SOMO: ZIJUE HATUA 11 ZINAZOKAMILISHA TOBA HALISI - MCHUNGAJI MADUMLA


 Na Mchungaji Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Siku ya leo,ndani yangu ninawiwa nikueleze hatua kumi na moja muhimu utakazozitumia kukamilisha toba yako. Hatua hizi hutumika mara kwa mara zikionesha mpangilio mzuri katika toba.

Hivyo basi,hatuna budi kuanza kujifunza ni nini haswa maana ya toba. Ili tutakapoziangalia hatua hizo zikawe msaada mkubwa kwetu;

Toba ni neno lenye asili ya lugha ya Kiebrania,lenye maana ya geuka.neno hili linapotumika lina maana ya kugeuka kutoka katika dhambi na kumuelekea Mungu kwa njia ya maungamo na kufuatiwa na matendo mema mara tu baada ya toba,kuonesha kwamba mtu huyu,sasa amebadilika kupitia maungamo yake.

Tuangalie mfano huu;

“ bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.” Matendo 26:20

Paulo anatuambia kwamba,alipowahubiria watu hao,kitendo kilichofuata;kilikuwa ni toba,yaani watu hao walipaswa kutubu,kugeuka kutoka katika dhambi na wamwelekee Mungu. Kisha wayatende matendo mema yenye kuambatana na kutubu kwao.

Kumbe toba yenye maana ni ile yenye kugeuka kutoka dhambini. Lakini ikiwa unatubu kisha uko vile vile,hakuna badiliko basi toba hiyo haitakuwa na maana kwako,kwa maana haiwezekani ukatubia dhambi ya uzinzi huku ukiwa umepanga kwenda kuifanya kesho yake.


Hivyo basi toba ni tendo la imani la kurejesha roho iliyopotea katika dhambi imuelekee MUNGU kwa njia ya kuungama dhambi zote kwa msaada wa Roho mtakatifu.

Neno Kuungama dhambi maana yake ni kukiri makosa yako mbele za Mungu bila kujiami wala kujitetea na kujutia dhambi zote ulizozifanya kisha kuweka adhimio kwamba hutarudia tena.

Katika maungamo yako,hutakiwi kujitetea au kujiami. Mfano wa mtu anayejitetea mbele za Mungu kipindi anatubia dhambi zake,Ni kama vile anasema hivi;

“…Baba,Mungu kwa kweli natubia dhambi hii ya wizi,lakini kwa kweli sasa ningefanyeje maana ela zenyewe zilikuwa wazi wazi,kwanza mtu yoyote yule asingeweza kuzikwepa,sasa Mungu unisamehe Bwana,maana ela zenyewe zilikuwa ni nyingi alafu zilikaa kiasara asara mimi ndio maana nilizichukua,nisamehe Mungu wangu...!”

Mtu wa namna hiyo,kwa kweli hajatubu chochote kile kwa sababu kwanza anajiami,na kujitetea,pili hana mpangilio maalumu. Tuangalie mfano wa Danieli alipokuwa akitubia dhambi za ndugu zake;

“Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;”Danieli 9:4-5

Kumbuka;Toba ya kweli ni lazima imuhusishe Roho mtakatifu. Kwa maana Yeye ndie amsaada wa kweli,Yeye ndie akukumbushae dhambi zako zote ulizozitenda. Kwa maana ziko dhambi nyingine huwezi kuzikumbuka kwa akili zako za kibinadamu,unamuhitaji Roho wa Bwana akukumbushe na kukupa wepesi wakati wa toba yako.

KWA NINI TUNATUBU?

Hivi umeshawahi kujiuliza hivyo? Au kwa nini tunarudia rudia toba? Au je vile tulivyotubu mara ya kwanza tulipoongozwa sala ya toba haikutosha?

Hayo ni maswali ya muhimu sana kujiuliza. Zipo sababu mbali mbali zinazotufanya kutubu kila siku,kila saa. Nimejaribu kukupatia sababu tatu za msingi zinazotufanya kutubu mara kwa mara;

01. Tunatubu kwa sababu miili tuliyonayo imebeba asili ya dhambi.

Ni ukweli usiopingika kwamba asili ya miili yetu ni dhambi. Tazama,mwili hutamani ukishindana na Roho,Roho nayo hushindana na mwili. Soma Wagalatia 5:17. Hivyo utagundua kwamba mwili humejawa na mambo mengi ya kidunia,hutamani,hupenda ya dunia. Kwa sababu hii ya mwili kuwa na asili ya dhambi,yatupasa kudumu katika toba. Biblia inazidi kutupa mwanga katika hili,tunasoma tena;

