SOMO: UNDANI WA MAOMBI (5) - MCHUNGAJI MADUMLA


Na Mchungaji Gasper Madumla

Kama ni msomaji mpya unaweza kusoma sehemu iliyopita kwa kubonyeza HAPA

Bwana Yesu asifiwe…

…utagundua kwamba,maombi ya kushukuru yana nguvu sana kwa yule anayeshukuru kwa kumaanisha kutoka rohoni. Katika aina hii ya kwanza ya maombi,sasa,tuangalie ;

Nguvu ya maombi ya kushukuru na mifano yake.

* NGUVU YA KUSHUKURU.

Katika kushukuru tunapokea vingi,mfano ndani ya maombi ya kushukuru tunapokea uponyaji,kufunguliwa,kupokea mema tusiyostahili N.K Unaweza ukajiuliza kivipi? Au inakuwaje kuwaje kuyapokea yote hayo;

Em tazama hapa katika mfano wa kwanza wa ule mkutano mkubwa wa waume elfu tano bila kuhesabu watoto na wanawake ambao waliketishwa chini wakala samaki na mikate. Biblia inasema kulikuwepo na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili tu,lakini mara baada ya maombi ya shukrani kufanyika,gafla pakawa na zidisho la mikate mingi na samaki wengi wa kulisha watu zaidi ya elfu tano. Napenda vile habari hii ilivyoandikwa katika injili ya Yohana,tusome hapa;

“Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka.” Yoh.6:11

Biblia haielezi kwamba Yesu aliomba maombi mengine, isipokuwa Yeye alishukuru tu. Je kwa nini Yesu alishukuru tu? Jibu; Bwana Yesu anataka kutufundisha kwamba kuna nguvu katika kushukuru kwa mtu wa rohoni.

Kumbuka ya kwamba Yeye Yesu alikuwa mwanadamu asilimia miamoja na alikuwa MUNGU asilimia miaamoja,lakini kule kuwa mwanadamu anatufundisha sisi namna ya kuishi kiimani,katika hekima yote tukimpendeza Mungu na wanadamu wenzetu.

Tazama,alipoitwaa ile mikate,alimuamini MUNGU kwamba lolote aliombalo kwa Baba atapewa sawa sawa na hitaji lake lililopo moyoni mwake. Hitaji kubwa lilikuwa ni kupata mikate mingi na samaki wengi wa kulisha mkutano mkubwa.

Mungu alilijua hilo,naye Bwana Yesu akashukuru sawa sawa na hitaji lililopo. Hata leo,unapoomba maombi yoyote yale,kabla ya kuomba ujue kwamba MUNGU anajua unalohitaji,hivyo ni vyema sana ukaanza na maombi ya kushukuru ukiamini kwamba MUNGU amekwisha kukupea hitaji lako maana Yeye ni Yehova yire ( Bwana anayejibu haja zetu) Mwanzo 22 :14.

Tazama tena hapa; habari ya kufufuliwa kwa Lazaro kule Bethania. Neno la Mungu linasema Yesu alimshukuru BWANA MUNGU kwa habari ya kifo cha Lazaro ili makutano wamtukuze Mungu na mwana atukuzwe kwa huo (Yoh.11:4) Angilia hapa jinsi maombi ya kushukuru yalivyoleta ufufuo kwa Lazaro;

“Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.” Yoh.11:41

Huwa mimi binafsi ninajiuliza swali moja,kwamba laiti ungelikuwa wewe ndio umepata nafasi ya kuomba katika mazingira kama haya aliyokutana nayo Yesu. Je ungeshukuru ?

Au ungeanza maombi ya kuvunja na kuteketeza nguvu za giza,na kuharibu roho ya mauti? Mimi sijui ungelifanyeje hapo!! Lakini sipati picha jinsi ingekuwa kwa mlokole wa leo kupata nafasi ya kuombea mtu aliyekufa,au kuombea jambo ambalo majibu yake ni kama vile hayapo.

Lakini,kumbe hupaswi kuomba maombi mengine ya kwako~ni lazima umsikilize Roho wa Bwana anataka nini katika mazingira magumu kama hayo. Kwa maana kama utamsikiliza vizuri Yeye anaweza kukuambia ushukuru tu basi na usiongeze chochote cha kwako,kisha ukifanya sawa sawa na muongozo huo basi ujue kwamba omba yako ya shukrani itajibiwa kwa mengi hata kwa yale ambayo hujayaomba.

~ Yesu anasema “…, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.” Andiko hili linatufunza kwamba,ukishukuru basi ni lazima uamini kwamba MUNGU anakusikia. Itakuwa haina maana kama utaomba pasipo imani.

Bwana Yesu anatufundisha zaidi kwamba tunapohitajika kuomba chochote kile basi ni lazima tuweke imani zetu kwa BWANA tukijua ya kwamba Yeye hutusikia tuombapo.

Katika mifano hiyo miwili tumeona maombi ya kushukuru yamesababisha muujiza ya kuzidishwa kwa mikate na samaki pia maombi ya kushukuru yameleta muujiza wa kufufuka kwa Lazaro. Lakini tambua hili; maombi ya shukrani yana nguvu sana kwa mtu yule aliye rohoni kama vile alivyokuwa Yesu.

Kuwa rohoni ni mchakato wa maisha ya utakatifu,ambapo kila mwenyekumfuata Yesu anapaswa aishi hivyo. Kwanza aokoke,kisha aweze kupata chakula kamili cha roho yake ambacho ni neno la Mungu yaani akulie wokovu wake pamoja na maombi ya nguvu. Na kuendelea kudumu katika kuyafanya mapenzi yote ya Mungu.

Anza kujizoeza kushukuru mara kwa mara katika maombi yako ili uanze kuwa na mabadiliko katika maombi yako,huku ukijua kwamba kushukuru kunaleta majibu mengi katika kila ombi…

ITAENDELEA…

Kwa msaada zaidi wa maombi,naomba usisite kunipigia kwa simu yangu hii~mimi nipo karibu nawe kwa maombi piga;+255 655 11 11 49.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

S.L.P 55051,DAR.TZ.

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.