SOMO: HATUA TATU ZA MTU KABLA HAJACHUKUA HATUA YA MAUAJIHATUA TATU ZA MTU KABLA HAJACHUKUA HATUA ZA KUJIUA AU KUUA MTU
Na Mchungaji Peter Mitimingi
Somo hili amefundisha kwenye kipindi EATV
1. MAWAZO YA NDANI KWA NDANI (SUCIDAL THOUGHTS)
Katika hatua hii mtu anakuwa amepatwa na msongo wa mawazo (stress) na mambo ambayo yanakuwa yanaulemea moyo wake kiasi cha kutamani kujiua au kuudhiwa na mtu kiasi cha kutamani kumuua huyo anayemuudhi. Hayo yote hufanyika ndani ya moyo kama mawazo pasipo kusema kwa muhusika wala kwa mtu yeyote. Yanakuwa ni mawazo tu ya ndani kwa ndani ya mhusika kwamba mimi ipo siku nitajiua au anawaza tu kwa maisha haya heri nijiue. Au mwingine anawaza kwajinsi anavyo nifanyia kuna siku mimi nitamuua nk.

2. MATAMSHI YA KUJIUA AU KUUA MTU (VERBAL-THOUGHTS)
Hatua ya pili ni pale inapofikia mtu anashindwa kuendelea kuyatunza ndani yale mawazo ya kujiua au kuua mtu na kujikuta akisema mara kwa mara kwa mtu au watu kwamba heri ningekufa tu, au kuanza kutamka kwamba kunasiku mimi nitajiua au ipo siku mimi nitakuua au nitaua mtu. Hii ni hatua ya pili ya ukomavu wa hatua za kuelekea kujiua au kuua mtu. Katika Saikolojia tunasema ukisikia mtu aanatoa matamshi ya kusema atakuja kujiua au heri nife au kuna siku mimi nitaua mtu, kauli kama hizo sio za kupuuzia kabisa ni vema ukafanyika utaratibu wa kujua kwanini mtu amefikia hapo nini kimeujaza moyo wake kiasi cha kujikinai na kukinai maisha mpaka kuona kifo ndio suluisho. Mtu kama huyo anatakiwa kupatiwa msaada wa ushauri (counseling) mapema iwezekanavyo maana hiyo ni dllili ya wazi kuelekea kwenye kifo chake au cha mtu mwingine.

3. HATUA YA UTEKELEZAJI WA KIFO CHENYEWE
Mtu anapofikia hatua ya kujiua au kuua mtu huwa sio tukio la ghafla tu amejikuta kajiua au kaua mtu. Kama nilivyosema tukio la kifo huwa lilishaanza siku nyingi sna akilini mwake akali-process kwa muda mrefu mpaka kupanga na ni nyenzo gani atatumia katika kutekeleza tukio hilo la kifo. Wakati tukio linatokea moyo wa mtu huyu unakuwa tayari umelemewa na hawezi tena kujidhibiti yeye mwenyewe na ile hali ya utu inakuwa imeshamtoka kiasi kwamba haogopi tena polisi au kukamatwa kama ataua mtu au kama chochote kitatokea anakuwa hana woga wowote.

UHUSIANAO WA HAIBA YA MTU NA TUKIO LA KIFO

SANGWINI
Kwa mtu mwenye haiba ya SANGWINI anapokuwa amelemewa na kuudhiwa sana, akifikia uamuzi wa kuwaza kifo huwa anajawa na hasira na kutekeleza tukio la mauaji kwa kumuua yule ambaye ndio anakuwa amemuudhi au kumsababishia hasira au maudhi hayo.

MELANKOLI:
Kwa mtu mwenye haiba ya Melankoli kwake yeye ni tofauti, anapokuwa amelemewa na maudhi na hasira zikafika juu kabisa, badala ya kumdhuru au kumuua yule aliyemkasirisha au aliyemsababishia yale maudhi yeye huwa anajiua yeye mwenyewe kutokana na maudhi ya mtu mwingine tofauti na Sangwini ambaye yeye anaweza kutumia chochote kilichopo mbele yake kumdhuru hata kumuua aliye muudhi.

HITIMISHO:
Hatua hizi ni kama hatua za mtu kujenga nyumba. Kwanza huanza kama wazo la nyumba anayotaka kuijenga. Wazo la kujenga nyumba linakuwa katika mawazo yake mwenyewe kwa muda mrefu. Kisha anaanza kuwaelezea watu juu ya maono ya nyumba anayotaka au tarajia kuijenga hata kama ni katika siku za usoni. mwishowe picha ya hiyo nyumba huwa inachorwa na baadae hatua za ujenzi wa ile nyumba hufanyika na nyumba kujengwa hata kukamilika. Hatua hizo hufanana kabisa na hatua za mtu anayetaka kujiuua au kuua mtu. Huanza kama wazo ndani kwa ndani, kisha kutoa matamshi ya wazo hilo kwa watu na kama hatasaidiwa baadaye kutekeleza uamuzi huo wa kujiua au kuua mtu.


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.