HOJA: CHANGAMOTO YA WIVU DHIDI YA WASIOKUWA NA HATIA

Wiki zimepita kupitia kipindi cha WAPO Radio cha TUAMKE PAMOJA, ambapo nilikuwa na ujumbe kuhusu changamoto za wivu dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Tafsiri ya wivu niliyosimamia kwa msamiati wa Kiswahili ni “kijicho” likimaanisha “tabia ya kutokupenda mtu mwingine apate mafanikio.” Nimeona leo sahemu ya ujumbe huu kwa muhtasari niuwasilishe kwako ili upate kujifunza chimbuko la wivu, aina zake na madhara yake na jinsi ya kujilinda nao:
Wivu tu ©Covermaker

Wivu ndio chanzo cha
ukatili na mauaji duniani

Mauaji ya kwanza kufanyika katika historia ya binadamu, na binadamu wa kwanza kufariki dunia chimbuko lake lilikuwa ni wivu! Biblia imesimulia kisa hiki cha aina yake kuhusu watoto wa binadamu wa kwanza ambao ni Kaini na Habili. Hawa ni watoto wa Adamu na Eva ambao ni binadamu wa kwanza walioumbwa kwa mikono ya Mungu mwenyewe.
Askofu Sylvester Gamanywa

Baada ya anguko la dhambi walifukuzwa kwenye bustani wakaenda kuanza upya maisha ya kujitegemea. Watoto wao Kaini na Habili walipokuwa wakubwa, kila mmoja alichagua mfumo wa maisha ya kujitegemea. Kaini alichagua kuwa mkulima na Habili kuwa mfugaji. Kwa maagizo ya wazazi kuhusu suala la ibada kwa Mungu waliagizwa kumtolea Mungu sadaka au dhabihu ili kupokea kibali, kufunikwa dhambi zao kupitia sadaka zao. Ni wakati wa kutoa dhabihu ulipofika ndipo tunashuhudia kisa cha kwanza kinachohusu wivu na madhara yake:

"Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;  bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana..." (MWA.4:4-5)

Kaini alighadhabika kwa sababu alihisi alistahili kupata baraka kwa sadaka zake kama mdogo wake Habili alivyopata baraka kwa sadaka zake. Kaini alihisi kudhalilika mbele za Habili kwa kutakaliwa sadaka zake. Badala ya Kaini kumsikiliza Mungu ili afanye ibada kwa usahihi, akamhesabu Habili ndiye mbaya wake anayemzuilia baraka za Mungu

Mungu kwa uaminifu wake na hali alikijua Kaini amekusudia kumdhuru mdogo wake aliongea na Kaini ili kumwonya asifanye dhambi: "BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?  Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde." (MWA.4:6-7)

Hapa Mungu alimthibitishia Kaini kwamba kiini cha tatizo la kukataliwa sadaka yake sio Habili ila ni yeye hakuzingatia masharti ya sadaka. Lakini WIVU ulikwisha kumjaa Kaini hakutaka kumsikiliza Mungu:"Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.  BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?  Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi." (MWA. 4:8-10).

Haya ndiyo mauaji ya kwanza katika historia ya binadamu duniani. Wivu umesababisha ukatili dhidi ya damu isiyo na hatia. Hivi ninapoongea wakati huu, kuna watu wasiokuwa na hatia ambao wamo magerezani kwa sababu ya WIVU wa watu waliokuwa kinyume nao kwa sababu ya mafanikio yao, au kwa sababu wamewatafsiri kuwa wanawazibia milango ya mafanikio yao wakati kumbe sivyo. 


Chimbuko la tabia ya wivu
Wivu katika asili yake ni hisia hasi ndani ya nafsi ya mtu. Hisia hii hujidhihirisha pale ambapo mwenye kuwa na wivu anapokuwa mbinafsi kwa maana ya kujihisi yeye bora zaidi au kujidhani anastahili kuliko wengine wanaomzunguka. Jambo jingine linalochochea wivu ni “kutokujisikia salama” kwa maana ya kuwa na hofu ya kupoteza heshima, umaarufu au maslahi fulani.

