SOMO: NAMNA YA KUISIKIA SAUTI YA MUNGU KWA URAHISI ZAIDI (2)

Mara ya mwisho tulitazama utangulizi wa somo na kujifunza kuhusu milango ya ufahamu iliyoko kwenye mwili, nafsi na roho. unaweza kusoma sehemu ya kwanza ya somo hili kwa kubofya hapa. Kisha tuendelee na sehemu ya pili ya somo letu.

Utendaji kazi wa milango ya fahamu ya Roho

Kama tulivyojifunza kwamba roho inayo milango mitatu ya fahamu, mawasiliano na Mungu, kujulishwa na dhamiri. Hebu tuangalie utendaji wa mlango mmoja mmoja.

Uhusiano kati ya mtu na Mungu unajengwa katika kuwasiliana naye. Mawasiliano ya kawaida katika maeneo yote ya kiroho yanapitia mlango huu wa fahamu wa mawasiliano.

Mfano
Unapohubiriwa na kufikia kulikubali neno la Mungu unapolielewa na kukubaliana nalo, huwa ni Mungu ndiye anayezungumza na wewe kupitia njia hii. Unapotafakari neno la Mungu huwa ni mlango huu wa mawasiliano unatumika.

Mahusiano ya kila siku ya kawaida kati ya mtu na Mungu. Mungu anapozungumza ujumbe maalumu kwa mtu, huzungumza kupitia mlango huu, kama vile ufunuo fulani, neno la maarifa, neno la hekima, kupambanua roho n.k.

Ni hali ya kutojisikia amani wakati ukiwa katika hali ambayo Mungu hataki uwepo mahali hapo au hali ya kujisikia amani iwapo utakuwa katika hali inayompendeza Mungu.

Mfano
Umepanda gari ukiwa kwenye gari hilo unakosa amani rohoni, hapo ina maana kuwa Mungu hataki upande gari hilo. Mungu amezungumza na wewe kwa njia ya dhamiri yako kukushuhudia kuwa uko mahali ambako Mungu hataki uwepo hivyo unatakiwa kushuka kwenye hilo gari. Tafuta gari linguine na usiulize kwa nini. Mungu ndio anajua ni kwa nini hakutaka upande hilo gari, na linaweza kwenda na kufika salama lakini pengine uwepo wako ndani ya hilo gari Mungu aliona mitego ya adui.

Roho ilitoka kwa Mungu, hivyo inazo tabia za Mungu. Mungu anapokuja kwa mtu hufikia kwenye roho, hivyo roho daima inatawaliwa na Mungu. Hivyo hata milango ya fahamu yote ya fahamu ya roho hutumiwa na Mungu peke yake. Hapa tunaona kwamba sauti ya Mungu hufika kwenye mawazo ikitokea rohoni na sauti ya shetani hufika kwenye mawazo ikitokea mwilini.

Mtu ambaye hajaokoka roho yake imekufa, hivyo milango ya fahamu ya roho haiwezi kufanya kazi kwa sababu roho yake imekufa. Hivyo mtu huyu hatakuwa na mawasiliano na Mungu. Hata kama sauti ya Mungu itazungumza naye kwenye mawazo yake,hiyo sauti ya Mungu haitakuwa na nguvu, wala haitapata kibali maana nafsi na milango yote ya fahamu ya nafsi itakuwa inatawaliwa na shetani.

Hapo tulipofika sasa tunaweza kuielewa sauti ya Mungu bila matatizo. Sauti ya Mungu bila kujali ni mlango gani wa fahamu wa roho uliotumika ndio inamwongoza mkristo katika kila kitu cha ki-Mungu. Mungu huongoza na kusimamia kila kitu katika maeneo mbalimbali ya maisha ya mkristo. Hivyo mkristo ambaye hataisikia sauti ya Mungu hawezi kufanikiwa kiroho na kimwili. Katika mambo yote tunayoyafanya Mungu anataka azungumze nasi na kutuongoza na kutuelekeza nini cha kufanya. Mambo kama kuomba, kuhubiri, utoaji, kutenda miujiza, kazi, biashara, kilimo, masomo, n.k.