“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.” 1 Yoh.1:8&10

02. Tunatubia dhambi kwa sababu ya kurejesha ushirika kati yetu sisi na MUNGU wetu.

Kumbuka,dhambi ilipoingia ulimwenguni, ilitengeneza kiambaza kilichomtenga mtu na Mungu wake. Kiasi kwamba Mungu hakuwa na mawasiliano ya karibu kama jinsi ilivyokuwa,hivyo ushirika kati ya Mungu na mwanadamu ukapotea. Isaya 59:2

Mtu huyu,akapoteza mfanano na Mungu wake kwa sababu ya uwepo wa dhambi. Tazama vile Yesu asemavyo katika Luka 19:10; kwamba Yeye alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichokuwa kimepotea ( yaani ushirika,ulipotea) Tunapotubu tunarejesha mfanano wa mwanzo na kufanyika rafiki wa Mungu.

Kumbuka;Dhambi yoyote ile inakutenga mbali na Mungu wako kwa maana hukumu ya dhambi zote ziko sawa,ni katika ziwa la moto wa milele. Hivyo basi hakuna dhimbi ndogo wala dhambi kubwa~dhambi ni dhambi,tubia sasa urejeshwe.

03.Tunatubu mara kwa mara kwa sababu ya kujiandaa na safari yetu ya mbinguni kwa maana hatujui siku wala saa.

HATUA KUMI NA MOJA ZINAZOKAMILISHA TOBA YAKO.

Hatua hizi,zapendeza kuzifuata katika toba yako,nazo ni

01. Mshukuru Bwana Mungu wako.

Kushukuru ni hatua ya kwanza katika toba yako. Hakikisha unamshukuru Bwana Mungu kwa kupata fursa ya toba,maana si wengi wapatao fursa hiyo.

Kwa sababu wapo watu ambao walitamani wapate japo dakika 1 tu ya toba lakini hawakupata nao hivi sasa ni marehemu,wengine vinywa vyao vimefungwa akili zimeruka wapo vitandani hospitalini,sasa wewe ni nani basi hata upate muda kama huo wa toba! Je si neema na rehema za BWANA? Ukitambua hilo,utamshukuru MUNGU kabla ya kuanza toba yako. Zab.138:1-2

02.Lisifu jina la Bwana Mungu wako.

Kumbuka Mungu hushuka katika sifa zake. Hivyo kusifu kwapendeza sana kabla ya kuomba chochote kile. Mungu alishuka kipindi cha ibada ya sifa na maombi ya akina Paulo na Sila Soma Matendo 16:25-26.

Tumia neno la Mungu katika kusifu kwako wakati unajiandaa kutubu,mfano waweza kutumia

“…kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.” Yoeli 2:13

03.Omba msaada wa Roho mtakatifu.

Ni lazima ujue kwamba wewe pasipo Roho mtakatifu hauwezi kabisa. Maombi yoyote yale yanahitaji Roho mtakatifu ayaongoze,kadhalika hata maombi ya toba yanamuhitaji Roho ayatawale na kuyaongoza. Sisi wenyewe hatujui kuomba ipasavyo,bali Roho hutusaidia udhaifu wetu.

“ Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”Warumi 8:26 Soma pia Yohana14:26

04. Samehe wote waliokuudhi.

Huwezi kusamehewa dhambi zako ikiwa wewe hujawasamehe wakosa wako. Kipimo cha msamaha kwako ni kuwasamehe wakosa wako;

“Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” Mathayo 6:14-15

Hivyo basi,tangaza msamaha kwa wote waliokukosa. Waachilie watoke moyoni mwako na wala usiwe na uchungu maana uchungu ni ukuta katika toba yako. Fanya hivyo kwa kumaanisha kabisa,kabla hujaanza kuomba toba katika haja zako binafsi.

05. Eleza dhambi zako zote,unazozikumbuka na usizozikumbuka.

Hakikisha unaeleza dhambi zako zote,bila kuficha ficha. Zile unazozikumbuka omba toba,hata zile usizozikumbuka mwambie Mungu “natubia hata dhambi ambazo nimezitenda lakini sizikumbuki kwa sasa,Ee Roho mtakatifu unisaidie...” Umjulishe Bwana dhambi zako zote,ili usamehewe. Mungu ukimficha,utakuwa unajidanganya mwenyewe kwa maana Yeye anazijua zote;

“Nalikujulisha dhambi yangu,Wala sikuuficha upotovu wangu.Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.” Zab.32:5.

06.Jutia dhambi zako zote.