Kwa hapa ninatoa ushahidi wa kisa maarufu sana kati ya mfalme wa kwanza wa Israeli aliyeitwa Sauli na kijana mdogo Daudi ambaye alipata kibali mbele za Mungu cha KUWA mfalme badala ya Sauli. Sauli alianza kutawala Israeli akiwa na miaka 30. Katika ufalme wake Sauli hakumtii Mungu na akapoteza sifa za kuendelea kuwa mfalme wa Israeli. Mungu aliamua kwenda kumpaka mafuta Daudi Akiwa mdogo wa umri miaka 15 akiwa bado anachunga kondoo wa baba yake

Umaarufu wa Daudi uliibuka ghafla Alipojitoa mhanga wa kupambana na   Goliati aliyekuwa tishio kubwa la majeshi ya Israeli. Wakati huo alikwisha kupambana na kuua wanyama hatari ambao ni simba na dubu waliokuja kushambulia kondoo wa babake porini. Kwa uzoefu huu Daudi alipata ridhaa ya Sauli kwenda kupambana na Goliathi. 

"Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.  Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile." (1 SAM. 18:6-9)

Unasikia maneno ya Sauli anasemaje hapa? Anasema "wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata isipokuwa ni ufalme?... Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile...." Sauli amesahau jinsi alivyokwisha kutabiriwa na nabii Samweli kwamba ufalme wake hautadumu kwa sababu amekiuka miiko na maagizo aliyopewa na Mungu. Sasa hasira zake anakuja kuzitupa juu ya Daudi ambaye si yeye akijipendekeza kwa Mungu dhidi ya ufalme wa Sauli. ni Mungu ndiye aliyemkataa Sauli na kumchagua Daudi. Uadui wa Sauli dhidi y Daudi ulichukua miaka 8 akimwinda ili apate kumwua kwa sababu tayari alikwisha kuwa tishio dhidi ya kiti chake cha ufalme.

Japokuwa Sauli hakufanikiwa kumwua Daudi kwa sababu Mungu alimlinda sana Daudi; tunajifunza kwamba WIVU wa Sauli ulitokana na HOFU ya Sauli mwenyewe ya Kupoteza umaarufu na nafasi yake ya utawala. Kama ilivyo ada WIVU unapofusha macho ya mtu kuona matatizo yake binafsi yanayomkwamisha kufanikiwa na anajihami kwa kutupa lawama na kuwaandama wengine wanaoonekana kufanikiwa zaidi yake kwenye mambo yale anayoyatamani lakini Hana sifa tena sifa za kuwa nayo. Anajidanganya nafsi kwa kudhani kwamba, akiwazuia, kudhibiti, kuwahujumu, mafanikio yao yatakuwa kwake. 

Wivu wa kitaasisi
katika huduma za Injili
Wivu katika huduma za Injili nimeutafsiri kuwa ni WIVU WA KITAASISI. Hapa nina maana watu ndani ya taasisi kuoneana wivu wenyewe kwa wenyewe; au kuwaonea wivu watu wa taasisi nyingine inayofanikiwa kuliko ya kwao. "Wivu wa kitaasisi" dhidi ya taasisi nyingine unatokana na hofu ya kupoteza wafuasi au kupoteza umaarufu wa kitaasisi katika jamii: "Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli.  Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya." (YAK. 3:14-16)

Hawa ni jamii ya watu wenye imani moja ndani ya kanisa. Lakini wanaoneana wivu kwa sababu ya tofauti za vipawa na karama za Roho. Kuna baadhi ya waamini ambao wanasumbuliwa na wivu hasa wanapowaona waamini wenzao ambao pengine ni wachanga, au hawana muda mrefu katika imani kama wao, wakitumiwa na Roho Mtakatifu badala ya kutumiwa wao wanaojiona wamekuwepo kanisani kwa muda mrefu.

