SOMO: NAMNA YA KUISIKIA SAUTI YA MUNGU KWA URAHISI ZAIDI (4)

Baada ya kitambo kidogo kupita na hata kupata fursa ya kutafakari somo letu kuanzia mwanzo wake (bofya kusoma) sehemu ya pili (bofya kusoma) na sehemu ya tatu (bofya kusoma), sasa tunaendelea na sehemu ya nne kwa kumaliz an ushuhuda.

Siku Nilipomfanyia Mungu wangu Ujeuri

Naona nimalizie hili somo kwa ushuhuda wangu mwenyewe ambao ningechagua kichwa cha ushuhuda huu ningeuita SIKU NILIPOMFANYIA MUNGU WANGU JEURI.


Mungu amenipa neema nyingi sana za kiroho ambazo wakati mwingine zimenisaidia sana katika kuelewa mambo mengi kiundani na hasa baada ya kuijua na kuisikia sauti ya Mungu.

Nakumbuka siku moja Mungu alitaka nifanye kitu ambacho mimi sikutaka kukifanya na nilikuwa tayari hata kuharibu uhusiano wangu na Yeye, tulibishana sana kwa zaidi ya masaa matatu sababu mimi kosa nililofanya sikuona kama lilikuwa kosa kubwa kiasi hicho.
Mwalimu Furaha Amon

Nakumbuka nilikuwa nimealikwa kwenda kufundisha katika kanisa moja ambalo liko nje kidogo ya mji wetu wa Tanga, kwa maana hiyo nilikuwa nimefunga ili kupata nafasi nzuri ya kuwasiliana na Mungu kusikia sauti ya Mungu kwa ajili ya ujumbe ambao nilitakiwa kuufundisha katika kanisa hilo.
Nakumbuka siku hiyo niliamka mapema nyumbani kama kawaida nikajiandaa kuelekea kazini, nilipanda gari ya kazini na tukapita katika vituo mbalimbali kuwachukua wenzetu kama ambavyo ratiba ya vituo vya gari letu lilivyohitaji.

Nilipofika kazini wakati nikiwa nashuka kwenye basi la kazini alikuja kijana mmoja mfanyakazi mwenzangu akaniuliza habari za binti fulani ambaye alikuwa mwanafunzi wangu wa fani ya uigizaji ambaye kwa wakati huo alikuwa haishi Tanga ila alikuwa amekuja Tanga kwa wazazi wake; aliniuliza kama nafahamu habari hiyo na kama nimeonana naye. Mimi kwa nia nzuri ya kiroho sana nilimjibu kwamba sijaonana naye, lakini ukweli vijana wengi ambao wamekuwa wanafunzi wangu wanapokuja Tanga huwa wanapenda kuja kunisalimu, na huyo binti alikuja ila mimi kwa nia njema ya kiroho na kwa sababu nilitaka niwe na utulivu niliona nikimjibu ukweli pengine angetaka stori nyingi zaidi kwa hiyo niliona busara ni kupunguza maneno ili niwe na muda na Bwana.

Baada ya kuachana na huyo ndugu hazikupita dakika nyingi nikaanza kujisikia vibaya na moyo kukosa amani katika namna ambayo ni ngumu kuielezea nikahisi nimemkosea Mungu mahali fulani, ilibidi nisimame kwanza nianze kufikiria nimemkosea Mungu wapi?Kkwanza nikahisi labda kuna maagizo niliyopewa katika ndoto na nimesahau kuyawakilisha, nikaona hakuna. Nikaangalia jinsi nilivyoamka na kuongea na familia yangu asubuhi, nikaona pia hakuna kosa.

Nikaangalia jinsi nilivyopanda gari la kazini na watu ambao nimeongea nao na aina ya maongezi yetu katika mzunguko mzima wa toka nyumbani mpaka kazini, nikaona pia hakuna shida, nikaangalia jinsi nilivyoshuka kwenye gari na watu ambao nimeongea nao, nilipofikiria jinsi nilivyoongea na yule mfuasi wangu kuhusu yule binti nikakumbuka kwamba nimekosea kusema uongo.

Nikamshukuru Mungu kwa kugundua dosari hiyo na nikamuomba Mungu kwamba kwa kuwa ninakwenda kwenye chumba cha maombi nitafanya toba nitakapoingia kwenye chumba cha maombi ambako ndiko nilikuwa naelekea.

Bwana akanijibu akasema hapana, mimi nataka uende ukamuombe msamaha yule kijana na umueleze ukweli. Hili jambo likawa gumu sana kwa sababu kwa mila za kazini kwangu mimi siwezi kumuomba msamaha mfuasi wangu, wala sitakiwi kujieleza kwake hata kama nimemkosea, mila zetu zinasema mkubwa huwa hakosei.

Nikamwambia hapana Bwana kwa sababu huyu kikazi ni mfuasi wangu na itakuwa vibaya kama atajua kuwa sikusema kweli kwa hiyo naomba nijitakase kwako Bwana kwa kuwa wewe ndio umeona hili kosa na halina madhara yeyote kwa huyu mfuasi wangu.

Bwana akaniambia, sasa kwa ukali kidogo kwamba kwani ungemueleza ukweli ungepungukiwa na nini, ni kwa nini unashindwa kuelewa mtego mdogo kama huu wa shetani, sasa ni lazima uende ukamuombe radhi na umwambie ukweli.