Mungu huzugumza na watu wake kwa njia mblimbali kama vile ndoto, maono, sauti ya dhahiri masikioni, au sauti ya ndani kama mawazo ambayo tunajifunza n.k. vyovyote itakavyokuwa lakini Mungu huhakikisha kuwa anaongea na watu wake. Njia ya Mungu kuongea na mtu mmoja inaweza ikatofautiana na mwingine lakini Mungu anahakikisha ameongea na watu wake.
Wakristo wengi husikia sauti ya Mungu kutokana na uzoefu wa kuishi na Mungu, lakini kwa kupewa mafundisho inakuwa ni nadra sana. Hii inawafanya wakristo hata wanaposikia sauti ya Mungu wanakuwa na mashaka mashaka kuitekeleza. Hivyo wanaisikia kwa kubahatisha. Hawajui kanuni kamili ya jinsi kuisikia sauti ya Mungu.

Biblia inasema Basi imani, chanzo chake ni kusikia: na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).

Kwa kigriki maandiko yanaitwa grapha. Hii ni andiko la aina yoyote ile, liwe na maana au lisiwe na maana. Wagiriki wakatofautisha maandiko ya kawaida na maandiko ya neno la Mungu. Maandiko ya neno la Mungu wakaita Logos. Logos ni neno la Mungu ambalo tayari lipo tumepewa kama vile Biblia na vitabu mbalimbali vya neno la Mungu vinavyoandikwa  na watumishi wa Mungu mbalimbali.

Wagiriki wakaona neno la Mungu ni pana sana. Hivyo wakaona watofautishe Logos na neno la Mungu lingine wakaita Rhema. Rhema ni neno la Mungu ambalo Mungu anazungumza na mtu moja kwa moja saa hiyo (live). Unaweza ukawa unasoma  andiko katika Biblia msitari fulani, ukawa unaendelea kusoma kila siku. Huo msitari utaendelea kuwa Logos lakini siku moja unaweza ukausoma mstari huo na Mungu akazungumza na wewe moja kwa moja kupitia mstari huo akakupa ujumbe fulani. Siku hiyo huo mstari utakuwa Rhema. Rhema ni sauti ya Mungu au ni neno la Mungu analozungumza na mtu moja kwa moja. Inaweza kuwa wazo fulani,hata kama Mungu atazungumza na wewe kwa njia nyingine ya ndoto, maono, nk.

Baada ya maelezo hayo, hebu turudi kwenye andiko letu Basi imani, chanzo chake ni kusikia: na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17). Sasa tujiulize swali je tusikie neno lipi kati ya Logos na Rhema ambalo ukilisikia litazaa imani?.

Neno ambalo ukilisikia huzaa imani ni Rhema siyo Logos, Logos haizai imani. Hii ndio maana watu wengi wanasoma Biblia lakini haijawasaidia wala kuwafanya waokoke. Wakristo wengi wameshindwa kuwa na imani ya kutenda miujiza kwa sababu hawajui kanuni hii ya miujiza kutendeka. Kwa maana hiyo tumeona ili uwe na imani yenye kutenda miujiza ni lazima usikie Rhema (usikie kutoka kwa Mungu anakuagiza kutenda jambo).

Hakuna mtu wa Mungu yeyote ambaye Mungu hazugumzi naye, tatizo ni uhakika wa kujua kuwa hii ndiyo sauti ya Mungu, kwa sababu neno la Mungu linasema kondoo wanaijua sauti ya mchungaji wao. Mungu huongea na watu wake na kuwaongoza na kuwaelekeza nini wafanye. Lakini wakristo huwa hawatii hiyo sauti ya Mungu. Kwa hiyo Mungu huamua kutoendelea kuongea nao tena . unapokuwa mtii Kwa sauti ya Mungu ndipo Mungu anakuwa anazungumza na wewe na baadae unaizowea sauti na inakuwa dhahiri kabisa kwako bila mashaka mashaka. Mkristo ambaye sio mwombaji wa kuomba maombi marefu sauti ya Mungu itampa shida kidogo kuitambua.

Mungu anazo njia nyingi za kuongea na watu wake, anaweza kuongea kwa ndoto, maono, sauti ya masikioni na sauti ya ndani kama wazo, nk. Hata kama Mungu amezungumza na wewe kwa njia kati ya hizo, hiyo ndio Rhema.