Hiki ni kitendo cha kusikitikia dhambi ulizozitenda. Kwamba kwa nini umefanya dhambi hizo? Hakikisha majuto haya yatoke moyoni mwako,isiwe kwa mdomo tu.

“Kwa maana nitaungama uovu wangu,Na kusikitika kwa dhambi zangu” Zab.38:18

Mfano; Mtazame Petro alipotenda dhambi ya kumkana Bwana Yesu,alitubu kwa majonzi,huku ndiko kujutia dhambi zako;

“Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.” Mathayo 26:75

07.Omba msamaha,omba rehema mbele za Mungu.

Sasa hapa ndipo kwenye kiini chenyewe cha toba yako. Omba msamaha kwa kumaanisha kabisa,waweza kuanza kutumia maneno ya toba katika Zab. ya 51 yote.

“ Ee Mungu, unirehemu,Sawasawa na fadhili zako.Kiasi cha wingi wa rehema zako,Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu,Unitakase dhambi zangu.” Zab. 51:1-2

08.Ialike damu ya YESU,ikaoshe dhambi zako.

Toba yoyote ile ya kweli ni lazima ihusishe damu ya Yesu,kwa maana damu ndio itakasayo dhambi. Damu ni ya muhimu sana katika toba;

“kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” Mathayo 26:28

“ Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Waefeso 1:7

09. Hakikisha unapata amani ya msamaha kwa kila dhambi unayotubu.

Mfano; unataka kutubia dhambi za aina tatu,chukulia ya kwanza ni dhambi ya wizi,dhambi ya uzinzi,na dhambi ya kiburi. Sasa, unapoanza kutubia dhambi ya wizi,basi hakikisha umeimaliza yote na kupata amani ya msamaha kwa dhambi hiyo ndiposa uingie kutubia dhambi nyingine ya uzinzi nayo ni vivyo hivyo,kisha umalizie dhambi ya kiburi.

Haitakiwi kuruka ruka,kwamba umetubia kidogo tu mara umeingia kutubia nyinge tena gafla ukaanza na nyingine, hapana sio hivyo!

10.Weka adhimio kwamba hutarudia tena.

Ukimaliza kutubu,na upo vizuri kwamba amani ya Kristo Yesu imepatikana basi usisahau kuweka adhimio kwamba“sitarudia tena dhambi hii,Ee Roho mtakatifu unisaidie”

“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.“Mithali 28:13

11.Mshukuru Mungu kwa kuamini yote uliyoomba umeyapokea.

Kumbuka,ukiomba jambo lolote lile usisahau kumalizia na shukrani kwa Bwana Mungu ukiamini lile uliloliomba limekuwa lako.

“Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.”Mathayo 21:22

FAIDA ZA TOBA YA KWELI.

01.Kuponywa magonjwa.

Toba halisi huleta uponyaji, kwa sababu magonjwa mengi husababishwa na uwepo wa dhambi. Hivyo ikiwa dhambi itaondolewa basi afya urejea.

“Akusamehe maovu yako yote,Akuponya magonjwa yako yote,”Zab. 103:3

02. Kuwa na uhakika na uzima wa milele.

Mtu aliyesamehewa dhambi huwa na uhakika na kuupata uzima wa milele kwa sababu sasa amehuishwa tena,kwamba alikuwa amepotea sasa amepatikana.

03.Kupata kibali.

Fikiri ukiwa rafiki wa Mungu,je hutapata kibali? Au fikiria mtu aliyesamehewa dhambi hatakubalika mbele za Mungu. Na akikubalika mbele za Mungu,basi ujue hata kwa wanadamu hukubalika katika kibali kikuu.

“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Mithali 28:13.

Angalia; yule atakaye zificha dhambi zake hatafanikiwa,kinyume chake ni sawa na kusema atakayeziungama dhambi zake atafanikiwa.

MADHARA YA KUTOTUBU.

Yapo madhara mengi kwa mtu anayeishi maisha bila kutubu kwa Mungu wake. Haya yafuatayo ni machache tu;

01. Kutawaliwa na roho ya hasira,visasi na malipizi.

02.Kushindwa kusamehe wengine.

03.Kutembea katika laana.

04. Kokosa tumaini la maisha ya uzima wa milele. N.K

Hivyo basi,yatupasa kuishi maisha ya toba kila siku. Sisemi utengeneze makosa ili utubu kila siku,hapana! Bali pale unapoingia katika maombi yako,anza na toba,na wala usije kujihesabia haki.

Inawezekana labda ulishawahi mara nyingi kutubu,lakini bado warudia dhambi ile ile kila siku,na umeshindwa kuiacha,naomba niombe na wewe leo,nipigie sasa kwa namba hii;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya Bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.