SOMO: MAJARIBU MAKUBWA MATATU KATIKA UTUMISHI WAKO,WALAKINI YAKUPASA UYASHINDE

Maombi ni silaha ya ushindi ©followingthetruth

Na Mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Yapo majaribu mengi katika imani zetu katika Kristo Yesu haswa pale unapokuwa umeokoka. Kitendo tu cha kuokoka ni kutangaza vita dhidi ya shetani na mapepo yake,kwa maana nguvu ya giza kamwe haipendi wokovu wako. Ikumbukwe ya kwamba kadri unavyokuwa kiimani ndivyo majaribu yanaongezeka na hii ni kweli kabisa. Lakini twajipa moyo vile tusomapo;

“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” 1 Wakorintho 10:13

Kumbe;Hatuwezi kujaribiwa kupita tuwezavyo,lakini pia kumbe kila jaribu lina mlango wake. Bwana Mungu ameweka njia ya kutokea kwa kila jaribu kwa sababu Yeye Mungu ni mwaminifu,kwamba yeyote atakaye liitia jina la Bwana katika yale ayapitiayo,mtu huyo ataokoka na jaribu hilo.

Ikumbukwe kuwa,hatuwezi kuomba majaribu yasije kwa maana majaribu hayazuiliwi kwa maombi bali tunaweza kuomba kuvuka katika kila jaribu lijalo katika jina la Yesu Kristo. Hivyo basi, unapopanda ngazi ya utumishi tegemea kukutana na majaribu makubwa matatu. Majaribu haya hayaletwi na Mungu kwa maana MUNGU hamjaribu mtu (Yakobo 1:13).

shetani ndio mwenye kuyaleta ili akuangushe katika utumishi wako. Majaribu haya ni mitego ya shetani kukuondoa katika kusudi la MUNGU,tazama mitego hii ;

01.TAMAA YA UZINZI.

shetani hutumia mbinu hii kuwanasa watumishi wa Mungu wengi katika kanisa la leo. Tazama,ikiwa wewe ni mtumishi wa Mungu wa kiume,basi shetani atakuletea mwanamke mzuri mwenye roho ya ushawishi akujaribu na ikiwa wewe ni mwanamke shetani atakuletea mwanaume akujaribu.

Lengo kubwa ni kuangusha utumishi wako. Mara nyingi tumesikia watumishi wakidondoka katika dhambi ya uzinzi,hii ikiashilia kwamba shetani amewaweza kuwanasa katika mtengo huo.

02.KUPENDA FEDHA KUPINDUKIA.

Ikumbukwe ya kwamba kupenda fedha kupindukia ni shina baya sana,linalowafarakanisha wengi na imani yao.

“ Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” 1 Timotheo 6:10

Tunajua ya kwamba;kila mtu anapenda fedha,lakini tunatofautiana katika kupenda. Wapo watumishi wa Mungu ambao kwa kweli wanapenda fedha sana kiasi kwamba mpaka uwape pesa ndio afanye huduma. Yaani yeye huuza huduma kwa pesa tena ni pesa taslimu. Huu ni mtego wa shetani na ni jaribu ambalo wengi wamenaswa humu.

Tazama wapo watumishi walionaswa kiasi kwamba udiriki kutengeneza mafundisho fulani ya kutengeneza pesa kwa matoleo na mara nyingi mafundisho haya huwa ni makali sana kuwatisha watu kwamba wasipotoa hawatabarikiwa na hata kufa watakufa. Au wengine wamenaswa na jaribu hili kiasi kwamba hutengeneza miujiza feki,kwa lengo la kuwavuta watu watoe pesa. N.K

03.ROHO YA KUJIINUA.

Ikumbukwe kwamba kila mtu hupenda sifa fulani au kusifiwa. Lakini ni bora watu wakusifie kuliko kujisifia wewe mwenyewe.Tabia hii ya kujisifia ikikua huzaa roho ya kudharahu wengine wote,tena kumbuka roho hii ni ya shetani. roho ya kujiinua ni pale ambapo mtu hutumia nguvu kubwa za kwake mwenyewe kusudi awe juu pasipo MUNGU kuhusika.

Ni sawa na roho ya kiburi ndani ya mtu. Hivyo jaribu hili limeachiliwa tayari katika huduma zetu. Wapo walionaswa na ni wengi maana utakuta mtumishi akijisifia madhabahuni badala ya kutoa neno la Mungu. Wengine hujiita majina ya ajabu ajabu ya sifa kuonesha wao ni bora kuliko wakristo wote duniani. Biblia inasema;

“ Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Luka 14:11

Laiti kama tunajua kwamba tukijikweza,tutashushwa basi tungeepukana na tabia hii.

NINI CHA KUFANYA?

Jambo kubwa la kufanya litakalokupa ushindi katika maeneo yote hayo matatu ni; Kukuaa uweponi mwa BWANA MUNGU kila wakati.

Maana katika uwepo,hakuna roho ya uzinzi itakayoshinda hata ijapoachiliwa kwako,tena hakuna roho ya kupenda fedha,wala majivuno hayatakuwepo. Uwepo wa Bwana unakufanya kupungua zaidi ili Bwana awe juu zaidi,na ndipo utakapoziona nguvu za MUNGU katika utumishi wako.~Kwa huduma ya maombezi na ushauri,piga sasa +255 655 11 11 49.

Mchungaji Madumla Gasper.

Beroya Bible fellowship Church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

    Pata wimbo "Machozi" kutoka kwao Tumaini Shangilieni Choir St James ArushaShare on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.