Wakati mwingine wivu wa kitaasisi ndani ya taasisi unakuwa ndani ya viongozi wa taasisi ambao wanahofia kupoteza nafasi zao za uongozi au kupoteza heshima na umaarufu wao mbele za waamini. Wanapoinukia viongozi wapya wenye ushawishi wa kiutendaji tayari wanakuwa tishio dhidi ya viongozi wanaoshindwa kufanya vizuri kama wanavyotarajiwa na wafuasi wao.

Aina ya pili ya wivu wa kitaasisi ni pale ambapo wafuasi wa taasisi moja kuwaonea wivu wafuasi wa taasisi nyingine na hasa taasisi mpya inayoonekana kuja na ushawishi mkubwa wa kufanya wafuasi kuhamia kwenye taasisi hiyo mpya: "Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.  Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa." (MDO13:45-46)

Hawa ni wafuasi wa taasisi ya kiyahudi waliomwonea wivu Paulo ambaye aliihama taasisi yao na kujiunga na taasisi mpya ya Kanisa ambalo lina ujumbe wenye ushawishi kuliko dini ya kiyahudi. Haya, huu nao ni wivu wa kitaasisi, unaosababishwa na hofu ya kupoteza wafuasi kwenda kwenye taasisi nyingine, ndio huzalisha mbinu na mizengwe ya kuwadhibiti isivyostahili viongozi wa taasisi nyingine yenye kutishia maslahi na heshima ya taasisi yao.

Wakati mwingine kwa sababu ya huo wivu hufanyika mikakati ya kuwafanyia fujo ili mradi tu kupunguza au kudhoofisha juhudi za taasisi wanayoiona kuwa tishio kwao.“Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; (MDO17:4-5)

Ni nini kilitakiwa kufanyika kwa taasisi yenye wivu wa kitaasisi dhidi ya taasisi nyingine? Kwanza ni kujitathimini kiitikadi kama kweli wako sahihi kiitikadi na kama wanatimiza wajibu wa kutangaza itikadi yao kwa usahihi. Taasisi ikijitathmini na kujitambua imepungukiwa au imepoa au imetoka kwenye misingi sahihi, badala ya kuona wivu dhidi ya taasisi nyingine zinazofanya vizuri wajirekebishe na kujipanga upya kwa kujiboresha vile inavyotakiwa.

Madhara ya wivu
Madhara ya wivu ni mtambuka. Hayawaathiri tu wanaoonewa wivu bali huwaathiri hata wenye kuona wivu dhidi ya wengine. Madhara ya dhidi ya wenye kuona wivu hayajulikani kwa waathirika kwa sababu ya uelewa mdogo kuhusu elimu ya hisia. Kila binadamu ameumbwa na hisia. Hapo mwanzo kabla ya anguko katika dhambi hisia za binadamu zilikuwa chanya na hazina upungufu.

Dhambi ilipoingia katika maumbile ya binadamu ikasababisha madhara ya kimaumbile zikiwemo hisia zake. Ndipo zikaibuka hisia hasi ambazo zimejengwa juu ya Hofu. Ndiyo maana baada ya Adamu na Eva kutenda dhambi waliamua kujificha kwenye bustani ili Mungu asiwaone. Wivu nao ni hisia hasi kama ilivyo hofu nayo ni hisia hasi. Biblia imeandika habari za wivu katika kitabu cha Mit. 14:30: “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; bali husuda ni ubovu wa mifupa.” Hapa neno husuda maana yake ni wivu. Kwa hiyo, wivu kama hisia hasi ina madhara kwa afya ya mwili yenye kuathiri mfumo wa mifupa.

Lakini imebainika pia kwamba wivu kwa kuwa huchochea hisia ya uchungu, kinyongo, huzuni, na hasira hali hizi husababisha maradhi ya shinikizo la juu la damu, maumivu ya kifua, udhaifu mfumo wa kinyesi, maumivu ya kichwa, kukosa usingizi na mengineyo mengi. Kisaikolojia mtu mwenye wivu hushindwa kutumia muda wake kwa mambo ya kujiendeleza kwa sababu muda mwingi huutumia kuwaza mambo ya wengine ambao ni mahasimu wake na hutafakari ni jnsi gani apate kukwamisha maendeleo yao. Hii husababisha msongo wa mawazo na wakati mwingine kuchanganyikiwa akili.