Wakristo wengi wanafikiri kuwa katika agano la kale, manabii huenda Mungu alikuwa na njia maalumu sana ya kuongea nao tofauti na sisi. Hao watu walikuwa kama sisi, waliishi hapahapa, walikula chakula hikihiki n.k. hawakutofautiana na sisi. Mungu alizungumza nao kwa njia hii hii ambayo ndiyo anazungumza na sisi leo, hakuna tofauti.

Kwa hiyo ndugu yangu usipoweza kumtii Mungu katika mambo ya kila siku ya kawaida na hata katika mambo madogomadogo, Mungu hawezi kuendelea kuongea na wewe, Mungu anaposema tuishi kwa imani yaani maana yake tuishi kwa kumsikiliza yeye.

Biblia inasema,
Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani: naye akisita sita Roho yangu haina furaha naye (Waebrania 10:38).

Tumeona kuwa, imani chanzo chake ni kusikia. Sasa andiko hili linasema Ataishi kwa imani. Maana yake ni kwamba, ataishi kwa kusikia kutoka kwa Mungu (kwa sababu imani chanzo chake ni kusikia).

Kuishi ni nini?
Kuishi ni kule kuwa hai kila sekunde inayopita. Uhai ukisimama sekunde moja mtu atakufa. Hivyo kila sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwaka, unapokuwa bado uko hai huko ndiko kuishi.

Mungu anataka uishi kwa kumsikiliza yeye. Mungu anataka yeye ndiye akuongoze akuagize nini cha kufanya kila sekunde katika maisha yako ya kimwili na kiroho.
Wakristo wengi wanajiendea tu na kujifanyia mambo yao wenyewe bila ya kuongozwa na Mungu. Hii imekuwa hivi kwa sababu hawajui nini maana ya kuishi kwa imani. Kuishi kwa imani wanafikiri ni kuishi maisha ya shida, kubahatisha kupata riziki, maisha ya kubangaiza yasiyokuwa na uhakika. Kuisi kwa imani ni kuishi maisha ya kumsikiliza Mungu anakuagiza kufanya nini.

Wakristo wengi wanaishi kwa kujionea wenyewe, ndio maana wamejaa shida, dhiki na kukosa mafanikio. Wengi wanafanya mambo ambayo Mungu hajawaagiza na wengi wapo mahali ambapo Mungu hajawaagiza kuwa pale. Wanafanya na wapo pale kwa mapenzi yao wenyewe si kwa mapenzi ya Mungu.
Watumishi wa Mungu wengi wana wito lakini wanafanya wito ambao hawakuitiwa. Ni sawa wameitwa kumtumikia Mungu, lakini je ni mitume, nabii, mwinjilisti, mchungaji au mwalimu na je kituo au mji walipo ndipo Mungu anataka wawepo? Shida ni kwamba wengi hawajui kuisikia sauti ya Mungu

Sauti ya Mungu inapokuja kwako inakuwa ina mambo mawili. Ni kama kifurushi chenye vitu viwili ndani yake  ambayo ni maagizo ya kufanya na nguvu ya Mungu ya kuyatekeleza maagizo hayo. Hivyo ukitenda uliyoagizwa na Mungu unafanikiwa. Ukitenda maagizo ya shetani kunatokea uharibifu. Hakikisha unatenda maagizo ya Mungu na pia hakikisha uko mahali ambapo Mungu amekuagiza uwe. Sisemi uache kufanya lolote sababu Mungu hajazungumza na wewe, wewe endelea kufanya mambo kama kawaida yako, hata kama Mungu hajazungumza na wewe, na wakati huohuo ukimsikiliza Mungu, endapo Mungu atasema na wewe basi fanya lile aliloguagiza.

Tukutane tena Jumanne katika mwendelezo wa somo hili, ambapo tutajifunza Sauti ya Mungu katika kutenda muujiza.

Mwalimu Furaha Amon ni Mchungaji wa Kanisa la Vijana, KLPT Tanga. Anapatikana kupitia namba 0713461593 na barua pepe mwakasege.furaha@yahoo.com
Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.