawazo yako na imani. Mawazo yako hayawezi kuzaa imani na muujiza ukatendeka. Hata kama hayo mawazo yataambatana na neno la Mungu la kusimamia, bado hakuna kitu kitakachofanyika. Mawazo yako yanaweza kuwa ni mazuri sana, hata hivyo hayawezi kuleta imani utendeke muujiza kutokana na wazo lako.

Wakristo wengi wamechelewa kufanikiwa kwa sababu wamekuwa wakitegemea mawazo yao yawe  chanzo cha imani. Imani chanzo chake ni sauti ya Mungu. (usisahau kuwa ndani yako kuna wazo la Mungu, la shetani na la kwako mwenyewe). Ninaposema sauti ya Mungu maana yake ni wazo lililotoka kwa Mungu. Na ninaposema wazo lako, ni lile linalotokana na wewe kama tulivyojifunza huko nyuma. Wote waliotenda miujiza kwenye Biblia waliagizwa kufanya hivyo na Mungu. Baada  ya kuisikia na kuijua sauti ya Mungu.

Hebu tuangalie mifano ya watumishi wachache kutoka kwenye Biblia agano la kale; tumwangalie Musa alitenda miujiza mingi sana tena mikubwa hebu fuatilia miujiza yake yote utaweza kuelewa vizuri ninachofundisha. Hebu tuangalie muujiza wa kukausha bahari ya Shamu, ili tujue ni nani alitoa wazo la kukausha bahari hiyo.

Biblia inasema:
Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao na tazama,wamisri wanakuja nyuma yao, wakaogopa sana, wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, je, kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Neno hili silo tulilokwambia huko Misri, tukisema tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, msiogope ,simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo: kwa maana  hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaa kimya (Kutoka 14:10,14).

Kitu ambacho ninataka ukifahamu kwenye maandiko hayo hapo juu ni kuwa, tunawaona wana Israeli wanamlilia Musa. Musa anawatuliza hawa watu. Musa hapa halii lakini anawatuliza hawa watu. Anawatuliza watu kuwa, Mungu anakwenda kuwapigania. Atawapigania vipi, hili hata Musa bado alikuwa halijui.

Hapa tunaona Musa kama kiongozi hakupaswa kulia mbele ya watu anaowaongoza. Hii ndio maana hatumuoni analia. Lakini Musa naye aliliona hili jaribu na hakuwa na jibu katika jaribu hili. Musa naye alimtegemea Mungu ndiye atoe jibu, kabla Mungu kuleta jibu Musa aliliona jaribu kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli wengine na lilimuumiza kama wengine japokuwa alikuwa halii wakati alipokuwa mbele  ya wana wa Israeli. Lakini alipojitenga alikuwa analia, alikuwa anamlilia Mungu atoe jibu kwa sababu ya hilo jaribu.

Biblia inasema,
BWANA akamwambia Musa, mbona unanililia mimi (Kutoka 14:15)
Kama Musa angekuwa anajua jibu la jaribu hili, angelitoa wala asingelia, bali kwa vile alikuwa hajui itakavyokuwa ndiyo maana alilia. Musa alipokuwa analia alikuwa hajapata jibu. Alikuwa hajasikia sauti ya Mungu akimwagiza nini cha kufanya. Baadaye akiwa kwenye kulia ndipo Mungu anamwambia jambo la kufanya ili kulishinda hilo jaribu.

Mungu anaendelea kuzungumza na Musa,
……waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyooshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya: nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. (Kutoka 14: 15,16.
Hii ni Rhema inazungumza na Musa. Anaambiwa au anaagizwa akanyooshe fimbo juu ya bahari ambapo muujiza utatokea wa bahari kukauka. Tumeona kuwa kukausha bahari, halikuwa wazo la Musa bali aliagizwa na Mungu kufanya hilo. Kama hujaangalia kwa utulivu unaweza ukafikiri kuwa Musa aliinua tu fimbo kwa kutamani kwake na bahari ikafunguka sio hivyo ndugu.

Mfano wa Mtumishi mwingine katika Agano la kale. Eliya alitenda miujiza sana, mmojawapo ni wa kuzuwia mvua kwa miaka mitatu. Je, lilikuwa wazo lake au Mungu ndiye aliyeamua na kumuagiza kuufanya?

