SOMO: TUJIKUMBUSHE ULE MFANO WA NDEGE WA ANGANI - MCHUNGAJI MADUMLA


Na Mchungaji Gasper Madumla

Ninajua weweza ukawa umesahau ule mfano alioutoa BWANA YESU kuhusu ndege wa angani vile ambavyo hawapandi wala hawavuni ghalani lakini hula chakula kila siku. Imekuwa vyema leo tukumbushane mfano huo,sababu ndege wa angani wana mengi ya kutufunza katika imani zetu.

Sasa, Sijui wala sina hakika kwamba inaweza ikatokea siku moja ambapo ndege wa angani akalala na njaa siku nzima kwa sababu ya kukosa chakula,la hasha! Bali hula siku zote. Au je inawezekana hilo? Yesu anasema leo;

“ Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?” Mathayo 6:26

Ndipo sasa nikajifunza,imani waliyokuwa nayo ndege ni imani ya kujifunza,kwa maana wenyewe hawaiangalii kesho yao kama vile tuiangaliavyo,lakini kula wanakula,kunywa wanakunywa. Kumbe ni MUNGU ndie awapaye chakula cha kila siku.

Nikiyasoma maisha ya ndege wa angani,huwa nafarijika sana kwa maana ninapata mafunzo mengi mno. Ndege wa angani hawana shamba wanalolima,wala hawavuni. Ndege hupenda kujitengenezea viota vyao kwa kukusanya manyasi na kisha hukaa humo. Ndege menyewe anakijua kiota chake,huwezi kumdanganya tena wala hapotei kwake;huruka huku na huku na mwisho hurudi katika kiota chake.

Ikiwa kama utajaribu kumdanganya umuwekee kiota cha bandia basi uwe na uhakika hawezi kuingia humo ngoo! La! Akiingia atatoka mara! Bali ataakikisha anaingia katika kiota chake.

Hapo najifunza vile ambavyo mwamini wa leo asivyoweza kulijua kanisa la kweli,kwamba ukimdanganya na kumuwekea kanisa la bandia la miungu,basi aweza kuingia na kukaa humo akidhani mahali alipo ndipo alitakiwa kuwepo. Tazama watoto wa ndege hutambua mahali kiota chao kilipo,huruka na kuingia humo wote tena,kuruka pamoja na mama yao.

Lakini leo,sisi wengi hatutambui uwepo wa kanisa,na hata tukitambua basi hatuingii wote mara nyingi tunawaacha wengine nyuma. Tena mara nyingi hatutembei na mchungaji katika roho moja. Lakini sivyo kwa mama ndege na watoto wake. Lakini cha zaidi tukimuangalia ndege tunaona kwamba;

Ndege wa angani,hana msongo wa mawazo ya kufikiri kwamba kesho atakula nini. Wala hana msongo wa mawazo kufikiri kwamba kesho hali ya hewa itakuwaje. Na labda ndege angelikuwa anavaa mavazi kama wanadamu nafikiri asingeliwaza atavaa nguo gani,au atavaa kiatu gani kesho,au atavaa sketi/suluani gani siku ya kesho.

Hivyo basi,ndege hawaisumbukii kesho yake,lakini hula na kunywa kila siku. Yesu anasema “... Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. “. Hapo nikajifunza kwamba, suala la kesho ni la BWANA. Maana hakuna aijuaye kesho yake isipokuwa BWANA tu.

Tunaweza kujifunza mengi kuhusu simulizi za ndege wa angani. Katika mambo mengi yanayomuhusu ndege,tunagundua kwamba neema ya Mungu i juu yao. Kwa sababu neema ni upendeleo wa kiungu usiostahili. Ndege wamepewa upendeleo wasio stahili wa kula pasipo kupanda wala kuvuna. Alikadhalika tukirejea kwetu sisi wanadamu tunagundua kwamba nasi tunaishi kwa upendeleo huo huo; Vile tunavyovuta pumzi hii ya bure,maisha tunayoishi,vyote hivi ni kwa neema tu. N.K


Kile tunachojifunza katika mfano huu wa ndege wa angani ni kwamba,tusiyasumbukie mavazi,wala chakula kwa maana hata mataifa huyasumbukia hayo,bali sisi tutafute kwanza ufalme wa mbinguni na haki yake na hayo yote tutazidishiwa.(Mathayo 6:33)

Siku moja naliamka asubuhi sana na kuelekea barabarani nikitokea mahali nilipokuwa nimepanga maeneo ya Kimara Kilungure. Nikaelekea barabarani Kimara Baruti,siku hiyo niliona watu wakiwa bize kuwahi mjini kwenye sehemu zao za kazi.

Kwa sababu ya foleni,naliona wengine wakishuka katika madala dala na kupanda boda boda kuelekea mjini kuwahi kazi,wengine walikuwa wakitembea baada ya kuona foleni kali,wengine wapo katika bajaji,yaani basi ilimladi kila mmoja alikuwa na pilika pilika ya namna yake, ya kuwahi kule aendako. Nikajiuliza ikiwa kama hawa wote wangelikuwa wanawahi katika nyumba za ibada kwa staili hii,basi hakika mambo yao mengine yangezidishiwa.

Shida iliyopo leo ni pale ambapo wewe unaangaikia maisha kuliko kuutafuta ufalme wa MUNGU kwanza. Ni lazima ifike wakati tujue kwamba maisha haya tuliyonayo sasa ni ya kitambo tu. Tujifunze mfano wa ndege wa angani,tena tujifunze kwa mfano wa maua ya mashamba jinsi yameavyo hayafanyi kazi wala hayasokoti.

Hivi ni kwa nini mambo ya MUNGU unayaweka nyuma kuliko mambo yako binafsi? Mbona suala la kuchelewa ibadani kwako limekuwa ni la kawaida,lakini papo hapo huwezi kuchelewa kazini mwako? Kumbuka Mungu hadhiakiwi,tafuta kwanza ufalme wake na haki yake na hayo yote utazidishiwa.

Utakuta mkristo akisahau simu nyumbani,gafla hurudi na kuichukua au atafanya maarifa yoyote yale ilimradi aipate ile simu. Lakini akisahau biblia utamsikia akisema“si,nikirudi nitaikuta tu” yaani wala hashtuki tena hata kama kaisahau katika dala dala utakuta akisema“Aaah ! nitanunua nyingine,siyo ishuu bhana” Lakini ingelikuwa ndio simu,weee! Angerudi kuitafuta huku akilia. Hii ni mbaya sana,kwa nini tunaweka mambo ya Mungu nyuma? Je ni kweli tu wajinga kiasi hiki?

Au unafikiri neno la Mungu limedanganya?au limekosea?La! Neno la BWANA ni amini na kweli. Ukihitaji kuzidishiwa katika mambo yako basi tanguliza kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu.

Mungu amepanga kuwapa chakula cha kila siku ndege wa angani ambao si bora zaidi yako. Kumbe chakula,mavazi yote hayo tayari MUNGU ameyaachilia kwa ajili yako,lakini kile unachotakiwa ni kugeuka kuutafuta ufalme wa Mbinguni.

Kumbuka;Watu wa mataifa hutafuta chakula na mavazi bali wewe kaza kuutafuta ufalme wa MUNGU.

Kwa maombi na ushauri,piga+255 655 11 11 49.

Mch.Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.