SOMO: UNDANI WA MAOMBI (2) - MCHUNGAJI MADUMLA

Katika maombi ©fearlessconversations


Kama hukusoma sehemu iliyopita BONYEZA HAPA 
Bwana Yesu asifiwe…

Karibu mpendwa tuendelee kujifunza tena siku hii ya leo;

(ii) Maombi ni njia aliyoichagua Mungu kutupatia mahitaji yetu.

Kwa sababu binadamu hajakamilika bado,hivyo basi anahitaji msaada utokao kwa Mungu. Mungu hutumia njia hii ya maombi kutujibu mahitaji yetu. Tazama,kila mtu ana haja yake ndani ya moyo wake. Ikiwa ni hivyo,kwamba maombi ni njia ya mahitaji yetu,basi tusipoomba hatuwezi kupokea. Labda tuangalie mfano mdogo wa kawaida kabisa;

Chukulia una watoto watatu nyumbani mwako,alafu mtoto wako mmoja akawa na uhitaji wa kununuliwa daftari la mazoezi la hesabati. Kisha;mtoto huyo akawa kimya akisubiri umnunulie pasipo yeye kukuomba anachokihitaji kutoka kwako. Swali,je utamnunulia hilo daftari pasipo kukuomba? Utajuaje kama daftari lake limeisha na anahitaji daftari jingine? Ukweli ni kwamba,hutaweza kumnunulia kwa sababu hajakuomba,na inawezekana usijue kama limeisha.

Na hata kama akikulalamikia kwamba “baba,mbona uninunulii daftari? Ujui kama daftari langu la mazoezi la hesabu limekwisha?...” Lakini tazama atakavyosema baba yake “ mwanangu,mbona hukuniomba? Kumbe ilimpasa kijana huyu aombe. Vile anasoma shule sio ishu! Kusoma shule hakumgarantii kupewa mahitaji yake yote kama hataomba.


Kwa mfano huo ninajifunza kwamba, kuomba ni jambo la lazima ikiwa kama tunahitaji kupokea,tena Mungu huangalia njia hii ili ashushe mahitaji yetu. Biblia inasema;

“Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” Isaya 43:26

Bwana Mungu anakualika usongee mbele zake,ueleze mambo yako ili upate haki yako. Hivi,waweza ukajiuliza kwamba;“ kwani Mungu anioni,mpaka nianze kujieleza,kuombaa wee,Yeye si ananiona lakini!,anipe haki yangu” Kukuona anakuona,ila anakuhitaji wewe umuombe,umkumbushe ili akupatie hitaji lako. Ndio maana ameweka utaratibu wa maombi,kwamba sisi wanadamu tumuombe Yeye kila siku,hii ni njia maalumu~angalia tena hapa;“ Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. “Isaya 1:18a

(iii) Maombi ni mawasiliano ya kiroho kwa njia ya lugha kati ya MUNGU aliye hai na watu wake. Mawasiliano haya ni mawasiliano kati ya Roho na roho,ambapo roho hushuka ili Roho ipande. Na katika eneo hili ambapo roho yako itashuka katika mawasiliano na Roho wa Bwana,basi hapo ndipo pana ujazo wa nguvu za Mungu.

02.KWA NINI TUNAOMBA?

Zipo sababu nyingi za msingi zinazotufanya tudumu katika maombi. Na kila sababu ina nguvu ya kipekee kutusukuma tuzidi kuomba;Zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo;

01.Tunaomba kwa sababu maombi ni agizo maalumu lenye ahadi.

Wajibu wa kila mkristo ni kuhakikisha anaomba kila siku kwa sababu tumeagizwa na Bwana kuomba bila kukoma,bila kukata tamaa;

“ Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.” Luka 18:1

Neno “ kupasa,” lina maana ya lazima,na sio hiyari. Neno hili linapotumika huonesha hali ya ulazima wa jambo fulani. Mfano mtu akikuambia “imekupasa kwenda kazini leo” hii ni sawa anakuambia “lazima uende kazini leo”.Hivyo tunaomba kwa sababu tumeamriwa kuomba. Amri yoyote ya BWANA ni kubwa nayo ina nguvu tena ni lazima tuifuatwe kama ilivyo amriwa.

Bwana akisema “ omba” na usipoomba ujue umefanya dhambi mbele zake. Lazima ujue kwamba,mtu yeyote asiyeomba kwa Mungu katika jina la Yesu Kristo afanya dhambi. Kwa sababu tumeamriwa kuomba,basi hatuna budi kuomba kila siku pasipo kukata tamaa. Soma 1 Wathesalonike 5:17,Wakolosai 4:2

Laiti kama maombi yasingekuwa ni lazima,basi yamkini tusingeliomba. Wewe,unahitajika kuomba kila siku.

(ii) Tunaomba Kwa sababu ya matatizo na dhiki tunazopitia.

Ni ukweli usiopingika kwamba ulimwenguni tunayo dhiki walakini twapaswa kujipa moyo (Yoh. 16:33). Dhiki na matatizo tunayopitia kila siku yamekuwa sababu kubwa ya kutufanya kumuomba MUNGU kwa bidii. Changamoto za maisha zinatusukuma kumtafuta Bwana Mungu kwa njia ya maombi.

Waweza kujipima wewe mwenyewe vile ambavyo ulivyo sasa,na vile ulivyokuwepo kipindi cha dhiki na shida kwamba ni kipindi kipi ulikaza kuutafuta uso wa BWANA kwa njia ya maombi. Tukimwangalia Daudi,tunagundua naye alikaza kusema na Bwana vipindi vyote,haswa katika shida, Daudi anasema;

“ Katika shida yangu nalimwita BWANA;” Zab.118:5a

Angalia tena hapa;“Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. ” 2 Samweli 21:1a

Kuna kipindi ambapo matatizo yanakubana kila kona na unakosa mlango wa kutokea isipokuwa kwa njia ya maombi tu. Tazama jambo hili kwa mtu anayeumwa,utakuta mtu anapitia kati hali mbaya ya magonjwa,hospitalini ametibiwa wee lakini hakuna majibu bado. Hata inafika wakati daktari wake anamshauri ajaribu njia ya kuombewa. Watu wa namna hii wakiombewa kwa jina la Yesu Kristo hupona.

Sasa angalia; shida ilivyochangia kumfanya mtu ambaye hakuwa na time na Mungu,kuanza kuwa na time na Mungu akimtafuta kwa njia ya maombi. Fikiria jambo hili, kwamba laiti kama maisha yetu yangelikuwa murua yaani safii,hakuna shida,hakuna magonjwa wala hakuna dhiki,Je idadi ya watu kwenye vikundi vya maombi ingeikuwaje? Au je hali ingelikuwaje huko makanisani? Watu wangelifunga na kuomba? Waweza kupata picha hapo jinsi hali angelikuwaje. Hivyo changamoto za maisha zinatufanya tuzidi kumtafuta Bwana Mungu kwa njia ya maombi…

ITAENDELEA…

Inawezekana kabisa somo hili limegusa sehemu ya maisha yako,na unahitaji ushauri wa kiroho pamoja na kuombewa. Basi piga sasa kwa namba hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church (Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.