Habari za nyuma za Eliya kabla ya tukio hili hazisemwi katika Biblia, hivyo hatuwezi kuona wakati Mungu anamwagiza Eliya kutenda huo muujiza. Biblia inaanza kuelezea habari za Eliya akiwa mbele ya mfalme akizuwia mvua.
Baada ya Eliya kuzuwia mvua miaka mitatu inapita,sasa Eliya anarudisha mvua. Je, wazo la kurudisha mvua alilitoa yeye au aliagizwa kuirudisha na Mungu?.

Biblia inasema,
Ikawa baada ya siku nyingi, neno la BWANA likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda ukajionyeshe kwa Ahabu, nami nitaleta  mvua juu ya Nchi (1Wafalme 18:1).
Eliya asingeagizwa kwenda kuirudisha mvua, mvua isingerudi. Ni hivyo hivyo iwapo kurudi kwa mvua ni Mungu aliagiza, ina maana hata wakati Eliya anazuia mvua napo aliagizwa na Mungu.

Mifano hii miwili nafikiri inatosha kukusaidia kuelewa nini ninachotaka ukifahamu, lakini ningeweza kuelezea muujiza mmoja mmoja hadi miujiza yote iliyoko kwenye Biblia ungeweza kuona sauti ya Mungu ilivyotenda miujiza hiyo. Cha kuzingatia ni kwamba hawa watu hawakuwa tofauti na sisi bali ni kwa njia hii tunayojifunza waliweza kutenda mambo mengi makubwa. Wewe pia Mungu anaweza kukuagiza utende muujiza. Mungu anataka watu jasiri, watiifu ambao akiwaagiza kufanya jambo fulani, watafanya bila woga. Unaposikia sauti ya Mungu ikikuagiza kufanya jambo fulani, fanya usiache. Hata kama siku za mwanzo mwanzo hutaweza kutofautisha vizuri kati ya mawazo yako na ya Mungu ambayo kama hauko vizuri kiroho huwa yanafanana sana. Lakini ni bora kutenda hata kama litakuwa wazo lako, kuliko kuogopa kutenda, kumbe lilikuwa wazo la Mungu.

Mungu alimwambia Yoshua awe hodari na moyo wa ushujaa.  Mungu ndiye alikuwa anaenda kutenda, hivyo Yoshua alitakiwa awe na moyo wa ujasiri. Mtu asiye jasiri akiagizwa na Mungu kutenda muujiza fulani, ataogopa kutenda. Kila mkristo huagizwa na Mungu kutenda mambo mengi mbalimbali madogomadogo na makubwa, ya kawaida na ambayo sio ya kawaida. Wakristo wamekuwa wakiogopa kutenda wanachoagizwa kutenda.

Biblia inasema,
Vivyo hivyo imani, isipokuwa ina matendo imekufa nafsini mwake (Yakobo 2:17).
Kusikia + Kutenda = Muujiza.
Mungu hutenda miujiza na watu jasiri. Mungu alipokuwa anamchagua Musa, Musa alikataa, akamwambia Mungu kuwa yeye ana kigugumizi hawezi kuongea vizuri. Musa akamwambia Mungu amchague Haruni. Mungu alimkataa Haruni pamoja na kwamba Haruni anajua  sana kuongea Mungu alimtaka Musa kwa sababu Musa alikuwa jasiri, hakuwa mwoga. Haruni hakuwa jasiri, kumbuka Musa alipopanda mlimani akakaa siku arobaini, huku nyuma Haruni aliongoza watu kuchonga sanamu iwaongoze kurudi Misri. Kujua kuhubiri sana bila kuisikia sauti ya Mungu na kuchukua hatua za kijasiri huwezi kutumiwa kutenda miujiza.

kwa leo tuishie hapa, ila mshirikishe na mwenzako kuhusu somo hili kisha tukutane Ijumaa kwenye mwendelezo wake.

Mwalimu Furaha Amon ni Mchungaji wa Kanisa la Vijana, KLPT Tanga. Anapatikana kupitia namba 0713461593 na barua pepe mwakasege.furaha@yahoo.com


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.