Kijamii, mtu mwenye wivu hana mahusiano mazuri na wengine, kuanzia kwenye familia, majirani, mahali pa kazi au kwenye shughuli za uzalishaji. Kwa sababu ni mbinafsi sana mwenye kutaka kufanikiwa dhidi ya wengine, hujihusisha kwenye vitendo vya kuhujumu mafanikio ya wengine kwa njia za fitina na uchongezi dhidi ya asiopenda mafanikio yao. Hata kukithiri kwa vitendo vya uchawi na ushirikina kunakosababisha kulogana na kuuana chimbuko lake ni wivu ulioanza ndani ya mioyo na ndipo huamua kutafuta mbinu za kudhibiti, kuzuia, kukwamisha mafanikio ya wengine ili wao wafanikio kupitia migongo ya wengine.

Kiroho mtu mwenye wivu hawezi kumwabudu Mungu kwa ukamilifu, kwa sababu, nafsi yake imejaa mawazo mabaya dhidi ya mwenzake, hivyo ibada zake huwa ni batili mbele za Mungu. Mara nyingi anaposikia mambo ya Mungu hushtakiwa na dhamiri yake kwa kutokuwa na mawazo safi na hivyo huishia kufanya usanii na maigizo ya kiibada ili aonekane mcha Mungu wakati sio kweli.

Matokeo yake hujitengenezea maadui ambao nao huamua kulipiza kisasi na hapo ndipo Biblia isemapo kwamba: “Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo na machafuko, na kila tendo baya.” (Yk.3:16). Wivu ni mojawapo ya dhambi za siri. Mwenye wivu hufanya mambo yake kwa siri ili wale anaowaonea wivu wasimgundue mpaka hapo anapokuwa ametimiza njama zake za hujuma. Ndiyo maana wivu umehusishwa na uchawi kwa vile walogaji hufanya hujuma na ukatili wao gizani, mahali ambapo hawawezi kuonekana hadharani.

Pamoja na kwamba wivu una madhara mengi kuanzia athari za kiafya, kisaikolojia, kijamii mpaka kiroho; ukweli mwingine unaojitegemea ni kwamba wivu haulipi kabisa. Wivu hauna faida hata kidogo. Kwa sababu mwenye wivu ameshindwa kufanikiwa basi hataki na wengine wafanikiwe na anataka wote waishie kwenye mkwamo wa kimaisha. Uzoefu umeonyesha kwamba, wenye kuonewa na wivu ni wenye nafasi au uwezo wa mafanikio na hawataki kuachia nafasi walizo nazo au hawataki kuwawezesha wengine wafanikiwe kama wao. Mwenye nafasi Fulani anataka yeye ndiye aendelee kuwepo kwenye nafasi hiyo hata kama uwezo wake wa kiutendaji umekwisha kupungua viwango vya ubora.

Kwa mtu kama huyu kila aliye chini yake mwenye sifa na uwezo wa kushika nafasi yake anaonekana kuwa tishio dhidi ya nafasi yake, na huanza kutafuta njama za kumdhibiti hata kumhujumu ili asije akafikia kumwondoa kwenye nafasi yake. Kwa kufanya hivyo wenye wivu wanaua nguvu kazi ya watu wenye uwezo na sifa bora ambao kama wangepewa nafasi wangeleta tija kwenye taasisi au katika jamii au katika huduma za kikanisa. Badala ya taasisi au jamii kuinuka kimaendeleo inazidi kudidimia kwa sababu walioshika nafasi wamepoteza sifa na uwezo lakini hawataki kuwatia moyo na kuwahamasisha wengine.

Kwa sababu ya wivu viwango vya ubora havizingatiwi, makampuni yanafilisika, mashirika yanashindwa kutoa huduma bora, na makanisa yanadumaa badala ya kukua yanashindwa kutimiza lengo kuu la kufanya mataifa kuwa wanafunzi wa Yesu.


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.