Mimi nikaamua kuipuuza hiyo sauti, nikalazimisha kuingia kwenye chumba cha maombi na kuanza toba. Wakati wa toba ya kulala chini ya ardhi, vile najiandaa ili nisujudu hapo niliona nguvu fulani ya ajabu ni kama mtu amenisukumiza nikahisi kizungungu na pua inanuka damu kama mtu aliyepigwa ngumi nzito ya pua.

Niliinuka na kutoka katika kile chumba kama mtu aliyefukuzwa kwa kutupiwa vilago vyake, hapo na mimi nikasikwa na hasira nikaamua kususa na kuiondoa hiyo sauti ambayo ambayo ilikuwa ikizunguka katika fahamu zangu, nikaingia kwenye chumba fulani ambacho wanakaa rafiki zangu, nikawaomba waniwekee muziki mzuri wa kizungu au sebene la DRC.

Wenyewe wakashangaa wakauliza kwa nini hutaki nyimbo za kwaya leo kuna nini, nikawaambia leo kuna kitu nataka kujifunza kwenye muziki. wakaniwekea harafu wao wakaondoka kwenda kazini, nikiwa peke yangu sauti nikawa siisikii kwa sababu nimeweka muziki kwa sauti kubwa.
Lakini bado kukawa na tatizo kukawa na hali ya kushituka na kukosa amani kusiko kwa kawaida, yaani kama kuna bonge la janga ambalo litanipata nikaona kule ndani hakukaliki nikaamua kutoka nje.

Nikamwambia Bwana, kwa nini unanishikia bango kwa kosa dogo namna hii mbona mimi nafahamu watu wengi ambao wanamakosa makubwa kabisa makanisani mbona umewaacha tu lakini mimi kosa dogo kama hili unataka kuniaibisha kabisa. Akaniambia sasa wewe unasimama na kuwafundisha watu unafundisha nini kama huwezi kugundua mtego mdogo kama huu. Kama huwezi kushinda mtego kama huu kuna sababu gani ya kuwafundisha watu habari zangu ikiwa mwenyewe unashindwa.

Akaniambia ni lazima uende ukamuombe msamaha hakuna njia nyingine. Nikamwambia kwa kweli Bwana sitakwenda ni bora tukosane. Akaniambia lazima utakwenda tu. Nakumbuka mgogoro ulianza kama saa moja na nusu asubuhi mpaka wakati huu ilikuwa karibu saa tatu na nusu za asubuhi, kwa kazini kwangu muda huu ni muda wa chai, nikaona huu ni muda mzuri wa kwenda mess kwa ajili ya kupata chai, nikaamini kwamba nitakapojichanganya na watu wengi itakuwa njia rahisi ya kuikwepa kuisikia sauti ya Mungu ambayo nilikuwa sikubaliani nayo.

Mwendo wa kutoka nilipokuwa mpaka mess ni kama mita mia tatu hivi na njiani ilibidi nikutane na watu mbalimbali ambao kwa jinsi ninavyoishi nao ni watu ambao tumezoweana sana na tunachangamkiana sana.

Lakini siku hiyo niliona kitu cha ajabu sana, kila mtu niliyekutana naye hakunichangamkia hawakuwa na muda na mimi, wananiangalia kama mtu ambaye nimefanya makosa makubwa kiasi kwamba watu wameambiwa wasiongee na mimi.

Nilijihisi kwamba pengine nimekuwa na sura ya tofauti maana hata wale niliowachangamkia na kuwasemesha walionekana kama hawana muda na mimi, nikaamua kabla ya kuingia mess niende kwenye kioo nijiangalie labda niko tofauti. Nikajiona niko kama kawaida.

Lakini kilichonishitua zaidi ni pale nilipoingia mess ambapo kwa kawaida tunakuwa wengi kiasi inabidi tusubiriane viti meza niliyokaa ilikuwa na viti vinne (4) baada ya kukaa na kuagiza chai palikuwa na viti vitatu havikukaliwa na mtu wakati wengine wamesimama kwa kukosa viti, hapo ndipo nikajua nashindana na nguvu ambayo sio ya kawaida, nikajiuliza ni kwa nini watu wameshindwa hata kuona viti vitupu, nikaacha chai nikatoka nje sasa nikasema kwa sauti ya wazi kwamba Bwana wewe ni Mungu mwenye nguvu leo nimeuona uweza wako nami natubu naomba unisamehe.

Nikaamua kumtafuta yule kijana nikamkuta sehemu amejipumzisha kwa raha zake. Nikamwita kwa jina lake nikamuuliza hivi uliponiuliza habari za Yule binti nilikujibu vipi, akaniambia ulisema kwamba hamkuonana. Nikamwambia basi naomba ndugu yangu nisamehe, ukweli ni kwamba alikuja nyumbani na tuliongea naye sana. Akaniambia mbona haina shida mkuu kwa nini unaomba radhi, nikamwambia kwa kweli hakukuwa na sababu ya kusema uongo. Baada ya kumaliza maneno hayo nilijisikia amani kubwa mno moyoni mwangu. Kila nikikumbuka huwa namkumbuka sana Yona aliyetumwa kwenda ninawi. Mpaka hapo ninaona utakuwa umepata kitu kupitia ushuhuda huu na Mungu akubariki sana.

Tukutane tena Ijumaa ambapo tutatazama namna ambavyo Mungu hutumia maneno yanayohubiriwa kuzungumza na wewe.

Mwalimu Furaha Amon ni Mchungaji wa Kanisa la Vijana, KLPT Tanga. Anapatikana kupitia namba 0713461593 na kwa barua pepe mwakasege.furaha@yahoo.com

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.